نُبذَةٌ فِي العَقِيدَةِ الإِسْلَامِيَّة (شَرْحُ أُصُولِ الإِيمَانِ)
Dondoo kuhusu Itikadi ya Kiislamu
بِقَلَم فَضِيلَة الشَّيخ العَلَّامَة
مُحَمَّدِ بْنِ صَالِحٍ العُثَيمِين
غَفَرَ اللَّهُ لَهُ وَلِوَالِدَيْهِ وَلِلْمُسْلِمِين
Mwanachuoni
Muhammad Bin Swaleh Al-Uthaymeen
Mwenyezi Mungu amsamehe yeye, wazazi wake, na Waislamu wote.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu
Utangulizi
Hakika kila sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, tuna mhimidi na tunamtaka msaada, na tunamuomba msamaha na kutubia kwake. Na tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na shari za nafsi zetu na matendo yetu mabaya. Mwenye kuongozwa na Mwenyezi Mungu hakuna wa kumpoteza, na mwenye kupotezwa na Mwenyezi Mungu hakuna wa kumuongoza. Na nina shuhudia kuwa hapana mungu apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu peke yake, hana mshirika. Na ninashuhudia kuwa Muhammad ni mja wake na Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na juu ya aali zake, na Maswahaba zake, na wote wanaowafuata kwa wema.
Ama baada ya hayo: "Elimu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu" ndiyo elimu tukufu zaidi, na kuu zaidi kwa hadhi, na yenye wajibu mkubwa zaidi kutafutwa; kwa sababu ni elimu ya kumfahamu Mwenyezi Mungu Mtukufu, na majina yake, na sifa zake, na haki zake juu ya waja wake; na kwa sababu ndiyo ufunguo wa njia ya kumfikia Mwenyezi Mungu Mtukufu, na msingi wa Sheria zake.
Na kwa hiyo, Mitume wote walikubaliana kwa kauli moja juu ya kuwaita watu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَمَآ أَرۡسَلۡنَا مِن قَبۡلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِيٓ إِلَيۡهِ أَنَّهُۥ لَآ إِلَٰهَ إِلَّآ أَنَا۠ فَٱعۡبُدُونِ 25﴾
"Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipokuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu." [Al-Anbiyaa: 25].
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akajishuhudia Mwenyewe juu ya Upweke wake, na Malaika wake na watu wenye elimu wakashuhudia hilo kwa ajili yake. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿شَهِدَ ٱللَّهُ أَنَّهُۥ لَآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ وَٱلۡمَلَٰٓئِكَةُ وَأُوْلُواْ ٱلۡعِلۡمِ قَآئِمَۢا بِٱلۡقِسۡطِۚ لَآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ٱلۡعَزِيزُ ٱلۡحَكِيمُ 18﴾
"Mwenyezi Mungu, na Malaika, na wenye elimu, wameshuhudia kuwa hakika hapana mungu ila Yeye, ndiye Mwenye kusimamisha uadilifu; hapana mungu ila Yeye Mwenye nguvu na Mwenye hekima." [Al Imran: 18].
Na kwa kuwa jambo la Tauhidi lipo namna hii, imekuwa ni lazima kwa kila Muislamu alichukulie uzito kwa kujifunza, kufundisha, kulitafakari na kuliitakidi; ili ajenge dini yake juu ya msingi ulio salama, na kwa utulivu na kunyenyekea; ili afurahie matunda yake na matokeo yake.
Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kufanikisha.
Mtunzi
Dini ya Uislamu
Dini ya Uislamu ndiyo dini ambayo Mwenyezi Mungu alimtuma nayo Mtume wake Muhammad -rehema na amani ziwe juu yake-, na akazihitimisha nayo dini zote, na ameukamilisha kwa waja wake, na akawatimizia neema yake kwa hiyo, na akairidhia kuwa dini yao. Basi haikubaliwi mbele ya Mwenyezi Mungu kwa yeyote dini isiyokuwa hiyo. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَآ أَحَدٖ مِّن رِّجَالِكُمۡ وَلَٰكِن رَّسُولَ ٱللَّهِ وَخَاتَمَ ٱلنَّبِيِّـۧنَۗ وَكَانَ ٱللَّهُ بِكُلِّ شَيۡءٍ عَلِيمٗا 40﴾
"Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua zaidi kila kitu." [Al-Ahzaab: 40].
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...ٱلۡيَوۡمَ أَكۡمَلۡتُ لَكُمۡ دِينَكُمۡ وَأَتۡمَمۡتُ عَلَيۡكُمۡ نِعۡمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ ٱلۡإِسۡلَٰمَ دِينٗاۚ...﴾
"Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimeku timizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini yenu." [Al-Maidah: 3].
Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّ ٱلدِّينَ عِندَ ٱللَّهِ ٱلۡإِسۡلَٰمُ...﴾
"Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu..." [Al-Imran: 19].
Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَمَن يَبۡتَغِ غَيۡرَ ٱلۡإِسۡلَٰمِ دِينٗا فَلَن يُقۡبَلَ مِنۡهُ وَهُوَ فِي ٱلۡأٓخِرَةِ مِنَ ٱلۡخَٰسِرِينَ 85﴾
"Na anayetafuta Dini isiyokuwa Uislamu, haita kubaliwa kutoka kwake. Naye Akhera atakuwa miongoni mwa wenye kupata hasara." [Al-Imran: 85].
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amewajibisha juu ya watu wote waifuate dini hii kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kisha akamwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani zimfikie, akasema:
﴿قُلۡ يَٰٓأَيُّهَا ٱلنَّاسُ إِنِّي رَسُولُ ٱللَّهِ إِلَيۡكُمۡ جَمِيعًا ٱلَّذِي لَهُۥ مُلۡكُ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضِۖ لَآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ يُحۡيِۦ وَيُمِيتُۖ فَـَٔامِنُواْ بِٱللَّهِ وَرَسُولِهِ ٱلنَّبِيِّ ٱلۡأُمِّيِّ ٱلَّذِي يُؤۡمِنُ بِٱللَّهِ وَكَلِمَٰتِهِۦ وَٱتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمۡ تَهۡتَدُونَ 158﴾
"Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume kwenu nyinyi nyote, niliyetumwa na Mwenyezi Mungu, Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Hapana mungu ila Yeye anayehuisha na anayefisha. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Nabii asiyejua kusoma na kuandika, ambaye anamuamini Mwenyezi Mungu na maneno yake. Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka." [Al-A'araf: 158].
Na ilisimuliwa katika Sahihi Muslim, kutoka kwa Abuu Huraira, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba alisema: "Ninaapa kwa yule ambaye nafsi ya Muhammadi iko mkononi mwake, hatosikia yeyote kuhusu mimi katika umma huu, Myahudi wala Mkristo, kisha akafa hali ya kuwa hajayaamini yale niliyotumwa nayo, isipokuwa atakuwa ni katika watu wa Motoni."1
Na kumuamini ni: Kukiri yale aliyokuja nayo pamoja na kuyakubali na kusalimu amri, si kukiri tu; na kwa sababu hiyo Abuu Twalib hakuwa mwenye kumuamini Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- licha ya kukiri kwake yale aliyokuja nayo, na kushuhudia kwake kwamba dini aliyoileta ni miongoni mwa dini bora.
Na Dini ya Uislamu inajumuisha masilahi yote yaliyo bebwa na dini zilizotangulia, na imejitofautisha nazo kwa kuwa yenye kufaa katika kila zama na mahala na umma. Amesema Mtukufu akimueleza Mtume wake:
﴿وَأَنزَلۡنَآ إِلَيۡكَ ٱلۡكِتَٰبَ بِٱلۡحَقِّ مُصَدِّقٗا لِّمَا بَيۡنَ يَدَيۡهِ مِنَ ٱلۡكِتَٰبِ وَمُهَيۡمِنًا عَلَيۡهِ...﴾
"Na tumekuteremshia wewe, kwa haki, Kitabu hiki kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda..." [Al-Maaidah: 48].
Na maana ya kuwa Dini hii inafaa kwa kila zama, na sehemu, na Umma ni kwamba kushikamana nayo haku pingani na masilahi ya Umma katika zama zozote au sehemu yoyote, bali kwa hiyo ndiko kutengemaa kwake. Wala maana ya hilo si kwamba inasalimu amri kwa mfumo wa kila zama na sehemu na Umma, kama wanavyotaka baadhi ya watu.
Na Dini ya Uislamu ndiyo Dini ya kweli ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu amemhakikishia yeyote atakayeshikamana nayo kikamilifu kuwa atamnusuru, na ataidhihirisha juu ya dini nyingine zote. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿هُوَ ٱلَّذِيٓ أَرۡسَلَ رَسُولَهُۥ بِٱلۡهُدَىٰ وَدِينِ ٱلۡحَقِّ لِيُظۡهِرَهُۥ عَلَى ٱلدِّينِ كُلِّهِۦ وَلَوۡ كَرِهَ ٱلۡمُشۡرِكُونَ 9﴾
"Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na Dini ya Haki ipate kushinda dini zote, ijapokuwa washirikina watachukia." [As-Swaffu: 9].
Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَعَدَ ٱللَّهُ ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ مِنكُمۡ وَعَمِلُواْ ٱلصَّٰلِحَٰتِ لَيَسۡتَخۡلِفَنَّهُمۡ فِي ٱلۡأَرۡضِ كَمَا ٱسۡتَخۡلَفَ ٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِهِمۡ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمۡ دِينَهُمُ ٱلَّذِي ٱرۡتَضَىٰ لَهُمۡ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّنۢ بَعۡدِ خَوۡفِهِمۡ أَمۡنٗاۚ يَعۡبُدُونَنِي لَا يُشۡرِكُونَ بِي شَيۡـٔٗاۚ وَمَن كَفَرَ بَعۡدَ ذَٰلِكَ فَأُوْلَٰٓئِكَ هُمُ ٱلۡفَٰسِقُونَ 55﴾
"Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba hakika atawafanya mahalifa katika ardhi kama alivyo wafanya mahalifa wale wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyowapendelea, na atawa badilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wana niabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na watakaokufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu." [An-Nur: 55].
Uislamu ni itikadi na sheria. Kwa hivyo, umekamilika katika itikadi yake na sheria zake.
1- Unaamrisha kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mtukufu na unakataza ushirikina.
2- Unaamrisha ukweli na unakataza uongo.
3- Unaamrisha uadilifu na unakataza dhuluma. Na uadilifu ni kusawazisha baina ya vinavyofanana na kutofautisha baina ya vinavyotofautiana. Wala uadilifu si usawa wa jumla bila uainishaji kama wasemavyo baadhi ya watu wanaposema: "Uislamu ni dini ya usawa," wakalitoa neno hilo kwa upana wake; kwani kusawazisha yaliyotofautiana ni dhuluma ambayo Uislamu haukuja nayo, wala hasifiwi anayelitenda.
4- Unaamrisha kutekeleza amana na kukataza hiyana:
5- Unaamrisha kutekeleza makubaliano na kukataza usaliti.
6- Huamrisha kuwatendea wema wazazi wawili, na hukataza kuwaasi wazazi wawili.
7- Huamrisha kuunga udugu, nao ni wale wa karibu katika ukoo, na unakataza kukata udugu.
8- Unaamrisha ujirani mwema, na unakataza ujirani mbaya.
Kwa ujumla, Uislamu unaamrisha kila tabia njema, na unakataza kila tabia mbaya. Na unaamrisha kila tendo jema na unakataza kila tendo baya.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّ ٱللَّهَ يَأۡمُرُ بِٱلۡعَدۡلِ وَٱلۡإِحۡسَٰنِ وَإِيتَآيِٕ ذِي ٱلۡقُرۡبَىٰ وَيَنۡهَىٰ عَنِ ٱلۡفَحۡشَآءِ وَٱلۡمُنكَرِ وَٱلۡبَغۡيِۚ يَعِظُكُمۡ لَعَلَّكُمۡ تَذَكَّرُونَ 90﴾
"Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhuluma. Anakupeni mawaidha ili mpate kukumbuka." [An-Nahli: 90].
Nguzo za Uislamu
Nguzo za Uislamu ndiyo misingi yake ambayo ume jengwa juu yake, nazo ni tano: Imetajwa katika yale aliyoyasimulia bin Omari -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake yeye na baba yake- kutoka kwa Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- kwamba amesema: "Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano: juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu -na katika riwaya nyingine: Juu ya tano-: Kushuhudia kwamba hapana mungu apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu, na kwamba Muhammad ni Mja wake na Mtume wake, na kusimamisha Swala, na kutoa Zaka, na kufunga Ramadhani, na kufanya Hija." Mwanamume mmoja akasema: Je, Hija, na swaumu ya Ramadhani? Akasema: Hapana, kufunga Ramadhani na kufanya Hija. Hivi ndivyo nilivyosikia kauli hii kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe juu yake.2
1- Ama shahada ya kuwa hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na kuwa Muhammadi, rehema na amani ziwe juu yake, ni mja wake na Mtume wake, basi ni itikadi ya yakini thabiti inayoelezwa kwa ulimi kwa kutamka shahada hii, kana kwamba kwa uthabiti wa yakini yake katika hilo analiona kwa macho. Na shahada hii imefanywa kuwa nguzo moja ijapokuwa yaliyoshuhudiwa ni mawili:
Ama kwa kuwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, anafikisha ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, basi kumshuhudia kuwa ni mja wa Mwenyezi Mungu na ni Mtume wake ni miongoni mwa ukamilifu wa shahada ya kwamba hapana mungu anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu.
Au kwa sababu shahada mbili hizi ndizo msingi wa usahihi wa matendo na kukubalika kwake; kwani hakuna usahihi wa matendo wala kukubalika kwake, ila kwa ikhlasi (utakasifu) kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumfuata Mtume wake, rehema na amani zimshukie.
Basi kwa ikhlasi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, inathibitika shahada ya kwamba hapana mungu apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu; na kwa kumfuata Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, inathibitika shahada ya kwamba Muhammad ni Mja wake na Mjumbe wake.
Na miongoni mwa matunda ya ushuhuda huu mkubwa ni: Kuweka huru moyo na nafsi kutokana na utumwa kwa viumbe, na kuacha kuwafuata wasiokuwa Mitume wa Mwenyezi Mungu.
2- Na ama kusimamisha swala: Ni kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kuitekeleza kwa namna ya unyoofu na ukamilifu katika nyakati zake zilizowekwa, na kwa taratibu na miundo yake.
Na miongoni mwa matunda yake ni kukunjuka kwa moyo, tulizo la jicho, na kukataza uchafu na maovu.
3- Kutoa zaka: Nayo ni ibada ya mali kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutoa kiwango cha wajibu katika mali zinazostahiki kutozwa zaka.
Na miongoni mwa matunda yake ni kuisafisha na kuitakasa nafsi kutokana na tabia mbovu ya ubahili, na kukidhi mahitaji ya Uislamu na Waislamu.
4- Ama kuhusu kufunga mwezi wa Ramadhani, hilo ni kumuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kujizuia mbali na mambo yenye kufunguza katika mchana wa Ramadhani.
Na miongoni mwa matunda yake ni kuizoesha nafsi kuacha yale yanayopendwa; kwa kutafuta radhi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
5- Kuhiji Nyumba: Nako ni kumuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kuiendea Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu; kwa ajili ya kutekeleza ibada za Hija.
Na miongoni mwa matunda yake ni: Kuizoeza nafsi kutoa mali na nguvu ya mwili katika kutekeleza utiifu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu; na kwa sababu hii, Hija ni aina ya Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Na matunda haya tuliyoyataja kuhusu misingi hii, na yale ambayo hatukuyataja, hufanya umma kuwa umma wa Kiislamu msafi uliotakasika, unaomuabudu Mwenyezi Mungu kwa dini ya haki, na kuwatendea haki viumbe kwa uadilifu na ukweli; Kwa sababu mengineyo miongoni mwa sheria za Uislamu hutengemaa kwa kutengemaa kwa misingi hii, na hali za Umma hutengemaa kwa kutengemaa kwa dini yake, na hukosa katika kutengemaa kwa hali zake kwa kiasi ilivyokosa katika kutengemaa kwa dini yake.
Na anayetaka kupata ubainifu wa hilo, basi na asome kauli yake aliyetukuka:
﴿وَلَوۡ أَنَّ أَهۡلَ ٱلۡقُرَىٰٓ ءَامَنُواْ وَٱتَّقَوۡاْ لَفَتَحۡنَا عَلَيۡهِم بَرَكَٰتٖ مِّنَ ٱلسَّمَآءِ وَٱلۡأَرۡضِ وَلَٰكِن كَذَّبُواْ فَأَخَذۡنَٰهُم بِمَا كَانُواْ يَكۡسِبُونَ 96 أَفَأَمِنَ أَهۡلُ ٱلۡقُرَىٰٓ أَن يَأۡتِيَهُم بَأۡسُنَا بَيَٰتٗا وَهُمۡ نَآئِمُونَ 97 أَوَأَمِنَ أَهۡلُ ٱلۡقُرَىٰٓ أَن يَأۡتِيَهُم بَأۡسُنَا ضُحٗى وَهُمۡ يَلۡعَبُونَ 98 أَفَأَمِنُواْ مَكۡرَ ٱللَّهِۚ فَلَا يَأۡمَنُ مَكۡرَ ٱللَّهِ إِلَّا ٱلۡقَوۡمُ ٱلۡخَٰسِرُونَ 99﴾
"Na lau kuwa watu wa miji wangeliamini na wakamcha Mungu, kwa yakini tungeliwafungulia baraka kutoka mbinguni na katika ardhi. Lakini walikanusha, basi tukawapatiliza kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.
Je, watu wa mijini wana amani ya kuwa adhabu yetu haitawafika usiku, nao wamelala?
Au watu wa mijini wana amani ya kuwa adhabu yetu haitawafika mchana, nao wanacheza?
Je, wana amani dhidi mipango mibaya ya Mwenyezi Mungu? Kwani hawawi na amani dhidi ya mipango mibaya ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye kupata hasara." [Al-A'araf: 96-99].
Na atazame katika historia ya waliomtangulia; hakika historia ni mazingatio kwa wenye akili kamilifu, na ni yenye kufungua macho kwa yule ambaye moyo wake haukuzuiliwa na pazia lolote, na Mwenyezi Mungu ndiye wa kuombwa msaada.
Misingi ya itikadi ya Kiislamu
Dini ya Uislamu - kama tulivyotangulia kufafanua - ni itikadi na sheria; na tumegusia baadhi ya sheria zake, na tumezitaja nguzo zake ambazo huchukuliwa kuwa misingi ya sheria zake.
Ama itikadi ya Kiislamu, misingi yake ni: Kumuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Mwisho, na kuamini Kadari kheri yake na shari yake.
Na misingi hii imebainishwa na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake, rehma na amani ziwe juu yake.
Basi katika Qur'ani tukufu amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿لَّيۡسَ ٱلۡبِرَّ أَن تُوَلُّواْ وُجُوهَكُمۡ قِبَلَ ٱلۡمَشۡرِقِ وَٱلۡمَغۡرِبِ وَلَٰكِنَّ ٱلۡبِرَّ مَنۡ ءَامَنَ بِٱللَّهِ وَٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِ وَٱلۡمَلَٰٓئِكَةِ وَٱلۡكِتَٰبِ وَٱلنَّبِيِّـۧنَ...﴾
"Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii..." [Al-Baqara: 177] Na akasema katika Kadari (Mipango ya Mwenyezi Mungu):
﴿إِنَّا كُلَّ شَيۡءٍ خَلَقۡنَٰهُ بِقَدَرٖ 49 وَمَآ أَمۡرُنَآ إِلَّا وَٰحِدَةٞ كَلَمۡحِۭ بِٱلۡبَصَرِ 50﴾
"Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo.
Na amri yetu haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa jicho." [Al-Qamar: 49-50].
