الدُّرُوسُ الْمُهِمَّةُ لِعَامَّةِ الْأُمَّةِ
MASOMO MUHIMU KWA UMMA WOTE
لِسَمَاحَةِ الشَّيْخِ العَلَّامَةِ
عَبْدِ العَزِيزِ بْنِ عَبْدِ اللهِ بْنِ بَازٍ
رَحِمَهُ اللهُ
Abdulaziz bin Abdullah bin Baaz, Mwenyezi Mungu amrehemu
بِسْمِ اللهِ الرَّحمَنِ الرَّحِيمِ
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu
Utangulizi wa Mwandishi
Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote, na mwisho mwema ni kwa wacha Mungu, na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wake na Mtume wake, Nabii wetu Muhammad, na jamaa zake na maswahaba wake.
Ama baada ya hayo:
Haya ni maneno mafupi katika kufafanua baadhi ya yale ambayo watu wote wanapaswa kuyajua kuhusu dini ya Uislamu, niliyaita: “Masomo muhimu kwa umma wote”.
Ninamuomba Mwenyezi Mungu awanufaishe kwayo Waislamu, na aipokee kutoka kwangu, kwani yeye ndiye Mpaji, Mkarimu.
Abdulaziz bin Abdullah bin Baaz, Masomo Muhimu kwa umma wote1
Somo la 1: Surat Al-Fatihah na Sura zingine fupi fupi
Surat Al-Fatihah na kile kinachowezekana miongoni mwa sura fupi fupi kama vile Surat Al-Zilzalah hadi Surat An-Nas, kuhusiana na kuzipokeza, kusahihisha kisomo, kuhifadhisha na kueleza yanayolazimu kuyajua.
Somo la 2: Nguzo za Uislamu
Kueleza nguzo tano za Uislamu, ya kwanza yake na kuu yake: Kushuhudia ya kwamba hakuna mungu mwingine anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu; kwa kufafanua maana yake na kueleza masharti ya shahada ya hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu. Na maana ya "Hakuna mungu" ni kukanusha kila kitu kinachoabudiwa kando na Mwenyezi Mungu. Nayo "isipokuwa Mwenyezi Mungu" ni kum thibitishia Mwenyezi Mungu peke yake ibada bila ya kuwa na mshirika yeyote. Na ama masharti ya "hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu peke yake" ni: kuwa na elimu inayoondoa kutoijua, na yakini inayoondoa shaka, na kumnyenyekea Mwenyezi Mungu tu ambako kunaondoa kumshirikisha, na ukweli ambao unaondoa uongo, na upendo ambao unaondoa chuki, na utiifu unaoondoa ushirikina, na kukubali kunakoondoa kukataa, na kukufuru vyote vinavyo abudiwa kando na Mwenyezi Mungu.
Haya yamekusanywa katika beti mbili zifuatazo:
Elimu, yakini, ikhlasi na ukweli wako Pamoja na upendo, utiifu na kuyakubali Na zidisha la nane ambalo ni kukufuru kwako Vyote viabudiwavyo visivyokuwa Mwenyezi Mungu
Pamoja na kufafanua shahada ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na matakwa yake ni: kumsadiki katika yale aliyosema, kumtii katika yale aliyoamrisha, kujiepusha mbali na yale aliyokataza na kukemea, na kwamba asiabudiwe Mwenyezi Mungu isipokuwa kama alivyoamrisha Mwenyezi Mungu Mtukufu katika sheria na Mtume wake, rehema na amani ziwe juu yake. Kisha amfafanulie mwanafunzi nguzo tano zilizobakia za Uislamu, ambazo ni: Swala, Zaka, kufunga saumu katika mwezi wa Ramadhani, na kufanya Hija kwenye Nyumba Takatifu ya Mwenyezi Mungu kwa mwenye uwezo wa hilo.
Somo la 3: Nguzo za Imani
Nazo ni sita: Kumwamini Mwenyezi Mungu, Malaika wake, Vitabu vyake, Mitume wake, na Siku ya Mwisho, na kuamini Kadari na mipango ya Mwenyezi Mungu; kwamba mazuri na mabaya yote hutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Somo la 4: Aina za Tauhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) na aina za ushirikina
Kufafanua aina za Tauhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu). Nazo ni tatu: Kumpwekesha katika umola wake, kumpwekesha katika uungu wake, na kumpwekesha katika majina na sifa zake.
1. Kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika umola wake. Na hilo ni kuamini kwamba Mwenyezi Mungu aliyetakasika ndiye Muumba wa kila kitu, anayeendesha kila kitu, hana mshirika katika hilo.
2. Kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika uungu. Na hilo ni kwa kuamini kwamba Mwenyezi Mungu aliyetakasika ndiye anayepasa kuabudiwa kwa haki, hana mshirika katika hilo, na hiyo ndiyo maana ya laa ilaaha illallah. Kwani maana yake ni: Hakuna mungu apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo ibada zote kama vile swala, kufunga saumu na nyinginezo ni lazima akusudiwe kwazo Mwenyezi Mungu peke yake, na wala hairuhusiki kumfanyia yeyote chochote katika ibada hizo isipokuwa Yeye.
3. Kumpwekesha katika majina na sifa zake. Na hilo ni kwa kuamini yote yaliyotajwa ndani ya Qur-ani Tukufu, au Hadithi sahihi miongoni mwa majina na sifa za Mwenyezi Mungu, na kumthibitishia hilo Mwenyezi Mungu peke yake kwa namna inayomfailia Yeye aliye takasika, bila ya kuyabadilisha, kuyakataa, kuyaeleza jinsi yalivyo hasa, wala kuyapigia mfano, kwa kufanyia kazi maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿قُلۡ هُوَ ٱللَّهُ أَحَدٌ 1 ٱللَّهُ ٱلصَّمَدُ 2 لَمۡ يَلِدۡ وَلَمۡ يُولَدۡ 3 وَلَمۡ يَكُن لَّهُۥ كُفُوًا أَحَدُۢ4﴾
"1. Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee.
