PHPWord

 

 

 

حُكْمُ السِّحْرِ وَالكِهَانَةِ

وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهَا

 

HUKUMU YA UCHAWI, UGANGA NA MAMBO YANAYOHUSIANA NA HAYO

 

لِسَمَاحَةِ الشَّيْخِ العَلَّامَةِ

عَبْدِ العَزِيزِ بْنِ عَبْدِ اللهِ بْنِ بَازٍ

رَحِمَهُ اللهُ

 

Mtunzi Mheshimiwa, Sheikh,

Abdulaziz bin Abdillah bin Baaz

 

 

 


بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Makala ya tisa: Hukumu ya uchawi na ukuhani na yanayohusiana na mawili hayo1

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu peke yake, na rehema na amani ziwe juu ya yule ambaye hakuna Nabii baada yake. Ama baada ya hayo:

Kwa kuzingatia ongezeko la hivi karibuni la wachawi miongoni mwa wale wanaodai kuwa madaktari wanaotibu kwa njia ya uchawi au ukuhani, na kuenea kwao katika baadhi ya nchi, na kuwatumia kwao vibaya walio wajinga miongoni mwa watu ambao wengi wao mara nyingi hawana elimu, niliona, kama aina ya nasaha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na waja wake, kwamba nieleze hatari kubwa iliyo ndani ya hayo juu ya Uislamu na Waislamu, kwa sababu ya yale yaliyo ndani yake ya kujifungamanisha na asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kuhalifu amri yake na amri ya Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.

Kwa hivyo ninasema, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, kwamba inaruhusiwa kutafuta matibabu kulingana na makubaliano ya watu wote, na Muislamu anaweza kwenda kwa daktari wa magonjwa ya ndani, upasuaji, mishipa au mengineyo; ili ampime ugonjwa wake na kumtibu kwa dawa zinazofaa zinazoruhusiwa kwa mujibu wa sheria za Kiislamu, kulingana na anachojua katika elimu ya tiba. Kwa sababu hili linaingia katika mlango wa kuchukua visababu vya kawaida na wala halipingani na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu aliyetakasika, aliyetukuka aliteremsha ugonjwa na akateremsha dawa yake pamoja nao. Wanaijua wanaoijua (dawa hiyo) na hawaijui wasioijua. Hata hivyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu hakufanya ponya ya waja wake katika yale aliyo waharamishia.

Hivyo basi, mgonjwa haruhusiwi kwenda kwa wapiga ramli wanaodai kuwa wanajua mambo yaliyofichika ili kujua ugonjwa wake kutoka kwao, kama vile haruhusiwi kusadiki wanayomwambia, kwa sababu wanasema kwa kukisia tu mambo ya ghaibu, au wanawaleta majini ili wapate wanachotaka kwa msaada wao. Hawa hukumu yao ni kwamba wamekufuru na wamepotea ikiwa wanadai kuwa wanajua ghaibu.

Muslim amepokea katika Sahihi yake kwamba Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: "Atakayekwenda kwa mtabiri na akamuuliza jambo, swala zake hazitakubaliwa kwa siku arobaini."

 

 

"Atakayekwenda kwa kuhani (mchawi, mtabiri) na akasadiki anayoyasema, basi hakika ameshakufuru yale yaliyoteremshwa kwa Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake." Atakaye muendea kuhani na akamsadikisha kwa yale anayoyasema, basi hakika amekufuru yale yaliyoteremshwa kwa Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Imepokelewa na Abuu Daudi na pia wanazuoni wa vile Vitabu vinne vya Sunna, naye Al-Hakim akasema ni kwamba ni hadithi sahihi, kutoka kwa Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwa matamshi yafuatayo: “Atakayemuendea mpiga ramli au kuhani na akamsadikisha kwa yale anayoyasema, basi hakika ameshakufuru yale yaliyo teremshwa kwa Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.”

Na imesimuliwa kutoka kwa Imran bin Huswain, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, kwamba alisema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Si miongoni mwetu aathirikaye na vitu (kama vile ndege), au anaye fanyiwa hilo la kuathirika, au kuhani (mpiga ramli) au mwenye kupigiwa ramli, au mchawi, au mwenye kufanyiwa uchawi. Na atakayekwenda kwa kuhani na akasadiki anayosema, basi hakika ameshakufuru yale yaliyoteremshwa kwa Muhammad rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Imepokelewa na Al-Bazzaar kwa msururu mzuri wa wasimulizi.

