مِنْ أَحْكَامِ الصِّيَامِ
Miongoni mwa hukumu za Funga (swaumu)
اللَّجْنَةُ العِلْمِيَّةُ
بِرِئَاسَةِ الشُّؤُونِ الدِّينِيَّةِ بِالمَسْجِدِ الحَرَامِ وَالمَسْجِدِ النَّبَوِيِّ
Kamati ya Kielimu ya usimamizi wa mambo ya Dini ya Msikiti Mtukufu wa Makkah na Madinah
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ
Miongoni mwa hukumu za Funga (swaumu)
Sehemu ya Kwanza:
Maana ya Funga, na ulazima wa kufunga Ramadhani
Jambo la kwanza: Maana ya Funga
Kufunga ni: Ni kumuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kujizuilia na vitu vyote vyenye kufunguza, kuanzia kuchomoza kwa alfajiri, hadi kutua kwa jua.
Jambo la pili: Ulazima wa kufunga Mwezi mtukufu wa Ramadhani
Kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani ni nguzo miongoni mwa nguzo za Uislamu, nguzo ambazo Uislamu wa mtu hauwezi kusimama imara bila ya hizo. Kufunga kulikuwa lazima kwa umma zote hata kama namna ya ufungaji na wakati wake ulitofautiana, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ كُتِبَ عَلَيۡكُمُ ٱلصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى ٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِكُمۡ لَعَلَّكُمۡ تَتَّقُونَ 183﴾
"Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyoandikiwa wale waliokuwa kabla yenu ili mpate kuchamungu." (Al-Baqara: 183) Maana ya neno (Kutiba) ni imelazimishwa.
Na ushahidi unaothibitisha ulazima wake ni Qur'ani, Sunnah na kukubaliana kwa wanachuoni:
Ama ushahidi katika Qur'ani ni maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ كُتِبَ عَلَيۡكُمُ ٱلصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى ٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِكُمۡ لَعَلَّكُمۡ تَتَّقُونَ 183 أَيَّامٗا مَّعۡدُودَٰتٖ...﴾
"Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyoandikiwa wale waliokuwa kabla yenu ili mpate kuchamungu.
(Mfunge) siku maalumu za kuhisabika." (Al-Baqara: 183-184)
Ama ushahidi katika Sunna, ni maneno yake Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Uislamu umejengwa juu ya mambo matano: Kushuhudia kuwa hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, kusimamisha swala, kutoa zaka, kufunga Ramadhani na kuhiji katika Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu."1
Na ama ushahidi wa kukubaliana kwa wanazuoni, kwa hakika wamekubaliana Waislamu wote juu ya ulazima wa kufunga Mwezi mtukufu wa Ramadhani, na kwamba mwenye kupinga ulazima wa kuufunga, basi huyo ni kafiri.
Sehemu ya pili:
Ubora wa kufunga Mwezi mtukufu wa Ramadhani
Mwezi huu mtukufu una sifa maalumu kubwa na ubora mbalimbali ambao unaoutofautisha mwezi huu na miezi mingine. Miongoni mwake ni:
1. Kuteremshwa Qur'ani tukufu ndani ya mwezi huu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿شَهۡرُ رَمَضَانَ ٱلَّذِيٓ أُنزِلَ فِيهِ ٱلۡقُرۡءَانُ...﴾
"Mwezi wa Ramadhani ndio ambao imeteremshwa humo Qur'ani ." (Al-Baqara: 185)
2. Hufunguliwa ndani ya mwezi huo milango ya Pepo; na hilo ni kwa sababu ya wingi wa matendo mema yanayofanywa ndani yake.
3. Hufungwa milango ya Moto katika mwezi huu; na hilo ni kutokana na uchache wa maovu.
Na ushahidi wa hilo umekuja katika maneno yake Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Unapokuja Mwezi wa Ramadhani, inafunguliwa milango ya Pepo, na inafungwa milango ya Moto, na mashetani wanafungwa minyororo."2
4. Na miongoni mwa ushahidi wa fadhila zake, ni maneno ya Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Hakuna tendo lolote jema atakalolifanya mwanadamu isipokuwa ataandikiwa mema kumi hadi mizidisho mia saba. Amesema Mwenyezi Mungu: 'Isipokuwa funga (suamu). Hakika hiyo ni yangu, na mimi ndiye nitakayeilipa. Mfungaji anaacha matamanio yake na chakula chake kwa ajili yangu. Funga ni kinga, na mwenye kufunga ana furaha mbili: Furaha wakati anapofungua na furaha pindi atakapokutana na Mola wake Mlezi. Na hakika harufu itokayo kwenye kinywa cha mwenye kufunga ni nzuri zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko harufu ya miski."3 Hivyo basi, mizidisho ya fadhila za kufunga haiishii kwenye idadi maalumu.
5. Kwamba kufanya kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu katika kufunga kunakuwa zaidi kuliko ibada nyingine, kwa maneno yake Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Amewacha matamanio yake, chakula chake na vinywaji vyake kwa ajili yangu."4
6. Kwamba Mwenyezi Mungu ameweka mlango maalumu uitwao Rayyan miongoni mwa milango ya Peponi kwa ajili ya wenye kufunga. Hawataingia humo wasiokuwa wao.