Na katika Sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, amesema Mtume rehema na amani ziwe juu yake akimjibu Jibril alipomuuliza kuhusu imani: "Imani: Ni kumuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Mwisho, na kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu, ya kheri yake na ya shari yake."3
Kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu
Ama kumuamini Mwenyezi Mungu, hilo linajumuisha mambo manne:
Jambo la kwanza: Kuamini kuwepo kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Na vinavyoonyesha kuwepo kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni: Maumbile, akili, sheria, na hisia.
Ama ushahidi wa maumbile juu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu ni kwamba kila kiumbe kimeumbwa kwa maumbile ya kuamini Muumbaji wake bila kutanguliwa na kufikiri wala kufundishwa, wala hatenguki na yanayomlazimisha maumbile haya isipokuwa yule ambaye moyo wake umeathiriwa na jambo linalomgeuza kutoka kwayo; Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Hakuna mtoto yeyote anayezaliwa isipokuwa anazaliwa katika maumbile ya asili, kisha wazazi wake wanamfanya kuwa Myahudi au Mkristo au Mmajusi."4
2- Na ama ushahidi wa kiakili juu ya kuwepo kwa Mwenyezi Mungu aliyetukuka ni kwamba viumbe hivi, vilivyotangulia na vilivyofuatia, ni lazima viwe na muumbaji aliyevileta kuwapo; kwani haviwezi kujileta vyenyewe, wala haiwezekani viwepo kwa bahati nasibu.
Haiwezekani kitu kujileta chenyewe; kwani kitu hakiwezi kujiumba chenyewe; kwa kuwa kabla ya kuwepo kwake kilikuwa hakipo, basi inawezekanaje kiwe Muumbaji?!
Wala haiwezekani kuwepo jambo la ghafla; kwa sababu kila chenye kuzuka ni lazima kiwe na mletaji. Na kwa kuwa kuwepo kwa viumbe hivi juu ya mfumo huu wa ajabu, na ulinganifu uliopatana, na uhusiano ulioshikamana kati ya sababu na visababishi vyake, na kati ya viumbe wenyewe kwa wenyewe, kunakata kabisa uwezekano wa kuwa kuwepo kwao ni kwa bahati nasibu; kwani kilichopatikana kwa bahati nasibu hakina mfumo katika asili ya kuwepo kwake, basi kinawezaje kuwa na mpangilio madhubuti wakati wa kubakia kwake na maendeleo yake?!
Na iwapo haiwezekani viumbe hivi kujileta vyenyewe, wala kuwepo kwa kuzuka; hapo imebainika kuwa lazima viwe na mletaji, naye ni Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu.
Na ametaja Mwenyezi Mungu Mtukufu ushahidi huu wa kiakili na hoja thabiti ya yakini katika Suratu-Tuur; nayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿أَمۡ خُلِقُواْ مِنۡ غَيۡرِ شَيۡءٍ أَمۡ هُمُ ٱلۡخَٰلِقُونَ 35﴾
"Au wao wameumbwa pasipo kuumbwa na kitu chochote, au ni wao ndio waumbaji?" [Attur: 35]. Yaani, hawakuumbwa bila kuwako mwenye kuwaumba na kuwapatisha, wala wao hawakujiumba wenyewe; na kwa hivyo, inalazimika kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliyewaumba. Na kwa sababu hii, aliposikia Jubairi bin Mutwim -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- akisoma surat Tur, alipofikia aya hizi:
﴿أَمۡ خُلِقُواْ مِنۡ غَيۡرِ شَيۡءٍ أَمۡ هُمُ ٱلۡخَٰلِقُونَ 35 أَمۡ خَلَقُواْ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَۚ بَل لَّا يُوقِنُونَ 36 أَمۡ عِندَهُمۡ خَزَآئِنُ رَبِّكَ أَمۡ هُمُ ٱلۡمُصَۜيۡطِرُونَ 37﴾
"Au wao wameumbwa pasipo kuumbwa na kitu chochote, au ni wao ndio waumbaji?
Au wao wameziumba mbingu na ardhi? Bali hawana na yakini.
Au wanazo hazina za Mola wako Mlezi au wao ndio wenye madaraka?" [Attur: 35-37].
Na Jubairi siku hiyo alikuwa mshirikina, akasema: "Moyo wangu ulikaribia kuruka, na hilo lilikuwa mara ya kwanza imani ilipothibiti ndani ya moyo wangu."5
Na tupige mfano unaobainisha hilo, nao ni lau mtu akikusimulia juu ya kasri la kifahari lililojengwa kwa uimara, ambalo mabustani yamelizunguka pande zote, na kati ya mabustani hayo mito ikitiririka, na limejaa matandiko na vitanda, na limepambwa kwa aina mbali mbali za mapambo miongoni mwa vipengele vyake vya msingi na vya kukamilisha. Akakuambia: Hakika kasri hili na ukamilifu uliomo ndani yake limejiumba lenyewe, au limetokea hivi hivi kwa bahati nasibu bila Muumba; bila kusita ungeliharakisha kulikanusha jambo hilo na kumkadhibisha, na ungeuhesabu usemi wake kuwa ni kauli ya upuuzi. Je, baada ya hayo, inawezekanaje kudhani kuwa huu ulimwengu mpana, pamoja na ardhi yake, na mbingu zake, na anga zake, na hali zake, na mfumo wake wa ajabu wa kustaajabisha, umejiumba wenyewe? Au umepatikana ghafla bila kuwepo Mola Muumba?!
3- Ama ushahidi wa Sheria juu ya kuwepo kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kwakuwa Vitabu vya mbinguni vyote vinatamka hilo, na hukumu za haki zilizoletwa kupitia Vitabu hivyo, zinazojumuisha masilahi ya viumbe, ni ushahidi kwamba vilitoka kwa Mola Mlezi Mwenye hekima, Mwenye kujua zaidi masilahi ya viumbe wake. Na kile ambacho vilikuja nacho katika habari za kiulimwengu, ambacho hali halisi ya mambo imeshuhudia ukweli wake, ni ushahidi kwamba vilitoka kwa Mola Mlezi Mwenye Uwezo wa kuyaumba yale aliyojulisha juu yake.
4- Ama kuhusu hoja za kihisia juu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu; hizo ziko namna mbili:
Ya kwanza: Kwamba tunasikia na tunashuhudia, kutokana na kujibiwa kwa waombao dua na kuokolewa kwa waliopatwa na dhiki, hayo ni ushahidi thabiti usiopingika juu ya uwepo wake aliyetukuka. Mwenyezi Mungu Mtakatifu amesema:
﴿وَنُوحًا إِذۡ نَادَىٰ مِن قَبۡلُ فَٱسۡتَجَبۡنَا لَهُۥ...﴾
"Na Nuhu alipoita zamani, nasi tukamuitikia..." [Al-Anbiya: 76] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِذۡ تَسۡتَغِيثُونَ رَبَّكُمۡ فَٱسۡتَجَابَ لَكُمۡ...﴾
"Mlipokuwa mnamuomba msaada Mola wenu Mlezi, naye akakujibuni..." [Al-Anfal: 9].
Na katika Sahihi Bukhari kutoka kwa Anas bin Malik -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- amesema: "Aliingia bedui mmoja siku ya Ijumaa, na Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani ziwe juu yake - alikuwa anahutubu, akasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, mali zimeangamia, na familia zina njaa, basi muombee Mwenyezi Mungu kwa ajili yetu. Basi akainua mikono yake na akaomba dua, mara mawingu yakatanda kama milima, na hakuishuka mimbari yake mpaka nikaona mvua ikitiririka kutoka katika ndevu zake."6
Na katika Ijumaa ya pili, akasimama yule bedui, au mwingine, akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, majengo yameporomoka, na mali imezama, basi muombe Mwenyezi Mungu kwa ajili yetu. Basi akanyanyua mikono yake, akasema Mtume rehema na amani ziwe juu yake: "Ewe Mola tuteremshie mvua pembezoni mwetu na wala usituteremshie juu yetu." Basi hakuashiria upande wowote ila ukaachana.7
Na bado Mwenyezi Mungu Mtukufu huwaitikia wanaoomba dua ni jambo linaloshuhudiwa hadi leo hii, kwa yule aliye mkweli katika kuelekea kwake, na akitimiza masharti ya kuitikiwa dua.
Jambo la pili: Kwamba ishara za Manabii zinazoitwa miujiza ambazo watu huzishuhudia au husikia habari zake ni ushahidi usiopingika juu ya kuwepo kwa Aliye watuma wao, naye ni Mwenyezi Mungu Mtukufu; kwa sababu hayo ni mambo yaliyo nje ya uwezo wa binadamu, na Mwenyezi Mungu Mtukufu anazipitisha kupitia mikono yao ili kuwapa nguvu Mitume wake amani iwe juu yao na kuwanusuru.
Mfano wa hilo ni ile ishara ya Musa, amani iwe juu yake, wakati Mwenyezi Mungu aliyetukuka alipomwamuru apige bahari kwa fimbo yake, naye akaipiga; basi bahari ikapasuka njia kumi na mbili za nchi kavu, na maji yaliyo baina yake yakawa kama majabali makubwa. Amesema Mwenyezi Mungu aliyetukuka:
﴿فَأَوۡحَيۡنَآ إِلَىٰ مُوسَىٰٓ أَنِ ٱضۡرِب بِّعَصَاكَ ٱلۡبَحۡرَۖ فَٱنفَلَقَ فَكَانَ كُلُّ فِرۡقٖ كَٱلطَّوۡدِ ٱلۡعَظِيمِ 63﴾
"Tulimletea wahyi Musa tukamwambia: 'Piga bahari kwa fimbo yako.' Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa." [Ash-Shu'ara: 63].
Na mfano wa pili: Muujiza wa Nabii Issa amani iwe juu yake, wakati alipokuwa anawafufua wafu, na kuwatoa makaburini mwao kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Akasema Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kuhusu yeye:
﴿...وَأُحۡيِ ٱلۡمَوۡتَىٰ بِإِذۡنِ ٱللَّهِ...﴾
"...na ninawafufua maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu..." [Al Imran: 49] Na alisema:
﴿...وَإِذۡ تُخۡرِجُ ٱلۡمَوۡتَىٰ بِإِذۡنِي...﴾
"...na ulipokuwa ukiwafufua wafu kwa idhini yangu..." [Al-Maaidah: 110].
Na mfano wa tatu ni wa Muhammad -rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie- pale Makuraishi walipomtaka awaonyeshe muujiza, akauashiria mwezi, ukapasuka vipande viwili, watu wakauona. Na katika hilo amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿ٱقۡتَرَبَتِ ٱلسَّاعَةُ وَٱنشَقَّ ٱلۡقَمَرُ 1 وَإِن يَرَوۡاْ ءَايَةٗ يُعۡرِضُواْ وَيَقُولُواْ سِحۡرٞ مُّسۡتَمِرّٞ 2﴾
"Saa imekaribia, na mwezi umepasuka! Na wakiona ishara yoyote, hugeuka na kusema: 'Huu ni uchawi wa kudumu.'" [Al-Qamar: 1-2].
Basi hizi ishara (miujiza) zinazohisika ambazo Mwenyezi Mungu Mtukufu huzifanya kwa ajili ya kuwatia nguvu Mitume wake na kuwanusuru, zinathibitisha kwa ushahidi usiokuwa na shaka uwepo wake Mtukufu.
Jambo la pili miongoni mwa yanayojumuishwa katika kumuamini Mwenyezi Mungu ni kuuamini umola wake; yaani kwamba Yeye peke yake ndiye Mola Mlezi, hana mshirika wala msaidizi katika hilo.
Arrabbu (Bwana) ni Yule mwenye Uumbaji, Ufalme na amri. Basi hakuna Muumba ila Mwenyezi Mungu, wala hakuna Mmiliki ila Yeye, wala amri ni yake peke yake. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...أَلَا لَهُ ٱلۡخَلۡقُ وَٱلۡأَمۡرُ...﴾
"Fahamuni! Kuumba ni kwake na amri (ni yake)." [Al-A'araf: 54] Na alisema:
﴿...ذَٰلِكُمُ ٱللَّهُ رَبُّكُمۡ لَهُ ٱلۡمُلۡكُۚ وَٱلَّذِينَ تَدۡعُونَ مِن دُونِهِۦ مَا يَمۡلِكُونَ مِن قِطۡمِيرٍ﴾
"Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Na hao mnaowaomba badala yake hawamiliki hata ugozi wa kokwa la tende." [Faatwir: 13].
Hakujulikana kuwapo mtu yeyote miongoni mwa viumbe aliyekana umola wa Mwenyezi Mungu aliyetakasika, isipokuwa awe mwenye ukaidi asiyeamini anachokisema, kama ilivyotokea kwa Firauni, alipowaambia kaumu yake:
﴿فَقَالَ أَنَا۠ رَبُّكُمُ ٱلۡأَعۡلَىٰ 24﴾
"Akasema: Mimi ndiye Mola wenu Mlezi mkuu kabisa." [An-Nazi'at: 24], na akasema:
﴿...يَٰٓأَيُّهَا ٱلۡمَلَأُ مَا عَلِمۡتُ لَكُم مِّنۡ إِلَٰهٍ غَيۡرِي...﴾
"Enyi waheshimiwa! Sijui kama mnaye mungu asiyekuwa mimi." [Al-Qasas: 38]. Lakini hilo halikuwa kutokana na itikadi. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَجَحَدُواْ بِهَا وَٱسۡتَيۡقَنَتۡهَآ أَنفُسُهُمۡ ظُلۡمٗا وَعُلُوّٗا...﴾
"Na wakazikataa kwa dhuluma na kujivuna, na hali ya kuwa nafsi zao zina yakini nazo..." [An-Namli: 14].
Na alisema Mussa, amani iwe juu yake, kumwambia Firauni, katika yale aliyoeleza Mwenyezi Mungu kuhusu yeye:
﴿...لَقَدۡ عَلِمۡتَ مَآ أَنزَلَ هَٰٓؤُلَآءِ إِلَّا رَبُّ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضِ بَصَآئِرَ وَإِنِّي لَأَظُنُّكَ يَٰفِرۡعَوۡنُ مَثۡبُورٗا﴾
"...Wewe unajua bila ya shaka kuwa haya haku yateremsha ila Mola Mlezi wa mbingu na ardhi ili kuwa ni ushahidi wa kuonekana. Na hakika mimi bila ya shaka nakuona wewe, Firauni, kuwa umekwisha angamizwa." [Al-Israa: 102] Na kwa sababu hii washirikina walikuwa wakikiri Umola wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, pamoja na wao kumshirikisha Yeye katika ibada. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
﴿قُل لِّمَنِ ٱلۡأَرۡضُ وَمَن فِيهَآ إِن كُنتُمۡ تَعۡلَمُونَ 84 سَيَقُولُونَ لِلَّهِۚ قُلۡ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ 85 قُلۡ مَن رَّبُّ ٱلسَّمَٰوَٰتِ ٱلسَّبۡعِ وَرَبُّ ٱلۡعَرۡشِ ٱلۡعَظِيمِ 86 سَيَقُولُونَ لِلَّهِۚ قُلۡ أَفَلَا تَتَّقُونَ 87 قُلۡ مَنۢ بِيَدِهِۦمَلَكُوتُ كُلِّ شَيۡءٖ وَهُوَ يُجِيرُ وَلَا يُجَارُ عَلَيۡهِ إِن كُنتُمۡ تَعۡلَمُونَ 88 سَيَقُولُونَ لِلَّهِۚ قُلۡ فَأَنَّىٰ تُسۡحَرُونَ 89﴾
"Sema: Ni ya nani ardhi na vilivyomo ndani yake, kama nyinyi mnajua? Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Sema: Basi, je, hamkumbuki? Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu saba na Mola Mlezi wa Arshi Tukufu? Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Sema: Basi, je, hamchi Mungu? Sema: Ni nani ambaye mkononi mwake umo ufalme wa kila kitu, naye ndiye anayelinda na hakuna anayeweza kulindwa dhidi yake, kama nyinyi mnajua? Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Sema: Basi, vipi mnapotoshwa?" [Muminun: 84-89].
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَلَئِن سَأَلۡتَهُم مَّنۡ خَلَقَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَ لَيَقُولُنَّ خَلَقَهُنَّ ٱلۡعَزِيزُ ٱلۡعَلِيمُ 9﴾
"Na ukiwauliza: Nani aliyeziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Kaziumba Mwenye nguvu, Mwenye kujua zaidi." [Azzukhruf: 9].
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَلَئِن سَأَلۡتَهُم مَّنۡ خَلَقَهُمۡ لَيَقُولُنَّ ٱللَّهُۖ فَأَنَّىٰ يُؤۡفَكُونَ 87﴾
"Na ukiwauliza ni nani aliyewaumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu! Basi ni wapi wanako geuziwa?" [Az-Zukhruf: 87].
Na amri ya Mwenyezi Mungu - kutakasika mbali na machafu ni kwake - inajumuisha yale ya kimajaaliwa na ya kisheria; basi kama vile Yeye ndiye anayeuendesha ulimwengu na anahukumu humo atakavyo, kulingana na yale ambayo inahitaji hekima yake, vivyo hivyo ndiye anayehukumu humo kwa kuwawekea waja wake sheria za ibada na hukumu za miamala, kulingana na yale ambayo inahitaji hekima yake. Na yeyote atakayeweka pamoja na Mwenyezi Mungu aliyetukuka mweka sheria katika ibada, au akamfanya hakimu katika miamala, basi hakika amemshirikisha Mwenyezi Mungu, na hajatimiza imani.
Jambo la tatu katika yanayojumuishwa katika kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kuamini uungu wake; yaani kwamba Yeye peke yake ndiye anayepasa kuabudiwa kwa haki, hana mshirika katika hilo. Na 'ilaah' maana yake ni 'ma-aluuh', yaani anayefanyiwa ibada kwa upendo na taadhima.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَإِلَٰهُكُمۡ إِلَٰهٞ وَٰحِدٞۖ لَّآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ٱلرَّحۡمَٰنُ ٱلرَّحِيمُ 163﴾
"Na Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, hapana mungu ila Yeye. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu." [Al-Baqara: 163] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿شَهِدَ ٱللَّهُ أَنَّهُۥ لَآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ وَٱلۡمَلَٰٓئِكَةُ وَأُوْلُواْ ٱلۡعِلۡمِ قَآئِمَۢا بِٱلۡقِسۡطِۚ لَآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ٱلۡعَزِيزُ ٱلۡحَكِيمُ 18﴾
"Mwenyezi Mungu, na Malaika, na wenye elimu wameshuhudia kuwa hakika hapana mungu ila Yeye, ndiye Mwenye kusimamisha uadilifu; hapana mungu ila Yeye Mwenye nguvu, Mwenye hekima." [Al Imran: 18] Na kila anayemfanya mungu pamoja na Mwenyezi Mungu, akamuabudu kinyume na Mwenyezi Mungu; basi uungu wa huyo mungu ni batili. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿ذَٰلِكَ بِأَنَّ ٱللَّهَ هُوَ ٱلۡحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدۡعُونَ مِن دُونِهِۦ هُوَ ٱلۡبَٰطِلُ وَأَنَّ ٱللَّهَ هُوَ ٱلۡعَلِيُّ ٱلۡكَبِيرُ 62﴾
"Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Wa Kweli, na kwamba wale wanaowaomba badala yake, ni baatili, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye juu, Mkubwa." [Surat Al-Hajj: 62]. Na kuiita miungu hakukuwapa haki ya Uungu. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu (masanamu) Lata, Uzza na Manat:
﴿إِنۡ هِيَ إِلَّآ أَسۡمَآءٞ سَمَّيۡتُمُوهَآ أَنتُمۡ وَءَابَآؤُكُم مَّآ أَنزَلَ ٱللَّهُ بِهَا مِن سُلۡطَٰنٍ...﴾
"Hayo hayakuwa ila ni majina mliyowapa nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuleta uthibitisho wowote juu ya hayo." [An-Najm: 23].