Kwa hivyo, katika Hadithi hizi tukufu, kuna katazo la kwenda kwa wapiga ramli, makuhani, wachawi na mfano wao, na kuwauliza na kuwasadiki, na pia zina ahadi ya adhabu juu ya kufanya hivyo.

Kwa hivyo, hairuhusiwi kudanganyika na ukweli wao katika baadhi ya mambo, wala kwa wingi wa watu wanaowajia, kwani wao hawajui kitu na hairuhusiwi kwa watu kudanganyika nao. Kwa sababu Mtume -rehema na amani zimshukie- alikataza kuwaendea, kuwauliza na kuwasadikisha; kwa sababu katika hilo, kuna uovu mkubwa, hatari kubwa na matokeo mabaya zaidi, na kwa sababu wao ni waongo, waovu.

Hadithi hizi pia zina ushahidi wa kukufuru kwa kuhani (mtabiri) na mchawi, kwa sababu wanadai kuwa wanayajua mambo ya ghaibu, na hilo ni kufuru, na kwa sababu hawawezi kufikia lengo lao isipokuwa kwa kuwatumikia majini na kuwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, jambo ambalo ni kumkufuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumshirikisha. Na mwenye kuwasadiki katika yale wanayodai kwamba wanajua mambo ya ghaibu anakuwa kama wao. Na kila anayepokea mambo haya kutoka kwa mtu anaye yafanya, basi Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - yuko mbali sana naye.

Vile vile, Muislamu haruhusiwi kusalimu amri kwa wanachodai kuwa ni tiba, kama vile kuongea maneno yasiyoeleweka na kumimina risasi, na mengineyo miongoni mwa ushirikina wanaoufanya. Hayo yote ni katika ukuhani na kuwachanganya watu. Na mwenye kuyakubali hayo, basi hakika atakuwa amewasaidia katika batili yao na ukafiri wao.

Vile vile, hairuhusiwi kwa Muislamu yeyote kuwaendea ili kuwauliza kuhusu yule ambaye mtoto wake au jamaa yake atamuoa, au kuhusu mapenzi, uaminifu, uadui na utengano utakaokuwa baina ya wanandoa na familia yao, na mfano wa hayo. Kwa sababu hayo yote ni katika ghaibu ambayo haijui isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu tu.

Hivyo basi, la wajibu kwa watawala, watu wanao amrisha mema na kukataza maovu (Ahlul-Hisbah), na wengineo wenye uwezo na mamlaka, ni kukataza kwenda kwa wapiga ramli, watabiri na wengineo, na kumzuia yeyote anayejishughulisha na lolote katika hayo sokoni na kwingineko, na kuwakataza vikali zaidi, na kumkataza yeyote anayewaendea.

Vile vile uchawi. Kwani huo ni katika makatazo ya kikafiri, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mtukufu kuhusu wale Malaika wawili:

 

 

﴿...وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنۡ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَآ إِنَّمَا نَحۡنُ فِتۡنَةٞ فَلَا تَكۡفُرۡۖ فَيَتَعَلَّمُونَ مِنۡهُمَا مَا يُفَرِّقُونَ بِهِۦ بَيۡنَ ٱلۡمَرۡءِ وَزَوۡجِهِۦۚ وَمَا هُم بِضَآرِّينَ بِهِۦ مِنۡ أَحَدٍ إِلَّا بِإِذۡنِ ٱللَّهِۚ وَيَتَعَلَّمُونَ مَا يَضُرُّهُمۡ وَلَا يَنفَعُهُمۡۚ وَلَقَدۡ عَلِمُواْ لَمَنِ ٱشۡتَرَىٰهُ مَا لَهُۥ فِي ٱلۡأٓخِرَةِ مِنۡ خَلَٰقٖۚ وَلَبِئۡسَ مَا شَرَوۡاْ بِهِۦٓ أَنفُسَهُمۡۚ لَوۡ كَانُواْ يَعۡلَمُونَ﴾

"Wala hao hawakumfundisha yeyote mpaka wamwambie: "Hakika sisi ni mtihani; basi usikufuru." Wakajifunza kwa hao wawili yale ya kumtenganisha mtu na mkewe. Wala hawawezi kumdhuru mtu ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na wanajifunza yatakayo wadhuru wala hayawanufaishi. Na hakika wanajua kwamba aliyekhiari haya, hatakuwa na fungu lolote katika Akhera. Na hakika ni kiovu mno walichojiuzia nafsi zao laiti wangelijua." [Al-Baqara: 102].

