التَّحْذِيرُ مِنَ البِدَعِ
TAHADHARI DHIDI YA UZUSHI
لِسَمَاحَةِ الشَّيْخِ العَلَّامَةِ
عَبْدِ العَزِيزِ بْنِ عَبْدِ اللهِ بْنِ بَازٍ
رَحِمَهُ اللهُ
Mtunzi Mheshimiwa, Sheikh,
Abdulaziz bin Abdillah bin Baaz
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ
Makala ya Tano:
Hukumu ya kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume na kuzaliwa kwa wengineo
Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, na watu wa familia yake, Maswahaba wake na wote wanaofuata uongofu wake.
Ama baada ya hayo: Swali lilirudiwa kutoka kwa wengi kuhusu hukumu ya kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, na kumsimamia, na kumtolea salamu na mambo mengine yanayofanywa katika sherehe hizi za kuzaliwa.
Jibu ni kusema: Hairuhusiwi kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake au kuzaliwa kwa mtu mwingine yeyote, kwa sababu hili ni miongoni mwa uzushi uliozushwa katika dini, kwa sababu Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, hakufanya hivyo, wala makhalifa wake waongofu, wala wasiokuwa hao miongoni mwa Maswahaba, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, wala wale waliowafuata kwa wema katika karne zote bora, na wao ndio wajuzi zaidi wa Sunna, na wenye upendo kamili kabisa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, na wenye kufuata zaidi sheria yake kuliko wale waliokuja baada yao. Na amesema Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka katika Kitabu chake kilicho wazi:
﴿...وَمَآ ءَاتَىٰكُمُ ٱلرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَىٰكُمۡ عَنۡهُ فَٱنتَهُواْ...﴾
"Na anachokupeni Mtume, chukuenii. Na anacho kukatazeni, jiepusheni nacho."
[Al-Hashr: 7] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...فَلۡيَحۡذَرِ ٱلَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنۡ أَمۡرِهِۦٓ أَن تُصِيبَهُمۡ فِتۡنَةٌ أَوۡ يُصِيبَهُمۡ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴾
"Basi nawatahadhari wanaokhalifu (kwenda kinyume na) amri yake, usijeukawapata msiba au ikawapata adhabu chungu. [An-Nur: 63] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿لَّقَدۡ كَانَ لَكُمۡ فِي رَسُولِ ٱللَّهِ أُسۡوَةٌ حَسَنَةٞ لِّمَن كَانَ يَرۡجُواْ ٱللَّهَ وَٱلۡيَوۡمَ ٱلۡأٓخِرَ وَذَكَرَ ٱللَّهَ كَثِيرٗا21﴾
"Hakika nyinyi mnayo ruwaza (kiigizo) chema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana". [Al-Ahzab: 21]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَٱلسَّٰبِقُونَ ٱلۡأَوَّلُونَ مِنَ ٱلۡمُهَٰجِرِينَ وَٱلۡأَنصَارِ وَٱلَّذِينَ ٱتَّبَعُوهُم بِإِحۡسَٰنٖ رَّضِيَ ٱللَّهُ عَنۡهُمۡ وَرَضُواْ عَنۡهُ وَأَعَدَّ لَهُمۡ جَنَّٰتٖ تَجۡرِي تَحۡتَهَا ٱلۡأَنۡهَٰرُ خَٰلِدِينَ فِيهَآ أَبَدٗاۚ ذَٰلِكَ ٱلۡفَوۡزُ ٱلۡعَظِيمُ100﴾
"Na wa wale waliotangulia, wa kwanza, miongoni mwa walio hama, na Answari (waliowapokea), na walio wafuata kwa wema, Mwenyezi Mungu ameridhika nao, na wao wameridhika naye, na amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa." [At-Tauba: 100]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...ٱلۡيَوۡمَ أَكۡمَلۡتُ لَكُمۡ دِينَكُمۡ وَأَتۡمَمۡتُ عَلَيۡكُمۡ نِعۡمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ ٱلۡإِسۡلَٰمَ دِينٗا...﴾
"Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini." [Al-Maidah: 3] Na aya zenye maana hii ni nyingi sana. Na imethibiti kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba alisema: "Yeyote atakayezua katika jambo letu hili kitu ambacho hakimo, basi hicho kitakataliwa." Yaani atarudishiwa yeye mwenyewe. Na alisema katika hadithi nyingine: "Shikamaneni na Sunna zangu na Sunna za makhalifa wanyoofu waongofu wa baada yangu. Zikamateni na kuzing'ata kwa magego. Na jihadharini na mambo mapya (katika dini). Kwani kila jambo jipya ni uzushi, na kila uzushi ni upotofu." Katika Hadithi hizi mbili kuna onyo kali dhidi ya kuanzisha uzushi na kuufanyia kazi. Na kuzua mfano wa sherehe hizi za kuzaliwa inafahamika kwa jambo hilo kwamba Mwenyezi Mungu aliyetakasika hakuukamilishia umma huu dini, na kwamba Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, hakufikisha yale ambayo umma huu unapaswa kuyafanyia kazi, mpaka hawa wa nyuma walipokuja, wakazua katika sheria yale ambayo Mwenyezi Mungu hakuyaidhinisha, wakidai kuwa haya ndiyo yanayowaleta karibu na Mwenyezi Mungu. Bila shaka kuna hatari kubwa ndani yake, na nikuweka pingamizi kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, rehema na amani ziwe juu yake, na Mwenyezi Mungu amewatimizia waja wake dini, na akatimiza neema zake juu yao. Na Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alifikisha ujumbe ulio wazi, na wala hakuacha njia inayomfikisha mtu Peponi, na kumuweka mbali na Moto isipokuwa aliubainishia umma huu, kama ilivyothibiti katika hadithi sahihi kutoka kwa Abdullah bin Amri, Mwenyezi Mungu awe radhi naye kwamba alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, alisema: "Mwenyezi Mungu hakumtuma Nabii yeyote ila ilikuwa ni haki juu yake kuwaonyesha umma wake heri anayoijua kwao, na kuwaonya dhidi ya uovu anaoujua kwao." Imesimuliwa na Muslim katika Sahihi yake.
Inajulikana kuwa Mtume wetu, rehema na amani ziwe juu yake, ndiye mbora wa Manabii na wa mwisho wao, na mkamilifu wao zaidi katika kufikisha na kunasihi. Kwa hivyo, kama maadhimisho ya kuzaliwa kwake yangekuwa katika dini ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu anairidhia, Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, angewaelezea umma wake, au angeyafanya katika maisha yake, au wangeyafanya Maswahaba wake, Mwenyezi Mungu awe radhi nao. Basi pindi hakuna lolote katika haya lililotokea, ikajulikana kwamba huo sio chochote katika Uislamu. Bali ni miongoni mwa uzushi ambao Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, aliuonya umma wake dhidi yake, kama lilivyotangulia kutajwa hilo katika Hadithi mbalimbali. Na Aya na hadithi katika mlango huu ni nyingi.
Na limekemea wazi kundi la wanachuoni suala la kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake na kutahadharisha dhidi yake, kwa mujibu wa ushahidi uliotajwa hapo juu na ushahidi mwingineo. Lakini baadhi ya watu waliokuja baadaye walikwenda kinyume kwa hivyo wakaruhusu hilo ikiwa halitajumuisha uovu wowote, kama vile kupita kiasi katika kumsifu Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, na kama vile kuchanganyika wanawake na wanaume, kutumia ala za burudani, na mambo mengineyo ambayo yanakatazwa na Sheria tukufu, na wakaona kwamba ni katika uzushi mzuri.
Lakini kanuni ya kisheria ni kurudisha chochote ambacho watu wanazozana ndani yake katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓاْ أَطِيعُواْ ٱللَّهَ وَأَطِيعُواْ ٱلرَّسُولَ وَأُوْلِي ٱلۡأَمۡرِ مِنكُمۡۖ فَإِن تَنَٰزَعۡتُمۡ فِي شَيۡءٖ فَرُدُّوهُ إِلَى ٱللَّهِ وَٱلرَّسُولِ إِن كُنتُمۡ تُؤۡمِنُونَ بِٱللَّهِ وَٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِۚ ذَٰلِكَ خَيۡرٞ وَأَحۡسَنُ تَأۡوِيلًا59﴾
"Enyi mlio amini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo, basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema". [An-Nisaa: 59] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَمَا ٱخۡتَلَفۡتُمۡ فِيهِ مِن شَيۡءٖ فَحُكۡمُهُۥٓ إِلَى ٱللَّهِ ...﴾
"Na mkihitilafiana katika jambo lolote, basi hukumu yake iko kwa Mwenyezi Mungu." [Ash-Shuraa: 10].
Basi tumelirejesha suala hili, ambalo ni: kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu, na tukakikuta kinatuamrisha kumfuata Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, katika yale aliyokuja nayo, na kutuonya juu ya yale aliyoyakataza, na kinatujulisha kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ameukamilishia umma huu dini yake, na sherehe hii sio katika yale aliyokuja nayo Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, kwa hivyo linakuwa si katika dini ambayo Mwenyezi Mungu ametukamilishia na akatuamrisha kumfuata Mtume ndani yake.
Pia tumelirudisha hilo katika Sunna ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake; na hatukupata ndani yake kwamba alifanya hivyo, wala hata hakuamrisha hivyo, wala Maswahaba wake Mwenyezi Mungu awe radhi nao hawakufanya hivyo, kwa hivyo tukajua kwa hayo kwamba hilo si katika dini, bali ni katika uzushi uliozushwa, na ni katika kuwaiga watu wa Kitabu miongoni mwa Mayahudi na Wakristo katika sikukuu zao.