Na imesemwa kuhusu Huud, amani iwe juu yake, kwamba hakika alisema kuwaambia watu wake:
﴿...أَتُجَٰدِلُونَنِي فِيٓ أَسۡمَآءٖ سَمَّيۡتُمُوهَآ أَنتُمۡ وَءَابَآؤُكُم مَّا نَزَّلَ ٱللَّهُ بِهَا مِن سُلۡطَٰنٖۚ...﴾
"Mnabishana nami kwa ajili ya majina tu mliyoyaita nyinyi na baba zenu ambayo kwayo Mwenyezi Mungu hakuteremsha uthibitisho?" [Al-A'araf: 71].
Na imesemwa kuhusu Yusuf, amani iwe juu yake, kwamba aliwaambia wenzake wawili gerezani:
﴿يَٰصَٰحِبَيِ ٱلسِّجۡنِ ءَأَرۡبَابٞ مُّتَفَرِّقُونَ خَيۡرٌ أَمِ ٱللَّهُ ٱلۡوَٰحِدُ ٱلۡقَهَّارُ 39 مَا تَعۡبُدُونَ مِن دُونِهِۦٓ إِلَّآ أَسۡمَآءٗ سَمَّيۡتُمُوهَآ أَنتُمۡ وَءَابَآؤُكُم مَّآ أَنزَلَ ٱللَّهُ بِهَا مِن سُلۡطَٰنٍۚ...﴾
"Enyi wafungwa wenzangu wawili! Je, mabwana wengi wanaofarikiana wao kwa wao ni bora au Mwenyezi Mungu Mmoja, Mwenye nguvu? Hamuabudu badala yake ila majina mliyoyaita nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuteremsha kwa hayo uthibitisho wowote..." [Yusuf: 39-40].
Na kwa sababu hii Mitume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao walikuwa wakiwaambia watu wao:
﴿...ٱعۡبُدُواْ ٱللَّهَ مَا لَكُم مِّنۡ إِلَٰهٍ غَيۡرُهُ...﴾
"Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye." [Al-A'raf: 59]. Lakini washirikina walikataa hilo, na wakawafanya wasiokuwa Mwenyezi Mungu kuwa ni waungu, wakawa wanawaabudu pamoja na Mwenyezi Mungu, aliyetakasika, aliyetukuka, wakitarajia wapate kusaidiwa nao, na wakiwaomba msaada wa kuokolewa.
Na hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu amebatilisha kitendo cha washirikina cha kujiwekea miungu hii kwa hoja mbili za kiakili:
Ya kwanza: Kwamba hakuna katika miungu hii waliyo iweka chochote katika sifa mahususi za uungu; haiumbi chochote, bali hiyo inaumbwa, wala haiwaletei waabudu wake manufaa, wala haiwazuilii madhara, wala haiwa milikii uhai, wala mauti, wala haimiliki chochote katika mbingu, wala kushiriki humo.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَٱتَّخَذُواْ مِن دُونِهِۦٓ ءَالِهَةٗ لَّا يَخۡلُقُونَ شَيۡـٔٗا وَهُمۡ يُخۡلَقُونَ وَلَا يَمۡلِكُونَ لِأَنفُسِهِمۡ ضَرّٗا وَلَا نَفۡعٗا وَلَا يَمۡلِكُونَ مَوۡتٗا وَلَا حَيَوٰةٗ وَلَا نُشُورٗا 3﴾
"Na wamechukua badala yake miungu ambayo haiumbi chochote, bali hiyo inaumbwa, haijimilikii nafsi zao madhara wala manufaa, wala haimiliki mauti, wala uhai, wala kufufuka." [Al-Furqan: 3].
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿قُلِ ٱدۡعُواْ ٱلَّذِينَ زَعَمۡتُم مِّن دُونِ ٱللَّهِ لَا يَمۡلِكُونَ مِثۡقَالَ ذَرَّةٖ فِي ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَلَا فِي ٱلۡأَرۡضِ وَمَا لَهُمۡ فِيهِمَا مِن شِرۡكٖ وَمَا لَهُۥ مِنۡهُم مِّن ظَهِيرٖ 22 وَلَا تَنفَعُ ٱلشَّفَٰعَةُ عِندَهُۥٓ إِلَّا لِمَنۡ أَذِنَ لَهُۥ...﴾
"Sema: Waite mnaodai kuwa ni badala ya Mwenyezi Mungu, hawamiliki uzito hata wa tembe hichi, katika Mbingu wala Ardhi, wala hawana ushirika wowote humo, wala yeye hana msaidizi miongoni mwao, wala haufaidi uombezi mbele yake ila kwa yule aliyempa idhini..." [Saba': 22-23]
﴿أَيُشۡرِكُونَ مَا لَا يَخۡلُقُ شَيۡـٔٗا وَهُمۡ يُخۡلَقُونَ 191 وَلَا يَسۡتَطِيعُونَ لَهُمۡ نَصۡرٗا وَلَآ أَنفُسَهُمۡ يَنصُرُونَ 192﴾
"Ati wanawafanya viumbe kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu, nao hawaumbi, bali wao ndio wanaumbwa? Wala hawawezi kuwasaidia, wala kujisaidia wenyewe." [Al-A'raf: 191-192].
Basi ikiwa hali ya miungu hiyo ndivyo ilivyo, basi kuwafanya miungu ni upumbavu mkubwa zaidi ya upumbavu wote, na ubatilifu mkubwa zaidi ya ubatilifu wote.
Ya pili: Washirikina wa zamani walikuwa wakikiri kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu peke yake ndiye Mola Mlezi na Muumba, ambaye mikononi mwake imo milki ya kila kitu, naye ndiye mwenye kutoa hifadhi, wala hakuna wa kumkinga dhidi yake. Na hili linawajibisha wampwekeshe katika uungu, kama walivyompwekesha katika umola. kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿يَٰٓأَيُّهَا ٱلنَّاسُ ٱعۡبُدُواْ رَبَّكُمُ ٱلَّذِي خَلَقَكُمۡ وَٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِكُمۡ لَعَلَّكُمۡ تَتَّقُونَ 21 ٱلَّذِي جَعَلَ لَكُمُ ٱلۡأَرۡضَ فِرَٰشٗا وَٱلسَّمَآءَ بِنَآءٗ وَأَنزَلَ مِنَ ٱلسَّمَآءِ مَآءٗ فَأَخۡرَجَ بِهِۦ مِنَ ٱلثَّمَرَٰتِ رِزۡقٗا لَّكُمۡۖ فَلَا تَجۡعَلُواْ لِلَّهِ أَندَادٗا وَأَنتُمۡ تَعۡلَمُونَ 22﴾
"Enyi watu! Muabuduni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni nyinyi na wale wa kabla yenu, ili mpate kuokoka. Aliyekufanyieni ardhi kuwa tandiko na mbingu kuwa paa, na akateremsha maji kutoka mbinguni, na kwa hayo akatoa matunda kuwa ni riziki kwenu. Basi msimfanyie Mwenyezi Mungu washirika, na hali mnajua." [Al-Baqara: 21-22].
Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَلَئِن سَأَلۡتَهُم مَّنۡ خَلَقَهُمۡ لَيَقُولُنَّ ٱللَّهُۖ فَأَنَّىٰ يُؤۡفَكُونَ 87﴾
"Na ukiwauliza ni nani aliyewaumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu! Basi ni wapi wanako geuziwa?" [Az-Zukhruf: 87].
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿قُلۡ مَن يَرۡزُقُكُم مِّنَ ٱلسَّمَآءِ وَٱلۡأَرۡضِ أَمَّن يَمۡلِكُ ٱلسَّمۡعَ وَٱلۡأَبۡصَٰرَ وَمَن يُخۡرِجُ ٱلۡحَيَّ مِنَ ٱلۡمَيِّتِ وَيُخۡرِجُ ٱلۡمَيِّتَ مِنَ ٱلۡحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ ٱلۡأَمۡرَۚ فَسَيَقُولُونَ ٱللَّهُۚ فَقُلۡ أَفَلَا تَتَّقُونَ 31 فَذَٰلِكُمُ ٱللَّهُ رَبُّكُمُ ٱلۡحَقُّۖ فَمَاذَا بَعۡدَ ٱلۡحَقِّ إِلَّا ٱلضَّلَٰلُۖ فَأَنَّىٰ تُصۡرَفُونَ 32﴾
Sema: Ni nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Au ni nani anaye miliki kusikia na kuona? Na nani amtoaye aliye hai kutoka kwa maiti, na akamtoa maiti kutoka aliye hai? Na nani anaye yadabiri (kuyapangilia) mambo yote? Watasema: Mwenyezi Mungu. Basi sema: Je! Hamchi? Huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu wa haki. Basi baada ya haki ni nini isipokuwa upotovu? Basi mna elekezwa wapi? [Yunus: 31-32].
Jambo la nne miongoni mwa yale yanayojumuishwa katika kumuamini Mwenyezi Mungu ni kuamini majina ya Mwenyezi Mungu na sifa zake:
Ni kuthibitisha yale aliyoyathibitisha Mwenyezi Mungu kuhusu nafsi yake katika Kitabu chake, au katika Sunna ya Mtume wake - rehema na amani ziwe juu yake - miongoni mwa majina yake na sifa zake, kwa namna inayomfaa Yeye aliyetakasika, bila ya kuyabadilisha, kuyakataa, kuyaeleza jinsi yalivyo hasa, wala kuyapigia mfano. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَلِلَّهِ ٱلۡأَسۡمَآءُ ٱلۡحُسۡنَىٰ فَٱدۡعُوهُ بِهَاۖ وَذَرُواْ ٱلَّذِينَ يُلۡحِدُونَ فِيٓ أَسۡمَٰٓئِهِۦۚ سَيُجۡزَوۡنَ مَا كَانُواْ يَعۡمَلُونَ 180﴾
"Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri kabisa, basi muombeni kwa hayo. Na waacheni wale wanao haribu utakatifu wa majina yake. Hao watakujalipwa waliyokuwa wakiyatenda." [Al-A'raf: 180]
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...وَلَهُ ٱلۡمَثَلُ ٱلۡأَعۡلَىٰ فِي ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضِۚ وَهُوَ ٱلۡعَزِيزُ ٱلۡحَكِيمُ﴾
"Na naye ndiye mwenye mfano bora kabisa katika mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima." [Ar-Rum: 27].
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...لَيۡسَ كَمِثۡلِهِۦ شَيۡءٞۖ وَهُوَ ٱلسَّمِيعُ ٱلۡبَصِيرُ﴾
"Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona." [Ash-shura: 11].
Na hakika makundi mawili yamepotea katika jambo hili:
La kwanza: Wenye kukataa, waliokanusha majina na sifa, au baadhi yake, wakidai kuwa kuzithibitisha kwa Mwenyezi Mungu kunalazimu mfanano, yaani kumfananisha Mwenyezi Mungu Mtukufu na viumbe wake. Na madai haya ni batili; kwa hoja kadhaa, miongoni mwazo:
Ya kwanza: Kwamba linapelekea matokeo batili; kama mkinzano katika maneno ya Mwenyezi Mungu aliyetakasika. Na hilo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu aliyetukuka amejithibitishia majina na sifa, na amekanusha kuwa kuna kitu chochote chenye kufanana naye. Na lau ingekuwa kuthibitisha sifa hizo kungelisababisha kumfananisha Mwenyezi Mungu na viumbe, basi inge lazimu kuwe na mgongano katika maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na baadhi yake kuyakanusha baadhi mengine.
Ya pili: Kwamba hailazimu kutokana na kulingana kwa vitu viwili katika jina au sifa kwamba viwe vime fanana. Basi waona watu wawili wakilingana kwamba kila mmoja wao ni mwanadamu mwenye kusikia, mwenye kuona, mwenye kunena. Wala si lazima kutokana na hilo kufanana katika maana za kibinadamu, na katika kusikia, kuona, na kusema.
Na unaona wanyama wana mikono, miguu na macho; wala halilazimu kutokana na kufanana huku kwamba mikono yao, miguu yao na macho yao yawe sawasawa.
Ikidhihirika tofauti kati ya viumbe katika yale yanayo fanana kwa majina au sifa, basi tofauti kati ya Muumba na viumbe ni dhahiri zaidi na kuu zaidi.
Kundi la pili: Wanafananisha, ambao wanathibitisha majina ya Mwenyezi Mungu na sifa zake, huku waki mfananisha Mwenyezi Mungu na viumbe vyake, wakidai kuwa hili ndilo linaloashiriwa na ushahidi wa maandiko; kwa kuwa Mwenyezi Mungu anawahutubia waja kwa wanayoyaelewa. Na madai haya ni batili kwa sababu kadhaa; miongoni mwazo ni:
Kwanza: Kumfananisha Mwenyezi Mungu aliyetukuka na viumbe wake ni jambo lililo batili kwa mujibu wa akili na Sheria, na haiwezekani makusudio ya maandiko ya Kitabu na Sunna yawe jambo batili.
Pili: Kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amewahutubia waja kwa yale wanayoyafahamu katika asili ya maana; ama hakika na kiini cha maana hiyo jinsi ilivyo, hilo ni miongoni mwa yale ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu amehusisha kwa elimu yake, yahusuyo Dhati yake na Sifa zake.
Basi Mwenyezi Mungu alipoithibitishia nafsi yake kuwa Yeye ni Mwenye kusikia. Basi kusikia kunajulikana kwa mujibu wa asili ya maana yake, yaani ni utambuzi wa sauti; lakini hakika ya hilo kwa kuhusiana na usikivu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu haijulikani; kwani hakika ya usikivu hutofautiana hata miongoni mwa viumbe; hivyo tofauti hiyo baina ya Muumba na kiumbe ndiyo iliyo dhahiri zaidi na kubwa zaidi.
Na anapotoa habari Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu Yeye Mwenyewe kwamba Yuko juu ya Arshi yake, basi ‘kuwa juu’ kwa asili ya maana yake kuna julikana; lakini uhalisia wa kuwa juu alio nao Yeye haujulikani kwetu kuhusiana na kuwa juu kwa Mwenyezi Mungu juu ya Arshi yake; kwani uhalisia wa kuwa juu hutofautiana kwa upande wa viumbe. Basi si sawa kuwa juu ya kiti thabiti na kuwa juu ya tandiko la ngamia mkaidi tena mwenye kushituka na kukimbia. Hivyo basi, ikitofautiana kwa upande wa kiumbe, basi tofauti hiyo kati ya Muumba na kiumbe ni dhahiri zaidi na kubwa zaidi.
Na kumuamini Mwenyezi Mungu aliyetukuka, kama tulivyoeleza, huwaletea Waumini matunda adhimu; miongoni mwake ni:
La kwanza: Kutimiza suala la kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mtukufu, kiasi kwamba asiweke matumaini yake kwa asiyekuwa Yeye, wala kuogopa asiyekuwa Yeye, na wala asiabudiwe yeyote ila Mwenyezi Mungu Mtukufu.
La pili: Ukamilifu wa mapenzi kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumtukuza kwa mujibu wa majina yake mazuri mno na sifa zake tukufu.
La tatu: Kutekeleza ibada ya Mwenyezi Mungu kwa kuyafanya yale aliyoyaamrisha, na kujiepusha na yale aliyoyakataza.
***
Kuamini Malaika
Malaika ni viumbe wasioonekana, walioumbwa, na ni waja wa Mwenyezi Mungu Mtukufu; wala hawana sifa zozote za Umola na Uungu. Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwaumba kutokana na nuru, na akawajalia utiifu uliokamilika wa amri yake, na nguvu ya kuutekeleza. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...وَمَنۡ عِندَهُۥ لَا يَسۡتَكۡبِرُونَ عَنۡ عِبَادَتِهِۦ وَلَا يَسۡتَحۡسِرُونَ 19 يُسَبِّحُونَ ٱلَّيۡلَ وَٱلنَّهَارَ لَا يَفۡتُرُونَ 20﴾
"Na walioko kwake hawafanyi kiburi wakaacha kumuabudu, wala hawachoki. Wanamtakasa usiku na mchana bila kuchoka." [Al-Anbiyaa: 19-20].
Nao Malaika ni wengi, idadi yao haiwezi kuhesabiwa isipokuwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na imethibiti katika vile vitabu viwili sahihi kutokana na hadithi ya Anas -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- katika kisa cha safari ya miraji ya kwamba Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- ilinyanyuliwa ikaletwa kwake Baitul-Ma'muri (nyumba iliyoimarishwa kwa ibada) mbinguni, wanaswali ndani yake kila siku Malaika elfu sabini, ambapo wakishatoka, wote hawarudi humo tena.
Na kuamini Malaika kunakusanya mambo manne:
La kwanza: Kuamini uwepo wao.
Jambo la pili: Kuwaamini kwa majina wale tuliowajua kwa jina miongoni mwao (kama vile Jibril), na wale tusiojua majina yao tunawaamini kwa ujumla.
Jambo la tatu: Kuamini yale tuliyofahamishwa kuhusu sifa zao, kama vile sifa ya Jibrili. Kwani Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alieleza kwamba alimuona katika sura yake aliyoumbwa nayo, naye ana mbawa mia sita zilizoziba anga.
Na huenda Malaika akabadilika kwa amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu akaonekana katika umbo la mwanamume. Kama ilivyotokea kwa Jibril - amani iwe juu yake - alipotumwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Maryam, akajitokeza kwake kwa sura ya mwanadamu kamili. Na alipokuja kwa Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- naye akiwa amekaa pamoja na Masahaba wake, alimjia kwa sura ya mtu mwenye nguo nyeupe mno, mwenye nywele nyeusi mno, haonekani kuwa na athari za safari, wala hakuna yeyote amjuaye miongoni mwa Masahaba wake; akakaa karibu na Mtume -rehema na amani ziwe juu yake-, akakunja magoti yake kwa kuyaunganisha na magoti ya Mtume (mithili ya tahiyatu), na akaweka viganja vyake juu ya mapaja yake, kisha akamuuliza Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- kuhusu Uislamu, na Imani, na Ihisani, na Kiyama, na alama zake. Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- akamjibu, akaondoka, kisha Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- akasema: "Huyu ni Jibril; amekuja kwenu kukufundisheni dini yenu."8.
Na vivyo hivyo, Malaika ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwatuma kwa Ibrahim na Lut, amani iwe juu yao, walikuwa katika sura ya wanaume.
La nne miongoni mwa yanayojumuishwa katika kuamini Malaika ni kusadikisha yale tuliyoyajua miongoni mwa kazi zao wanazozitekeleza kwa amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; kama vile kumtakasa Yeye, na kumuabudu Yeye usiku na mchana bila kuchoka wala kulegea.
Na huenda baadhi yao wakawa na kazi maalumu.
Kama vile Jibrili, amani iwe juu yake, Mwaminifu katika kufikisha Ufunuo (Wahyi) wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambaye Mwenyezi Mungu humtuma nao kwa Manabii na Mitume.
Na kama vile Mikaeli ambaye kapewa jukumu la mvua na mimea.
Kama vile Israfili amani iwe juu yake, aliyepewa jukumu la kupuliza kwenye baragumu Siku ya Kiyama na kufufuliwa kwa viumbe.
Na mfano wake ni Malaika wa mauti, aliyepewa jukumu la kuzitoa roho pindi mauti yanapofika.
Na mfano ni Maliki aliyepewa jukumu la Moto, na yeye ndiye mlinzi wa Moto.
Na mfano wa hilo ni Malaika waliokabidhiwa jukumu juu ya vijusi vilivyomo matumboni; mwanadamu anapo kamilisha miezi minne tumboni mwa mama yake, Mwenyezi Mungu humtumia Malaika, akamwamuru kuandika riziki yake, na muda wake, na matendo yake, na kwamba ni muovu au mwema.
Na mfano wake ni Malaika waliopewa jukumu la kuhifadhi matendo ya wanadamu na kuyaandika; kila mtu ana Malaika wawili: mmoja upande wa kulia na wa pili upande wa kushoto.