Aya hizi tukufu zinaashiria kuwa uchawi ni ukafiri na kwamba wachawi wanamtenganisha mtu na mkewe. Pia zinaonyesha kwamba uchawi haufanyi kazi wenyewe tu, iwe ni kunufaisha au kudhuru. Bbali unafanya kazi kwa idhini ya Mwenyezi Mungu ya kiulimwengu na ya kimipango yake. Kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba heri na shari.

Aya hii tukufu pia inaashiria kwamba wale wanaoamiliana na uchawi wanaamiliana na yanayowadhuru na hayawanufaishi, na kwamba hawana fungu lolote kwa Mwenyezi Mungu. Na hii ni ahadi kubwa inayoashiria hasara yao kubwa hapa duniani na Akhera, na kwamba walijiuza wenyewe kwa thamani ya chini kabisa, na ndiyo maana Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka akawakashifu juu ya hilo kwa kauli yake:

﴿...وَلَبِئۡسَ مَا شَرَوۡاْ بِهِۦٓ أَنفُسَهُمۡۚ لَوۡ كَانُواْ يَعۡلَمُونَ﴾

"Na hakika ni kiovu mno walichojiuzia nafsi zao laiti wangelijua." [Al Baqara: 102] Neno 'shiraa' hapa linamaanisha kuuza.

Na hakika, madhara yamekuwa makubwa na hali imezidi kuwa mbaya kwa sababu ya hawa wazushi waliorithi elimu hizi kutoka kwa washirikina, na wakazitumia kuwachanganya wenye akili dhaifu. Basi sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake Yeye tutarejea. Na Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ndiye Mtegemewa bora zaidi.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuepushe na atupe salama kutokana na shari za wachawi, makuhani na walaghai wengineo wote. Pia tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awalinde Waislamu kutokana na uovu wao, na awawezeshe watawala wa Kiislamu kujihadhari nao na kutekeleza hukumu ya Mwenyezi Mungu juu yao; ili waja wapate nafuu kutokana na madhara yao na matendo yao machafu. Hakika, Yeye ndiye Mpaji, Mkarimu.

Na hakika, Mwenyezi Mungu Mtukufu amewawekea waja wake katika sheria, yale wanayoweza kujikinga kwayo shari ya uchawi kabla haujatokea, na akawaelezea cha kujitibu kwacho baada ya kutokea kwake, kama rehema yake na wema wake kwao na kuwakamilishia neema zake juu yao.

Yafuatayo ni maelezo ya mambo ambayo mtu anaweza kujikinga kwayo hatari ya uchawi kabla haujatokea na mambo anayoweza kujitibu kwayo baada ya kutokea kwake, miongoni mwa mambo yanayoruhusiwa kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu. Na maelezo yake ni kama ifuatavyo:

Kwanza: Yale yanayotumika katika kujilinda dhidi ya hatari ya uchawi kabla ya kutokea kwake. La muhimu na lenye manufaa zaidi katika hayo ni: Kujilinda kwa nyiradi za kisheria, dua mbalimbali, na mambo mbalimbali ya kujikinga kwayo, yaliyosimuliwa kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, ikiwa ni pamoja na kusoma Ayatul-Kursii - ambayo ndiyo aya kubwa zaidi katika Qur’ani Tukufu - baada ya kila swala iliyofaradhishwa baada ya salamu. Nayo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿ٱللَّهُ لَآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ٱلۡحَيُّ ٱلۡقَيُّومُۚ لَا تَأۡخُذُهُۥ سِنَةٞ وَلَا نَوۡمٞۚ لَّهُۥ مَا فِي ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَمَا فِي ٱلۡأَرۡضِۗ مَن ذَا ٱلَّذِي يَشۡفَعُ عِندَهُۥٓ إِلَّا بِإِذۡنِهِۦۚ يَعۡلَمُ مَا بَيۡنَ أَيۡدِيهِمۡ وَمَا خَلۡفَهُمۡۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيۡءٖ مِّنۡ عِلۡمِهِۦٓ إِلَّا بِمَا شَآءَۚ وَسِعَ كُرۡسِيُّهُ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَۖ وَلَا يَـُٔودُهُۥ حِفۡظُهُمَاۚ وَهُوَ ٱلۡعَلِيُّ ٱلۡعَظِيمُ255﴾