2. Mwenyezi Mungu ndiye Mkusudiwa.
3. Hakuzaa wala hakuzaliwa.
4. Na hakuna anayelingana naye hata mmoja." [Al-Ikhlaas: 1-4]. Na amesema Mwenye nguvu, Mtukufu:
﴿...لَيۡسَ كَمِثۡلِهِۦ شَيۡءٞۖ وَهُوَ ٱلسَّمِيعُ ٱلۡبَصِيرُ﴾
"Hakuna kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona." [Ash-Shuraa: 11]. Na baadhi ya wanazuoni waliifanya kuwa aina mbili tu kwa kuingiza pamoja kumpwekesha katika majina na sifa zake na kumpwekesha katika umola wake, na hakuna ukinzani katika hilo, kwa sababu makusudio yako wazi katika migawanyiko yote miwili.
Na aina za ushirikina ni: ushirikina mkubwa, ushirikina mdogo na ushirikina uliofichikana.
Ushirikina mkubwa: Huu unalazimu kuharibika kwa matendo na kukaa milele Motoni kwa wale wanaokufa bila ya kuuacha, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...وَلَوۡ أَشۡرَكُواْ لَحَبِطَ عَنۡهُم مَّا كَانُواْ يَعۡمَلُونَ﴾
"Na lau wangelimshirikisha, yangeliwaharibikia yale waliyokuwa wakiyatenda." [Al-An'am: 88]. Na amesema Mwenyezi Mungu aliyetakasika:
﴿مَا كَانَ لِلۡمُشۡرِكِينَ أَن يَعۡمُرُواْ مَسَٰجِدَ ٱللَّهِ شَٰهِدِينَ عَلَىٰٓ أَنفُسِهِم بِٱلۡكُفۡرِۚ أُوْلَٰٓئِكَ حَبِطَتۡ أَعۡمَٰلُهُمۡ وَفِي ٱلنَّارِ هُمۡ خَٰلِدُونَ 17﴾
"Haikuwa kwa washirikina kwamba waiimarishe misikiti ya Mwenyezi Mungu, hali ya kuwa wana zishuhudia nafsi zao wenyewe ukafiri. Hao matendo yao yaliharibika, na katika Moto wao watadumu." [At- Tawba: 17]. Na kwamba yeyote atakayekufa bila ya kuuacha, hatasamehewa, na itakuwa haramu kwake kuingia Peponi, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَغۡفِرُ أَن يُشۡرَكَ بِهِۦ وَيَغۡفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَآءُ...﴾
"Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kushirikishwa, na husamehe madhambi yasiyokuwa shirki kwa amtakaye." [Surat An-Nisaa: 48].
Na amesema Mwenyezi Mungu aliyetakasika:
﴿...إِنَّهُۥ مَن يُشۡرِكۡ بِٱللَّهِ فَقَدۡ حَرَّمَ ٱللَّهُ عَلَيۡهِ ٱلۡجَنَّةَ وَمَأۡوَىٰهُ ٱلنَّارُۖ وَمَا لِلظَّٰلِمِينَ مِنۡ أَنصَارٖ﴾
“Kwani anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu atamharamishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na waliodhulumu hawatakuwa na wowote wa kuwanusuru.” [Al-Maida: 72].
Na katika aina zake ni kuwaomba dua wafu, masanamu, kuwaomba msaada, kuwawekea nadhiri, kuwachinjia na mfano wa hayo.
Ama ushirikina mdogo, nao ni kile kinachoitwa shirki ambacho kilithibitishwa kwa maandiko kutoka kwenye Qur-ani au Sunnah, lakini si katika aina za ushirikina mkubwa; kama vile kujionyesha kwa watu katika baadhi ya matendo, kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na kusema: “Mwenyezi Mungu akipenda na mtu fulani akipenda”, na mfano wa hayo; kwa mujibu wa maneno ya Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Kitu ninachowahofia zaidi ni ushirikina mdogo." Akaulizwa kuhusu ushirikina mdogo, akasema: "Ni kujionyesha."2 Imepokelewa na Imam Ahmad, At-Twabarani, na Al-Bayhaqi, kutoka kwa Mahmud bin Labiid Al-Answari - Mwenyezi Mungu amridhie - kwa msururu mzuri wa wasimulizi. Na imepokelewa na At-Twabarani kwa misururu mizuri ya wasimulizi, kutoka kwa Mahmud bin Labiid, kutoka kwa Rafi' bin Khadiij, kutoka kwa Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.
Na kauli ya Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie: 'Anayeapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, basi hakika ameshirikisha.'3 Imepokelewa na Imamu Ahmad kwa msururu sahihi wa wasimulizi, kutoka kwa Umar bin al-Khattwab, Mwenyezi Mungu amridhie. Imepokelewa na Abu Daudi na At-Tirmidhi kwa msururu sahihi wa wasimulizi kutoka kwa Hadithi ya Ibn Umar, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba alisema: “Mwenye kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, basi hakika amekufuru au ameshirikisha."4 Na kauli ya Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie: "Msiseme: Ni kwa kutaka Mwenyezi Mungu na fulani, lakini semeni: Akitaka Mwenyezi Mungu kisha akataka fulani."5 Imepokelewa na Abu Daudi kwa msururu sahihi wa wasimulizi kutoka kwa Hudhayfah bin al-Yamaan, Mwenyezi Mungu amridhie.
Aina hii hailazimu mtu kutoka katika Uislamu, wala haimfanyi mtu kukaa Motoni milele, lakini inapingana na ukamilifu wa lazima wa kumpwekesha Mwenyezi Mungu.