Basi kwa hayo, inakuwa wazi kwa kila mtu ambaye ana ufahamu hata mdogo tu na hamu ya kujua haki na uadilifu katika kutafuta kwake haki, kwamba kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, si katika dini ya Uislamu, bali ni katika uzushi uliozushwa, ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume wake, rehema na amani ziwe juu yake, wameamrisha kuuwacha na kujitahadhari nao. Na kwamba mwenye akili timamu hafai kudanganyika na wingi wa watu wanaofanya hivyo katika pande zote za Dunia, kwa sababu haki haijulikani kwa wingi wa watendaji wake.
Bali inajulikana kwa ushahidi wa kisheria, kama alivyosema Mwenyezi Mungu kuhusu Mayahudi na Wakristo:
﴿وَقَالُواْ لَن يَدۡخُلَ ٱلۡجَنَّةَ إِلَّا مَن كَانَ هُودًا أَوۡ نَصَٰرَىٰۗ تِلۡكَ أَمَانِيُّهُمۡۗ قُلۡ هَاتُواْ بُرۡهَٰنَكُمۡ إِن كُنتُمۡ صَٰدِقِينَ111﴾
"Na walisema: Hataingia Peponi ila aliyekuwa Yahudi au Mkristo. Hayo ni matamanio yao. Sema: Leteni ushahidi wenu kama nyinyi ni wasema kweli." [Al-Baqarah: 111] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَإِنْ تُطِعْ أَكْثَرَ مَنْ فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ...﴾
“Na ukiwatii wengi katika hawa waliomo duniani, watakupoteza mbali na Njia ya Mwenyezi Mungu." [Al-An'am: 116]
Zaidi ya hayo, nyingi ya sherehe hizi za kuzaliwa, licha ya kwamba ni uzushi, hazikosi maovu mengine, kama vile kuchanganyika wanawake na wanaume, matumizi ya nyimbo na muziki, kunywa vileo na dawa za kulevya, na maovu mengineyo. Na kunaweza kutokea ndani yake kitu kikubwa zaidi kuliko hayo, ambacho ni ushirikina mkubwa, na hilo huwa kwa kupitiliza mipaka kuhusiana na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, au wengineo katika Mawalii (wachamungu), na kumuomba dua na kumlilia, na kumuomba usaidizi, na kuamini kwamba anajua mambo ya ghaibu, na mfano wa hayo miongoni mwa mambo ya kufuru ambayo watu wengi huyafanya wakati wa kusherehekea sherehe hizi za kuzaliwa kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, na wengineo miongoni mwa wale wanaowaita Mawalii. Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, kwamba alisema: "Jiepusheni na kupitiliza kiasi katika dini, kwani wale waliotangulia kabla yenu waliangamizwa na kupitiliza kiasi katika dini." Na amesema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Msinisifu sana kama Wakristo walivyomsifu sana mwana wa Mariamu. Hakika mimi ni mja tu. Basi semeni: Mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake." Imepokelewa na Bukhari, katika Sahihi yake kutoka katika Hadithi ya Omari, Mwenyezi Mungu awe radhi naye.
Na katika maajabu na mambo yasiyo ya kawaida ni kwamba watu wengi wanakuwa wakakamavu na wanajitahidi katika kuhudhuria sherehe hizi za uzushi, na kuzitetea, na anakosa kufanya kile ambacho Mwenyezi Mungu amemuwajibisha kama vile kuhudhuria swala za jamaa na tena hata hajali hilo na wala haoni kwamba amefanya ovu kubwa, na hakuna shaka kwamba hili ni katika udhaifu wa imani, uchache wa ufahamu, na kutu nyingi ya madhambi na maasi iliyo mioyoni mwao. Tunamuomba Mwenyezi Mungu salama, sisi pamoja na Waislamu wote.
Na katika hayo ni kwamba baadhi yao wanadhani kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, anahudhuria katika sherehe za kuzaliwa kwake, na hii ndiyo sababu wanasimama kwa ajili yake wakimsalimia na kumkaribisha. Na hili ni katika batili kubwa zaidi na ujinga mbaya kabisa. Kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, hawezi kutoka kaburini kwake kabla ya Siku ya Kiyama, na wala hawasiliani na yeyote katika watu, wala hahudhurii mkutano wao. Bali yuko kaburini mwake mpaka Siku ya Kiyama, na roho yake iko juu ya walio juu kabisa kwa Mola wake katika nyumba ya utukufu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿ثُمَّ إِنَّكُمْ بَعْدَ ذَلِكَ لَمَيِّتُونَ15 ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ تُبْعَثُونَ16﴾
"Kisha hakika nyinyi baada ya hayo mtakufa".
Kisha hakika nyinyi Siku ya Kiyama mtafufuliwa". [Al-Muminun: 15-16]
Na amesema Mtume rehema na amani zimshukie: "Mimi ndiye wa kwanza ambaye kaburi lake litafunguka siku ya Kiyama, na mimi ndiye muombezi wa kwanza na wa kwanza atakayekubaliwa uombezi wake." Rehema na amani bora zaidi ziwe juu yake kutoka kwa Mola wake Mlezi.
Basi Aya hizi mbili tukufu na Hadithi hii tukufu, na Aya na Hadithi zilizokuja na maana yake, zote zinaashiria kwamba Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, na watu wengineo waliokufa watatoka makaburini mwao Siku ya Kiyama tu. Hili ni jambo ambalo kuna maafikiano juu yake miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu, na hakuna mvutano wowote juu yake baina yao. Kwa hivyo kila Muislamu anapaswa kuwa na ufahamu wa mambo haya, na kutahadhari na yale waliyozua wajinga na mfano wao miongoni mwa mambo ya uzushi na uchawi ambayo Mwenyezi Mungu hakuyateremshia ushahidi wowote. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye ombwa msaada, naye ndiye Mtegemewa, na wala hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa Yeye.
Ama kumuombea Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, hayo ni miongoni mwa ibada bora za kujiweka kwazo karibu na Mwenyezi Mungu, na ni miongoni mwa matendo mema, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّ ٱللَّهَ وَمَلَٰٓئِكَتَهُۥ يُصَلُّونَ عَلَى ٱلنَّبِيِّۚ يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ صَلُّواْ عَلَيۡهِ وَسَلِّمُواْ تَسۡلِيمًا56﴾
"Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamsalia Nabii. Enyi mlio amini! Msalieni na mumsalimu kwa salamu." [Al-Ahzab: 56] Na amesema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie: "Yeyote atakayeniswalia mara moja, Mwenyezi Mungu atamswalia mara kumi kwa hilo." Hilo linaruhusiwa katika wakati wote, na linasisitizwa mwishoni mwa kila swala. Bali ni wajibu kwa mujibu wa kundi la wanachuoni katika Tahiyatu ya mwisho katika kila sala. Hali yake ya kuwa sunna inasisitizwa katika sehemu nyingi; ikiwa ni pamoja na baada ya adhana, wakati anapotajwa yeye rehema na amani ziwe juu yake, siku ya Ijumaa na usiku wake, kama zilivyo onyesha hilo hadithi nyingi.
Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuombwa atuongoze sisi na Waislamu wengine wote katika kuifahamu dini yake na kuwa imara juu yake, na amneemeshe kila mtu kushikamana na Sunna, na kujihadhari na uzushi. Hakika Yeye ndiye Mpaji, Mkarimu mno.
Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad na familia yake na Maswahaba zake.
***
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ
Makala ya Sita:
Hukumu ya kusherehekea usiku wa Al-Israa na Mi'raj
Sifa njema zote anastahiki Mwenyezi Mungu, na rehema na amani zimfikie Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake na Maswahaba wake.
Ama baada ya hayo: Hakuna shaka kwamba Al-Israa na Mi'raj ni miongoni mwa alama kubwa za Mwenyezi Mungu, zinazoashiria ukweli wa Mtume wake Muhammad, rehema na amani zimshukie, na ukuu wa hadhi yake mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama vile ni ushahidi wa uwezo mkubwa wa Mwenyezi Mungu na kuwa kwake juu ya viumbe vyake vyote. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:
﴿سُبۡحَٰنَ ٱلَّذِيٓ أَسۡرَىٰ بِعَبۡدِهِۦ لَيۡلٗا مِّنَ ٱلۡمَسۡجِدِ ٱلۡحَرَامِ إِلَى ٱلۡمَسۡجِدِ ٱلۡأَقۡصَا ٱلَّذِي بَٰرَكۡنَا حَوۡلَهُۥ لِنُرِيَهُۥ مِنۡ ءَايَٰتِنَآۚ إِنَّهُۥ هُوَ ٱلسَّمِيعُ ٱلۡبَصِيرُ1﴾
"Ametakasika Yule aliyemchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyouzunguka, ili tumu onyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona". [Al-Israa: 1].
Imesimuliwa kwa wingi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe juu yake kwamba alipanda mbinguni, na akafunguliwa milango yake mpaka akapita mbingu ya saba, na Mola wake Mlezi Mtukufu akamsemesha akamwambia kile alichotaka, na akamfaradhishia swala tano. Hapo awali Mwenyezi Mungu Mtukufu alikuwa amemfaradhishia swala hamsini, lakini Nabii Muhammad rehema na amani ziwe juu yake hakuacha kumrudia na kumuomba azipunguze, mpaka akazifanya kuwa tano. Basi ni tano katika wajibu, na ni hamsini katika malipo; kwa sababu jema moja linalipwa mfano wake mara kumi. Kwa hivyo sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu na shukrani kwa neema zake zote.