Na mfano wake ni Malaika waliopangiwa kumuuliza maiti anapowekwa kaburini mwake; humfikia Malaika wawili, wanamuuliza kuhusu Mola wake Mlezi, na kuhusu Dini yake, na Nabii wake.
Na kuamini Malaika hutoa matunda tukufu, miongoni mwake:
La kwanza: Elimu. Nayo ni kuujua Ukuu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na Nguvu zake, na Mamlaka yake; kwani Ukuu wa kiumbe ni ushahidi juu ya Ukuu wa Muumbaji.
La pili: Ni kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa uangalizi wake kwa wanadamu; kwamba amewawekea miongoni mwa hawa Malaika watukufu wale wanao walinda, na kuandika matendo yao, na mengineyo katika masilahi yao.
Msingi wa tatu: Kuwapenda Malaika kwa sababu ya yale waliyoyatekeleza katika kumuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Na baadhi ya waliopotoka wamekanusha kuwa Malaika wana mili, na wakasema: kwamba wao ni nguvu za kheri zilizofichika ndani ya viumbe; na hili ni kukadhibisha Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu, na Sunnah ya Mtume wake -rehema na amani ziwe juu yake-, na makubaliano ya Waislamu.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿ٱلۡحَمۡدُ لِلَّهِ فَاطِرِ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضِ جَاعِلِ ٱلۡمَلَٰٓئِكَةِ رُسُلًا أُوْلِيٓ أَجۡنِحَةٖ مَّثۡنَىٰ وَثُلَٰثَ وَرُبَٰعَ...﴾
"Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi, aliyewafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa, mbili-mbili, na tatu- tatu, na nne-nne..." [Faatwir: 1].
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَلَوۡ تَرَىٰٓ إِذۡ يَتَوَفَّى ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ ٱلۡمَلَٰٓئِكَةُ يَضۡرِبُونَ وُجُوهَهُمۡ وَأَدۡبَٰرَهُم...﴾
"Na laiti ungeliona Malaika wanapowafisha wale waliokufuru wakiwapiga nyuso zao na migongo yao..." [Al-Anfaal: 50].
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...وَلَوۡ تَرَىٰٓ إِذِ ٱلظَّٰلِمُونَ فِي غَمَرَٰتِ ٱلۡمَوۡتِ وَٱلۡمَلَٰٓئِكَةُ بَاسِطُوٓاْ أَيۡدِيهِمۡ أَخۡرِجُوٓاْ أَنفُسَكُمُ...﴾
"...Na lau ungeliwaona madhalimu wanavyokuwa katika mahangaiko ya mauti, na Malaika wame wanyooshea mikono yao wakiwaambia: Zitoeni roho zenu!..." [Al-An'am: 93].
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...حَتَّىٰٓ إِذَا فُزِّعَ عَن قُلُوبِهِمۡ قَالُواْ مَاذَا قَالَ رَبُّكُمۡۖ قَالُواْ ٱلۡحَقَّۖ وَهُوَ ٱلۡعَلِيُّ ٱلۡكَبِيرُ﴾
"...Hadi itakapoondolewa hofu kwenye nyoyo zao, watasema: Mola wenu Mlezi kasema nini? Watasema: Yaliyo kweli! Na Yeye ndiye Aliye juu, Mkubwa." [Saba': 23].
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu watu wa Peponi:
﴿...وَٱلۡمَلَٰٓئِكَةُ يَدۡخُلُونَ عَلَيۡهِم مِّن كُلِّ بَابٖ سَلَٰمٌ عَلَيۡكُم بِمَا صَبَرۡتُمۡۚ فَنِعۡمَ عُقۡبَى ٱلدَّارِ﴾
"Na Malaika wanawaingilia katika kila mlango, Salamu iwe juu yenu kwa mlivyosubiri. Basi ni bora mno malipo ya Nyumba ya Akhera." [Ar-Ra'di: 23-24].
Na katika Sahihi Bukhari kutoka kwa Abuu Huraira radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake kutoka kwa Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alisema: "Mwenyezi Mungu anapompenda mja, humuita Jibril: 'Hakika Mwenyezi Mungu anampenda fulani, basi mpende.' Kwa hivyo Jibril anampenda. Kisha Jibril huwaita Malaika wa mbinguni: 'Hakika Mwenyezi Mungu anampenda fulani, basi mpendeni.' Kwa hivyo Malaika wa mbinguni wanampenda. Kisha mtu huyo hujaaliwa kukubalika duniani."9.
Na kutoka kwa Abuu Huraira pia -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- amesema: Amesema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Inapokuwa siku ya Ijumaa, huwa katika kila mlango miongoni mwa milango ya Misikiti Malaika wakiandika mmoja baada ya mwingine. Anapokaa Imamu, Malaika hao hukunja Vitabu vyao, na wanakuja kusikiliza Ukumbusho."10
Maandiko haya yako wazi kabisa kwamba Malaika ni viumbe wenye miili, si nguvu za kimaana (zisizo za kimwili) kama walivyosema waliopotoka; na kwa mujibu wa maandiko haya Waislamu wameafikiana kwa kauli moja.
***
Kuamini Vitabu
Vitabu ni wingi wa Kitabu, nalo ni neno la Kiarabu lenye maana ya "Kilichoandikwa".
Na makusudio hapa ni Vitabu ambavyo kaviteremsha Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Mitume wake, iwe ni rehema kwa viumbe, na muongozo kwao; ili waweze kufika katika furaha ya dunia na akhera.
Na kuamini Vitabu, kunaingia ndani yake kuamini mambo manne:
1- Kuamini kuwa kuteremshwa kwake kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni kwa hakika.
Jambo la pili: Kuviamini vile ambavyo tumevijua kwa majina yake miongoni mwavyo; kama vile Qur’ani iliyoteremshwa kwa Muhammadi -rehema na amani ziwe juu yake. Na Taurati iliyoteremshwa kwa Musa, amani iwe juu yake. Na Injili iliyoteremshwa kwa Issa - rehema na amani ziwe juu yake. Na Zaburi aliyopewa Daudi, amani iwe juu yake. Na ama kile ambacho hatujui jina lake, tunakiamini kwa ujumla.
Msingi wa tatu: Kusadikisha yale yaliyothibiti katika habari zake; kama vile habari za Qur’ani Tukufu, na habari za yale ambayo hayajabadilishwa na kugeuzwa miongoni mwa Vitabu vilivyotangulia.
Nne: Kufanyia kazi hukumu zote ambazo hazijafutwa miongoni mwa hukumu za Qur'ani, na kuziridhia na kuzikubali, iwe tumeielewa hekima yake au hatujaielewa. Na vitabu vyote vilivyotangulia vimefutwa na Qur'ani Tukufu. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَأَنزَلۡنَآ إِلَيۡكَ ٱلۡكِتَٰبَ بِٱلۡحَقِّ مُصَدِّقٗا لِّمَا بَيۡنَ يَدَيۡهِ مِنَ ٱلۡكِتَٰبِ وَمُهَيۡمِنًا عَلَيۡهِۖ...﴾
"Na tumekuteremshia wewe, kwa haki, Kitabu hiki kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Vitabu na kuyadhibiti..." [Al-Maida: 48] Yaani: Iwe ni yenye kuvihukumu.
Na kwa msingi huu, haijuzu kufanyia kazi hukumu yoyote miongoni mwa hukumu za Vitabu vilivyotangulia, isipokuwa ile iliyo sahihi na kukubaliwa na Qur'ani.
Na kuamini Vitabu kunazaa matunda makubwa, miongoni mwake:
Kwanza: Ni Elimu ya uangalizi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa waja wake; kwani aliwateremshia kila kaumu Kitabu ili kuwaongoza nacho.
Pili: Ni kujua hekima ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika sheria yake; ambapo ameyaweka kuwa sheria kwa kila kaumu yale yanayoafikiana na hali zao. kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...لِكُلّٖ جَعَلۡنَا مِنكُمۡ شِرۡعَةٗ وَمِنۡهَاجٗاۚ...﴾
"Kila mmoja katika nyinyi tumemwekea Sheria yake na njia yake." [Al-Maaidah: 48].
Tatu: Kushukuru neema ya Mwenyezi Mungu katika hilo.
***
Kuamini Mitume
Mitume ni wingi wa "Rasuul" yaani "Aliyetumwa kufikisha kitu (Ujumbe)."
Kinachokusudiwa hapa ni yule aliyeteremshiwa Ufunuo utokanao na sheria miongoni mwa wanadamu na akaamrishwa kuufikisha.
Mtume wa kwanza ni Nuhu, amani iwe juu yake, na wa mwisho wao ni Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿ إِنَّآ أَوۡحَيۡنَآ إِلَيۡكَ كَمَآ أَوۡحَيۡنَآ إِلَىٰ نُوحٖ وَٱلنَّبِيِّـۧنَ مِنۢ بَعۡدِهِ...﴾
"Hakika Sisi tumekuletea wahyi wewe kama tulivyo wapelekea wahyi Nuhu na Manabii waliokuwa baada yake..." [An-Nisaa: 163].
Na ilikuja katika Sahihi Bukhari kutoka kwa Anasi bin Maliki, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika hadithi ya uombezi, ya kwamba Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alisema: "Watu watamwendea Adam ili awatetee mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, basi atatoa udhuru kwao na atasema: Nendeni kwa Nuhu, Mtume wa kwanza aliyemtuma Mwenyezi Mungu." Na imetajwa hadithi kwa ukamilifu wake.11
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu yeye Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake:
﴿مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَآ أَحَدٖ مِّن رِّجَالِكُمۡ وَلَٰكِن رَّسُولَ ٱللَّهِ وَخَاتَمَ ٱلنَّبِيِّـۧنَۗ...﴾
"Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii..." [Al-Ahzaab: 40].
Wala hakuna Umma uliokosa Mtume anayetumwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu akiwa na sheria ya kipekee kwa kaumu yake, au Nabii anayeteremshiwa ufunuo wa sheria ya Mtume aliyemtangulia ili aihuishe. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:
﴿وَلَقَدۡ بَعَثۡنَا فِي كُلِّ أُمَّةٖ رَّسُولًا أَنِ ٱعۡبُدُواْ ٱللَّهَ وَٱجۡتَنِبُواْ ٱلطَّٰغُوتَۖ...﴾
"Na kwa hakika kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni Shetani..." [An-Nahli: 36].
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...وَإِن مِّنۡ أُمَّةٍ إِلَّا خَلَا فِيهَا نَذِيرٞ﴾
"Na hapana umma wowote ila ulipata muonyaji kati yao." [Surat Faatir: 24]
Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّآ أَنزَلۡنَا ٱلتَّوۡرَىٰةَ فِيهَا هُدٗى وَنُورٞۚ يَحۡكُمُ بِهَا ٱلنَّبِيُّونَ ٱلَّذِينَ أَسۡلَمُواْ لِلَّذِينَ هَادُواْ...﴾
"Hakika Sisi tuliteremsha Taurati yenye uongofu na nuru, ambayo kwayo Manabii walionyenyekea kiislamu, na wacha Mungu, na wanazuoni, waliwahukumu Mayahudi..." [Al-Ma’idah: 44].
Na Mitume ni viumbe walioumbwa na Mwenyezi Mungu, hawana chochote katika sifa za vitendo vya Mwenyezi Mungu (kama vile kutoa riziki na kuhuisha nk.), wala sifa za kuabudiwa. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu Nabii wake Muhammadi - rehema na amani ziwe juu yake-, naye ndiye bora wa Mitume na mwenye hadhi kuu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu:
﴿قُل لَّآ أَمۡلِكُ لِنَفۡسِي نَفۡعٗا وَلَا ضَرًّا إِلَّا مَا شَآءَ ٱللَّهُۚ وَلَوۡ كُنتُ أَعۡلَمُ ٱلۡغَيۡبَ لَٱسۡتَكۡثَرۡتُ مِنَ ٱلۡخَيۡرِ وَمَا مَسَّنِيَ ٱلسُّوٓءُۚ إِنۡ أَنَا۠ إِلَّا نَذِيرٞ وَبَشِيرٞ لِّقَوۡمٖ يُؤۡمِنُونَ 188﴾
"Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara, ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa ninayajua ya ghaibu ningejizidishia mema mengi, wala ovu lisingenigusa. Mimi si chochote ila ni muonyaji na mtoa bishara kwa watu wanaoamini." [Surat Al-A'raaf: 188] .
Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿قُلۡ إِنِّي لَآ أَمۡلِكُ لَكُمۡ ضَرّٗا وَلَا رَشَدٗا 21 قُلۡ إِنِّي لَن يُجِيرَنِي مِنَ ٱللَّهِ أَحَدٞ وَلَنۡ أَجِدَ مِن دُونِهِۦ مُلۡتَحَدًا 22﴾
"Sema: Mimi sina mamlaka ya kukudhuruni wala kukuongozeni. Sema: Hakika hakuna yeyote atakaye niokoa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wala sitapata kimbilio lolote kando yake." [Al-Jinni: 21-22].
Na zinawapata sifa za kibinadamu: Miongoni mwa hayo ni ugonjwa, mauti, na uhitaji wa chakula na kinywaji, na mengineyo. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema kuhusu Ibrahim, amani iwe juu yake, katika kumuelezea Mola wake Mlezi, Mtukufu:
﴿وَٱلَّذِي هُوَ يُطۡعِمُنِي وَيَسۡقِينِ 79 وَإِذَا مَرِضۡتُ فَهُوَ يَشۡفِينِ 80 وَٱلَّذِي يُمِيتُنِي ثُمَّ يُحۡيِينِ 81﴾
"Na ambaye ndiye ananilisha na kuninywesha. Na ninapougua, ndiye ananiponya. Na ambaye ananifisha kisha ananihuisha." [Ash-Shu'ara: 79-81].
Amesema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie: "Hakika, mimi ni mwanadamu tu kama nyinyi; ninasahau kama mnavyosahau. Basi nikisahau, nikumbusheni."12
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaelezea kuwa ni waja wake katika madaraja yao ya juu kabisa, na katika muktadha wa kuwasifu wao; Basi akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu Nuhu, amani imfikie:
﴿...إِنَّهُۥ كَانَ عَبۡدٗا شَكُورٗا﴾
"Hakika yeye alikuwa mja mwenye shukrani sana." [Al-Israa: 3] Na akasema kuhusiana na Muhammadi, rehema na amani zimshukie:
﴿تَبَارَكَ ٱلَّذِي نَزَّلَ ٱلۡفُرۡقَانَ عَلَىٰ عَبۡدِهِۦ لِيَكُونَ لِلۡعَٰلَمِينَ نَذِيرًا 1﴾
"Ametukuka aliyeteremsha Furqani kwa mja wake, ili awe muonyaji kwa walimwengu wote." [Al-Furqaan: 1].
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusiana na Ibrahim, Is'haq na Ya'qub, amani ziwe juu yao:
﴿وَٱذۡكُرۡ عِبَٰدَنَآ إِبۡرَٰهِيمَ وَإِسۡحَٰقَ وَيَعۡقُوبَ أُوْلِي ٱلۡأَيۡدِي وَٱلۡأَبۡصَٰرِ 45 إِنَّآ أَخۡلَصۡنَٰهُم بِخَالِصَةٖ ذِكۡرَى ٱلدَّارِ 46 وَإِنَّهُمۡ عِندَنَا لَمِنَ ٱلۡمُصۡطَفَيۡنَ ٱلۡأَخۡيَارِ47﴾
"Na wakumbuke waja wetu, Ibrahim na Is-haqa na Yaa'qubu waliokuwa na nguvu na busara. Hakika tuliwachagua kwa sifa maalumu ya kukumbuka Akhera. Na hakika wao kwetu ni miongoni mwa wateule wema." [Swad: 45-47].
Na akasema kuhusiana na Issa (Yesu) mwana wa Mariamu, amani iwe juu yake:
﴿إِنۡ هُوَ إِلَّا عَبۡدٌ أَنۡعَمۡنَا عَلَيۡهِ وَجَعَلۡنَٰهُ مَثَلٗا لِّبَنِيٓ إِسۡرَٰٓءِيلَ 59﴾
"Hakuwa yeye (Isa) isipokuwa ni Mtumwa tuliye mneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili." [Az-Zukhruf: 59].
Na kuamini Mitume kunaingia ndani yake mambo manne:
Jambo la kwanza: Kuamini kuwa utume wao ni haki kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na yeyote atakaye mkufuru mmoja katika Mitume hao, basi hakika atakuwa amewakufuru wote. kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿كَذَّبَتۡ قَوۡمُ نُوحٍ ٱلۡمُرۡسَلِينَ 105﴾
"Kaumu ya Nuhu waliwakadhibisha Mitume." [Ash-Shu'arā: 105] Basi hapo Mwenyezi Mungu akawafanya kuwa wenye kuwakadhibisha Mitume wote, ingawa hakukuwa na Mtume mwingine isipokuwa yeye wakati walipomkadhibisha. Na kwa msingi huo, Manaswara waliomkadhibisha Muhammad -rehema na amani ziwe juu yake- na hawakumfuata; hao ni wenye kumkadhibisha Masihi bin Mariyama - amani iwe juu yake - na wala si wafuasi wake pia, hasa kwa kuwa yeye aliwapa bishara ya Muhammad rehema na amani ziwe juu yake. Na hakuna maana ya bishara hiyo kwao isipokuwa kwamba yeye ni Mtume kwao, ambaye kwa yeye Mwenyezi Mungu atawaokoa kutokana na upotofu na kuwaongoza kwenye njia iliyonyooka.
Jambo la pili: Kuwaamini Mitume ambao tumewajua majina yao miongoni mwao kwa kuyataja majina yao, kama vile: Muhammad, Ibrahim, Musa, Isa, na Nuhu rehema na amani ziwe juu yao. Na hawa watano ndio Manabii wastahamilivu, na Mwenyezi Mungu Mtukufu amewataja katika sehemu mbili katika Qur’ani, katika maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَإِذۡ أَخَذۡنَا مِنَ ٱلنَّبِيِّـۧنَ مِيثَٰقَهُمۡ وَمِنكَ وَمِن نُّوحٖ وَإِبۡرَٰهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَى ٱبۡنِ مَرۡيَمَۖ وَأَخَذۡنَا مِنۡهُم مِّيثَٰقًا غَلِيظٗا 7﴾
"Na tulipochukua agano kwa Manabii na kwako wewe, na Nuhu na Ibrahim na Musa na Isa mwana wa Mariamu, na tulichukua kwao agano gumu!" [Al-Ahzaab: 7] Na kauli yake Mwenyezi Mungu :
﴿شَرَعَ لَكُم مِّنَ ٱلدِّينِ مَا وَصَّىٰ بِهِۦ نُوحٗا وَٱلَّذِيٓ أَوۡحَيۡنَآ إِلَيۡكَ وَمَا وَصَّيۡنَا بِهِۦٓ إِبۡرَٰهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَىٰٓۖ أَنۡ أَقِيمُواْ ٱلدِّينَ وَلَا تَتَفَرَّقُواْ فِيهِۚ كَبُرَ عَلَى ٱلۡمُشۡرِكِينَ مَا تَدۡعُوهُمۡ إِلَيۡهِۚ ٱللَّهُ يَجۡتَبِيٓ إِلَيۡهِ مَن يَشَآءُ وَيَهۡدِيٓ إِلَيۡهِ مَن يُنِيبُ 13﴾
"Amekuamrisheni Dini ile ile aliyomuusia Nuhu na tuliyokufunulia wewe, na tuliyowausia Ibrahim na Musa na Isa, kwamba shikeni Dini wala msifarikiane kwayo. Ni magumu kwa washirikina hayo unayowaitia. Mwenyezi Mungu humteua kwake amtakaye, na humu ongoa kwake aelekeaye." [As-Shuuraa: 13].