Aina ya tatu: Ushirikina Tashahudi. Na ushahidi ni kauli ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, "Je, nisikuambieni ni nini kinachohofiwa zaidi juu yenu kuliko Masihi Dajjal (Mpinga Kristo)?" Wakasema: "Ndiyo, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu." Akasema: "Ushirikina uliojificha, ambapo mtu ana nyanyuka akaanza kuswali na hapo akaipamba swala yake kwa sababu ya kuangaliwa na mtu."6 Imepokelewa na Imamu Ahmad katika Musnad yake, kutoka kwa Abu Said Al-Khudrii, Mwenyezi Mungu amridhie.
Ushirikina unaweza pia kugawanywa katika aina mbili tu:
Ushirikina mkubwa na mdogo. Ama ushirikina ulio fichika, huo unaingia katika aina mbili hizi. Unaingia katika mkubwa, kama vile ushirikina wa wanafiki, kwa sababu wanaficha itikadi zao batili. Wanadhihirisha Uislamu kwa ajili ya kuonyesha watu na kujihofia wenyewe.
Na inakuwa katika ushirikina mdogo, kama vile kujionyesha, kama ilivyo katika hadithi ya Mahmud bin Labiid al-Answari iliyotajwa hapo awali na hadithi ya Abu Sa'id. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuwezesha mafanikio.
Somo la 5: Kufanya ibada kwa wema
Nguzo ya Ihsan ni kumwabudu Mwenyezi Mungu kana kwamba unamwona, na kama humwoni, basi anakuona.
Somo la 6: Masharti ya swala
Nazo ni tisa:
Uislamu, akili timamu, upambanuzi, kuondoa hadathi, kuondoa najisi, kufunika uchi, kuingia kwa wakati wa swala, kuelekea Kibla na kuweka nia.
Somo la 7: Nguzo za swala
Nazo ni kumi na nne:
Kusimama wima kwa mwenye uwezo, Takbiratul-Ihram (Takbira ya kuanza Swala), kusoma Al-Fatiha, kurukuu (kuinama), kuinuka kutoka kwenye rukuu na kusimama wima, kusujudu juu ya viungo saba, kuinuka kutoka kwenye sijda, kukaa kati ya sijda mbili, utulivu katika matendo yote, kufuatanisha nguzo kwa mpangilio wa sawasawa, kusoma Tashahudi kwa mara ya mwisho, kukaa kwa ajili ya Tashahudi, na kumswalia Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - na kutoa salamu mbili.
Somo la 8: Wajibu za swala
Nazo ni nane:
Takbira zote isipokuwa Takbiratul-Ihram (Takbira ya kuanza Swala), na kusema: Samia' llahu liman hamida (Mwenyezi Mungu amemsikia mwenye kumsifu) kwa Imam na mtu binafsi. Na kusema: Rabbana walakal hamd (Mola wetu Mlezi ni zako sifa njema) kwa wote. Na kusema: Subhana Rabbiyal Adhwim (Ametakasika Mola wangu Mlezi, Mkuu) katika rukuu, na kusema: Subhana Rabbiyal A'alaa (Ametakasika Mola wangu Mlezi wa juu zaidi) katika sijda. Na kusema: Rabbighfirliy (Mola wangu Mlezi, nisamehe) baina ya sijda mbili, na Tashahudi ya kwanza, na kukaa kwa ajili yake.
Somo la 9: Kufafanua Tashahudi
Ni kusema:
At-twahiyyatu lillahi was-swalawaatu wat-tayyibaatu. As-salaamu 'alayka ayyuhan-Nabiyyu wa rahmatullahi wabarakatuhu. As-salamu 'alayna wa 'ala 'ibaadillah As-swalihiin. Ash-hadu allaa ilaaha illallah wa ash-hadu anna Muhammadan 'abduhuu warasuuluhuu (Maamkizi yote ni ya Mwenyezi Mungu, na swala zote na mazuri yote. Amani iwe juu yako, ewe Nabii na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka zake. Amani iwe juu yetu na juu ya waja wema wa Mwenyezi Mungu. Ninashuhudia kuwa hapana mungu ila Mwenyezi Mungu. Na ninashuhudia kuwa Muhammad ni mja wake na Mtume wake).
Kisha atamswalia na kumuombea baraka Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - kwa kusema: Allahumma swalli 'alaa Muhammad wa 'alaa aali Muhammad kamaa swallaita 'alaa Ibraahima wa 'alaa aali Ibraahim, innaka hamiidum-majid. Wa baarik 'alaa Muhammad wa 'alaa aali Muhammad kamaa barakta 'alaa Ibraahima wa 'alaa aali Ibraahim, innaka hamiidum-majid (Ewe Mwenyezi Mungu mshushie Muhammad rehema, na jamaa zake Muhammad, kama ulivyomshushia rehema Ibrahim na jamaa za Ibrahim. Hakika Wewe ni Msifiwa, Mtukufu. Na mbariki Muhammad na jamaa zake Muhammad, kama ulivyombariki Ibrahim na jamaa zake Ibrahim. Hakika Wewe ni Msifiwa, Mtukufu).
Kisha, katika Tashahudi ya mwisho ajikinge kwa Mwenyezi Mungu kutokana na adhabu ya Motoni, na kutokana na adhabu ya kaburini, na kutokana na majaribio ya uhai na mauti, na majaribio ya Masihi Dajjal (Mpinga Kristo). Kisha achague dua anayotaka, hasa zile zilizosimuliwa kutoka kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake:
Allahumma a'innii 'alaa dhikrika washukrika wahusni 'ibaadatika (Ewe Mwenyezi Mungu, nisaidie katika kukukumbuka, kukushukuru na kukufanyia ibada vizuri). Allahumma innii dhwalamtu nafsii dhulman kathiiran wala yaghfirudhdhunuuba illaa anta. Faghfirlii maghfiratan min 'indika warhamnii innaka antal-ghafuurur-rahiim (Ewe Mwenyezi Mungu, nimejidhulumu dhuluma nyingi, na hakuna anayesamehe dhambi ila Wewe. Basi nisamehe msamaha utokao kwako na unirehemu, kwani Wewe ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu mno).