 

"Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye aliye Hai, Msimamia mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni vyake pekee vyote vilivyomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kufanya uombezi mbele yake bila ya idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui chochote katika vilivyo katika ujuzi wake, ila kwa atakalo mwenyewe. Mahali inapokanyaga miguu yake (Kursii) pametanda mbingu na dunia; na wala haemewi na kuvilinda viwili hivyo. Na Yeye ndiye aliye juu zaidi, Mkuu." [Al-Baqara: 255]. Na pia kuisoma wakati wa kulala. Kwani ilipokelewa kwa njia sahihi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani zimshukie, kwamba alisema: "Mwenye kusoma Ayatul-Kursi usiku, ataendelea kuwa na mlinzi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na hakuna shetani atakaye mkaribia mpaka afike asubuhi."

Na miongoni mwake ni kusoma:

﴿قُلۡ هُوَ ٱللَّهُ أَحَدٌ1﴾

"Sema: 'Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee'".

﴿قُلۡ أَعُوذُ بِرَبِّ ٱلۡفَلَقِ1﴾

"Sema: 'Ninajikinga kwa Mola Mlezi wa mapambazuko.'".

﴿قُلۡ أَعُوذُ بِرَبِّ ٱلنَّاسِ1﴾

"Sema: 'Ninajikinga kwa Mola Mlezi wa wanaadamu.'" [An-Nas: 1] Baada ya kila Swala ya lazima.

Pia azisome sura hizi tatu mara tatu tatu mwanzoni mwa mchana baada ya swala ya Alfajiri, na mwanzoni mwa usiku baada ya swala ya Maghrib.

Na miongoni mwake ni kusoma zile aya mbili za mwisho za Surat Al-Baqara mwanzoni mwa usiku, ambazo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿ءَامَنَ ٱلرَّسُولُ بِمَآ أُنزِلَ إِلَيۡهِ مِن رَّبِّهِۦ وَٱلۡمُؤۡمِنُونَۚ كُلٌّ ءَامَنَ بِٱللَّهِ وَمَلَٰٓئِكَتِهِۦ وَكُتُبِهِۦ وَرُسُلِهِۦ لَا نُفَرِّقُ بَيۡنَ أَحَدٖ مِّن رُّسُلِهِۦۚ وَقَالُواْ سَمِعۡنَا وَأَطَعۡنَاۖ غُفۡرَانَكَ رَبَّنَا وَإِلَيۡكَ ٱلۡمَصِيرُ285﴾

"Mtume ameamini yale yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake Mlezi, na Waumini vile vile. Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake na Mitume wake. Hatutofautishi baina ya yeyote katika Mitume wake, na (Waumini) husema: Tumesikia na tumetii. Tunakutaka maghfira Mola wetu Mlezi! Na marejeo ni kwako." Hadi mwisho wa sura.

Haya ni kwa sababu imepokelewa kwa njia sahihi kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba alisema: "Mwenye kusoma aya mbili za mwisho za Surat Al-Baqarah nyakati za usiku, zitamtosheleza." Maana yake - na Mwenyezi Mungu ndiye anayejua zaidi - ni kwamba zitamtosheleza kutokana na kila uovu. Na miongoni mwa hizo ni kujikinga kwa wingi kwa kusema: "Najilinda kwa maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyotimia kutokana na uovu wa alivyoviumba." usiku na mchana, na anapoingia katika mahali popote kama vile nyumbani, jangwani, hewani au baharini, kulingana na kauli ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Atakayeshuka mahala popote kisha akasema: 'A'udhu bikalimaati-llaahit-taammaati min sharri maa khalaqa (Ninajilinda kwa maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyotimia, kutokana na uovu wa vile alivyoviumba)', hakitomdhuru chochote mpaka atakapoondoka mahala pake hapo."