Usiku huu ambao ilifanyika Isra na Mi’raj ndani yake, haukubainishwa haswa ulikuwa upi katika Hadithi sahihi, si katika Rajab wala katika mwezi wowote ule. Kila kilichokuja katika kuteua muda wake haswa, hicho hakikuthibiti kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwa mujibu wa wanazuoni wa elimu ya Hadithi. Na Mwenyezi Mungu anayo hekima kubwa zaidi ya kuwasahaulisha watu usiku huo. Na hata kama ingejulikana kwamba yalitokea katika usiku fulani unaojulikana, basi wasinge ruhusiwa kuuadhimisha. Kwa sababu Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na Maswahaba zake, Mwenyezi Mungu awawie radhi, hawakuuadhimisha, wala hawakuuwekea kitu chochote maalumu. Na kama kuuadhimisha kungekuwa jambo lililoko katika sheria, basi Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, angeliuelezea umma wake hilo; ima kwa kauli au kwa vitendo. Na kama lingetokea jambo kama hilo, basi lingejulikana na kuwa maarufu, na Maswahaba, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, wangelitufikishia sisi. Kwani wao walisimulia kutoka kwa Mtume wao, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kila kitu ambacho umma unakihitaji, na hawakupuuza chochote katika Dini. Bali wao ndio waliokuwa wa kwanza kuiendea kila heri. Kwa hivyo, kungekuwa kuadhimisha usiku huu kuko katika sheria, basi wangekuwa watu wa kwanza kufanya hivyo. Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ndiye mwenye kunasihi zaidi kuliko watu wote, na alikwishafikisha ujumbe kufikisha kwa hali ya juu zaidi, na akatekeleza amana. Kwa hivyo, kungekuwa kuuadhimisha usiku huu na kuusherehekea kunatoka kwa Mwenyezi Mungu, basi Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, hangekosa kujua hilo, na hangelificha. Na pindi hakuna chochote kilichotokea katika hayo, ikajulikana kuwa kuusherehekea na kuuadhimisha si katika Uislamu hata kidogo. Na tayari Mwenyezi Mungu alishaukamilishia umma huu dini yake, akautimizia neema zake, na akawakanusha wale wanaotunga sheria katika dini yale ambayo Mwenyezi Mungu haku yaruhusu. Amesema Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka katika Kitabu chake kilicho wazi:
﴿...ٱلۡيَوۡمَ أَكۡمَلۡتُ لَكُمۡ دِينَكُمۡ وَأَتۡمَمۡتُ عَلَيۡكُمۡ نِعۡمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ ٱلۡإِسۡلَٰمَ دِينٗا...﴾
"Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini." [Al-Maidah: 3] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿أَمۡ لَهُمۡ شُرَكَٰٓؤُاْ شَرَعُواْ لَهُم مِّنَ ٱلدِّينِ مَا لَمۡ يَأۡذَنۢ بِهِ ٱللَّهُۚ وَلَوۡلَا كَلِمَةُ ٱلۡفَصۡلِ لَقُضِيَ بَيۡنَهُمۡۗ وَإِنَّ ٱلظَّٰلِمِينَ لَهُمۡ عَذَابٌ أَلِيمٞ21﴾
"Au hao wana miungu ya kishirikina iliyowatungia dini asiyoitolea idhini Mwenyezi Mungu? Na lau lisingekuwako neno la kupambanua, basi wangelikatiwa hukumu baina yao. Na hakika wenye kudhulumu watapata adhabu chungu). [Ash-Shura: 21].
Na ilithibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika Hadithi sahihi kwamba alitahadharisha dhidi ya uzushi na akatangaza wazi kwamba ni upotofu ili kutanabahisha umma wake juu ya ukubwa wa hatari yake, na kuwaweka mbali na kuufanya, ikiwa ni pamoja na yale yaliyothibiti katika Sahihi mbili kutoka kwa Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, kwamba alisema: "Yeyote atakayezua katika jambo letu hili kitu ambacho hakimo, basi hicho kitakataliwai." Katika simulizi ya Muslim: "Mwenye kufanya amali ambayo hatukuiamrisha, basi amali hiyo itakataliwa." Na katika Sahihi Muslim, kutoka kwa Jabir Mwenyezi Mungu awe radhi naye alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe juu yake alikuwa akisema katika hotuba yake siku ya Ijumaa: "Ama baada ya hayo. Hakika mazungumzo bora ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Na muongozo bora ni muongozo wa Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Na mambo mabaya zaidi ni mambo ya kuzushwa. Na kila uzushi ni upotevu." Aliongeza Imam Nasai kwa mlolongo mzuri wa wasimulizi kwamba: "Na kila upotofu ni Motoni." Na katika Sunan, imesimuliwa kutoka kwa Al-'Irbat bin Sariyah, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, kwamba alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alituaidhi mawaidha makali sana. Nyoyo zikajaa hofu kwa sababu yake, na macho yakamiminika machozi kwa sababu yake, basi tukasema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni kama kwamba ni mawaidha ya anayeaga. Basi tuusie." Akasema: "Ninawausia kumcha Mwenyezi Mungu, na kusikia na utii, hata kama atakutawaleni mtumwa. Kwani hakika yeyote kati yenu atakayeishi, ataona tofauti nyingi. Kwa hivyo shikamaneni na Sunna yangu na Sunna ya makhalifa wanyoofu waongofu baada yangu. Zikamateni na kuzing'ata kwa magego. Na jihadharini na mambo ya kuzushwa. Kwani kila jambo jipya (katika dini) ni uzushi, na kila uzushi ni upotofu." Na kuna hadithi nyingi zenye maana hii.
Ilithibiti kutoka kwa Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, na kutoka kwa watangulizi wema wa baada yao, kutahadharisha dhidi ya uzushi na kutisha kutokana nao. Hili si isipokuwa kwa sababu tu ni kuongeza katika dini na kutunga sheria ambayo Mwenyezi Mungu hakuidhinisha, na ni kujifananisha na maadui wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa Mayahudi na Wakristo katika kuongeza katika dini yao, na katika kuzua kwao ndani yake kile ambacho Mwenyezi Mungu hakuidhinisha, na kwa sababu hilo linamaanisha kwamba kuna upungufu katika dini ya Kiislamu, kuishutuhumu kwamba si kamilifu, lakini hili linajulikana kwamba ni uharibifu mkubwa, uovu mbaya sana, na kugongana na maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...ٱلۡيَوۡمَ أَكۡمَلۡتُ لَكُمۡ دِينَكُمۡ...﴾
"Leo nimekukamilishieni dini yenu." [Al-Maidah: 3] Na kwenda kinyume wazi wazi na hadithi za Mtume, rehema na amani ziwe juu yake zinazoonya dhidi ya uzushi na zinazomuweka mtu mbali na hilo.
Ni hayo, na ninatumai kwamba ushahidi tulioutaja utamtosha na kumridhisha mtafutaji haki katika kukataza uzushi huu. Ninamaanisha uzushi wa kusherehekea usiku wa Israai na Mi'raj, na kuonya dhidi yake, na kwamba hauhusiani na dini ya Kiislamu hata kidogo.
Na kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwajibisha kuwapa Waislamu nasaha, na kubainisha yale ambayo Mwenyezi Mungu amewawekea sheria yake katika dini, na kuharamisha kuficha elimu, niliona niwatanabahishe ndugu zangu Waislamu juu ya uzushi huu, ambao umeenea katika sehemu nyingi, mpaka baadhi ya watu wakadhani kwamba hilo ni katika dini.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu arekebishe hali za Waislamu wote, awape ufahamu wa dini na atuwezeshe sisi na wao kushikamana na haki na kuwa imara juu yake, na kuacha yenye kwenda kinyume. Hakika Yeye ndiye Msimamizi wa hayo na Mwenye uwezo juu yake.
Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Nabii wetu Muhammad, na familia yake na Maswahaba wake.
***
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ
Makala ya Saba:
Hukumu ya kusherehekea usiku wa nusu ya Shaaban
Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye tukamilishia Dini, na akatutimizia neema, na rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimfikie Nabii wake na Mtume wake Muhammad, Nabii wa toba na rehema.
Ama baada ya hayo: Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:
﴿...ٱلۡيَوۡمَ أَكۡمَلۡتُ لَكُمۡ دِينَكُمۡ وَأَتۡمَمۡتُ عَلَيۡكُمۡ نِعۡمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ ٱلۡإِسۡلَٰمَ دِينٗا...﴾
"Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini." [Al-Maidah: 3] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿أَمۡ لَهُمۡ شُرَكَٰٓؤُاْ شَرَعُواْ لَهُم مِّنَ ٱلدِّينِ مَا لَمۡ يَأۡذَنۢ بِهِ ٱللَّهُ...﴾
"Au hao wana miungu ya kishirikina iliyowatungia dini asiyoitolea idhini Mwenyezi Mungu?" [Ash-Shura: 21]. Na katika Sahihi mbili kutoka kwa Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, ya kwamba Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alisema: "Yeyote atakayezua katika jambo letu hili kitu ambacho hakimo, basi kitu hicho kitakataliwai." Na katika Sahihi Muslim, kutoka kwa Jabir Mwenyezi Mungu amridhie, ya kwamba Mtume rehema na amani juu yake alikuwa akisema katika hotuba ya Ijumaa: "Ama baada ya hayo: Hakika mazungumzo bora ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Na muongozo bora ni muongozo wa Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Na mambo mabaya zaidi ni mambo ya kuzushwa. Na kila uzushi ni upotevu." Kuna Aya na Hadithi nyingi zenye maana hii, nazo ninaonyesha wazi kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ameukamilishia umma huu dini, na ameutimizia neema yake, na hakumfisha Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, isipokuwa baada ya Mtume kufikisha kufikisha kwa wazi, na akauelezea umma huu maneno na matendo yote ambayo Mwenyezi Mungu ameuwekea katika sheria yake. Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alieleza wazi kwamba kila kitu ambacho watu watazusha baada yake na kukinasibisha na dini ya Kiislamu, sawa kiwe ni maneno au vitendo, hivyo vyote ni uzushi utakaokataliwa na na arudishiwe aliyeuanzisha, hata kama nia yake ilikuwa njema. Maswahaba wa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, walilijua jambo hili, na vile vile wanavyuoni wa Kiislamu wa baada yao. Kwa hivyo, wakaukemea uzushi huo na kuonya dhidi yake, kama alivyotaja hilo kila aliyeandika juu ya kuheshimu Sunna na kukataza uzushi; kama vile Ibn Wadhwaah, At-Twartuushii, Abu Shaama na wengineo.