Ama yule ambaye hatujui jina lake miongoni mwao, tunamwamini kwa ujumla, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَلَقَدۡ أَرۡسَلۡنَا رُسُلٗا مِّن قَبۡلِكَ مِنۡهُم مَّن قَصَصۡنَا عَلَيۡكَ وَمِنۡهُم مَّن لَّمۡ نَقۡصُصۡ عَلَيۡكَۗ...﴾
"Na bila ya shaka tuliwatuma Mitume kabla yako. Wengine katika hao tumekusimulia habari zao, na wengine hatukukusimulia." [Ghafiri: 78].
La tatu: Kusadikisha yale yaliyothibiti kwa njia sahihi kutoka kwao katika habari zao.
Msingi wa nne: Kutekeleza sheria ya yule aliyetumwa kwetu miongoni mwao, naye ndiye wa mwisho wao, Muhammadi -rehema na amani ziwe juu yake- aliye tumwa kwa watu wote. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤۡمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيۡنَهُمۡ ثُمَّ لَا يَجِدُواْ فِيٓ أَنفُسِهِمۡ حَرَجٗا مِّمَّا قَضَيۡتَ وَيُسَلِّمُواْ تَسۡلِيمٗا 65﴾
"La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayohitilafiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utakayotoa, na wanyenyekee kabisa." [An-Nisaa: 65].
Miongoni mwa matunda adhimu ya kuamini Mitume ni:
Kwanza: Ni kujua rehema ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na uangalizi wake kwa waja wake; kwamba aliwatumia Mitume wake ili wawaongoze kwenye njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kuwabainishia jinsi ya kumuabudu Mwenyezi Mungu; kwa sababu akili ya kibinadamu haiwezi kujitosheleza katika kujua hayo.
Pili: Kumshukuru Mwenyezi Mungu juu ya neema hii kubwa.
La tatu: Kuwapenda Mitume -rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao- na kuwaadhimisha, na kuwasifu kwa yale yanayowastahiki; kwa kuwa wao ni Mitume wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, na kwa kuwa wametekeleza ibada Yake, na kuufikisha ujumbe Wake, na kuwanasihi waja Wake.
Na wenye ukaidi waliwakadhibisha Mitume wao wakidai kwamba Mitume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu si miongoni mwa binadamu! Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amelitaja dai hili, na akalibatilisha kwa kauli yake Mtukufu:
﴿وَمَا مَنَعَ ٱلنَّاسَ أَن يُؤۡمِنُوٓاْ إِذۡ جَآءَهُمُ ٱلۡهُدَىٰٓ إِلَّآ أَن قَالُوٓاْ أَبَعَثَ ٱللَّهُ بَشَرٗا رَّسُولٗا 94 قُل لَّوۡ كَانَ فِي ٱلۡأَرۡضِ مَلَٰٓئِكَةٞ يَمۡشُونَ مُطۡمَئِنِّينَ لَنَزَّلۡنَا عَلَيۡهِم مِّنَ ٱلسَّمَآءِ مَلَكٗا رَّسُولٗا 95﴾
"Na nini kilichowazuia watu kuamini ulipowajia uongofu isipokuwa walisema: 'Je! Mwenyezi Mungu humtuma mwanadamu kuwa ni Mtume?' Sema: Lau kuwa katika ardhi wangelikuwako Malaika wanao tembea kwa utulivu, basi tungeliwateremshia kutoka mbinguni Malaika kuwa ni Mtume." [Al-Israa: 94-95].
Basi Mwenyezi Mungu akabatilisha dai hili kwa kubainisha kwamba hapana budi Mtume awe wa jamii ya binadamu, kwa sababu ametumwa kwa watu wa ardhi nao ni wanadamu. Na lau kuwa watu wa ardhi wangelikuwa Malaika, bila ya shaka angeliwateremshia kutoka mbinguni Malaika awe Mtume wao, ili awe wa jinsi yao. Na hali kadhalika Mwenyezi Mungu Mtukufu ameeleza kuhusu waliokadhibisha Mitume kuwa walisema:
﴿...إِنۡ أَنتُمۡ إِلَّا بَشَرٞ مِّثۡلُنَا تُرِيدُونَ أَن تَصُدُّونَا عَمَّا كَانَ يَعۡبُدُ ءَابَآؤُنَا فَأۡتُونَا بِسُلۡطَٰنٖ مُّبِينٖ 10 قَالَتۡ لَهُمۡ رُسُلُهُمۡ إِن نَّحۡنُ إِلَّا بَشَرٞ مِّثۡلُكُمۡ وَلَٰكِنَّ ٱللَّهَ يَمُنُّ عَلَىٰ مَن يَشَآءُ مِنۡ عِبَادِهِۦۖ وَمَا كَانَ لَنَآ أَن نَّأۡتِيَكُم بِسُلۡطَٰنٍ إِلَّا بِإِذۡنِ ٱللَّهِۚ...﴾
"...Nyinyi si chochote ila ni wanadamu kama sisi. Mnataka kutuzuilia mbali na waliyokuwa wakiabudu baba zetu. Basi tuleteeni hoja iliyo wazi. Mitume wao wakawaambia: Sisi si chochote ila ni wanadamu kama nyinyi, lakini Mwenyezi Mungu humneemesha amtakaye katika waja wake. Wala hatuna uwezo wa kukuleteeni hoja ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu..." [Ibrahim: 10-11].
***
Kuamini Siku ya Mwisho
Siku ya mwisho ni Siku ya Kiyama ambayo watu watafufuliwa ndani yake kwa ajili ya kuulizwa juu ya matendo yao na kulipwa juu yake.
Na imeitwa hivyo kwa sababu hakuna siku nyingine baada yake; kwani baada ya hapo watatulizana watu wa Peponi katika makazi yao, na watu Motoni katika makazi yao.
Kuamini Siku ya Mwisho kunajumuisha mambo matatu:
La kwanza: Kuamini ufufuo. Nao ni kuwahuisha wafu litakapopulizwa baragumu mpulizo wa pili; kisha watu watasimama mbele ya Mola Mlezi wa walimwengu wote, wakiwa pekupeku, uchi, bila kutahiriwa, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...كَمَا بَدَأۡنَآ أَوَّلَ خَلۡقٖ نُّعِيدُهُۥۚ وَعۡدًا عَلَيۡنَآۚ إِنَّا كُنَّا فَٰعِلِينَ﴾
"Kama tulivyoanza umbo la mwanzo, tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika Sisi ni watendao." [Al-Anbiyaai: 104].
Na kufufuliwa ni haki iliyothabiti; ushahidi wake upo katika Kitabu, Sunna, na makubaliano ya Waislamu.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿ثُمَّ إِنَّكُم بَعۡدَ ذَٰلِكَ لَمَيِّتُونَ 15 ثُمَّ إِنَّكُمۡ يَوۡمَ ٱلۡقِيَٰمَةِ تُبۡعَثُونَ 16﴾
"Kisha hakika nyinyi baada ya hayo mtakufa. Kisha hakika nyinyi Siku ya Kiyama mtafufuliwa." [Al-Muminun: 15-16].
Amesema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie: "Siku ya Kiyama watu watakusanywa bila viatu, uchi, na wakiwa hawajatahiriwa."13. Wame kubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wake.
Waislamu wameafikiana juu ya kutokea kwake, na hilo ndilo matakwa ya hekima; kwani hekima inataka kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu awawekee viumbe hawa marejeo, ili awalipe humo kwa yale aliyoyaweka kuwa sheria kwao miongoni mwa yale aliyowatuma Mitume wake kwayo. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿أَفَحَسِبۡتُمۡ أَنَّمَا خَلَقۡنَٰكُمۡ عَبَثٗا وَأَنَّكُمۡ إِلَيۡنَا لَا تُرۡجَعُونَ 115﴾
"Je, mlidhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?" [Al-Mu’minun: 115]
Na akamwambia Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake:
﴿إِنَّ ٱلَّذِي فَرَضَ عَلَيۡكَ ٱلۡقُرۡءَانَ لَرَآدُّكَ إِلَىٰ مَعَادٖ...﴾
"Hakika aliyekulazimisha kuifuata Qur'ani, hapana shaka atakurudisha pahala pa marejeo..." [Al-Qasas: 85].
La pili: Kuamini kuhesabiwa na malipo. Mja atahesabiwa kwa matendo yake, na atalipwa kwa hayo. Na hilo limethibitishwa na Kitabu, na Sunna, na makubaliano ya Waislamu.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّ إِلَيۡنَآ إِيَابَهُمۡ 25 ثُمَّ إِنَّ عَلَيۡنَا حِسَابَهُم 26﴾
"Hakika ni kwetu Sisi ndio marejeo yao. Kisha ni juu yetu Sisi ndio hesabu yao." [Al-Ghashiya: 25-26] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿مَن جَآءَ بِٱلۡحَسَنَةِ فَلَهُۥ عَشۡرُ أَمۡثَالِهَاۖ وَمَن جَآءَ بِٱلسَّيِّئَةِ فَلَا يُجۡزَىٰٓ إِلَّا مِثۡلَهَا وَهُمۡ لَا يُظۡلَمُونَ 160﴾
"Afanyae wema, atalipwa mfano wake mara kumi. Na afanyae ubaya, hatalipwa ila sawa nao tu. Na wao hawatadhulumiwa." [Al-An'am: 160] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَنَضَعُ ٱلۡمَوَٰزِينَ ٱلۡقِسۡطَ لِيَوۡمِ ٱلۡقِيَٰمَةِ فَلَا تُظۡلَمُ نَفۡسٞ شَيۡـٔٗاۖ وَإِن كَانَ مِثۡقَالَ حَبَّةٖ مِّنۡ خَرۡدَلٍ أَتَيۡنَا بِهَاۗ وَكَفَىٰ بِنَا حَٰسِبِينَ 47﴾
"Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali, tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hesabu wa sawasawa." [Al-Anbiyaai: 47].
Na imesimuliwa kutoka kwa bin Omari, Mwenyezi Mungu awe radhi nao wote wawili, kwamba Mtume, rehema na amani ziwe juu yake na jamaa zake, alisema: "Atamsogeza Mwenyezi Mungu Muumini siku ya Kiyama, kisha atamuwekea pazia lake -yaani sitara yake- na amsitiri, kisha atasema: Je unalifahamu dhambi fulani? Je unalifahamu dhambi fulani? Atasema: 'Ndiyo Mola wangu Mlezi.' Mpaka atakapomtaka akiri madhambi yake, na akaona moyoni mwake kwamba ameangamia, atasema: 'Mimi niliyasitiri kwako madhambi haya duniani, na mimi leo hii ninakusamehe hayo.' Hapo atapewa faili la mema yake. Na ama makafiri na wanafiki, wataitwa hadharani mbele ya kadamnasi: 'Hawa ndio waliompinga Mwenyezi Mungu; Angalieni, laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu.'"14 Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wake.
Na ilithibiti kwa njia sahihi kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie: "Kwamba atakayekusudia kufanya jema kisha akalifanya, Mwenyezi Mungu humuandikia mema kumi mpaka ziada ya mia saba mpaka ziada nyingi zaidi. Na atakayekusudia kufanya jambo baya kisha akalifanya, Mwenyezi Mungu humu andikia dhambi moja."15
Na Waislamu wamekubaliana kwa kauli moja juu ya kuthibitisha hesabu na malipo juu ya matendo, na hilo ni matakwa ya hekima. Kwani Mwenyezi Mungu aliteremsha Vitabu na akawatuma Mitume, na akawa faradhishia waja wake kukubali yale waliyokuja nayo na kutenda yale yanayowapasa kutenda katika hayo, na akawajibisha kupigana na wanaompinga, na akahalalisha damu zao, kizazi chao, wanawake wao, na mali zao. Lau kusingekuwa na hesabu wala malipo, basi hili lingekuwa miongoni mwa mambo ya bure ambayo Mola Mwenye hekima ametakasika kutokana nalo. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ameashiria hilo kwa kauli yake:
﴿فَلَنَسۡـَٔلَنَّ ٱلَّذِينَ أُرۡسِلَ إِلَيۡهِمۡ وَلَنَسۡـَٔلَنَّ ٱلۡمُرۡسَلِينَ 6 فَلَنَقُصَّنَّ عَلَيۡهِم بِعِلۡمٖۖ وَمَا كُنَّا غَآئِبِينَ 7﴾
"Na kwa yakini tutawauliza wale waliopelekewa Ujumbe, na pia kwa yakini tutawauliza hao Wajumbe. Na kwa yakini tutawasomea kwa elimu yetu, na hatukuwa wenye kutokuwepo." [Al-A'raf: 6-7].
Ya tatu: Kuamini Pepo na Moto, na kuwa hizo ndizo hatima ya milele kwa viumbe.
Na Pepo ndiyo nyumba ya neema aliyoiandaa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ajili ya Waumini wacha Mungu, wale walioamini yale yote ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu amewalazimisha kuyaamini, na wakatekeleza utiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wakiwa ni wenye ikhlasi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na wakimfuata Mtume wake. Ndani yake kuna aina mbali mbali za neema. "Neema ambazo jicho halijawahi kuona wala sikio halikuwahi kusikia wala moyo wa mwanadamu yeyote haukuwahi kuyafikiria."16 Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّ ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَعَمِلُواْ ٱلصَّٰلِحَٰتِ أُوْلَٰٓئِكَ هُمۡ خَيۡرُ ٱلۡبَرِيَّةِ 7 جَزَآؤُهُمۡ عِندَ رَبِّهِمۡ جَنَّٰتُ عَدۡنٖ تَجۡرِي مِن تَحۡتِهَا ٱلۡأَنۡهَٰرُ خَٰلِدِينَ فِيهَآ أَبَدٗاۖ رَّضِيَ ٱللَّهُ عَنۡهُمۡ وَرَضُواْ عَنۡهُۚ ذَٰلِكَ لِمَنۡ خَشِيَ رَبَّهُۥ 8﴾
"Hakika walioamini na wakatenda mema, hao ndio bora wa viumbe. Malipo yao kwa Mola wao Mlezi ni Bustani za Milele zipitazo mito chini yake, wadumu humo milele. Mwenyezi Mungu ameridhika nao na wao wameridhika naye. Hayo ni kwa ajili ya anayemcha Mola wake Mlezi." [Al-Bayyina: 7-8] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿فَلَا تَعۡلَمُ نَفۡسٞ مَّآ أُخۡفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعۡيُنٖ جَزَآءَۢ بِمَا كَانُواْ يَعۡمَلُونَ17﴾
"Nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika hayo yanayofurahisha macho, ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyatenda." [Surat Sajda: 17].
Na ama Moto, huo ni nyumba ya adhabu ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu kaiandaa kwa ajili ya walio kufuru, madhalimu, waliomkufuru Yeye na kuwaasi Mitume wake. Humo kuna aina za adhabu na mateso ya kutisha yasiyokuja hata mawazoni.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَٱتَّقُواْ ٱلنَّارَ ٱلَّتِيٓ أُعِدَّتۡ لِلۡكَٰفِرِينَ 131﴾
"Na uogopeni Moto ambao umeandaliwa kwa ajili ya makafiri." [Al Imran: 131]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَقُلِ ٱلۡحَقُّ مِن رَّبِّكُمۡۖ فَمَن شَآءَ فَلۡيُؤۡمِن وَمَن شَآءَ فَلۡيَكۡفُرۡۚ إِنَّآ أَعۡتَدۡنَا لِلظَّٰلِمِينَ نَارًا أَحَاطَ بِهِمۡ سُرَادِقُهَاۚ وَإِن يَسۡتَغِيثُواْ يُغَاثُواْ بِمَآءٖ كَٱلۡمُهۡلِ يَشۡوِي ٱلۡوُجُوهَۚ بِئۡسَ ٱلشَّرَابُ وَسَآءَتۡ مُرۡتَفَقًا 29﴾
"Na sema: Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae. Hakika Sisi tumewaandalia wenye kudhulumu Moto ambao utawazingira kama hema. Na wakiomba msaada, wata saidiwa kwa kupewa maji kama mafuta yaliyotibuka. Yatakayowababua nyuso zao. Kinywaji hicho ni kiovu mno! Na matandiko hayo ya kupumzikia ni maovu mno!" [Al-Kahf: 29] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّ ٱللَّهَ لَعَنَ ٱلۡكَٰفِرِينَ وَأَعَدَّ لَهُمۡ سَعِيرًا 64 خَٰلِدِينَ فِيهَآ أَبَدٗاۖ لَّا يَجِدُونَ وَلِيّٗا وَلَا نَصِيرٗا 65 يَوۡمَ تُقَلَّبُ وُجُوهُهُمۡ فِي ٱلنَّارِ يَقُولُونَ يَٰلَيۡتَنَآ أَطَعۡنَا ٱللَّهَ وَأَطَعۡنَا ٱلرَّسُولَا۠ 66﴾
"Hakika Mwenyezi Mungu amewalaani makafiri na amewaandalia Moto unaowaka kwa nguvu. Wakae humo milele; hawatapata mlinzi wala msaidizi. Siku ambayo nyuso zao zitageuzwa katika Moto, watasema: 'Laiti tungalimtii Mwenyezi Mungu na tungalimtii Mtume!'" [Al-Ahzaab: 64-66]
Na kuamini Siku ya Mwisho kuna matunda adhimu, na miongoni mwa matunda hayo:
La kwanza: Shauku ya kufanya utiifu, na kuufanyia bidii; kwa kutafuta thawabu za siku hiyo.
Jambo la pili: Ni kuogopa kutenda maasi, na kuogopa kuridhia maasi; kwa kuogopa adhabu za siku hiyo.
La tatu: Maliwazo kwa Muumini kutokana na yale yanayompita miongoni mwa mambo ya dunia, akitarajia neema za Akhera na malipo yake.
Na kwa hakika wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu wameukataa ufufuo baada ya kifo; wakidai kwa ubatilifu kwamba hilo haliwezekani.
Na dai hili ni batili, ubatili wake umebainishwa na Sheria, na hisia na akili.
Ama kwa upande wa Sheria, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿زَعَمَ ٱلَّذِينَ كَفَرُوٓاْ أَن لَّن يُبۡعَثُواْۚ قُلۡ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبۡعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلۡتُمۡۚ وَذَٰلِكَ عَلَى ٱللَّهِ يَسِيرٞ 7﴾
"Wale waliokufuru wanadai kuwa hawatafufuliwa. Sema: Kwani? Naapa kwa Mola wangu Mlezi! Hapana shaka mtafufuliwa, na kisha hapana shaka mtaambiwa mliyoyatenda. Na hayo ni mepesi kwa Mwenyezi Mungu." [Surat Taghaabun: 7] Vitabu vyote vya mbinguni vimeafikiana juu ya hilo.
Na ama kwa upande wa hisia, hakika Mwenyezi Mungu amewaonyesha waja wake kuhuisha wafu katika maisha ya dunia hii. Na katika Suratul-Baqara ipo mifano mitano juu ya hilo, nayo ni:
Mfano wa kwanza: Kaumu ya Musa, amani iwe juu yake, walipomwambia:
﴿...لَن نُّؤۡمِنَ لَكَ حَتَّىٰ نَرَى ٱللَّهَ جَهۡرَةٗ ...﴾
"Hatutakuamini mpaka tumuone Mwenyezi Mungu waziwazi." (Al-Baqara: 55) Basi Mwenyezi Mungu Mtukufu akawafisha, kisha akawafufua. Na katika hilo amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu akiwasemesha Wana wa Israeli:
﴿وَإِذۡ قُلۡتُمۡ يَٰمُوسَىٰ لَن نُّؤۡمِنَ لَكَ حَتَّىٰ نَرَى ٱللَّهَ جَهۡرَةٗ فَأَخَذَتۡكُمُ ٱلصَّٰعِقَةُ وَأَنتُمۡ تَنظُرُونَ 55 ثُمَّ بَعَثۡنَٰكُم مِّنۢ بَعۡدِ مَوۡتِكُمۡ لَعَلَّكُمۡ تَشۡكُرُونَ 56﴾
"Na mliposema: 'Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumuone Mwenyezi Mungu waziwazi.' Ikakunyakueni radi nanyi mnaangalia. Kisha tukakufufueni baada ya kufa kwenu ili mpate kushukuru." [Al Baqara: 55-56].