Na ama katika Tashahudi ya kwanza, (hatamswalia Mtume, badala yake) baada ya kutoa zile shahada mbili, atasimama kwa ajili ya rakaa ya tatu katika swala ya Dhuhr, Asr, Maghrib na Ishaa. Na kama atamswalia Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ndiyo bora kwa mujibu wa ujumla wa hadithi zote zinazohusiana na hilo, kisha anyanyuke kwa ajili ya rakaa ya tatu.
Somo la 10: Sunna za swala
Nazo ni:
1. Kusoma dua ya kufungua swala.
2. Kuweka kiganja cha mkono wa kulia juu ya kiganja cha kushoto juu ya kifua wakati anapokuwa amesimama, kabla ya rukuu na baada yake.
3. Kuinua mikono huku vidole vimejikusanya pamoja huku imeinuliwa hadi usawa wa mabega au kwenye masikio wakati wa kutoa takbiratul-Ihram, na wakati wa kurukuu, na wakati wa kuinuka kutoka katika rukuu, na wakati wa kunyanyuka kutoka katika Tashahudi ya kwanza kwa ajili ya rakaa ya tatu.
4. Tasbihi ya zaidi ya moja wakati wa kurukuu na kusujudu.
5. Maneno yasemwayo zaidi ya haya: Rabbanaa walakalhamd (Mola wetu Mlezi, na sifa njema zote ni zako) baada ya kunyanyuka kutoka katika kurukuu, na chochote kisemwacho katika kuomba msamaha baina ya sijda mbili.
6. Kuweka kichwa usawa wa mgongo katika kurukuu.
7. Kuweka mikono mbali na mbavu, na kuweka tumbo mbali na mapaja, na kuweka mapaja mbali na miundi katika kusujudu.
8. Kuinua dhiraa (mikono) kutoka kwenye ardhi wakati wa kusujudu.
9. Mwenye kuswali kuukalia mguu wake wa kushoto huku ameulaza, na kuusimamisha wa kulia (juu ya vidole vyake vikielekea Kibla) katika Tashahudi ya kwanza na baina ya sijda mbili.
10. Kukalia tako la kushoto na kulaza na kuuingiza mguu wa kushoto chini ya mguu wa kulia na kuusimamisha wa kulia katika Tashahudi ya mwisho katika swala za rakaa nne na za rakaa tatu.
11. Kuashiria kwa kidole cha shahada katika tashahudi ya kwanza na ya pili kutoka anapoketi hadi mwisho wa Tashahudi na kukitikisa wakati wa kuomba dua.
12. Kumuombea rehema na baraka Muhammad, jamaa za Muhammad, Ibrahim na jamaa za Ibrahim katika Tashahudi ya kwanza.
13. Kuomba dua katika Tashahudi ya mwisho.
14. Kusoma kwa sauti kubwa katika swala ya Fajr, swala ya Ijumaa, swala mbili za Idi, na swala ya kuomba mvua inyeshe, na katika rakaa mbili za kwanza za swala ya Maghrib na Isha.
15. Kusoma kwa sauti ya chini katika swala ya Dhuhr, Asr, na katika rakaa ya tatu ya swala ya Maghrib, na katika rakaa mbili za mwisho katika swala ya Ishaa.
16. Kusoma sura zaidi ya Al-Fatiha kutoka katika Qur-ani, pamoja na kuzingatia Sunnah zinginezo zote zilizokuja kuhusiana na Swala kando na hizi tulizotaja, ikiwa ni pamoja na: Anachosema anayeswali zaidi ya kusema: Rabbanaa walakalhamd (Mola wetu Mlezi, na sifa njema zote ni zako), na baada ya kuinuka kutoka katika rukuu kwa imamu, maamuma na mtu anayeswali peke yake. Hayo yote ni Sunnah. Pia inajumuisha kuweka mikono juu ya magoti huku vidole vimefunguka wakati wa kurukuu.
Somo la 11: Mambo yanayobatilisha swala
Nayo ni manane:
1. Kuzungumza makusudi pamoja na kukumbuka na kuwa na elimu ya uharamu wa hilo. Ama aliye zungumza kwa kusahau na yule ambaye hajui hilo, basi hilo haliwabatilishii swala yao.
2. Kucheka.
3. Kula.
4. Kunywa.
5. Kufunuka uchi.
6. Kupinda sana kiasi cha kutoka kwenye mwelekeo wa Kibla.
7. Kufanya mchezo sana kwa kuendelea katika swala.
8. Kuharibika kwa udhu.
Somo la 12: Masharti ya udhu
Ni kumi:
Uislamu, akili timamu, utambuzi, nia, kuendeleza hukumu yake kwa kutoazimia kuikata mpaka amalize kujisafisha, kukatika kwa kinachosababisha udhu, kustanji au kutumia mawe kabla ya kutawadha, usafi wa maji na uhalali wake, kuondoa kinachozuia maji kufika kwenye ngozi na kuingia kwa wakati wa swala kwa yule ambaye daima anaharibikiwa udhu.