Na hakika miongoni mwa uzushi ambao baadhi ya watu wameuanzisha ni uzushi wa kusherehekea usiku wa nusu ya Sha’ban na kuiteua siku hiyo kwa ajili ya saumu. Hakuna ushahidi wowote unaoweza kutegemewa kwa hili. Ila kuna Hadithi dhaifu ambazo zimeripotiwa kuhusu ubora wake, ambazo hairuhusiwi kuzitegemea.
Ama kuhusu kile kilichokuja kuhusiana na fadhila za kuswali ndani yake, hizo zote ni za kutungwa na watu, kama wasomi wengi walivyotanabahisha juu ya hilo, na tutataja baadhi ya maneno yao baadaye, Mwenyezi Mungu akipenda.
Pia kuna simulizi zinazohusiana na hilo zilizosimuliwa kutoka kwa watangulizi wema miongoni mwa wanazuoni wa Sham na wengineo.
Wanavyuoni walio wengi wamekubaliana kwamba kusherehekea hilo ni uzushi, na kwamba Hadithi zilizosimuliwa kuhusu fadhila zake, zote ni dhaifu, na baadhi yake ni za kutungwa na watu. Miongoni mwa wale waliotanabahisha juu ya hilo ni Al-Hafidh Ibn Rajab katika kitabu chake "Latwa’if Al-Ma’arif" na wengineo. Na inajulikana kuwa Hadithi dhaifu zinaweza kutumika tu katika matendo ya ibada ambazo asili yake ilithibiti kwa ushahidi sahihi.
Ama kuhusu kusherehekea usiku wa nusu ya Sha'aban, hilo halina msingi sahihi; ndiyo utumike pamoja na hadithi dhaifu. Kanuni hii utukufu ilitajwa na Imam Abu Al-Abbas, Sheikh Al-Islam Ibn Taymiyyah, Mwenyezi Mungu amrehemu.
Nami ninakufikishia, ewe msomaji kile ambacho baadhi ya wasomi walisema katika suala hili, ili uweze kulifahamu vyema.
Wanavyuoni -Mwenyezi Mungu awarehemu- wame afikiana kwamba jambo la wajibu ni kurejesha mambo ambayo watu wanabishana ndani yake kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu mkubwa, na kwenye Sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Hapo, chochote kinachopingana na viwili hivyo, inakuwa ni lazima kukitupilia mbali. Na ibada yoyote ambayo haikuja katika viwili hviyo, basi hiyo ni uzushi ambao hauruhusiwi kuutenda, achilia mbali kuulingania na kuwahimiza watu juu yake. Amesema Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka:
﴿يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓاْ أَطِيعُواْ ٱللَّهَ وَأَطِيعُواْ ٱلرَّسُولَ وَأُوْلِي ٱلۡأَمۡرِ مِنكُمۡۖ فَإِن تَنَٰزَعۡتُمۡ فِي شَيۡءٖ فَرُدُّوهُ إِلَى ٱللَّهِ وَٱلرَّسُولِ إِن كُنتُمۡ تُؤۡمِنُونَ بِٱللَّهِ وَٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِۚ ذَٰلِكَ خَيۡرٞ وَأَحۡسَنُ تَأۡوِيلًا59﴾
"Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo, basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema". [An-Nisaa: 59] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿َمَا ٱخۡتَلَفۡتُمۡ فِيهِ مِن شَيۡءٖ فَحُكۡمُهُۥٓ إِلَى ٱللَّهِ...﴾
"Na mkihitilafiana katika jambo lolote, basi hukumu yake iko kwa Mwenyezi Mungu." [Ash-Shuraa: 10]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿قُلۡ إِن كُنتُمۡ تُحِبُّونَ ٱللَّهَ فَٱتَّبِعُونِي يُحۡبِبۡكُمُ ٱللَّهُ وَيَغۡفِرۡ لَكُمۡ ذُنُوبَكُمۡ...﴾
"Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu". [Al-Imran: 31] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤۡمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيۡنَهُمۡ ثُمَّ لَا يَجِدُواْ فِيٓ أَنفُسِهِمۡ حَرَجٗا مِّمَّا قَضَيۡتَ وَيُسَلِّمُواْ تَسۡلِيمٗا65﴾
"La! Ninaapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayohitilafiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utakayotoa, na wanyenyekee kabisa". [An-Nisaa: 65] Na Aya zenye maana hii ni nyingi, nazo zinataja moja kwa moja kuwa ni wajibu kurudisha masuala ya hitilafu kwenye Kitabu na Sunna, na kwamba ni lazima kuridhia hukumu ya viwili hivyo, na kwamba hili ndilo hitaji la imani, na ndilo bora kwa waja duniani na akhera, na ndiyo yenye mwisho mwema.
Al-Hafith Ibn Rajab, Mwenyezi Mungu amrehemu, alisema katika kitabu chake: (Latwaif Al-Maarif) katika suala hili, baada ya maneno yaliyotangulia. Alisema hivi:
"Na usiku wa nusu ya Shaaban, wafuasi wa Masahaba waliokuwa huko Sham kama vile Khalid bin Ma'daan, Mak-huul, na Luqman bin Amir na wengineo, walikuwa wakiutukuza na kujibibiisha ndani yake kufanya ibada, na kutoka kwao ndio watu walichukua ubora wake na kuutukuza. Ilisemekana kuwa simulizi za Kiisraeli ziliwafikia katika suala hili, na wakati hili lilipojulikana kuhusiana nao katika nchi, watu wakatofautiana katika hilo. Basi baadhi yao wakalikubali kutoka kwao na wakaafikiana nao kuhusiana na kuutukuza, katika hao ni kikundi miongoni mwa wale wafanyao ibada sana katika watu wa Basra na wengineo. Hilo lilikataliwa na wanachuoni wengi wa Hijazi, ikiwa ni pamoja na Atwaa, na bin Abi Mulaika, na lilinukuliwa na 'Abdur-Rahman ibn Zaid ibn Aslam kutoka kwa wanazuoni wa watu wa Madina, nayo ndiyo kauli ya wafuasi wa Malik na wengineo, nao wote walisema: Huo wote ni uzushi.
Wanachuoni wa watu wa Sham walitofautiana katika njia ya kufanya ibada ndani yake kwa kauli mbili:
Ya kwanza: Kwamba inapendekezwa kufanya ibada ndani yake kwa kikundi ndani ya misikiti. Khalid bin Madan, na Luqman bin Amir na wengineo walikuwa wakivaa nguo zao bora, wakijifukizia moshi wa manukato na kupaka wanja, na kusimama msikitini usiku huo, na pia Ishaq bin Rahawaihi alikubaliana nao katika hayo. Alisema kuhusiana na kusimama kwa ajili ya swala misikitini katika jamaa: Huu si uzushi. Hili lilinukuliwa na Harb Al-Karmaani katika masuala yake.
Ya pili: Kwamba inachukiza kukutana ndani yake katika misikiti kwa ajili ya sala, kusimulia visa na kuomba dua, lakini haichukizi mtu kusali ndani yake yeye mwenyewe, na hivi ndivyo alivyosema Al-Awza'i, imamu wa watu wa Sham, faqihi wao na mwanachuoni wao, na hii ndiyo kauli iliyokaribu zaidi na usahihi, Mwenyezi Mungu akipenda." Hadi aliposema: “Na haijulikani Imam Ahmad alisema nini kuhusu usiku wa nusu ya Sha'aban, lakini zinaweza kutolewa riwaya mbili kutoka kwake zenye kupendekeza kuusimama kama zile riwaya mbili zilizopokelewa kutoka kwake zenye kupendekeza kusimama katika usiku wa Idi mbili. Katika masimulizi moja, hakupendekeza kusimama usiku wa Idi mbili katika jamaa; kwa sababu hilo halikupokelewa kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie na maswahaba wake. Na alipendekeza hilo (katika simulizi nyingine), kwa sababu Abdur-Rahman bin Yazid bin Al-Aswad alifanya hivyo, naye ni miongoni mwa wale waliokuja baada ya Maswahaba. Na vile vile kusimama kwa ajili ya ibada usiku wa nusu ya Shaban hakuna kilichothibiti kuhusiana na hilo kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, wala kutoka kwa Maswahaba wake. Na hilo lilithibiti tu kutoka kwa kundi la watu binafsi waliokuja baada ya Maswahaba miongoni mwa wanachuoni wa watu wa Sham.
Yamekwisha yaliyokusudiwa katika maneno ya Al-Hafidh Ibn Rajab, Mwenyezi Mungu amrehemu, na ndani yake ameeleza kwa uwazi kabisa kwamba hakuna chochote kilichothibiti kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, wala kutoka kwa Maswahaba zake kuhusu usiku wa katikati ya Sha’ban.