Na miongoni mwake ni Muislamu kusema mara tatu mwanzoni mwa mchana na mwanzo wa usiku: "Kwa jina la Mwenyezi Mungu ambaye hakuna chochote kinachoweza kudhuru pamoja na jina lake, ardhini wala mbinguni, naye ni Mwenye kusikia, ajuaye zaidi."

Kwa sababu kuna mahimizo sahihi juu ya hilo kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na kwamba hilo ni sababu ya kusalimika kutokana na madhara yote.

Pili: Yale yanayotumika kujitibu kwayo uchawi baada ya kutokea kwake. Hili pia linaweza kufanywa kwa mambo kadhaa:

 

 

La kwanza: Kuzidishia kumuomba Mwenyezi Mungu dua kwa unyenyekevu, na kumuomba Yeye aliyetakasika kuondoa madhara na dhiki hiyo.

Pili: Kufanya bidii kujua eneo la uchawi huo katika ardhi, mlima au sehemu nyingineyo. Basi utakapojulikana, ukatolewa na kuharibiwa, uchawi huo utabatilika. Hili ni miongoni mwa matibabu ya uchawi yenye manufaa zaidi.

Tatu: Kufanya ruqya pamoja na kusoma dhikri na nyiradi za kisheria ambazo ni nyingi. Miongoni mwa hizo ni:

Yale yaliyothibiti katika kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Ewe Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa watu, ondosha maumivu, na ponyesha. Wewe ndiye Mponyeshaji. Hakuna ponya ila ponya yako. Ponya isiyobakisha maradhi." Atayasema mara tatu.

Na miongoni mwake ni ruqya (dua mbalimbali) ambayo Jibril alimsomea Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Nazo ni kauli yake: "Kwa jina la Mwenyezi Mungu ninakusomea ruqya, kutokana na kila jambo linalokudhuru, na kutokana na kila nafsi au jicho la hasidi. Mwenyezi Mungu akuponye. Kwa jina la Mwenyezi Mungu, ninakusomea ruqya." Atayarudia haya mara tatu.

 

Na miongoni mwake - nayo ni tiba yenye manufaa kwa mwanamume aliyezuiliwa kumuingilia mke wake - ni kuchukua majani saba ya mkunazi wa kijani kibichi, kisha ayaponde kwa jiwe au kitu mfano wake, kisha ayaweke kwenye chombo na ayamiminie maji ya kumtosha kuoga, kisha asomee ndani yake:

Ayatul-Kursii

﴿قُلۡ يَٰٓأَيُّهَا ٱلۡكَٰفِرُونَ1﴾

"Sema: 'Enyi makafiri.'" [Al-Kaafiruun: 1], na

﴿قُلۡ هُوَ ٱللَّهُ أَحَدٌ1﴾

"Sema: 'Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee.'" [Al-Ikhlaas: 1], na

﴿قُلۡ أَعُوذُ بِرَبِّ ٱلۡفَلَقِ1﴾

"Sema: 'Ninajikinga kwa Mola Mlezi wa mapambazuko.'" [Al-Falaq: 1], na

﴿قُلۡ أَعُوذُ بِرَبِّ ٱلنَّاسِ1﴾

"Sema: 'Ninajikinga kwa Mola Mlezi wa wanadamu.'" [An-Nas: 1]

Na aya za uchawi zilizo katika Surat Al-A’raf. Nazo ni kauli ya Mwenyezi Mungu aliyetakasika:

﴿وَأَوۡحَيۡنَآ إِلَىٰ مُوسَىٰٓ أَنۡ أَلۡقِ عَصَاكَۖ فَإِذَا هِيَ تَلۡقَفُ مَا يَأۡفِكُونَ117 فَوَقَعَ ٱلۡحَقُّ وَبَطَلَ مَا كَانُواْ يَعۡمَلُونَ118 فَغُلِبُواْ هُنَالِكَ وَٱنقَلَبُواْ صَٰغِرِينَ119﴾

"Nasi tukamfunulia Musa kumwambia: Tupa fimbo yako. Mara ikavimeza vyote vile walivyovibuni. 117. Kweli ikathibiti na yakabatilika waliyokuwa wakiyatenda. 118. Kwa hivyo walishindwa hapo, na wakageuka kuwa wadogo."