Somo la 13: Faradhi za udhu
Ni sita:
Kuosha Uso na miongoni mwa hayo ni kusukutuwa na kuingiza maji puani, na kuosha mikono miwili mpaka kwenye kongo mbili, na kupaka kichwa chote maji na miongoni mwa kichwa ni masikio, na kuosha miguu miwili mpaka kwenye fundo mbili, na kupangilia, na kufuatanisha sawasawa. Inapendekezwa kurudia kuosha uso, mikono na miguu mara tatu, na vile vile kusuuza mdomo na pua. Lakini la wajibu katika hayo ni kufanya hivyo mara moja tu. Ama kupangusa kichwa, hai pendekezwi kurudia, kama ilivyoashiriwa na Hadithi sahihi mbalimbali.
Somo la 14: Mambo yanayoharibu udhu
Ni sita:
Kutokwa na chochote kwenye tupu mbili, chochote kilicho najisi (kichafu) kinachotoka kwa wingi kutoka kwenye mwili, kupoteza akili kwa kulala au vinginevyo, kugusa tupu ya mbele au ya nyuma kwa mkono bila ya kizuizi, kula nyama ya ngamia, kutoka katika Uislamu, Mwenyezi Mungu atukinge mbali na hilo sisi na Waislamu wote.
Tanbihi muhimu kuhusu kumuosha maiti. Kauli sahihi ni kwamba hilo halimharibii anayemuosha maiti udhu wake, nayo ni kauli ya wengi wa wanazuoni; kwa sababu hilo halina ushahidi, lakini ikiwa mkono wa mwenye kuosha utagusa tupu ya maiti bila ya kizuizi, hapo atalazimika kutawadha.
Na la wajibu kwake ni kutogusa tupu ya maiti isipokuwa kwa nyuma ya kizuizi, na vivyo hivyo kumgusa mwanamke hakuharibu udhu kabisa, sawa iwe ni kwa matamanio au bila ya matamanio kulingana na kauli sahihi zaidi ya wanazuoni mradi hakutokwa na chochote kwenye tupu yake, kwa sababu Nabii - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - alikuwa akiwabusu baadhi ya wake zake na kisha anaswali bila ya kurudia kutawadha.
Ama kuhusu maneno ya Mwenyezi Mungu katika aya ya surat An-Nisaa na surat Al-Maida:
﴿...أَوۡ لَٰمَسۡتُمُ ٱلنِّسَآءَ...﴾
"au mkawagusa wanawake..." [An-Nisaa: 43] [Al-Maida: 6], kinachokusudiwa hapa ni kujamiiana, kulingana na kauli sahihi zaidi katika zile kauli mbili za wanazuoni, nayo ndiyo kauli ya Ibn Abbas, radhi Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote wawili, na kundi katika watangulizi wetu wema na wale waliokuja baadaye. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kufanikisha.
Somo la 15: Kila Muislamu kujipamba na maadili mema
Hayo ni pamoja na: ukweli, uaminifu, kuwa mbali na machafu, staha, ujasiri, ukarimu, kutimiza agano, kujiepusha na kila alichoharamisha Mwenyezi Mungu, ujirani mwema, kuwasaidia wenye mahitaji kulingana na uwezo, na maadili mengineyo ambayo Qur-ani au Sunnah vimeashiria kwamba ni katika sheria.
Somo la 16: Kuwa na adabu za Kiislamu
Hizo ni pamoja na: salamu, bashasha, kula na kunywa kwa mkono wa kulia, kutaja jina la Mwenyezi Mungu unapoanza kula au kunywa, kumsifu Mwenyezi Mungu baada ya kumaliza kula au kunywa, kumshukuru Mwenyezi Mungu baada ya kupiga chafya, kumuombea dua aliyepiga chafya ikiwa amemshukuru Mwenyezi Mungu, kuwa tembelea wagonjwa, kufuata jeneza ili kumswalia maiti na kumzika, maadili ya kisheria ya wakati wa kuingia na kutoka msikitini au nyumbani, na wakati wa kusafiri, na ukiwa pamoja na wazazi, jamaa na majirani, watu wazima na watoto, kumpongeza aliyejaaliwa mtoto, kumuombea baraka aliyeoa, kumliwaza aliye katika msiba, na maadili mengineyo ya Kiislamu kuhusiana na kuvaa na kuvua nguo na ndara.
Somo la 17: Kutahadharisha dhidi ya ushirikina na aina mbalimbali za maasi
Miongoni mwake ni mambo saba yaangamizayo, ambayo ni: kumshirikisha Mwenyezi Mungu, uchawi, kuua nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharamisha isipokuwa kwa haki, kula riba, kula mali ya yatima, kukimbia kutoka katika uwanja wa vita (dhidi ya maadui wa Waislamu) na kuwasingizia wanawake wema walio safi, Waumini.
Na miongoni mwake ni kutotii wazazi, kuwakata jamaa, kutoa ushahidi wa uongo, viapo vya uongo, kumdhuru jirani, kuwadhulumu watu kuhusiana na damu, mali na heshima zao, na kunywa pombe, kucheza kamari, kusengenya, uvumi, na mambo mengineyo ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu au Mtume wake - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - walikataza.
Somo la 18: Kumuandaa maiti, kumswalia na kumzika
Haya hapa maelezo yake ya kina:
Kwanza: Ni katika sheria kumtamkisha mtu anayekaribia kufa shahada ya: "Hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu." kwa mujibu wa maneno ya Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Mtamkisheni maiti wenu: Laa ilaaha illallah."7 Imepokelewa na Muslim katika Sahihi yake. Na aliyekusudiwa katika hadithi hii ni mtu ambaye ameonyesha ishara za kifo.
Pili: Inapohakikishwa kwamba tayari ameshakufa, yatafungwa macho yake na ifungwe sawasawa midomo yake; kwa sababu hayo yamekuja katika Sunnah.
Tatu: Ni lazima kumuosha maiti Muislamu isipokuwa ikiwa ni shahidi aliyefia vitani. Huyo haogeshwi wala hasaliwi, bali anazikwa katika nguo zake; kwani Nabii rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie hakuwaosha watu waliouawa katika vita vya Uhud na wala hakuwaswalia.