Ama kuhusu kile ambacho Al-Auza'i alichagua -Mwenyezi Mungu amrehemu- kupendekeza mtu binafsi kusimama kwa ajili ya ibada na kuchagua kwake Al-Hafidh Ibn Rajab kauli hii, hilo ni geni na dhaifu. Kwa sababu kila kitu ambacho hakikuthibiti kwa ushahidi wa kisheria kwamba ni katika sheria, hairuhusiwi kwa Muislamu kukizua katika dini ya Mwenyezi Mungu, sawa akifanye peke yake au katika jamaa, na sawa akifanye kwa siri au wazi wazi; kwa ujumla wa kauli ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake: "Mwenye kufanya tendo ambalo hatukuliamrisha, basi hilo litakataliwa." Na ushahidi mwingine wa kukanusha na kuonya dhidi ya uzushi.
Imam Abu Bakar at-Tartushi, Mwenyezi Mungu amrehemu, alisema katika kitabu chake Al-Hawaadith wal-Bida'u:
"Na amesimulia bin Wadhwaah kutoka kwa Zaid bin Aslam, ya kuwa, alisema: Hatukuwahi kuona yeyote kati ya Mashekhe wetu au wanasheria wetu akizingatia (suala la kusimama usiku wa) nusu ya Sha'baan, wala kuzingatia hadithi ya Mak-hul, wala hata hawakuwa wakiona kuwa kuna ubora wowote kuliko usiku mwingineo."
Na aliambiwa bin Abi Mulaikah: Ziadi An-Numairi anasema: "Hakika malipo ya usiku wa nusu ya Sha'baan ni kama malipo ya usiku wa Cheo (Lailatul-Qadr)." Akasema: "Laiti ningemsikia huku nikiwa na fimbo mkononi, basi ningempiga nayo." Na Ziadi alikuwa msimuliaji wa visa. Yamekamilika makusudio.
Na amesema Ash-Shaukani –Mwenyezi Mungu amrehemu– katika kitabu “Al-Fawa’id Al-Majmu’ah” yafuatayo:
Hadithi ya: “Ewe Ally, mwenye kusali rakaa mia katika usiku wa nusu ya Shaaban akisoma Al-Fatiha katika kila rakaa na Qul huwallahu ahad mara kumi, Mwenyezi Mungu atamtimizia kila haja yake." n.k. Ni hadithi waliyoitunga watu, na mtu hawezi kuwa na shaka yoyote kuhusu maneno yake yanayosema wazi wazi juu ya thawabu zake kwamba hayo yalitungwa tu na watu, na hata wasimulizi wake hawajulikani vyema, na pia ilisimuliwa katika njia ya pili na ya tatu, ambazo zote zimetungwa tu na watu na wasimulizi wake hawajulikani. Na alisema katika "Al-Mukhtaswar": Hadithi ya kuswali katika nusu ya Sha'ban ni batili. Ibn Hibban alisimulia hadithi ya Ali: "Unapokuwa usiku wa nusu ya Sha'ban, simameni usiku wake, na fungeni saumu mchana wake." ni dhaifu. Alisema katika "Alla-alii": (Kuswali) Rakaa mia moja katika nusu ya Shaaban kwa ikhlas ni (kama rakaa) elfu moja." pamoja na urefu wa fadhila yake. Hii imepokelewa na Ad-Dailami na wengineo, lakini ni ya kutungwa tu na watu, wengi wa wasimulizi wake katika njia zake tatu hawajulikani na ni madhaifu. Na akasema: "Na rakaa kumi na mbili kwa ikhlas ni (kama rakaa) mia tatu na sitini". Nayo pia ni hadithi ya kutungwa na watu. Alisema: "Na rakaa kumi na nne" Pia ni hadithi ya kutungwa na watu.
Kuna kundi la mafaqihi (wanachuoni) lililoizingatia hadithi hii, kama vile mwandishi wa (Al-Ihyaa) na wengineo, vile vile wengineo miongoni mwa wafasiri. Na imepokelewa swala ya usiku huu - ninamaanisha: Usiku wa nusu ya Sha'ban - kwa njia tofauti toafauti, ambazo zote ni batili. Hili halipingani na riwaya ya At-Tirmidhi kutoka kwa Hadithi ya Aisha, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, kuhusu kwenda kwake Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, huko Al-Baqi’, na kushuka kwa Mola Mlezi katika usiku wa katikati ya Sha'ban hadi mbingu ya chini kabisa, na kwamba Yeye husamehe zaidi ya idadi ya nywele za kondoo wa kabila la Kalb. Kwani hapa suala linahusiana na swala hii iliyotungwa na watu katika usiku huu. Hata hivyo, hadithi hii ya Aisha ina udhaifu na usimulizi wake haufiki kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kama vile hadithi ya Ali, ambayo imetajwa hapo awali kuhusu kusimama kwa ajili ya swala katika usiku wa nusu ya Shaban haipingani na hali ya kwamba swala hii imetungwa na watu, pamoja na udhaifu wake, kama tulivyotaja.
Al-Hafidh Al-Iraqi alisema: "Hadithi ya Swala ya usiku wa nusu ya Shaban imetungwa na watu na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, hakuisema na ni kumzulia uongo juu yake." Imam An-Nawawi alisema katika kitabu cha "Al-Majmu" kwamba: Swala inayo julikana kama swala ya arraghaaib, ambayo ni rakaaa kumi na mbili kati ya Maghrib na Isha, usiku wa Ijumaa ya kwanza ya Rajab, na swala ya usiku wa nusu ya Shaaban ambayo ni rakaa mia moja, sala hizi mbili ni uzushi unaopingwa, na mtu asidanganyike na kutajwa kwake katika kitabu cha "Quut Al-Quluub" na "Ihayaa 'Uluumud-Diin" wala katika hadithi yoyote ambayo zilitajwa ndani yake. Zote hizo ni batili, na wala mtu asidanganyike na baadhi ya maimamu waliotatizika kuhusiana na hukumu yake, kwa hivyo wakaandika makaratasi kuhusu kuzipendekeza, kwa sababu walikosea katika hilo."
Sheikh, Imamu, Abu Muhammad Abdul-Rahman bin Ismail al-Maqdisii aliandika kitabu chenye thamani kubwa katika kukanusha hayo, na akafanya kazi nzuri sana ndani yake. Na maneno ya wanazuoni katika suala hili ni mengi sana, na lau tungenukuu kila kitu tulichokiona katika maneno yaliyosemwa juu ya suala hili, basi maneno hayo yangekuwa marefu sana, na pengine tuliyoyataja yatamtosha na kumridhisha mtafutaji haki.
Kupitia Aya, Hadithi na maneno ya wanachuoni yaliyotangulia hapo juu, inadhihirika kwa mtafutaji haki kwamba kusherehekea usiku wa katikati ya Sha’ban kwa swala au mambo mengineyo, na kuuteua mchana wake kwa ajili ya saumu, ni uzushi unaokataliwa na wanavyuoni wengi, na hayo hayana msingi wowote katika Sheria safi. Bali ni miongoni mwa mambo mapya yaliyotokea katika Uislamu baada ya zama za Maswahaba, Mwenyezi Mungu awe radhi nao. Inamtosha mtafutaji haki katika mlango huu na wingineyo kauli ya Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu mkubwa:
﴿...ٱلۡيَوۡمَ أَكۡمَلۡتُ لَكُمۡ دِينَكُمۡ...﴾
"Leo nimekukamilishieni dini yenu." [Al-Maidah: 3] Na aya nyingizeno zilizokuja na maana yake, na maneno ya Mtume rehema na amani ziwe juu yake: "Yeyote atakayezua katika jambo letu hili kitu ambacho hakimo, basi hicho kitakataliwai." Na hadithi zilizokuja na maana yake.
Na katika Sahihi Muslim, kutoka kwa Abuu Huraira, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Msiuteuwe usiku wa Ijumaa kwa ajili ya kusimama katika usiku, na wala msiiteuwe siku yoyote ile kwa ajili ya kufunga saumu ndani yake, isipokuwa ikiwa ni katika kufanga saumu ambako mmoja wenu hufunga." Kama kungekuwa kuuteuwa usiku fulani kwa ajili ya ibada fulani kunaruhusiwa, basi usiku wa Ijumaa ungekuwa bora zaidi ya usiku mwingineo, kwa sababu mchana wake ndio mchana bora zaidi ambao jua limewahi kuuchomozea, kwa mujibu wa andiko la Hadithi sahihi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake. Basi pindi Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alipoonya dhidi ya kuuteuwa usiku huu kwa ajili ya ibada, hilo likaonyesha kwamba usiku mwingineo haufai zaidi, hairuhusiwi kuuteuwa kwa ajili ya ibada yoyote ile isipokuwa kwa ushahidi sahihi unaoonyesha uteuzi huo.
Kwa kuwa usiku wa Cheo (Lailatul-Qadr) na siku zote za Ramadhan tumeamrishwa kusimama kwa ajili ya ibada na kufanya bidii ndani yake, Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alitanabahisha dhidi ya hili, na akauhimiza umma kusimama ndani yake kwa ajili ya ibada, na mwenyewe akafanya hivyo, kama ilivyo katika Sahihi mbili kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ya kwamba alisema: "Atakayefunga Ramadhani kwa imani na kutarajia malipo (ya Mwenyezi Mungu), atasamehewa dhambi zake zilizotangulia. Na atakayesimama katika Lailatul-Qadri kwa ajili ya ibada kwa imani na kutarajia malipo, atasamehewa dhambi zake zilizotangulia." Basi kama usiku wa nusu ya Shaaban, au usiku wa kwanza wa Ijumaa katika mwezi wa Rajab, au usiku wa Al-Israa na Mi'raj, ungelikuwa ni katika sheria kuuteuwa kwa ajili ya sherehe au ibada fulani, basi Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, angeliuongoza umma kwake katika hayo, au angeyafanya yeye mwenyewe, na kama kingelitokea kitu kama hicho, basi Masahaba -Mwenyezi Mungu awe radhi nao- wangekifikisha kwa umma, na wasingekificha umma usikijue, na wao ndio watu bora kabisa, na na ndio wenye kunasihi zaidi watu baada ya Manabii, rehema na amani ziwe juu yao, na Mwenyezi Mungu aliwaradhia Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake na akawafanya kuridhia.