Mfano wa pili: Katika kisa cha yule aliyeuawa ambaye juu yake Wana wa Israeli walibishana, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu akawaamuru wamchinje ng’ombe, kisha wampige huyo aliyeuawa kwa kipande cha ngo'ombe huyo; ili awajulishe ni nani aliyemuua. Na katika hilo anasema Yeye Mtukufu:
﴿وَإِذۡ قَتَلۡتُمۡ نَفۡسٗا فَٱدَّٰرَٰءۡتُمۡ فِيهَاۖ وَٱللَّهُ مُخۡرِجٞ مَّا كُنتُمۡ تَكۡتُمُونَ 72 فَقُلۡنَا ٱضۡرِبُوهُ بِبَعۡضِهَاۚ كَذَٰلِكَ يُحۡيِ ٱللَّهُ ٱلۡمَوۡتَىٰ وَيُرِيكُمۡ ءَايَٰتِهِۦ لَعَلَّكُمۡ تَعۡقِلُونَ73﴾
"Na mlipomuuwa mtu, kisha mkahitilafiana kwayo, na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyatoa hayo mliyo kuwa mkiyaficha. Basi tukasema: 'Mpigeni kwa baadhi yake.' Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu huwahuisha wafu na anakuonyesheni ishara zake ili mpate kufahamu." [Al-Baqara: 72-73].
Mfano wa tatu: Katika kisa cha wale waliokimbia kutoka ardhi yao na nyumba zao, wakiwa ni maelfu kwa maelfu, wakiyakimbia mauti; basi Mwenyezi Mungu aliyetukuka akawafisha, kisha akawahuisha. Na kuhusu hilo, Mwenyezi Mungu aliyetukuka anasema:
﴿أَلَمۡ تَرَ إِلَى ٱلَّذِينَ خَرَجُواْ مِن دِيَٰرِهِمۡ وَهُمۡ أُلُوفٌ حَذَرَ ٱلۡمَوۡتِ فَقَالَ لَهُمُ ٱللَّهُ مُوتُواْ ثُمَّ أَحۡيَٰهُمۡۚ إِنَّ ٱللَّهَ لَذُو فَضۡلٍ عَلَى ٱلنَّاسِ وَلَٰكِنَّ أَكۡثَرَ ٱلنَّاسِ لَا يَشۡكُرُونَ 243﴾
"Hukuwaona wale waliotoka majumbani kwao kwa maelfu kwa kuogopa mauti? Mwenyezi Mungu akawaambia: 'Kufeni!' Kisha akawahauisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya watu, lakini wengi wa watu hawashukuru." [Al-Baqara: 243].
Mfano wa nne: Katika kisa cha yule aliyepita kwenye kijiji kilichokuwa kimekufa, akaona kuwa ni jambo lililo mbali kwamba Mwenyezi Mungu atakihuisha kijiji hicho; basi Mwenyezi Mungu akamfisha miaka mia moja, kisha akamhuisha. Na katika hilo Mwenyezi Mungu anasema:
﴿أَوۡ كَٱلَّذِي مَرَّ عَلَىٰ قَرۡيَةٖ وَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا قَالَ أَنَّىٰ يُحۡيِۦ هَٰذِهِ ٱللَّهُ بَعۡدَ مَوۡتِهَاۖ فَأَمَاتَهُ ٱللَّهُ مِاْئَةَ عَامٖ ثُمَّ بَعَثَهُۥۖ قَالَ كَمۡ لَبِثۡتَۖ قَالَ لَبِثۡتُ يَوۡمًا أَوۡ بَعۡضَ يَوۡمٖۖ قَالَ بَل لَّبِثۡتَ مِاْئَةَ عَامٖ فَٱنظُرۡ إِلَىٰ طَعَامِكَ وَشَرَابِكَ لَمۡ يَتَسَنَّهۡۖ وَٱنظُرۡ إِلَىٰ حِمَارِكَ وَلِنَجۡعَلَكَ ءَايَةٗ لِّلنَّاسِۖ وَٱنظُرۡ إِلَى ٱلۡعِظَامِ كَيۡفَ نُنشِزُهَا ثُمَّ نَكۡسُوهَا لَحۡمٗاۚ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُۥ قَالَ أَعۡلَمُ أَنَّ ٱللَّهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيۡءٖ قَدِيرٞ 259﴾
"Au kama yule aliyepita karibu na mji uliokwisha kuwa magofu tu, akasema: 'Ataufufuaje Mwenyezi Mungu mji huu baada ya kufa kwake?' Basi Mwenyezi Mungu alimfisha yeye muda wa miaka mia. Kisha akamfufua. Akamuuliza: 'Je umekaa muda gani?' Akajibu: 'Labda nimekaa siku moja au sehemu ya siku.' Akamwambia: Bali umekaa miaka mia wewe. Hebu angalia chakula chako na vinywaji vyako, havikuharibika. Na muangalie punda wako. Na ili tukufanye uwe ni Ishara kwa watu iangalie hii mifupa yake jinsi tunavyoinyanyua kisha tunaivisha nyama. Basi yalipo mbainikia alinena: 'Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.'" [Al-Baqara: 259].
Mfano wa tano: Katika kisa cha Ibrahim, mwandani wa Mwenyezi Mungu, alipomuomba Mwenyezi Mungu amuonyeshe jinsi anavyowafufua wafu; Mwenyezi Mungu akamuamrisha achinje ndege wanne, na awagawanye vipande vipande na kuvitawanya juu ya milima iliyo mzunguka, kisha awaite; basi vile vipande vikajumuika, kila kipande kikarudia vyenzake, nao wakamjia Ibrahim mbio. Na katika hilo Mwenyezi Mungu anasema:
﴿وَإِذۡ قَالَ إِبۡرَٰهِـۧمُ رَبِّ أَرِنِي كَيۡفَ تُحۡيِ ٱلۡمَوۡتَىٰۖ قَالَ أَوَلَمۡ تُؤۡمِنۖ قَالَ بَلَىٰ وَلَٰكِن لِّيَطۡمَئِنَّ قَلۡبِيۖ قَالَ فَخُذۡ أَرۡبَعَةٗ مِّنَ ٱلطَّيۡرِ فَصُرۡهُنَّ إِلَيۡكَ ثُمَّ ٱجۡعَلۡ عَلَىٰ كُلِّ جَبَلٖ مِّنۡهُنَّ جُزۡءٗا ثُمَّ ٱدۡعُهُنَّ يَأۡتِينَكَ سَعۡيٗاۚ وَٱعۡلَمۡ أَنَّ ٱللَّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٞ 260﴾
"Na aliposema Ibrahim: 'Mola wangu Mlezi! Nionyeshe vipi unavyofufua wafu.' Mwenyezi Mungu akasema: 'Kwani huamini?' Akasema: 'Hasha! Lakini ili moyo wangu utue.' Akamwambia: Twaa ndege wanne na uwazoeshe kwako, kisha uweke juu ya kila kilima sehemu katika hao, kisha waite, watakujia mbio. Na ujue kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, na Mwenye hekima." [Al-Baqara: 260].
Hii ni mifano ya wazi iliyotokea inayoonyesha uwezekano wa kuhuisha wafu. Na imeshatangulia kutajwa yale aliyoyaweka Mwenyezi Mungu katika miujiza ya Issa bin Maryam: kuhuisha wafu na kuwatoa kutoka makaburini mwao, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu .
Ama ushahidi wa kiakili ni kwa namna mbili:
Mojawapo miongoni mwa hizo: kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye Muumba wa mbingu na ardhi, na vyote vilivyomo ndani yake, Muumba wao kwa kuanzisha kwa mara ya kwanza; na Mwenye uwezo wa kuanzisha uumbaji hawezi kushindwa kuurejesha tena. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَهُوَ ٱلَّذِي يَبۡدَؤُاْ ٱلۡخَلۡقَ ثُمَّ يُعِيدُهُۥ وَهُوَ أَهۡوَنُ عَلَيۡهِ...﴾
"Na Yeye ndiye anayeanzisha uumbaji, kisha ataurudisha mara nyingine. Na jambo hili ni jepesi zaidi kwake." [Ar-Rum: 27]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...كَمَا بَدَأۡنَآ أَوَّلَ خَلۡقٖ نُّعِيدُهُۥۚ وَعۡدًا عَلَيۡنَآۚ إِنَّا كُنَّا فَٰعِلِينَ﴾
"Kama tulivyoanza umbo la mwanzo, tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika Sisi ni watendao." [Al-Anbiyaai: 104]. Na akasema, akiamrisha kumjibu mwenye kukana kuhuishwa kwa mifupa nayo imekwisha mung'unyika:
﴿قُلۡ يُحۡيِيهَا ٱلَّذِيٓ أَنشَأَهَآ أَوَّلَ مَرَّةٖۖ وَهُوَ بِكُلِّ خَلۡقٍ عَلِيمٌ 79﴾
"Sema: Ataihuisha huyo huyo aliyeiumba hapo mara ya mwanzo. Na Yeye ni Mwenye kujua zaidi kila kuumba." [Yaasin: 79].
La pili: Kwamba ardhi huwa imekufa imetulia kimya, haina mti wa majani mabichi; lakini yanapoteremka juu yake maji ya mvua, husisimka ikawa kijani hai, na ndani yake huota kila namna ya mimea mizuri. Na aliyeweza kuihuisha baada ya kufa kwake ana uwezo wa kuhuisha wafu. Mwenyezi Mungu alisema:
﴿وَمِنۡ ءَايَٰتِهِۦٓ أَنَّكَ تَرَى ٱلۡأَرۡضَ خَٰشِعَةٗ فَإِذَآ أَنزَلۡنَا عَلَيۡهَا ٱلۡمَآءَ ٱهۡتَزَّتۡ وَرَبَتۡۚ إِنَّ ٱلَّذِيٓ أَحۡيَاهَا لَمُحۡيِ ٱلۡمَوۡتَىٰٓۚ إِنَّهُۥ عَلَىٰ كُلِّ شَيۡءٖ قَدِيرٌ 39﴾
"Na katika Ishara zake ni kwamba unaiona ardhi nyonge, lakini tunapoiteremshia maji, mara unaiona inataharaki na kuumuka. Bila ya shaka aliyeihuisha ardhi ndiye atakayehuisha wafu. Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu." [Fusswilat: 39] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَنَزَّلۡنَا مِنَ ٱلسَّمَآءِ مَآءٗ مُّبَٰرَكٗا فَأَنۢبَتۡنَا بِهِۦ جَنَّٰتٖ وَحَبَّ ٱلۡحَصِيدِ 9 وَٱلنَّخۡلَ بَاسِقَٰتٖ لَّهَا طَلۡعٞ نَّضِيدٞ 10 رِّزۡقٗا لِّلۡعِبَادِۖ وَأَحۡيَيۡنَا بِهِۦ بَلۡدَةٗ مَّيۡتٗاۚ كَذَٰلِكَ ٱلۡخُرُوجُ 11﴾
"Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji yaliyo barikiwa, na kwa hayo tukaotesha mabustani na nafaka za kuvunwa na mitende mirefu yenye matunda yaliyopangika vizuri, (iwe) riziki kwa waja. Na tumehuisha kwa hayo nchi iliyokufa. Hivi ndivyo kufufuliwa kutakavyo kuwa." [Surat Qaaf: 9-11]
Na inaingia katika kuamini Siku ya Mwisho, kuamini yote yatakayotokea baada ya kifo, kama vile:
(a) Majaribu ya kaburini: Nayo ni kuulizwa maiti baada ya kuzikwa kuhusu Mola wake, dini yake, na Nabii wake. Hapo, Mwenyezi Mungu huwapa uimara wale walioamini kwa kauli thabiti, naye husema: 'Mola wangu Mlezi ni Mwenyezi Mungu, dini yangu ni Uislamu, na Nabii wangu ni Muhammadi, rehema na amani ziwe juu yake.' Na Mwenyezi Mungu anawapoteza madhalimu, basi atasema kafiri: 'Haa, haa, sijui.' Na atasema mnafiki au mwenye shaka: 'Sijui; niliwasikia watu wakisema jambo fulani, nikalisema.'
(b) Adhabu za kaburi na neema zake: Hivyo adhabu ya kaburini itakuwa kwa madhalimu miongoni mwa wanafiki na waliokufuru. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...وَلَوۡ تَرَىٰٓ إِذِ ٱلظَّٰلِمُونَ فِي غَمَرَٰتِ ٱلۡمَوۡتِ وَٱلۡمَلَٰٓئِكَةُ بَاسِطُوٓاْ أَيۡدِيهِمۡ أَخۡرِجُوٓاْ أَنفُسَكُمُۖ ٱلۡيَوۡمَ تُجۡزَوۡنَ عَذَابَ ٱلۡهُونِ بِمَا كُنتُمۡ تَقُولُونَ عَلَى ٱللَّهِ غَيۡرَ ٱلۡحَقِّ وَكُنتُمۡ عَنۡ ءَايَٰتِهِۦ تَسۡتَكۡبِرُونَ﴾
"...Na lau ungeliwaona madhalimu wanavyokuwa katika mahangaiko ya mauti, na Malaika wamewanyooshea mikono yao wakiwaambia: 'Zitoeni roho zenu! Leo mtalipwa adhabu ya fedheha kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyasema juu ya Mwenyezi Mungu yasiyo ya haki, na mlivyokuwa mkizifanyia kiburi Ishara zake.'" [Al-An'am: 93].
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu watu wa Firauni:
﴿ٱلنَّارُ يُعۡرَضُونَ عَلَيۡهَا غُدُوّٗا وَعَشِيّٗاۚ وَيَوۡمَ تَقُومُ ٱلسَّاعَةُ أَدۡخِلُوٓاْ ءَالَ فِرۡعَوۡنَ أَشَدَّ ٱلۡعَذَابِ 46﴾
"Wanaonyeshwa Moto asubuhi na jioni. Na itapofika Saa ya Kiyama patasemwa: 'Waingizeni watu wa Firauni katika adhabu kali kabisa!'" [Ghafir: 46].
Na katika Sahihi Muslim, kutoka katika hadithi ya Zaidi bin Thabit, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: Basi laiti nisingeogopea kuwa mtaacha kuzikana, basi ningemuomba Mwenyezi Mungu akusikilizisheni sehemu ya adhabu za kaburi ninayoisikia. Kisha akaelekea kwa uso wake, akasema: "Jikingeni kwa Mwenyezi Mungu kutokana na adhabu ya Moto." Wakasema: 'Tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu dhidi ya adhabu ya Motoni.' Akasema: "Jilindeni kwa Mwenyezi Mungu kutokana na adhabu za kaburi." Wakasema: 'Tunaomba hifadhi kwa Mwenyezi Mungu kutokana na adhabu ya kaburi.' Akasema: "Jikingeni kwa Mwenyezi Mungu kutokana na majaribu, yaliyo dhahiri na yaliyofichika." Wakasema: 'Tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na majaribu yote, ya dhahiri na yaliyofichika.' Akasema: "Tafuteni hifadhi kwa Mwenyezi Mungu kutokana na majaribu ya Masihi Dajali." Wakasema: 'Tunajikinga kwa Mwenyezi Mungu kutokana na majaribu ya (Masihi) Dajali.'17
Ama kuhusu neema za kaburi, hizo ni kwa Waumini wakweli. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّ ٱلَّذِينَ قَالُواْ رَبُّنَا ٱللَّهُ ثُمَّ ٱسۡتَقَٰمُواْ تَتَنَزَّلُ عَلَيۡهِمُ ٱلۡمَلَٰٓئِكَةُ أَلَّا تَخَافُواْ وَلَا تَحۡزَنُواْ وَأَبۡشِرُواْ بِٱلۡجَنَّةِ ٱلَّتِي كُنتُمۡ تُوعَدُونَ 30﴾
"Hakika waliosema: 'Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu!' Kisha wakanyooka sawa, hao Malaika huwa teremkia wakawaambia: 'Msiogope, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa.'" [Fusswilat: 30]
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿فَلَوۡلَآ إِذَا بَلَغَتِ ٱلۡحُلۡقُومَ 83 وَأَنتُمۡ حِينَئِذٖ تَنظُرُونَ 84 وَنَحۡنُ أَقۡرَبُ إِلَيۡهِ مِنكُمۡ وَلَٰكِن لَّا تُبۡصِرُونَ 85 فَلَوۡلَآ إِن كُنتُمۡ غَيۡرَ مَدِينِينَ 86 تَرۡجِعُونَهَآ إِن كُنتُمۡ صَٰدِقِينَ 87 فَأَمَّآ إِن كَانَ مِنَ ٱلۡمُقَرَّبِينَ 88 فَرَوۡحٞ وَرَيۡحَانٞ وَجَنَّتُ نَعِيمٖ 89﴾
"Yawaje basi itakapofika roho kwenye koo, na ninyi wakati huo mnatazama. Na Sisi tuko karibu naye kuliko ninyi, lakini hamuoni. Na lau kuwa nyinyi hamtalipwa. Kwa nini hamuirudishi hiyo roho, ikiwa nyinyi mnasema kweli? Kwa hivyo, akiwa miongoni mwa wale walio karibu na Mwenyezi Mungu. Basi ni raha, na manukato, na Bustani zenye neema." [Al-Waqi’ah: 83-89]
Imesimuliwa kutoka kwa Baraa bin Aazib -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- kuwa: Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu -rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- alisema kuhusu Muumini anapo wajibu Malaika wawili kaburini mwake: "Atanadi mwenye kunadi kutoka mbinguni: 'Hakika mja wangu amesema ukweli; basi mtandikieni tandiko kutoka katika Pepo, na mvisheni vazi kutoka katika mavazi ya Peponi, na mfungulieni mlango wa kuelekea Peponi.' Akasema: 'Basi humfikia hewa yake yenye raha na manukato yake, na kupanuliwa kaburi lake kwa umbali wa mwisho wa kuangalia kwa macho yake.'" Kaipokea Ahmad na Abuu Daud katika hadithi ndefu.18
Na kwa hakika wamepotea baadhi ya watu wenye upotovu; wakakanusha adhabu za kaburi na neema zake, wakidai kwamba hilo haliwezekani kwa kuwa linakwenda kinyume na hali halisi. Wakasema: 'Lau maiti angefunuliwa katika kaburi lake, angepatikana yuko kama alivyokuwa, na kaburi halijabadilika kuwa pana wala kuwa na finyu.'
Na madai haya ni batili kisheria, kihisia, na kiakili:
Ama upande wa Sheria, tayari yamesha tangulia maandiko yanayoonyesha kuthibiti kwa adhabu za kaburi na neema zake.
Na katika Sahihi ya Bukhari, kutoka katika hadithi ya bin Abbas -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao- amesema: "Siku moja, Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alipokuwa anapita katika moja ya maeneo ya makaburi ya Madina, alisikia sauti za watu wawili ambao walikuwa wanaadhibiwa ndani ya makaburi yao" na imetajwa hadithi hiyo, na ndani yake: "Kwamba mmoja wao hakuwa akijisitiri kutokana na mkojo." Na katika upokezi mwingine: "Kutokana na mkojo wake." "Na kwamba mwingine alikuwa akitembea kwa uchonganishi." Na katika mapokezi ya Muslim: "Hakuwa akijitahadhari mbali na mkojo."19
Ama kuhusu hisia, basi mtu aliyelala huona usingizini mwake kwamba alikuwa katika mahali penye wasaa, mahali pa kupendeza, ananeemeka humo; au kwamba alikuwa katika mahali pa finyu pa kuogofya, akawa anaumia kutokana nalo; na huenda wakati mwingine akaamka kutokana na alichokiona. Na pamoja na hayo, yuko juu ya kitanda chake katika chumba chake kama alivyo; na usingizi ni ndugu ya kifo; na kwa sababu hiyo Mwenyezi Mungu Mtukufu ameuita "kuchukuliwa roho". Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿ٱللَّهُ يَتَوَفَّى ٱلۡأَنفُسَ حِينَ مَوۡتِهَا وَٱلَّتِي لَمۡ تَمُتۡ فِي مَنَامِهَاۖ فَيُمۡسِكُ ٱلَّتِي قَضَىٰ عَلَيۡهَا ٱلۡمَوۡتَ وَيُرۡسِلُ ٱلۡأُخۡرَىٰٓ إِلَىٰٓ أَجَلٖ مُّسَمًّى...﴾
"Mwenyezi Mungu huzipokea roho zinapokufa. Na zile zisizokufa wakati wa kulala kwake, huzishika zilizohukumiwa kufa, na huzirudisha nyingine mpaka ufike wakati uliowekwa..." [Az-Zumar: 42].