Nne: Namna ya kumuosha maiti
Ataanza kwa kumfunika uchi wake, kisha amuinue kidogo na amkamue tumbo lake kwa upole. Kisha muoshaji afunge kitambaa au kitu kama hicho kwenye mkono wake ili amsugue kwacho. Kisha amtawadhishe kama udhu wa swala. Kisha akioshe kichwa chake na ndevu zake kwa maji na mkunazi au mfano wake. Kisha aoshe upande wake wa kulia, kisha wa kushoto, kisha arudie kumuosha hivyo mara ya pili na ya tatu. Kila mara amkamue tumbo kwa mkono wake, na ikiwa kitu kitatoka ndani yake, basi na akioshe na afunge mahali hapo kwa pamba au mfano wake. Na ikiwa pamba haitashikilia, basi atumie udongo safi, au atumie njia za kisasa za kitabibu, kama vile plasta na mfano wake.
Atarudia kumtawadhisha, na ikiwa hatasafika kwa mara tatu, ataongeza hadi tano au saba. Kisha atamkausha kwa nguo, na atampaka manukato kwenye sehemu zake za siri na sehemu za kusujudia. Na kama atampaka manukato mwili wote, basi ndiyo vizuri. Pia atazifukiza sanda zake kwa moshi wa manukato. Ikiwa masharubu yake au kucha zake ni ndefu, atazipunguza. Na akiacha hilo, basi hakuna ubaya. Asinyooshe nywele zake, wala asinyoe nywele zake za siri wala asimtahiri. Kwa sababu hakuna ushahidi wowote wa hiyo. Mwanamke atasukwa nywele zake katika misuko ya pembe tatu na ziachiliwe zining'inie kwa nyuma yake.
Tano: Kumvisha sanda maiti
Ni bora kwa mwanamume kuvishwa sanda tatu nyeupe ambazo hazina shati wala kitambaa cha kichwani, kama alivyofanyiwa Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na ataingizwa ndani yake moja kwa moja. Na ikiwa atavishwa sanda ya shati, kikoi na shuka ya juu ya mwili, basi hakuna ubaya.
Mwanamke atafunikwa kwa sanda tano: nguo ya sehemu ya juu ya mwili, kitambaa cha kichwani, kikoi na shuka mbili za juu ya mwili. Mvulana atavishwa sanda moja hadi tatu, naye msichana mdogo atavishwa sanda ya shati na shuka mbili za juu ya mwili.
Kinacholazimu kwa kila mmoja wao ni nguo moja inayositiri mwili mzima wa maiti. Hata hivyo, ikiwa maiti yuko katika hali ya ihram, ataoshwa kwa maji na mkunazi, na atafunikwa kwa kikoi chake na shuka yake au kwa nguo nyinginezo, lakini hakifunikwi kichwa chake wala uso wake, wala hapakwi manukato. Kwa sababu atafufuliwa Siku ya Kiyama akitoa Talbiya (katika hali ya ihram), kama ilivyothibiti katika Hadithi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Na ikiwa mwenye kuhiji huyo ni mwanamke, atavikwa sanda kama wanawake wengine, lakini hatapakwa manukato, wala hatafunikwa uso wake kwa nikabu, wala mikono yake kwa glavu. Bali uso wake na mikono yake vita funikwa kwa sanda ambayo alifunikwa kwayo namna ilivyotangulia hapo awali kuhusiana na maelezo ya kumvalisha sanda mwanamke.
Sita: Watu wanaostahili zaidi kumuosha, kumswalia na kumzika
Yule aliyechaguliwa na maiti katika wasia wake kwa ajili ya hilo, kisha baba, kisha babu, kisha aliye wa karibu kwake zaidi miongoni mwa jamaa zake wa kiume wa upande wa baba.
Naye anayestahiki zaidi kumuosha mwanamke ni yule aliyechaguliwa na maiti katika wasia wake, kisha mama, kisha bibi, kisha mwanamke wa karibu zaidi katika jamaa zake. Na wanandoa kila mmoja wao anaweza kumuosha mwenzake; kwa sababu Abu Bakr Asswiddiiq - Mwenyezi Mungu amridhie - alimuosha mkewe, na kwa sababu Ali - Mwenyezi Mungu amridhie - alimuosha mkewe, Fatima, Mwenyezi Mungu amridhie.