Umekwishajua hivi karibuni kutokana na maneno ya wanachuoni kwamba hakuna chochote kilichothibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, wala kutoka kwa Maswahaba zake, Mwenyezi Mungu awawie radhi, kuhusu fadhila za usiku wa Ijumaa ya kwanza katika Rajab, wala usiku wa katikati ya Sha’ban, kwa hivyo ikajulikana kuwa kuzisherehekea ni uzushi ulioingizwa katika Uislamu, na vile vile kuziteua kwa ajili ya ibada fulani ni uzushi unaokatazwa. Vivyo hivyo, usiku wa ishirini na saba wa Rajab, ambao baadhi ya watu wanaamini kuwa ndio usiku wa Al-Israa na Mi'raj, hairuhusiwi kuuteuwa kwa ajili ya kitu chochote cha ibada, wala kuusherehekea; kwa sababu ya ushahidi uliotangulia. Lau hilo lingejulikana. Basi itakuwa vipi na ukweli katika kauli za wanachuoni ni kwamba halijulikani. Na kauli ya yule aliyesema: Ni usiku wa ishirini na saba wa Rajab, ni kauli batili na haina msingi wowote katika hadithi sahihi, na alisema vizuri sana aliyesema:
Na mambo bora zaidi ni yale yanayotokana na uongofu... na mambo mabaya zaidi ni mambo ya uzushi, na ya kubumbwa.
Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuombwa atuwezeshe sisi na Waislamu wote kushikamana na Sunna na kuwa imara juu yake na kuyatahadhari yale yaliyokwenda kinyume nayo. Hakika Yeye ni Mpaji, Mkarimu.
Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wake na Mtume wake, Mtume wetu Muhammad, na juu ya familia yake na Maswahaba wake wote.
***
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ
Makala ya Nane:
Tanbihi muhimu juu ya uongo wa wosia ulionasibishwa na
Sheikh Ahmad, mtumishi wa Msikiti mtukufu wa Mtume
Kutoka kwa Abdulaziz bin Abdullah bin Baz hadi kwa Waislamu watakaousoma, Mwenyezi Mungu awalinde kwa Uislamu, na atuepushe sisi na wao na uzushi mbaya wa wajinga na madhalimu. Amiin.
Assalaam alaikum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
Ama baada ya hayo: Niliona ujumbe unaohusishwa na Sheikh Ahmad, mtumishi wa Msikiti mtukufu wa Mtume, wenye kichwa cha habari: "Huu ni wosia kutoka Madina kutoka kwa Sheikh Ahmad, mtumishi wa Msikiti mtukufu wa Mtume," ambapo alisema:
"Nilikuwa ninakesha usiku wa Ijumaa nikisoma Qur'ani Tukufu, na baada ya kusoma usomaji wa Majina Mazuri ya Mwenyezi Mungu, nilipomaliza hilo, nilijiandaa kwa ajili ya kulala, na nikamuona mtu mwenye muonekano mzuri, Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, aliyekuja na Aya za Qur'ani na hukumu tukufu; viwe rehema kwa walimwengu wote, bwana wetu Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Akasema: Ewe Sheikh Ahmad. Nikasema: Nimekuitikia ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mtukufu wa viumbe vyote. Akaniambia: "Nimeaibika kwa matendo mabaya ya watu, na sikuweza kukutana na Mola wangu Mlezi wala Malaika; kwa sababu kuanzia Ijumaa hadi Ijumaa watu elfu mia moja na sitini walikufa mbali na dini ya Uislamu." Na kisha akataja baadhi ya dhambi ambazo watu waliingia ndani yake. Kisha akasema: "Huu hapa wasia ambao ni rehema kwao kutoka kwa Mwenye nguvu, atendaye atakavyo." Kisha akataja baadhi ya alama za Saa ya Kiyama, hadi aliposema: "Basi Sheikh Ahmad, waambie wasia huu, kwa sababu umenukuliwa kwa kalamu ya mipango ya Mwenyezi Mungu kutoka katika ubao uliohifadhiwa. Na yeyote anayeuandika na kupeleka kutoka nchi hadi nchi, na mahali hadi mahali, atajengewa kasri Peponi. Na yeyote asiyeuandika na kuutuma, atanyimwa uombezi wangu Siku ya Kiyama." Na yeyote atakayeuandika na alikuwa maskini, basi Mwenyezi Mungu atamajirisha, au ikiwa alikuwa na deni, Mwenyezi Mungu atamlipia deni lake, au alikuwa na dhambi, Mwenyezi Mungu atamsamehe yeye na wazazi wake kwa baraka ya wosia huu. Na yeyote ambaye hatauandika katika waja wa Mwenyezi Mungu, uso wake utakuwa mweusi duniani na Akhera. Na akasema: "Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu", mara tatu, "huu ni ukweli, na ikiwa mimi ni muongo, basi nitoke duniani nikiwa mimi si Muislamu. Na atakayeuamini, ataokoka na adhabu ya Moto. Na atakayeukanusha, atakuwa amekufuru."
Huu ndio muhtasari wa yale yaliyo katika wosia aliozuliwa uongo Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake. Na tumeshawahi kuusikia wosia huu wa uongo mara nyingi miaka mingi iliyopita, ukienezwa miongoni mwa watu mara kwa mara, na kusambazwa miongoni mwa watu wengi wa kawaida, na kuna tofauti katika maneno yake yenyewe. Na muongo wake anasema: Alimuona Mtume rehema na amani ziwe juu yake usingizini, kwa hivyo akambebesha wosia huu. Na katika chapa hii ya mwisho tuliyokutajia ewe msomaji, huyo mzushi alidai ndani yake kwamba alimuona Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alipokuwa anajitayarisha kulala, kwa hivyo maana yake ni kwamba alimuona akiwa macho!
Katika wasia huu, huyu mzushi alidai mambo mengi, ambayo ni uongo ulio wazi, na batili iliyo wazi mno. Nitakutanabahisha juu yake hivi karibuni katika neno hili, Mwenyezi Mungu akipenda. Na tayari nilikwisha tanabahisha juu yake katika miaka iliyopita, na nikawaelezea watu kwamba ni uongo ulio wazi, na batili iliyo wazi kabisa. Basi pindi niliposoma chapa hii ya mwisho, nilisita kuandika juu yake, kwa sababu ya kuonekana wazi kwa ubatili wake, na ujasiri mkubwa wa mzushi huyu kusema uongo, na sikudhani kwamba ubatili wake utamshawishi yeyote mwenye ufahamu hata mdogo tu, au maumbile sahihi ya kawaida. Hata hivyo, ndugu wengi waliniambia kwamba umesambazwa miongoni mwa watu wengi, na wanaupokezana na baadhi yao wakausadiki. Basi kwa sababu hii, niliona kwamba ni lazima juu ya watu kama mimi kuandika juu yake ili kuelezea ubatili wake, na kwamba umetungwa dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ili mtu yeyote asidanganyike nao. Na mwenye kuutafakari miongoni mwa wale wenye elimu na imani, au wenye maumbile sahihi na ya kawaida, na akili timamu, atajua kwamba ni uongo na uzushi kwa njia nyingi.
Na niliuliza baadhi ya jamaa wa Sheikh Ahmad, ambaye anahusishwa uzushi huu, kuhusu wosia huu, na wakanijibu kwamba ni uongo juu ya Sheikh Ahmad, na kwamba hata hakuusema. Sheikh Ahmad aliyetajwa hapo juu alikufa kitambo, na hata kama tutachukulia kwamba Sheikh Ahmad aliyetajwa hapo juu, au yeyote yule aliyemzidi umri, alidai kuwa amemuona Mtume rehema na amani ziwe juu yake akiwa usingizini au akiwa macho, na akamuusia wosia huu, tungejua kwa hakika kwamba yeye ni muongo, au aliyemwambia hayo ni shetani, si Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, kwa njia nyingi, miongoni mwake zikiwa ni:
Kwanza: Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, hamuonekanii mtu akiwa macho baada ya kufa kwake. Kwa hivyo, mwenye kudai miongoni mwa Masufi wajinga kwamba anaweza kumuona Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akiwa macho, au kwamba anahudhuria katika sherehe za kuzaliwa kwake, au mambo mfano wa hayo, basi amekosea kosa baya zaidi, akachanganyikiwa sana, akaingia katika kosa kubwa, na akahalifu Kitabu, Sunnah na makubaliano ya wanachuoni. Kwa sababu, wafu watatoka makaburini mwao Siku ya Kiyama tu, si katika dunia hii. Na yeyote atakayesema kinyume na hivi, basi huyo ni muongo uongo ulio wazi, au amekosea na amechanganyikiwa, hakuijua haki ambayo wema waliotangulia waliijua, na wakaifuata Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na wale waliokuja baada yao na wale walio wafuata kwa wema. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:
﴿ثُمَّ إِنَّكُم بَعۡدَ ذَٰلِكَ لَمَيِّتُونَ15 ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ تُبْعَثُونَ16﴾
"Kisha hakika nyinyi baada ya hayo mtakufa."