Kweli ikathibiti na yakabat'ilika waliyo kuwa wakiyatenda.

Kwa hivyo walishindwa hapo, na wakageuka kuwa wadogo. [Al-A'raf: 117-119]

Na aya za Surat Yunus. Nazo ni maneno ya Mwenyezi Mungu aliyetakasika:

﴿وَقَالَ فِرۡعَوۡنُ ٱئۡتُونِي بِكُلِّ سَٰحِرٍ عَلِيمٖ79 فَلَمَّا جَآءَ ٱلسَّحَرَةُ قَالَ لَهُم مُّوسَىٰٓ أَلۡقُواْ مَآ أَنتُم مُّلۡقُونَ80 فَلَمَّآ أَلۡقَوۡاْ قَالَ مُوسَىٰ مَا جِئۡتُم بِهِ ٱلسِّحۡرُۖ إِنَّ ٱللَّهَ سَيُبۡطِلُهُۥٓ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يُصۡلِحُ عَمَلَ ٱلۡمُفۡسِدِينَ81 وَيُحِقُّ ٱللَّهُ ٱلۡحَقَّ بِكَلِمَٰتِهِۦ وَلَوۡ كَرِهَ ٱلۡمُجۡرِمُونَ82﴾

"Na Firauni akasema: Nileteeni kila mchawi mjuzi! 79. Basi walipokuja wachawi, Musa aliwaambia: Tupeni mnavyovitupa! 80. Walipotupa, Musa alisema: Mliyoleta ni uchawi. Hakika Mwenyezi Mungu haitengenezi kazi ya waharibifu. 81. Na Mwenyezi Mungu huhakikisha Haki kwa maneno yake, hata wangachukia wakosefu."

Basi walipo kuja wachawi, Musa aliwaambia: Tupeni mnavyo tupa! 80

Walipo tupa, Musa alisema: Mliyo leta ni uchawi. Hakika Mwenyezi Mungu haitengenezi kazi ya waharibifu.

Na Mwenyezi Mungu huhakikisha Haki kwa maneno yake, hata wanga chukia wakosefu [Yunus: 79-82],

Na aya zilizoko katika Surat Twaha:

﴿قَالُواْ يَٰمُوسَىٰٓ إِمَّآ أَن تُلۡقِيَ وَإِمَّآ أَن نَّكُونَ أَوَّلَ مَنۡ أَلۡقَىٰ65 قَالَ بَلۡ أَلۡقُواْۖ فَإِذَا حِبَالُهُمۡ وَعِصِيُّهُمۡ يُخَيَّلُ إِلَيۡهِ مِن سِحۡرِهِمۡ أَنَّهَا تَسۡعَىٰ66 فَأَوۡجَسَ فِي نَفۡسِهِۦ خِيفَةٗ مُّوسَىٰ67 قُلۡنَا لَا تَخَفۡ إِنَّكَ أَنتَ ٱلۡأَعۡلَىٰ68 وَأَلۡقِ مَا فِي يَمِينِكَ تَلۡقَفۡ مَا صَنَعُوٓاْۖ إِنَّمَا صَنَعُواْ كَيۡدُ سَٰحِرٖۖ وَلَا يُفۡلِحُ ٱلسَّاحِرُ حَيۡثُ أَتَىٰ69﴾

"Wakasema: 'Ewe Musa! Je, utatupa wewe, au tutakuwa sisi wa kwanza kutupa?' 65. Akasema: 'Bali tupeni nyinyi!' Tahamaki, kamba zao na fimbo zao zikaonekana mbele yake, kwa uchawi wao, kuwa zinakwenda mbio. 66. Basi Musa akaingia hofu nafsi yake. 67. Tukasema: 'Usihofu! Hakika wewe ndiwe utakayeshinda. 68. Na kitupe kilicho katika mkono wako wa kulia; kitavimeza walivyoviunda. Hakika walivyounda ni hila za mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote afikapo.'"