Saba: Namna ya kumswalia maiti
Atafanya takbira mara nne, na atasoma baada ya ile ya kwanza: Al-Fatiha. Na akisoma pamoja nayo sura fupi au aya moja au mbili, basi ni vizuri. Kwani kuna Hadithi sahihi iliyokuja kuhusiana na hilo, kutoka kwa Ibn Abbas, Mwenyezi Mungu awe radhi nao. Kisha atafanya takbira ya pili na amswalie Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kama anavyomswalia katika tahiyatu (ya swala), kisha atafanya takbira ya tatu, na aseme: Allahumma ghfir lihayyinaa wamayyitinaa,washaahidinaa waghaaibinaa, waswaghiirinaa wakabiirinaa, wadhakarinaa waunthaanaa. Allahumma man ahyaytahuu minnaa fa ahyihi alal Islaam, waman tawaffaytahu minnaa fatawaffahu alal iiman. Allahumma ghfir lahu, warhamhu, wa'aafihi, wa'fu 'anhu, wa akrimu nuzulahu, wawasiu' mudkhalahu, waghsilhu bimaai wath-thalj wal barad. Wanaqqihi minal khatwaaya kamaa yunaqqath-thaub al-abyadh minad-danas. Wa abdilhu daaran khayran min daarihi, wa ahlan khayran min ahlihi, wa adkhilhul janna, wa a'idh-hu min 'adhaabil qabri, wa 'adhaabin-naar, wafsah lahu fii qabrihi, wanawwir lahu fiihi. Allahumma laa tahrimnaa ajrahu walaa tudhwilunaa ba'adahu (Ewe Mwenyezi Mungu, msamehe aliye hai katika sisi na aliyekufa, na aliyepo na asiyekuwepo, na mdogo wetu na mkubwa wetu, na mwanamume kati yetu na mwanamke. Ewe Mwenyezi Mungu, unayemueka hai kati yetu, basi muweke hai katika Uislamu, na uliyemfisha miogoni mwetu, basi mfishe katika Iman. Ewe Mwenyezi Mungu, msamehe na umrehemu, na umpe salama na umwachie, na mtukuze katika kushuka kwake na upanue mahali pake pa kuingia, na muoshe kwa maji na theluji na barafu, na mtakase kutokana na makosa kama inavyotakaswa nguo nyeupe kutokana na uchafu, na mbadilishie nyumba bora kuliko nyumba yake, na jamaa bora kuliko jamaa zake, na mke bora kuliko mke wake, na muingize Peponi, na mkinge mbali na adhabu ya kaburini, na adhabu ya Motoni, na mpanulie kaburi lake, na umuwekee nuru ndani yake. Ewe Mwenyezi Mungu, usitunyime thawabu zake wala usitupoteze baada yake). Kisha atatoa takbira ya nne, na atoe salamu moja tu upande wake wa kulia.
Na inapendekezwa anyanyue mikono yake pamoja na kila takbira. Na ikiwa maiti ni mwanamke, inasemwa: (Allahummaghfir lahaa (Ewe Mwenyezi Mungu, msamehe huyu wa kike...) hadi mwisho wake. Na ikiwa jeneza ni mbili, atasema: (Allahummaghfir lahumaa (Ewe Mwenyezi Mungu, wasamehe wawili hawa...) hadi mwisho wake. Na ikiwa jeneza ni zaidi ya mbili, atasema: (Allahu mmaghfir lahum (Ewe Mwenyezi Mungu, wasamehe hawa...) hadi mwisho wake. Na kama ni mtoto aliyekufa, basi atasema badala ya kumuombea msamaha: Allahumma ja'alhu faratwan wadhukhran liwaalideyhi, washafii'an mujaaba. Allahumma thaqqil bihi mawaazinahumaa, wa a'dhwim bihi ujuurahumaa, wa alhiqhu biswaalihi salafil muuminiin, waj'alhu fii kafaalati Ibraahim 'alayhis swalaatu wassalam, waqihi birahmatika 'adhabal jahiim (Ewe Mwenyezi Mungu, mjaalie kuwa ni mtangulizi na akiba kwa wazazi wake, na mwombezi mwenye kuku baliwa uombezi wake. Ewe Mwenyezi Mungu, kwa ajili yake zifanye nzito mizani za wazazi wake na yafanye malipo yao kuwa mengi, na mkutanishe na watangulizi wema katika Waumini, na mjaalie awe katika dhamana ya Ibrahim, amani iwe juu yake, na umuepushe kwa rehema yako kutokana na adhabu ya Moto).
Sunnah ni kwa imamu kusimama sambamba na kichwa cha mwanamume, na kwenye kiuno cha mwanamke. Na mwanamume awe karibu na imamu iwapo jeneza zitachanganyika (wanaume, wanawake, watoto wa kiume na wa kike), naye mwanamke awe karibu na Kibla. Na ikiwa kuna watoto miongoni mwao, basi mvulana atakuwa mbele ya mwanamke, kisha mwanamke huyo, kisha msichana mdogo. Na kichwa cha mvulana kiwe sambamba na kichwa cha mwanamume, na kiuno cha mwanamke kiwe sambamba na kichwa cha mwanamume. Vile vile, kichwa cha msichana kiwe sambamba na kichwa cha mwanamke, na kiuno chake kiwe sawa na kichwa cha mwanamume. Na wanaoswali wote wawe nyuma ya imamu, isipokuwa ikiwa mtu hakupata nafasi nyuma ya imamu, basi atasimama kuliani kwake.
Nane: Namna ya kumzika maiti
Sheria ni kwamba kaburi lichimbwe ndani sana kiasi cha kufikia kiunoni mwa mtu, na liwe na mwanandani kwenye upande wa ukuta wa Kibla. Kisha maiti atawekwa kwenye mwanandani huo kwa upande wake wa kulia, na yanaweza kufunguliwa mafundo ya mikanda ya sanda, lakini hayaondolewi, bali yaachwe tu. Uso wake usidhihirishwe sawa maiti awe ni mwanamume au mwanamke. Kisha atafungiwa humo kwa matofali na matope ili awe imara na kumzuilia kutokana na udongo. Ikiwa matofali hayawezi kupatikana, basi wanaweza kutumia kinginecho kama vile mbao au mawe ili yamkinge kutokana na udongo. Inapendekezwa kusema hivi wakati huo: "Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na kwa mwenendo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu." Kisha kaburi litanyanyuliwa kiasi cha shibri moja (kipimo cha urefu sawa na umbali kati ya dole gumba na kidole cha kati wakati mkono umetanuka). Kisha kaburi litawekewa kokoto ndogo juu yake ikiwa hilo litawezekana, na linyunyiziwe maji.