Kisha hakika nyinyi Siku ya Kiyama mtafufuliwa. [Al-Muminun: 15-16] Na alisema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie: "Mimi ndiye wa kwanza ambaye kaburi lake litafunguka siku ya Kiyama, na mimi ndiye muombezi wa kwanza na wa kwanza atakayekubaliwa uombezi wake." Na kuna hadithi nyingi zenye maana hii.
Pili: Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, hasemi chochote kinyume na haki, si wakati wa uhai wake wala baada ya kifo chake. Na wasia huu unapingana kwa uwazi na Sheria yake, na hilo ni kwa mambo mengi yatakayokuja. Lakini Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, anaweza kuonekana usingizini. Na mwenye kumuona katika usingizi kama alivyo katika muonekano wake wa heshima, basi amemuona; kwa sababu Shetani hawezi kuchukua sura yake, kama lilivyoelezwa hilo katika hadithi sahihi tukufu, lakini jambo kubwa hapa ni juu ya imani ya muonaji, ukweli wake, uadilifu wake, uelewa wake mzuri, dini yake na uaminifu wake, na je alimuona Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake katika sura yake au katika sura nyingine.
Kama kungekuwa na Hadithi kutoka kwa Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake ambayo aliisema maishani mwake, kupitia njia ya wasimulizi waaminifu, waadilifu, wenye uelewa mzuri, hiyo isingewezakutegemewa, na wala haingetumiwa kama hoja, au ikiwa ingekuja kupitia njia ya wasimulizi waaminifu, wenye uelewa mzuri lakini ikawa inapingana na simulizi ya yule ambaye aliihifadhi bora kuliko wao, na ikawa na ukiukaji mkubwa ambao haiwezekani kuunganisha baina ya simulizi hizi mbiili, basi moja yake angechukuliwa kwama ilifutiliwa mbali ambayo haiwezi kufanyiwa kazi, nayo ya pili inakuwa ndiyo iliyofuta na ambayo inafaa kufanyiwa kazi, ikiwa hilo linawezekana kwa masharti yake. Lakini kama haiwezekani kuunganisha wala hakuna moja iliyofutilia mbali nyingine, inakuwa ni lazima kutupilia mbali simulizi ya yule ambaye ana uwezo mdogo wa kuhifadhi, na uadilifu mchache, na inahukumiwa kwamba imekengeuka na haifanyiwi kazi.
Basi utakuwa vipi wasia usiojulikana aliyeusimulia kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na hata haujulikani uadilifu wake? Katika hali hii, ni haki zaidi kuutupilia mbali na kutouangalia, hata kama hauna kitu ndani yake kinachohalifu Sheria. Basi itakuwaje ikiwa wasia huo unajumuisha mambo mengi yanayoashiria ubatili wake, na kwamba amesingiziwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, na unajumuisha kutunga sheria ya dini ambayo Mwenyezi Mungu hakuiidhinisha?
Na alisema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Yeyote atakayesema juu yangu yale ambayo sikuyasema, basi na ajiandalie makazi yake Motoni." Na mzushi wa wasia huu alisema juu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, yale ambayo hakuyasema na akamdanganyishia uongo ulio wazi na hatari. Basi anafailia namna gani onyo hili kubwa la adhabu, na analistahiki namna gani; ikiwa hataharakisha kutubu, na kueneza kwa watu kwamba yaliyo katika wasia huu ni uongo dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake; kwa sababu yeyote anayeeneza batili miongoni mwa watu na kuuhusisha na dini; toba yake haitakuwa sahihi isipokuwa kwa kutangaza na kudhihirisha kinyume chake, ili watu wajue kwamba aliachana na uongo wake huo, na akabainisha kwamba yeye ni muongo, kwa mujibu wa maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّ ٱلَّذِينَ يَكۡتُمُونَ مَآ أَنزَلۡنَا مِنَ ٱلۡبَيِّنَٰتِ وَٱلۡهُدَىٰ مِنۢ بَعۡدِ مَا بَيَّنَّٰهُ لِلنَّاسِ فِي ٱلۡكِتَٰبِ أُوْلَٰٓئِكَ يَلۡعَنُهُمُ ٱللَّهُ وَيَلۡعَنُهُمُ ٱللَّٰعِنُونَ159 إِلَّا ٱلَّذِينَ تَابُواْ وَأَصۡلَحُواْ وَبَيَّنُواْ فَأُوْلَٰٓئِكَ أَتُوبُ عَلَيۡهِمۡ وَأَنَا ٱلتَّوَّابُ ٱلرَّحِيمُ160﴾
"Hakika wale wanaoficha tuliyoyateremsha, nazo ni hoja zilizo wazi na uongofu baada ya Sisi kuzibainisha kwa watu Kitabuni, hao anawalaani Mwenyezi Mungu, na wanawalaani kila wenye kulaani."
Isipokuwa wale waliotubu na wakatengeneza na wakabainisha, basi hao nitapokea toba yao, na Mimi ni Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu." [Al-Baqarah: 159, 160] Katika aya hii tukufu, Mwenyezi Mungu Mtukufu akaweka wazi kwamba yeyote anayeficha chochote katika haki, toba yake juu ya hilo haitakuwa sahihi isipokuwa baada ya kurekebisha na kubainisha. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu alisha wakamilishia waja wake dini, na akawatimizia neema kwa kumtuma Mtume wake Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na Mwenyezi Mungu akamfunulia sheria kamili, na wala hakumfisha isipokuwa baada ya kuikamilisha na kuibainisha, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...ٱلۡيَوۡمَ أَكۡمَلۡتُ لَكُمۡ دِينَكُمۡ وَأَتۡمَمۡتُ عَلَيۡكُمۡ نِعۡمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ ٱلۡإِسۡلَٰمَ دِينٗا...﴾
"Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini." [Al-Maidah: 3]
Na yule aliyeuzua wosia huu alikuja katika karne ya kumi na nne, akitaka kuwavisha watu dini mpya, ambayo mwenye kuifuata sheria yake ndiye atakayeingia Peponi, na kunyimwa Pepo na kuingia Motoni kwa yule ambaye hatafuata sheria yake. Anataka kuufanya wosia huu aliouzua kuwa mkubwa na bora kuliko Qur'ani, ambapo alizua ndani yake kwamba: Yeyote atakayeuandika na kuutuma kutoka nchi hadi nchi, au kutoka mahali hadi mahali, atajengewa kasri Peponi. Na yeyote ambaye hatauandika na kuutuma, atanyimwa uombezi wa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, Siku ya Kiyama. Hilo ni katika uongo mbaya zaidi, na miongoni mwa dalili za wazi kabisa za uongo wa wosia huu, na uchache wa staha ya yule alieyuzua, na ukubwa wa ujasiri wake katika kusema uongo; kwa sababu mwenye kuandika Qur'ani Tukufu na kuituma kutoka nchi moja hadi nyingine, au kutoka sehemu moja hadi sehemu nyingine, hawezi kupata ubora huu ikiwa hataifanyia kazi Qur'ani Tukufu. Kwa hivyo anawezaje kumpata hilo mwandishi wa uzushi huu na mwenezaji wake kutoka nchi moja hadi nchi nyingine? Na asiyeiandika Qur'ani na kuituma kutoka nchi moja hadi nchi nyingine, hawezi kunyimwa uombezi wa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ikiwa ni Mumini anayefuata sheria yake. Uzushi huu mmoja katika wosia huu unatosha kuonyesha ubatili wake, uongo wa mchapishaji wake, upuuzi wake, na upumbavu wake, na umbali wake na suala la kujua yale aliyokuja nayo Mtume rehema na amani ziwe juu yake ya uongofu.
Na katika wasia huu, isipokuwa yale yaliyotajwa, kuna mambo mengine, ambayo yote yanaonyesha ubatili wake na uongo wake, hata kama mzushi wake ataapa viapo elfu moja au zaidi kwamba ni sahihi, na hata kama atadai kwamba atapata adhabu kubwa zaidi na mateso makali zaidi ili kuonyesha kwamba yeye ni mkweli, hawezi kuwa mkweli wala wasia huo hauwezi kuwa sahihi. Bali huo -ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, tena ninaapa kwa Mwenyezi Mungu- ni katika batili kubwa na mbaya zaidi. Nasi tunamshuhudisha Mwenyezi Mungu aliyetakasika na waliotuhudhuria miongoni mwa Malaika, na yeyote atakayeliona andiko hili miongoni mwa Waislamu -basi ni ushahidi ambao tutakutana nao mbele ya Mola wetu Mezi Mtukufu- kwamba wosia huu ni uongo na uzushi dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, Mwenyezi Mungu amfedheheshe huyu aliyeuzua na amtendee kile anachostahili.