Ama kwa upande wa akili, basi hakika mwenye kulala katika usingizi wake huona ndoto ya kweli inayolingana na uhalisia, na huenda akamuona Mtume rehema na amani ziwe juu yake kwa sifa yake. Na atakayemuona kwa sifa yake, basi amemuona kweli. Na pamoja na hayo, mwenye kulala katika chumba chake juu ya kitanda chake yuko mbali na alichokiona. Hivyo, ikiwa hili linawezekana katika hali za dunia, basi je, halitakuwa jambo linalowezekana katika hali za Akhera?!
Ama kutegemea kwao katika madai yao kwamba lau angefunuliwa maiti katika kaburi lake angepatikana kama alivyokuwa, na kaburi halikubadilika kwa upana wala kwa ufinyu, basi jibu lake ni kwa njia kadhaa, miongoni mwake ni:
Namna ya kwanza: Ni kwamba haijuzu kupinga yale yaliyokuja na Sheria kwa kutumia mambo yenye kutatiza ya aina hii yaliyo batili. Kwani lau anayepinga kwa hayo angeyatafakari vilivyo yale yaliyokuja na Sheria, angeli tambua ubatili wa mambo haya yenye kutatiza. Na imesemwa:
'Na ni wangapi wanaokosoa kauli sahihi,
Na ilhali dosari yake inatokana na ufahamu (wake) mbovu.'
Jambo la pili: Kwamba hali za Barazahi ni miongoni mwa mambo ya ghaibu ambayo hayadirikiwi kwa hisia. Na lau yangekuwa yanadirikiwa kwa hisia, basi manufaa ya kuamini ghaibu yangepotea, na wale wanaoamini ghaibu na wanaokanusha wangekuwa sawa katika kuyasadikisha.
Ya tatu: Kwamba adhabu, na raha, na upana wa kaburi, na kubana kwake, ni maiti peke yake ndiye anayeyapitia, si mwingine yeyote. Na hili ni kama anavyoona anayelala katika usingizi wake kuwa yuko katika mahali penye kubana na ukiwa, au katika mahali pana penye furaha, na waliomzunguka hawalioni hilo wala hawalihisi. Na kwa yakini Mtume rehema na amani ziwe juu yake alikuwa akiteremshiwa Wahyi akiwa katikati ya Maswahaba wake, basi yeye akawa anasikia Wahyi, na Maswahaba hawasikii. Na mara nyingine Malaika alikuwa akijidhihirisha kwake kwa sura ya mwanamume akamsemesha, na Maswahaba hawamuoni huyo Malaika, wala hawamsikii.
La nne: Utambuzi wa viumbe umewekewa mipaka kwa yale tu ambayo Mwenyezi Mungu aliyetukuka amewawezesha kuyatambua; wala haiwezekani kwao kutambua kila kilichopo. Basi mbingu saba, na ardhi, na waliomo humo, na kila kitu, vyote vinamtakasa Mwenyezi Mungu kwa sifa zake, kwa kutakasa kwa hakika; na Mwenyezi Mungu aliyetukuka huwasikizisha hilo awatakao miongoni mwa viumbe wake wakati mwingine. Na pamoja na hayo, hilo limefichika kwetu; na katika hilo anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿تُسَبِّحُ لَهُ ٱلسَّمَٰوَٰتُ ٱلسَّبۡعُ وَٱلۡأَرۡضُ وَمَن فِيهِنَّۚ وَإِن مِّن شَيۡءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمۡدِهِۦ وَلَٰكِن لَّا تَفۡقَهُونَ تَسۡبِيحَهُمۡۚ...﴾
"Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vyote vilivyomo ndani yake. Na hapana kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake. Lakini nyinyi hamfahamu kutakasa kwake." [Al-Israa: 44] Na vivyo hivyo mashetani na majini huzunguka katika ardhi huku na huko. Na hakika majini walihudhuria kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wakamsikiliza akisoma Qur’ani, wakanyamaza, kisha walirudi kwa kaumu yao kwenda kuwaonya; na pamoja na hayo wao wamefichwa mbali nasi. Na kuhusu hilo Mwenyezi Mungu aliyetukuka anasema:
﴿يَٰبَنِيٓ ءَادَمَ لَا يَفۡتِنَنَّكُمُ ٱلشَّيۡطَٰنُ كَمَآ أَخۡرَجَ أَبَوَيۡكُم مِّنَ ٱلۡجَنَّةِ يَنزِعُ عَنۡهُمَا لِبَاسَهُمَا لِيُرِيَهُمَا سَوۡءَٰتِهِمَآۚ إِنَّهُۥ يَرَىٰكُمۡ هُوَ وَقَبِيلُهُۥ مِنۡ حَيۡثُ لَا تَرَوۡنَهُمۡۗ إِنَّا جَعَلۡنَا ٱلشَّيَٰطِينَ أَوۡلِيَآءَ لِلَّذِينَ لَا يُؤۡمِنُونَ 27﴾
"Enyi wanadamu! Asije Shetani kukufitinini kama alivyowatoa wazazi wenu Peponi, akawavua nguo zao kuwaonyesha tupu zao. Hakika yeye na kabila yake wanakuoneni, na nyinyi hamuwaoni. Hakika Sisi tumewafanya Mashetani kuwa ni marafiki wa wasioamini." [Al-A'araf: 27] Ikiwa viumbe hawakifikii kila kilichopo, basi haijuzu wao kukanusha yale yaliyothibiti katika mambo ya ghaibu, ijapokuwa hawajayafikia.
***
Kuamini Kadari
Neno Kadari (kwa kuweka vokali 'a' kwenye ‘daal’) ni mipango na kukadiria kwa Mwenyezi Mungu aliyetukuka juu ya viumbe, kulingana na yale yaliyotangulia katika elimu yake, na kama ilivyotakikana na hekima yake.
Na kuamini Kadari, kunaingia ndani yake kuamini mambo manne:
Jambo la kwanza: Kuamini kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwenye kujua kila kitu, kwa ujumla na kwa undani, tangu azali mpaka abadi, iwe ni yale yanayohusiana na vitendo vyake, au vitendo vya waja wake.
Jambo la pili: Kuamini kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu aliandika hilo katika Ubao uliohifadhiwa, na kuhusu mambo haya mawili anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿أَلَمۡ تَعۡلَمۡ أَنَّ ٱللَّهَ يَعۡلَمُ مَا فِي ٱلسَّمَآءِ وَٱلۡأَرۡضِۚ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَٰبٍۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى ٱللَّهِ يَسِيرٞ 70﴾
"Je, hujui kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na ardhini? Hakika hayo yamo Kitabuni. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi." [Al-Hajj: 70].
Na imesimuliwa katika Sahihi Muslim kutoka kwa Abdullahi bin Amru bin Aaswi radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na baba yake kuwa alisema: Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe juu yake akisema: "Mwenyezi Mungu aliandika Kadari (Mipango) ya viumbe kabla ya kuumba mbingu na ardhi kwa miaka elfu hamsini."20
Jambo la tatu: Ni kuamini kwamba kila kilichopo hakiwi ila kwa utashi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, iwe ni katika yale yanayohusiana na vitendo vyake au yanayohusiana na vitendo vya viumbe wake. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu yale yanayohusu vitendo vyake:
﴿وَرَبُّكَ يَخۡلُقُ مَا يَشَآءُ وَيَخۡتَارُ...﴾
"Na Mola wako Mlezi huumba na huteuwa atakavyo..." [Al-Qasas: 68] Na alisema:
﴿...وَيَفۡعَلُ ٱللَّهُ مَا يَشَآءُ﴾
"Na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo." [Ibrahim: 27] Na alisema:
﴿هُوَ ٱلَّذِي يُصَوِّرُكُمۡ فِي ٱلۡأَرۡحَامِ كَيۡفَ يَشَآءُ...﴾
"Yeye ndiye anayekuundeni ndani ya matumbo ya wazazi kwa namna apendayo..." [Al Imran: 6] Na Amesema Mtukufu kuhusu matendo ya viumbe:
﴿...وَلَوۡ شَآءَ ٱللَّهُ لَسَلَّطَهُمۡ عَلَيۡكُمۡ فَلَقَٰتَلُوكُمۡ...﴾
"...Na lau angelipenda Mwenyezi Mungu, angeliwapa nguvu dhidi yenu wakapigana nanyi..." [An-Nisaa: 90] Na alisema:
﴿...وَلَوۡ شَآءَ رَبُّكَ مَا فَعَلُوهُۖ فَذَرۡهُمۡ وَمَا يَفۡتَرُون﴾
"Na angelipenda Mola wako Mlezi, wasingelifanya hayo. Basi waache na wanayoyazua." [Al-An'am: 112].
Jambo la Nne: Kuamini kuwa kila kilichopo kimeumbwa. Alikiumba Mwenyezi Mungu Mtukufu, na aliumba dhati yake, na sifa zake, na harakati zake, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿ٱللَّهُ خَٰلِقُ كُلِّ شَيۡءٖۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيۡءٖ وَكِيلٞ 62﴾
"Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu, na Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu." [Az-Zumar: 62] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...وَخَلَقَ كُلَّ شَيۡءٖ فَقَدَّرَهُۥ تَقۡدِيرٗا﴾
"...na akaumba kila kitu na akakikadiria kwa kipimo." [Al-Furqan: 2] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu Nabii wake Ibrahim, amani iwe juu yake, kwamba aliwaambia watu wake:
﴿وَٱللَّهُ خَلَقَكُمۡ وَمَا تَعۡمَلُونَ 96﴾
"Na hali Mwenyezi Mungu ndiye aliyekuumbeni nyinyi na hivyo mnavyovifanya!" [As-Saffat: 96].
Na kuamini Kadari - kama tulivyoeleza - si kinyume na kuwa mja anayo matashi katika matendo yake ya hiari, na anao uwezo wa kuyatekeleza. Kwa sababu Sheria na uhalisia vinatoa ushahidi juu ya kulithibitisha hilo kwake.
Ama Sheria, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema katika kutaka:
﴿...فَمَن شَآءَ ٱتَّخَذَ إِلَىٰ رَبِّهِۦ مَـَٔابًا﴾
"Basi anayetaka, na ashike njia arejee kwa Mola wake Mlezi." [Al-Nabaa: 39]. Na alisema:
﴿...فَأۡتُواْ حَرۡثَكُمۡ أَنَّىٰ شِئۡتُمۡ...﴾
"...Basi ziendeeni konde zenu mtakavyo..." [Al-Baqara: 223] Na alisema katika kueleza uwezo:
﴿فَٱتَّقُواْ ٱللَّهَ مَا ٱسۡتَطَعۡتُمۡ وَٱسۡمَعُواْ وَأَطِيعُواْ...﴾
"Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo, na sikieni, na tiini..." [At-Taghabun: 16] Na alisema:
﴿لَا يُكَلِّفُ ٱللَّهُ نَفۡسًا إِلَّا وُسۡعَهَاۚ لَهَا مَا كَسَبَتۡ وَعَلَيۡهَا مَا ٱكۡتَسَبَتۡ...﴾
"Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kiasi cha iwezavyo. Faida ya iliyoyachuma ni yake, na hasara ya iliyoyachuma ni juu yake pia." [Al-Baqara: 286].
Ama hali halisi, basi hakika kila mwanadamu anajua kuwa ana utashi na uwezo; kwa utashi huo na uwezo huo hutenda, na kwa vyote viwili huacha. Na hutofautisha kati ya linalotokea kwa utashi wake kama vile kutembea, na linalotokea bila utashi wake kama vile kutetemeka. Lakini utashi wa mja na uwezo wake hutokea kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwa uwezo wake; kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿لِمَن شَآءَ مِنكُمۡ أَن يَسۡتَقِيمَ 28 وَمَا تَشَآءُونَ إِلَّآ أَن يَشَآءَ ٱللَّهُ رَبُّ ٱلۡعَٰلَمِينَ 29﴾
"Kwa yule miongoni mwenu anayetaka kwenda sawa. Na hamtaki ila atake Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote." [At-Takwir: 28-29] Na kwa kuwa ulimwengu wote uko chini ya ufalme wa Mwenyezi Mungu Mtukufu; basi hakuna kitu chochote kinachokuwapo katika ufalme wake bila ya elimu ya Mwenyezi Mungu na matashi ya Mwenyezi Mungu.
Na kuamini Kadari - kama tulivyoeleza - hakumpi mja hoja ya kuacha yale yaliyo wajibu, au ya kufanya dhambi. Basi kwa msingi huo, kutumia Kadari kama hoja ni batili kwa pande nyingi:
La kwanza: Kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿سَيَقُولُ ٱلَّذِينَ أَشۡرَكُواْ لَوۡ شَآءَ ٱللَّهُ مَآ أَشۡرَكۡنَا وَلَآ ءَابَآؤُنَا وَلَا حَرَّمۡنَا مِن شَيۡءٖۚ كَذَٰلِكَ كَذَّبَ ٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِهِمۡ حَتَّىٰ ذَاقُواْ بَأۡسَنَاۗ قُلۡ هَلۡ عِندَكُم مِّنۡ عِلۡمٖ فَتُخۡرِجُوهُ لَنَآۖ إِن تَتَّبِعُونَ إِلَّا ٱلظَّنَّ وَإِنۡ أَنتُمۡ إِلَّا تَخۡرُصُونَ 148﴾
"Watasema wale walioshirikisha: 'Lau kuwa Mwenyezi Mungu angetaka, tusingelishirikisha sisi wala baba zetu, wala tusingeliharamisha kitu chochote.' Vivi hivi ndivyo walivyokanusha wale waliokuwa kabla yao mpaka walipoonja adhabu yetu. Sema: 'Je, nyinyi mnayo elimu mtutolee? Nyinyi hamfuati ila dhana. Wala hamsemi ila uongo tu.'" [Al-An'am: 148] Na lau kama Kadari ingelikuwa ni hoja kwao, basi Mwenyezi Mungu asingeliwaonjesha adhabu yake.
Ya pili: Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿رُّسُلٗا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى ٱللَّهِ حُجَّةُۢ بَعۡدَ ٱلرُّسُلِۚ وَكَانَ ٱللَّهُ عَزِيزًا حَكِيمٗا 165﴾
"Mitume hao ni wabashiri na waonyaji, ili watu wasiwe na hoja juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kuletewa Mitume. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima." [An-Nisaai: 165]. Na lau Kadari ingelikuwa ni hoja ya kisingizio kwa wanao kwenda kinyume, isingeliondolewa kwa kuwatuma Mitume; kwani uhalifu baada ya kuwatuma Mitume hutokea kwa Kadari ya Mwenyezi Mungu aliyetukuka.
Ya tatu: Kile kilichopokelewa na Bukhari na Muslim -na lafudhi ni ya Bukhari- kutoka kwa Ally bin Abi Twalib -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- kwamba Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- amesema: "Hakuna yeyote miongoni mwenu isipokuwa amesha andikiwa makao yake Motoni au makao yake Peponi." Bwana mmoja miongoni mwa watu hao akasema: 'Je, kwa nini tusitegemee tu, ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu?' Akasema: La, fanyeni matendo. Kwani kila mtu amerahisishiwa." Kisha akasoma:
﴿فَأَمَّا مَنۡ أَعۡطَىٰ وَٱتَّقَىٰ 5﴾
"Ama mwenye kutoa na akamcha Mungu! [Al-Layl: 5]. Na katika tamko la Muslim: "Kwani kila mtu amerahisishiwa kwa kile alichoumbwa kwa ajili yake."21 Kwa hivyo, Mtume rehema na amani ziwe juu yake akawa amewaamrisha watu wafanye matendo, na akakataza kutegemea tu Kadari iliyoandikwa.
Jambo la Nne: Kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amemuamrisha mja na amemkataza, wala hamlazimishi mja ila kwa kiasi cha uwezo wake, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿فَٱتَّقُواْ ٱللَّهَ مَا ٱسۡتَطَعۡتُمۡ وَٱسۡمَعُواْ وَأَطِيعُواْ...﴾
"Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama muwezavyo, na sikieni, na tiini..." [At-Taghabun: 16] Na alisema:
﴿لَا يُكَلِّفُ ٱللَّهُ نَفۡسًا إِلَّا وُسۡعَهَا...﴾
"Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kiasi cha iwezavyo..." [Al-Baqara: 286]. Lau mja angekuwa analazimishwa kutenda, basi angekalifishwa kwa jambo asiloweza kujinasua nalo; na hili ni batili. Kwa hivyo, ikitokea kutoka kwake maasi kwa kutokujua, au kwa kusahau, au kwa kulazimishwa, basi hana dhambi juu yake; kwa kuwa amekubaliwa udhuru wake.
Jambo la tano: Kwamba makadirio (mipango) ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ni siri iliyositirika, hayajulikani ila baada ya kutokea kwa yaliyokadiriwa. Na matashi ya mwanadamu ya kile anachokifanya hutangulia kitendo chake; hivyo matashi yake ya kutenda hayajengwi juu ya kujua kwake makadirio ya Mwenyezi Mungu. Na wakati huo huondoka hoja yake ya kujitetea kwa makadirio; kwani mtu hana hoja katika yale asiyoyajua.
La sita: Kwamba tunamuona mwanadamu anawania kwa ari yale yanayomfaa katika mambo ya dunia yake; hadi ayafikie na kuyapata, wala habeuki kutoka kwayo kwenda katika yale yasiyomfaa; kisha akajitetea juu ya kuacha kwake kwa kisingizio cha Kadari; basi kwa nini aache yanayomfaa katika mambo ya dini yake akaelekea katika yale yanayomdhuru kisha ajitetee kwa Kadari? Je, si hali ya mambo haya mawili ni moja tu?!
Huu hapa mfano unaoweka wazi hayo:
Lau zingekuwapo mbele ya mwanadamu njia mbili: moja ya kumfikisha katika mji ambao wote ni machafuko: Mauaji, uporaji, ukiukaji wa heshima, hofu na njaa; na ya pili ya kumfikisha katika mji ambao wote ni nidhamu, na usalama ulio thabiti, na maisha ya starehe, na kuheshimiwa kwa nafsi, heshima za watu na mali; je, ni ipi katika njia hizo mbili atapita?
Kwa hakika atafuata njia ya pili inayomfikisha kwenye nchi ya nidhamu na usalama, wala haiwezekani kabisa kwa yeyote mwenye akili kufuata njia ya nchi ya machafuko na hofu, kisha akajitetea kwa hoja ya Kadari. Basi kwa nini katika jambo la Akhera anafuata njia ya kwenda Motoni badala ya kwenda Peponi, kisha akajitetea kwa alichopangiwa?
Na mfano mwingine ni kwamba tunaona mgonjwa akiagizwa kutumia dawa; akainywa, ilhali nafsi yake haiipendi. Na anakatazwa chakula kinachomdhuru, akakiacha, ilhali nafsi yake inakitamani. Haya yote ni kwa ajili ya kutafuta uponyaji na salama. Wala haiwezekani aache kunywa dawa, au ale chakula kinachomdhuru, kisha akatoa hoja kwa Kadari. Basi kwa nini mtu aache kile alichoamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake, au afanye kile alichokikataza Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha akaitumia mipango (Kadari) ya Mwenyezi Mungu kama hoja?