Na inaruhusiwa kisheria kwa waombolezaji kusimama kwenye kaburi na kumuombea maiti, kwa sababu Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alikuwa anapomaliza kumzika maiti, anasimama karibu yake na anasema: "Muombeeni msamaha ndugu yenu, na muombeeni uthabiti; kwani sasa anaulizwa."8
Tisa: Inaruhusiwa kisheria kwa wale ambao hawakumswalia wamswalie hata baada ya kuzikwa
Kwa sababu Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alifanya hivyo, kwa sharti kwamba hilo liwe ndani ya muda wa mwezi mmoja au chini ya hapo. Lakini ikiwa muda utakuwa zaidi ya hivyo, basi haitaruhusiwa kumswalia akiwa kaburini; kwa sababu haikupokewa kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba aliswalia kaburi baada ya mwezi mmoja baada ya maiti kuzikwa.
Kumi: Hairuhusiwi kwa familia ya maiti kuwapikia watu chakula
Kwa mujibu wa kauli ya Jarir bin Abdullah Al-Bajalii, swahaba mtukufu, Mwenyezi Mungu amridhie, kwamba alisema: "Tulikuwa tukizingatia kukusanyika pamoja na familia ya maiti na kupika chakula baada ya mazishi kwamba ni katika kuomboleza ambako kuliharamishwa."9 Imepokelewa na Imam Ahmad kwa msururu mzuri wa wasimulizi. Ama kuwapikia wao chakula, au wageni wao, basi hakuna ubaya katika hilo. Na inaruhusiwa kisheria kwa jamaa zao na majirani zao kuwaandalia chakula. Kwa sababu habari za kifo cha Ja’far bin Abi Twalib, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, zilipomjia Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kutoka huko Shamu, aliamuru jamaa zake kuandaa chakula kwa ajili ya familia ya Ja'far, na akasema: "Hakika wamefikwa na ya kuwa shughulisha."10
Hakuna ubaya kwa familia ya maiti kuwaalika majirani zao au watu wengine kula chakula walichopewa kama zawadi, na hilo halina wakati maalumu, kama tunavyojua kutoka katika Sheria.
Kumi na moja: Hairuhusiwi kwa mwanamke kuomboleza kwa kuacha mapambo zaidi ya siku tatu kwa sababu ya maiti yeyote, isipokuwa mume wake
Kwa hivyo, kama ni mumewe, itamlazimu aache mapambo kwa muda wa miezi minne na siku kumi, isipokuwa ikiwa ni mjamzito, basi atamaliza hilo kwa kuzaa. Hii ni kwa sababu zimethibiti Sunnah sahihi kutoka kwa Mtume – rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake – kuhusiana na haya.
Ama mwanamume, yeye haruhusiwi kuacha mapambo kwa ajili ya mtu yeyote katika jamaa zake au wengineo.
Kumi na mbili: Inaruhusiwa kisheria kwa wanaume kuzuru makaburi mara kwa mara ili kuwaombea, kuwatakia rehema na kukumbuka kifo na mambo ya baada yake
Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Tembeleeni makaburi, kwani yanakukumbusheni Akhera."11 Ime pokelewa hadithi hii na imamu Muslim katika Sahihi yake. Yeye, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alikuwa akiwafundisha maswahaba wake wanapotembelea makaburi, kwamba waseme: “Assalaamu 'alaikum ahlad-diyaari minal-mu`miniina wal-muslimiin, wa innaa in shaa`allaahu bikum laahiquun, nas`alullaaha lanaa wa lakumul-'aafiya, yarhamullaahul-mutaqaddimiina minnaa wal-musta-akhiriin (Amani iwe juu yenu, enyi wakazi wa makaburini miongoni mwa Waumini na Waislamu. Nasi hakika tutawafuata, Mwenyezi Mungu akipenda. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe salama sisi na nyinyi. Mwenyezi Mungu awarehemu waliotangulia miongoni mwetu na watakaokuja baada yetu).”12 Ama wanawake, hao hawaruhusiwi kuzuru makaburi. Kwa sababu Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie - alilaani wanawake wanaozuru makaburi. Na pia kwa sababu kuna hofu kwamba kuzuru kwao kutawaletea majaribu na kukosa subira. Vile vile, hawaruhusiwi kufuata jeneza kwenda makaburini. Kwa sababu Mtume – rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake – aliwakataza kufanya hivyo. Ama kuwaswalia maiti msikitini, au katika ukumbi wa swala, hilo linaruhusika kwa wanaume na wanawake
Huu ndio mwisho wa yale tuliyoweza kuyakusanya. Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad, familia yake na Maswahaba wake.
***
***
Imepokelewa na Imamu Ahmad 5/428, At-Twabarani katika Al-Kabiir 4/338, na Al-Bayhaqi katika Al-Shua’b 14/355. Alisema katika Majma’ Az-Zawa’id 1/121: Imepokelewa na Ahmad, na wasimulizi wake ni wasimulizi wa Vitabu vya hadithi sahihi.
Imepokelewa na Imaamu Ahmad 1/47.
Imepokelewa na Abu Daudi, nambari 3251 na At-Tirmidhiy, nambari 1535.
Imepokelewa na Abu Daudi, nambari 4980, na Ahmad 5/384.
Imepokelewa na Ibn Majah, nambari 4204 na Imamu Ahmad 3/30.
Imepokelewa na Muslim kwa nambari 916-917.
Imepokelewa na Abu Daudi, nambari 3221, na Al-Hakim 3/399.
Imepokelewa na Ibn Majah, nambari 1612, na Imam Ahmad 2/204.
Imaam Muslim katika Mazishi ya 976, An-Nasa’i katika Mazishi 2034, Abu Daudi katika Mazishi 3234, Ibn Majah katika Yaliyokuja kuhusu Mazishi 1569, Ahmad 2/441.
Imepokelewa na Ibn Majah, kwa nambari 1569, na Al-Albani alisema kwamba ni hadithi sahihi.
Imepokelewa na Muslim, nambari 977.
Mkusanyiko wa Fatwa (majibu) na Maneno Mengine Mbalimbali, Sehemu ya 3, ukurasa wa 288-298.