Na kuna mambo mengi kando na haya tuliyotaja ambayo yanaonyesha uongo wa wasia huu na ubatili wake, ikiwa ni pamoja na:
Jambo la kwanza: Kauli yake ndani yake: "Kwa sababu kuanzia Ijumaa hadi Ijumaa, wamekufa watu laki moja na sitini si katika dini ya Kiislamu." Kwa sababu hili ni katika elimu ya ghaibu, na wahyi ulikatwa kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, baada ya kufa kwake, na tena hata katika uhai wake alikuwa hajui ghaibu, basi itakuwa vipi baada ya kufa kwake? Kama alivyosema Mwenyezi Mungu aliyetakasika:
﴿قُل لَّآ أَقُولُ لَكُمۡ عِندِي خَزَآئِنُ ٱللَّهِ وَلَآ أَعۡلَمُ ٱلۡغَيۡبَ...﴾
"Sema: Mimi sikwambiini kuwa ninazo hazina za Mwenyezi Mungu. Wala sijui mambo yaliyofichikana." [Al-An'am: 50] Na kauli yake Mtukufu:
﴿قُل لَّا يَعۡلَمُ مَن فِي ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضِ ٱلۡغَيۡبَ إِلَّا ٱللَّهُ...﴾
"Sema: Hapana katika mbingu na ardhi ajuaye ya ghaibu isipokuwa Mwenyezi Mungu." [An-Naml: 65] Na katika Hadithi sahihi kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: “Watu fulani watafukuzwa kwenye hodhi langu Siku ya Kiyama, kwa hivyo nitasema: 'Ewe Mola Mlezi! Ni Maswahaba wangu, ni Maswahaba wangu.' Nataambiwa: 'Hakika wewe hujui walichokizua baada yako.' Kwa hivyo, nitasema kama alivyosema mja mwema: "Na mimi nilikuwa shahidi juu yao nilipokuwa nao. Na uliponifisha, ukawa Wewe ndiye Mwangalizi juu yao. Na Wewe ni shahidi juu ya kila kitu." [Al-Ma'idah: 117].
Jambo la pili: Miongoni mwa mambo yanayoashiria ubatili wa wasia huu na kwamba ni uongo, ni kusema kwake ndani yake: "Atakayeuandika na alikuwa masikini, Mwenyezi Mungu atamtajirisha, au alikuwa na deni, Mwenyezi Mungu atamlipia deni lake, au alikuwa na dhambi, Mwenyezi Mungu atamsamehe yeye na wazazi wake kwa baraka ya wasia huu." hadi mwisho wake. Hili ni katika uongo mkubwa zaidi, na ushahidi wa wazi kabisa wa uongo wa mzushi wake, na uchache wa staha yake mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya waja wake. Kwa sababu mambo haya matatu hayatokei tu kwa kuandika Qur'ani Tukufu, kwa hivyo yanawezaje kutokea kwa mwenye kuandika wasia huu batili! Badala yake, mtu huyu muovu anataka kuwachanganya watu, na kuwafungamanisha na wosia huu, ili wauandike na wafungamane na fadhila hii inayodaiwa, na waache visababu ambavyo Mwenyezi Mungu aliwawekea waja wake katika sheria, na akavifanya kuwa njia ya kuwafikisha katika utajiri na kulipa madeni, na kupata msamaha wa dhambi. Basi tunajikinga kwa Mwenyezi Mungu kutokana na sababu za kuachiliwa mbali (na Mwenyezi Mungu) na kutii matamanio na Shetani.
Jambo la tatu: Katika mambo ambayo yanaonyesha ubatili wa wasia huo, ni kusema kwake ndani yake: "Na yeyote asiyeuandika katika waja wa Mwenyezi Mungu, uso wake utakuwa mweusi katika dunia hii na Akhera." Hili pia ni katika uongo mbaya zaidi, na katika ushahidi wa wazi kabisa wa ubatili wa wosia huo, na uongo wa mzushi wake. Inaruhusiwa vipi katika akili timamu ya mtu kuandika wosia huu uliotoka kwa mtu asiyejulikana katika karne ya kumi na nne, akiuzua dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake akidai kwamba yeyote asiyeuandika, uso wake utakuwa mweusi katika dunia hii na Akhera. Na yeyote atakayeuandika, atakuwa tajiri baada ya kuwa masikini, na atasalimika kutokana na deni baada ya kuwa na madeni mengi, na atasamehewa madhambi aliyotenda!!
Utakatifu ni wako (Mwenyezi Mungu)! Huu ni uzushi mkubwa!! Na hakika ushahidi na hali halisi vinashuhudia uongo wa mzushi huyu, na ukubwa wa ujasiri wake dhidi ya Mwenyezi Mungu, na uchache staha yake mbele ya Mwenyezu Mungu na mbele ya watu. Kwani kuna watu wengi sana ambao hawakuuandika, na nyuso zao hazikuwa nyeusi. Na kuna umati mkubwa wa watu ambao hakuna anayeweza kuwahesabu isipokuwa Mwenyezi Mungu tu waliuandika mara nyingi, lakini madeni yao hayakulipwa, na umaskini wao haukuisha. Kwa hivyo tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na ukengeufu wa mioyo na kutu ya madhambi. Sifa hizi na malipo haya (aliyoandika) hayakuja katika Sheria tukufu kwa mwenye kuandika kitabu bora na kitukufu zaidi ambacho ni Qur'ani Tukufu. Basi atayapataje mwenye kuandika wosia unaojumuisha aina mbalimbali za batili, na sentensi nyingi za aina za ukafiri. Mwenyezi Mungu ametakasika! Ni mstahamilivu namna gani kwa mwenye kumfanyia ujasiri wa kumzulia uongo!
Jambo la nne: Katika mambo ambayo yanaonyesha kwamba wasia huu ni batili kubwa zaidi na uongo ulio wazi zaidi ni kauli yake ndani yake: "Na yeyote atakaye uamini, ataokoka na adhabu ya Moto. Na yeyote atakayeukanusha, atakuwa amekufuru." Hili pia ni katika kufanya ujasiri sana katika kusema uongo, na ni katika batili mbaya zaidi. Mzushi huyu anawaita watu wote kuamini uzushi wake, na anadai kwamba kwa kufanya hivyo, wataepukana na adhabu ya Moto, na kwamba yeyote atakayeukanusha, atakuwa amekufuru. Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, hakika muongo huyu amemsingizia Mwenyezi Mungu vikubwa sana, na ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba alisema jambo ambalo si la kweli. Kwa sababu mwenye kuusadiki, yeye ndiye anayestahiki kuwa kafiri si mwenye kuu kadhibisha. Kwa sababu ni uzushi, batili na uongo usio na msingi sahihi. Tunamshuhudisha Mwenyezi Mungu kwamba ni uongo, na kwamba mzushi wake ni muongo ambaye anataka kuwawekea watu sheria ya yale ambayo Mwenyezi Mungu hakuyaruhusu, na kuingiza katika dini yao yale yasiyo ndani yake ilhali Mwenyezi Mungu ameshaukamilishilia umma huu dini kabla ya uzushi huu kwa karne kumi na nne. Basi kuweni macho enyi wasomaji na ndugu zangu, na jihadharini na kuamini mfano wa uzushi huu, na kuueneza baina yenu. Kwani haki ina nuru juu yake isiyomchanganya mwenye kuitafuta. Kwa hivyo, itafuteni haki kwa ushahidi wake, na waulizeni wenye elimu juu ya yale yenye kuwatatiza, wala msidanganyike na viapo vya waongo. Kwani Ibilisi aliyelaaniwa aliwaapia wazazi wenu wawili Adam na Hawa kwamba anawapa nasaha ya kweli, ihali yeye ndiye haini mkubwa zaidi na muongo wa waongo, kama alivyosimulia hilo Mwenyezi Mungu Mtukufu. Akasema Yeye aliyetakasika na kutukuka:
﴿وَقَاسَمَهُمَآ إِنِّي لَكُمَا لَمِنَ ٱلنَّٰصِحِينَ21﴾
"Naye akawaapia: Kwa yakini mimi ni miongoni wa wanaowashauri". [Al-A'raf: 21]
Basi jihadharini naye, na jihadharini na wafuasi wake miongoni mwa wazushi. Kwani wana viapo vingapi vya uongo, ahadi wanazohaini, na maneno yaliyopambwa ya kudanganya na kupotosha! Ama alichotaja mzushi huyu kuhusu kuibuka maovu. Hilo ni ukweli, na Qur’ani Tukufu na Sunna safi zimeonya dhidi yake vikali sana, na ndani yake kuna uongofu na utoshelevu.
Ama kuhusu yale yaliyotajwa kuhusu alama za Kiyama, Hadithi mbalimbali za kinabii zilishabainisha alama za Kiyama zitakazokuwa, na Qur’ani Tukufu pia ikaashiria baadhi yake . Kwa hivyo, anayetaka kuzijua, atazikuta katika mahali pake katika vitabu vya Sunna na maandiko ya watu wa elimu na imani. Watu hawana haja ya kuelezewa na mzushi kama huyo, kuwachanganya kwake na kuingiza kwake haki ndani ya uongo. Mwenyezi Mungu anilinde mimi, nyinyi na Waislamu wote kutokana na shari za mashetani, majaribu ya wapotoshaji, kukengeuka kwa waliokengeuka na kuchanganya kwa maadui wa Mwenyezi Mungu, wana batili wanaotaka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao na kuwachanganya watu kuhusiana na dini yao. Na Mwenyezi Mungu ataikamilisha nuru yake na kuinusuru dini yake, hata kama watachukia maadui wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa mashetani na wafuasi wao katika makafiri na wakataajimungu (wapagani).
Na tunamuomba Mwenyezi Mungu aziboreshe hali za Waislamu, na awaneemeshe kuifuata haki, kukaa imara juu yake na kutubia kwa Mwenyezi Mungu aliyetakasika kutokana na madhambi yote. Kwani Yeye ndiye Mwenye kupokea toba, Mwingi wa kurehemu na Muweza wa kila kitu. Mwenyezi Mungu ndiye anaye tutosha, naye ndiye Mtegemewa bora. Na hakuna uwezo wala nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu, aliye juu, Mkuu.
Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa viumbe vyote, na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wake na Mtume wake mkweli na mwaminifu, na juu ya familia yake, Maswahaba wake na wote wanaomfuata kwa wema mpaka Siku ya Malipo.
***