Akasema: Bali tupeni nyinyi! Tahamaki kamba zao na fimbo zao zikaonekana mbele yake, kwa uchawi wao, kuwa zinapiga mbio.

Basi Musa akaingia khofu nafsi yake.

Tukasema: Usikhofu! Hakika wewe ndiye utakaye shinda.

Na kitupe kilicho katika mkono wako wa kulia; kitavimeza walivyo viunda. Hakika walivyo unda ni hila za mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote afikapo. [Twaha: 65-69].

Baada ya kusomea ndani ya maji kile kilichotajwa, atakunywa kwayo midomo mitatu na aoge kwa yaliyosalia, na kwa hayo ugonjwa utaondoka, Mwenyezi Mungu akipenda. Ikiwa kuna haja ya kufanya hivyo mara mbili au zaidi, basi hakuna ubaya mpaka ugonjwa huo uishe.

Dhikri hizi, kijikinga huku na njia hizi, ni miongoni mwa sababu kubwa za kujiepusha na uovu wa uchawi na maovu mengineyo, na pia ni silaha kubwa zaidi ya kuondoa uchawi baada ya kutokea kwake; kwa wale wanaozidumisha kwa ukweli na imani, na kuwa na imani na Mweyezi Mungu, kumtegemea Yeye na kufunguka kwa kifua kwa yale ambayo mambo haya yanaashiria.

Haya ndiyo nimeweza kueleza miongoni mwa mambo yanayotumika kujilinda kwayo dhidi ya uchawi na kujitibu kwayo, na Mwenyezi Mungu ndiye Muwezeshaji.

Hapa linakuja suala muhimu, ambalo ni kutibu uchawi kwa mambo wanayofanya wachawi ambayo hutimia kwa njia ya kujikurubusha kwa majini kwa kuwachinjia au kitu kinginecho miongoni mwa mambo ya kujiweka karibu nao. Hili haliruhusiwi. Kwa sababu, ni katika matendo ya Shetani. Bali ni miongoni mwa ushirikina mkubwa. Pia hairuhusiwi kuutibu kwa kuwauliza makuhani, wapiga ramli na wachawi, na kutumia wanayoyasema. Na kwa sababu wao hawaamini, na kwa sababu ni waongo na waovu wanaodai kuwa wanayajua mambo ya ghaibu na huwahadaa watu. Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alionya dhidi ya kuwaendea, kuwauliza na kuwaamini, kama ilivyoelezwa hapo awali mwanzoni mwa makala hii. Kwa hivyo, la wajibu ni kujihadhari na hilo. Imepokelewa kwa njia sahihi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba aliulizwa kuhusu kutibu kwa kutumia uchawi. Akasema: "Hilo ni katika matendo ya Shetani." Imepokelewa na Imaam Ahmad na Abuu Daudi kwa msururu mzuri wa wasimulizi.

Annushra ni kuufungua uchawi kutoka kwa waliorogwa. Na annushra aliyomaanisha Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, hapa ni ile waliyokuwa wakifanya watu wa zama za ujinga, ambayo ni kumtaka mchawi kuufungua uchawi fulani, au kuufungua kwa uchawi mfano wake kutoka kwa mchawi mwingine.

Ama kuufungua uchawi kwa njia ya ruqya, kinga za kisheria na dawa zinazoruhusiwa, basi hakuna ubaya hakita hayo, kama ilivyotangulia kutajwa. Hayo yamesemwa moja kwa moja na mwanachuoni mkubwa Ibn al-Qayyim, na Sheikh Abdul-Rahman bin Hassan katika Fat-hul Majiid, Mwenyezi Mungu awarehemu wote wawili, na hili pia limesemwa moja kwa moja na wanachuoni wengineo.

Basi Mwenyezi Mungu ndiye aombwaye kuwawezesha Waislamu kufikia usalama kutokana na kila maovu, na kwamba awahifadhie dini yao, na awaruzuku kuifahamu na awaweke mbali na kila chenye kuhalifu sheria yake.

Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wake na Mtume wake, Mtume wetu Muhammad, na juu ya familia yake na Mawahaba wake wote.

 

***