Wa Saba: Kwamba anayetumia Kadari kama hoja kwa yale aliyoyaacha miongoni mwa wajibu, au aliyoyatenda miongoni mwa maasi; lau mtu angemshambulia akachukua mali yake, au akaivunja heshima yake; kisha akatoa hoja kwa kadari, akasema: Usinilaumu, kwani uvamizi wangu ulikuwa kwa mipango ya Mwenyezi Mungu - basi asingekubali hoja yake hiyo. Basi vipi hakubali kuitumia Kadari kama hoja katika dhuluma ya mwingine dhidi yake, naye mwenyewe anaitumia kama hoja katika dhuluma yake dhidi ya haki ya Mwenyezi Mungu Mtukufu?!
Imetajwa kuwa Amiri wa Waumini ‘Omari bin Khattab, Mwenyezi Mungu amridhie, aliletwa kwake mwizi aliye stahiki hukumu ya kukatwa mkono; akaamuru akatwe mkono wake. Akasema: 'Subiri, ewe Amiri wa Waumini, mimi nimeiba kwa Kadari ya Mwenyezi Mungu.' ‘Omari akasema: Na sisi pia tunakata kwa Kadari ya Mwenyezi Mungu.
Miongoni mwa matunda adhimu ya kuamini Mipango ya Mwenyezi Mungu:
Jambo la kwanza: Kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu wakati wa kuchukua sababu, kiasi kwamba hategemei sababu yenyewe; kwa sababu kila kitu kinakuwa kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na mipango yake.
Ya pili: Asijikweze mtu pindi anapopata alilolikusudia; kwa sababu kuipata huko ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa yale aliyompangia miongoni mwa sababu za kheri na mafanikio, na kujikweza kwake kunamsahaulisha kumshukuru Mwenyezi Mungu juu ya neema hii.
Ya Tatu: Nafsi inapata raha na moyo unatulia kwa yale yanayompata kutokana na hukumu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; basi hawi na wasiwasi anapokosa akipendacho au akapatwa na jambo baya, kwa sababu hayo ni kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu ambaye kwake ndiko ufalme wa mbingu na ardhi, na ni jambo linalotokea tu hakuna namna, na kuhusu hilo amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿مَآ أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٖ فِي ٱلۡأَرۡضِ وَلَا فِيٓ أَنفُسِكُمۡ إِلَّا فِي كِتَٰبٖ مِّن قَبۡلِ أَن نَّبۡرَأَهَآۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى ٱللَّهِ يَسِيرٞ 22 لِّكَيۡلَا تَأۡسَوۡاْ عَلَىٰ مَا فَاتَكُمۡ وَلَا تَفۡرَحُواْ بِمَآ ءَاتَىٰكُمۡۗ وَٱللَّهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخۡتَالٖ فَخُورٍ 23﴾
"Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwishaandikwa katika Kitabu kabla hatujauumba. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi. Ili msihuzunike kwa yale yaliyokupiteni wala msifurahi kwa aliyokupeni. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila ajivunaye, ajifaharishaye." [Al-Hadid: 22-23] Na anasema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Ajabu iliyoje ya jambo la Muumini. Hakika jambo lake lote ni kheri, na hakuna hilo kwa yeyote ila kwa Muumini. Akipatwa na jambo lenye kufurahisha, anashukuru ikawa hilo ni kheri kwake. Na akipatwa na madhara, anasubiri likawa hilo ni kheri kwake."22
Na kwa hakika, katika masuala ya Kadari, makundi mawili yamepotea na kuwa kando na haki:
La kwanza: Madhehebu ya Jabriyya wanaosema kuwa mja kalazimishwa juu ya matendo yake, na wala hana utashi wala uwezo.
La pili: Kadariyya waliosema kwamba mja amejitegemea katika matendo yake kwa upande wa utashi wake na uwezo wake, na wala matakwa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu wala uwezo wake hayana athari ndani yake.
Kukijibu kikundi cha kwanza (Jabriyya) kwa Sheria na hali halisi:
Ama kuhusu Sheria, basi hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu amemthibitishia mja wake utashi, na akayahusisha matendo kwa mja huyo. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...مِنكُم مَّن يُرِيدُ ٱلدُّنۡيَا وَمِنكُم مَّن يُرِيدُ ٱلۡأٓخِرَةَ...﴾
"...Wapo miongoni mwenu wanaotaka dunia, na wapo miongoni mwenu wanaotaka Akhera..." [Al-Imran: 152]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَقُلِ ٱلۡحَقُّ مِن رَّبِّكُمۡۖ فَمَن شَآءَ فَلۡيُؤۡمِن وَمَن شَآءَ فَلۡيَكۡفُرۡۚ إِنَّآ أَعۡتَدۡنَا لِلظَّٰلِمِينَ نَارًا أَحَاطَ بِهِمۡ سُرَادِقُهَاۚ...﴾
"Na sema: Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi atakaye, na aamini. Na atakaye, akatae. Hakika Sisi tumewaandalia wenye kudhulumu Moto ambao utakaowazunguka kama hema..." [Al-Kahf: 29] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿مَّنۡ عَمِلَ صَٰلِحٗا فَلِنَفۡسِهِۦۖ وَمَنۡ أَسَآءَ فَعَلَيۡهَاۗ وَمَا رَبُّكَ بِظَلَّٰمٖ لِّلۡعَبِيدِ46﴾
"Anayetenda mema, basi anajitendea mwenyewe nafsi yake, na mwenye kutenda uovu basi ni juu ya nafsi yake vile vile; wala Mola wako Mlezi si mwenye kuwadhulumu waja." [Fusswilat: 46].
Ama hali halisi, ni kwa kuwa kila mtu anajua tofauti kati ya matendo yake ya hiari anayoyatenda kwa utashi wake, kama vile kula, kunywa, kuuza na kununua, na yale yanayomkuta bila ya utashi wake, kama vile kutetemeka kwa sababu ya homa, na kuanguka kutoka juu ya paa. Basi katika hilo la kwanza, yeye ni mtendaji mwenye hiari kwa utashi wake bila ya kulazimishwa, na katika hilo la pili si mwenye hiari, wala si mwenye kutaka kilichompata.
Na kukijibu kikundi cha pili, Kadariyya, kwa Sheria na akili:
Ama kuhusu sheria, basi hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye Muumba wa vitu vyote, na kila kitu kipo kwa matakwa yake, na Mwenyezi Mungu Mtukufu amebainisha katika Kitabu chake kwamba matendo ya waja hutokea kwa matakwa yake. Amesema Mola Mtukufu:
﴿...وَلَوۡ شَآءَ ٱللَّهُ مَا ٱقۡتَتَلَ ٱلَّذِينَ مِنۢ بَعۡدِهِم مِّنۢ بَعۡدِ مَا جَآءَتۡهُمُ ٱلۡبَيِّنَٰتُ وَلَٰكِنِ ٱخۡتَلَفُواْ فَمِنۡهُم مَّنۡ ءَامَنَ وَمِنۡهُم مَّن كَفَرَۚ وَلَوۡ شَآءَ ٱللَّهُ مَا ٱقۡتَتَلُواْ وَلَٰكِنَّ ٱللَّهَ يَفۡعَلُ مَا يُرِيدُ﴾
"Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angependa, wasinge lipigana wale waliokuwa baada yao baada ya kuwajia hoja zilizo wazi. Lakini walihitilafiana. Basi wapo kati yao walioamini, na wengine kati yao waliokufuru. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angependa, wasingelipigana. Lakini Mwenyezi Mungu hutenda atakavyo."
[Al-Baqara: 253]. Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَلَوۡ شِئۡنَا لَأٓتَيۡنَا كُلَّ نَفۡسٍ هُدَىٰهَا وَلَٰكِنۡ حَقَّ ٱلۡقَوۡلُ مِنِّي لَأَمۡلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنَ ٱلۡجِنَّةِ وَٱلنَّاسِ أَجۡمَعِينَ 13﴾
"Na lau tungelitaka, tungempa kila mtu uongofu wake. Lakini imekwishakuwa kauli iliyotoka kwangu: Kwa yakini nitaijaza Jahannamu kwa wote hawa, majini na watu." [As-Sajda: 13].
Ama akili, basi hakika ulimwengu wote uko chini ya umiliki wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na mwanadamu ni sehemu ya ulimwengu huo; hivyo naye yuko chini ya umiliki wa Mwenyezi Mungu. Wala haiwezekani kwa aliyemilikiwa kuendesha chochote ndani ya umiliki wa Mmiliki ila kwa idhini yake na matakwa yake.
***
Malengo ya Itikadi ya Kiislamu
Neno 'Al-hadaf' kilugha hutumiwa kwa maana kadhaa, miongoni mwazo ni shabaha inayosimamishwa ili kulengwa, na kila kitu kinachokusudiwa.
Malengo ya itikadi ya Kiislamu ni makusudio yake, na malengo yake tukufu, yanayotokana na kushikamana nayo; nayo ni mengi yenye aina mbalimbali; miongoni mwa hayo ni:
Kwanza: Kutakasa nia na ibada kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu peke yake; kwani yeye ndiye Muumba, hana mshirika. Basi imewajibika kuwa makusudio na ibada ziwe kwake peke yake.
La pili: Ni kuikomboa akili na fikira kutokana na mkanganyiko usio na mpangilio unaotokana na utupu wa moyo kwa kukosa itikadi hii; kwa sababu yule ambaye moyo wake umekosa itikadi hii, basi huwa ima ni mwenye moyo ulio tupu na asiye na itikadi yoyote, na ni mwabudu wa maada inayoonekana kwa hisia tu; au ni mwenye kupepesuka katika upotevu wa itikadi na hurafa (hadithi za uongo).
La tatu: Raha ya nafsi na ya fikira. Basi hatakuwa na wasiwasi katika nafsi wala mvurugiko katika fikira; kwa sababu itikadi hii inamuunganisha Muumini na Muumba wake, Mwenyezi Mungu; hivyo anamridhia Yeye kuwa Mola Msimamia mambo, na Mwenye kuhukumu tena Muweka Sheria; basi moyo wake unatulia kwa mipangilio yake, na kifua chake kinakunjuka kwa ajili ya Uislamu; wala hatatafuta mbadala wake.
Nne: Usahihi wa nia na matendo usio na mkengeuko katika ibada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, au katika muamala na viumbe; kwa kuwa miongoni mwa misingi yake ni kuamini Mitume, amani iwe juu yao, kunakohusisha kufuata njia yao iliyo salama katika nia na matendo.
Tano: Ukakamavu na juhudi katika mambo, kiasi kwamba hapotezi nafasi yoyote ya kufanya wema ila huitumia; kwa kutarajia thawabu, wala haoni mazingira ya dhambi ila hujitenga nayo; kwa kuogopa adhabu; kwa kuwa miongoni mwa misingi yake ni imani ya kufufuliwa, na malipo kwa matendo.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَلِكُلّٖ دَرَجَٰتٞ مِّمَّا عَمِلُواْۚ وَمَا رَبُّكَ بِغَٰفِلٍ عَمَّا يَعۡمَلُونَ 132﴾
"Na wote wana daraja mbali mbali kutokana na yale waliyoyatenda. Na Mola wako Mlezi si mwenye kughafilika mbali na yale wanayoyatenda." [Al-An'am:132] Na Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, amehimiza lengo hili katika kauli yake: ”Muumini mwenye nguvu ni bora na anapendeka kwa Mwenyezi Mungu kuliko muumini dhaifu, na katika kila kheri, Pupia yenye manufaa na wewe, na utake msaada kwa Mwenyezi Mungu na wala usishindwe, na likikusibu jambo usiseme: Lau ningefanya kadha basi ingelikuwa kadha na kadha, lakini sema: Hili ni kwa makadirio ya Mwenyezi Mungu naye hufanya alitakalo, maana neno "Lau" hufungua matendo ya shetani". Imepokelewa na Muslim23.
Jambo la sita: Kuunda umma madhubuti unaotoa kila kilicho ghali na rahisi katika kuimarisha dini yake na kuziimarisha nguzo zake, bila kujali yanayoupata kwa ajili ya hilo. Na katika hili amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّمَا ٱلۡمُؤۡمِنُونَ ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ بِٱللَّهِ وَرَسُولِهِۦ ثُمَّ لَمۡ يَرۡتَابُواْ وَجَٰهَدُواْ بِأَمۡوَٰلِهِمۡ وَأَنفُسِهِمۡ فِي سَبِيلِ ٱللَّهِۚ أُوْلَٰٓئِكَ هُمُ ٱلصَّٰدِقُونَ 15﴾
"Hakika Waumini ni wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake tena wasitie shaka kabisa, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao. Hao ndio wakweli." [Al-Hujrati: 15].
7. Kufikiwa kwa mafanikio ya dunia na Akhera kwa kusawazisha hali za watu binafsi na jamii, na kupata malipo na fadhila tukufu, na katika hilo amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿مَنۡ عَمِلَ صَٰلِحٗا مِّن ذَكَرٍ أَوۡ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤۡمِنٞ فَلَنُحۡيِيَنَّهُۥ حَيَوٰةٗ طَيِّبَةٗۖ وَلَنَجۡزِيَنَّهُمۡ أَجۡرَهُم بِأَحۡسَنِ مَا كَانُواْ يَعۡمَلُونَ 97﴾
"Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini, hakika tutamhuisha maisha mema; na hakika tutawapa ujira wao kwa (malipo) bora zaidi ya yale waliyokuwa wakiyatenda." [An-Nahli: 97].
Basi haya ni baadhi ya malengo ya itikadi ya Kiislamu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu ayatimize kwetu na kwa Waislamu wote; hakika Yeye ndiye Mpaji, Mkarimu mno. Na kila sifa njema ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad na ali zake na Maswahaba zake.
Imekamilika kwa kalamu ya mtunzi wake.
Muhammadi Swaleh Al-Uthaimiin.
***
Ameipokea Bukhari katika kitabu cha Imani, nambari 8, na Muslim katika kitabu cha Imani, mlango wa Kauli ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, "Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano", nambari 16.
Ameipokea Imamu Muslim katika Kitabu "Al Imaan", hadithi nambari 8; na Abuu Daud katika Kitabu As-Sunnah, Mlango wa Kadari, hadithi nambari 4695.
Imepokelewa na Bukhari katika Kitabu cha Janaiz, mlango wa Ikiwa mtoto akisilimu kisha akafariki, je, ataswaliwa juu yake, na je, Uislamu huwasilishwa kwa mtoto, nambari 1292, na Muslim katika Kitabu cha Kadari, mlango wa Maana ya Kila Mtoto huzaliwa juu ya Fitra, na Hukumu ya Kifo cha Watoto wa Makafiri na Watoto wa Waislamu, nambari 2658.
Imepokelewa na Bukhari: Sura ya At-Tuur, nambari 4854.
Ameipokea Bukhari katika Kitabu cha Ijumaa, mlango wa Kuomba mvua katika Hotuba ya Ijumaa, nambari 891.
Ameipokea Bukhari katika kitabu cha Ijumaa, mlango wa Kuomba mvua katika hotuba siku ya Ijumaa, nambari 891, na Muslim katika kitabu cha Swala ya Kuomba Mvua, mlango wa Dua katika kuomba mvua, nambari 897.
Ameipokea Imamu Muslim katika Kitabu cha Imani, Mlango wa Ufafanuzi wa Imani na Uislamu na Ihsan na wajibu wa kuamini kwa kuthibitisha Kadari ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Ta'ala, nambari 8.
Imepokelewa na Bukhari: Kitabu cha Mwanzo wa Uumbaji, Mlango wa Kutaja Malaika, nambari 3037, na Muslim: Kitabu cha Wema, Kuendeleza uhusiano wa kindugu, na Adabu, Mlango: Ikiwa Mwenyezi Mungu atampenda mja, humfanya apendwe kwa waja wake, nambari 2637.
Ameipokea Bukhari katika kitabu cha Ijumaa, mlango wa Kusikiliza Hotuba, nambari 887, na Muslim katika kitabu cha Ijumaa, mlango wa Fadhila ya kwenda mapema kwa ajili ya swala ya siku ya Ijumaa, nambari 850.
Ameipokea Bukhari katika kitabu cha Tawhidi, mlango wa Kauli ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: "..yule niliyemuumba kwa mikono yangu?" nambari 7410, na Muslim katika kitabu cha Imani, mlango wa mwenye daraja ya chini kabisa miongoni mwa watu wa Peponi, nambari 193.
Ameipokea Bukhari katika milango ya Kibla, mlango wa Kuelekea upande wa Kibla popote alipo, kwa nambari 392, na Muslim katika kitabu cha Misikiti na sehemu za swala, mlango wa Kusahau katika swala, na kusujudu kwa ajili yake, kwa nambari 572.
Imepokelewa na Muslim, katika kitabu cha Pepo na sifa zake, mlango wa kutoweka kwa dunia, na ufafanuzi wa mkusanyiko Siku ya Kiyama, nambari 2859.
Ameipokea Bukhariy katika Kitabu cha Dhuluma mlango wa kauli ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: "Angalieni! Laana ya Mwenyezi Mungu iwapate walio dhulumu.", namba 2309; na Muslim: Kitabu cha toba, mlango wa kukubaliwa toba ya muuaji, hata ikiwa amezidisha mauaji yake, namba 2768.
Ameipokea Muslim: Kitabu cha Imani, mlango: Iwapo mja atanuia jambo jema huandikwa, na akinuia jambo baya, haliandikwi, kwa nambari 131.
Ameipokea Al-Bukhari: Kitabu cha Tafsiri, mlango wa kauli Yake: "Nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika hayo yanayofurahisha macho", namba 4501; na Muslim: Kitabu cha Pepo na sifa ya neema zake na watu wake, namba 2824.
Ameipokea Muslim: Kitabu cha Pepo na sifa zake, mlango wa kuonyeshwa kwa maiti makazi yake ya Peponi au Motoni, na kuthibitisha adhabu ya kaburi na kujilinda nayo, kwa nambari 2867.
Ameipokea Abuu Daud: Kitabu cha Sunna, mlango wa kuulizwa katika kaburi na adhabu ya kaburi, nambari 4753, na Ahmad: Musnadul Kufiyyin, Hadithi ya Al-Baraa bin 'Azib, nambari 18534.
Ameipokea Bukhari katika kitabu cha Udhu, mlango wa yaliyokuja kuhusu kuosha mkojo, nambari 215.
Ameipokea hadithi hii Muslim katika Kitabu cha Kadari, mlango wa kuhojiana Adam na Musa, amani iwe juu yao, nambari 2653.
Imepokelewa na Bukhari katika Kitabu cha Kadari, mlango wa: Amri ya Mwenyezi Mungu ni jambo lililokadiriwa, nambari 6605, na Muslim katika Kitabu cha Kadari, mlango wa jinsi ya kuumbwa kwa mwanadamu katika tumbo la mama yake na kuandikwa kwa riziki yake, muda wake wa kuishi, matendo yake, na kuwa mwenye kuangamia au mwenye kufuzu, nambari 2647.
Ameipokea Muslim katika kitabu cha Kuipa dunia mgongo na vilainishaji, mlango wa Muumini jambo lake lote ni kheri, nambari 2999.
Ameitoa Muslim: kitabu cha Qadar, mlango wa kuamrisha kuwa na nguvu, na kuacha ajizi, na kuomba msaada kwa Mwenyezi Mungu , na kuyakabidhi makadirio kwa Mwenyezi Mungu , nambari 2664.
Ameipokea Muslim: Kitabu cha Imani, Mlango wa Wajibu wa kuamini ujumbe wa Nabii wetu Muhammad - rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na amani - kwa watu wote na kufuta dini yake dini zilizotangulia, nambari 153.