7. Kwamba mwenye kufunga, dua yake ni yenye kukubaliwa, kwa ushahidi wa maneno yake Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Mwenye kufunga wakati anapofungua ana maombi yasiyokataliwa."5
8. Maneno yake Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Yeyote atakayefunga Mwezi mtukufu wa Ramadhani, hali ya kumuamini Mwenyezi Mungu na kutarajia malipo kutoka kwake, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia."6
Hivyo basi, inampasa Muislamu kuufunga kwa imani na kutarajia thawabu ili apate malipo na msamaha wa dhambi.
Sehemu ya tatu:
Kinachothibitisha kuingia kwa Mwezi wa Ramadhani
Kunathibitika kuingia Mwezi wa Ramadhani kwa moja kati ya mambo mawili:
1. Kwa kuonekana kwa mwezi mwandamo; kwa ushahidi wa maneno yake Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Mtakapouona mwezi mwandamo, basi fungeni. Na mkiuona tena, basi funguweni. Lakini ikiwa utafichikana msiuone, basi ukadirieni."7 Na kwa maneno yake vilevile: "Msifunge mpaka muuone mwezi mwandamo. Na msifunguwe mpaka muuone."8
2. Ikiwa hawakuona mwezi mwandamo, watakamilisha idadi ya siku za mwezi wa Shaabani siku thelathini; kwa maneno yake Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Mwezi unakuwa ni usiku ishirini na tisa, hivyo msifunge mpaka muuone mwezi mwandamo. Na ikiwa utafichikana kwenu, basi kamilisheni idadi ya siku thelathini."9
Sehemu ya Nne:
Nia katika kufunga:
Nia ni sharti la kukubaliwa matendo yote, na ni lazima anuie kufunga Ramadhani kuanzia usiku; kwa maneno yake Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Yeyote atakayelala bila kunuia kufunga kabla ya kufika Al-fajiri, basi mtu huyo hana funga."10
Amesema Sheikhul-Islaam ibnu Taimiyat - Mwenyezi Mungu amrehemu- "Kila atakayetambua kwamba kesho ni Ramadhani, na anakusudia kufunga siku hiyo, basi hakika anakuwa mtu huyo amekwisha nuia kuifunga, ni sawasawa awe ametamka nia au hakutamka. Hivi ndivyo wanavyofanya Waislamu wote, wote wananuia hivi kufunga."11
Sehemu ya Tano:
Ni wajibu kwa nani kufunga?
Kufunga ni wajibu kwa kila Muislamu aliyebalehe, mwenye akili timamu.
Ikiwa atakuwa na siha njema na ni mkazi, basi ni wajibu juu yake kufunga. Na ikiwa ni mgonjwa, basi ni wajibu juu yake kulipa siku alizokosa.
Na akiwa ni mwenye afya njema na ni msafiri, basi amepewa hiyari ya kuchaguwa kati ya kufunga au kuwacha kufunga, na kuwacha kufunga ndiyo bora.
Na kufunga si wajibu kwa kafiri, na wala funga yake haiwi sahihi. Ikiwa atatubia katikati ya Mwezi wa Ramadhani, basi atafunga siku zilizobakia, na wala haimlazimu kulipa siku zilizompita akiwa katika ukafiri.
Kufunga sio wajibu kwa mtoto mdogo pia. Hata hivyo, inakubalika funga ya mtoto anayeweza kung'amua mambo, lakini kwake yeye inakuwa ni funga ya sunna.
Kupia sio wajibu kwa mwenda wazimu pia, na ikiwa atafunga akiwa katika hali ya uwendawazimu, basi funga yake haikubaliki; kwa sababu ya kukosekana nia.
Sehemu ya Sita:
Ni nani anayeruhusiwa kuwacha kufunga?
Anaruhusiwa kuwacha kufunga katika Mwezi wa Ramadhani:
(1) Mgonjwa ambaye funga kwake inakuwa ni ngumu, basi imependekezwa asifunge.
(2) Msafiri ambaye Mwezi umemwandamia akiwa yupo safarini au ameanzisha safari ndani ya Mwezi wa Ramadhani, na ikawa safari yenyewe inafika masafa ya kilomita themanini na zaidi.
(3) Ni haramu kwa mwenye hedhi na nifasi kufunga wakati wanapokuwa kwenye hedhi na nifasi; kwa ushahidi wa maneno ya Aisha - radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Tulikuwa tukipatwa na hedhi na nifasi, basi tukawa tunaamrishwa kulipa funga na wala hatuamrishwi kulipa swala."12
4. Mwenye kuuguwa maradhi ya kudumu yasiyotarajiwa kupona na yanamfanya ashindwe kufunga moja kwa moja, mgonjwa huyu atafunguwa na atalisha masikini kwa kila siku aliyofunguwa kiasi cha nusu kibaba ya chakula aina ya ngano au chakula kingine, na wala haitamlazimu kuzilipa siku alizozifunguwa.
5. Mzee mkongwe ambaye hawezi kufunga atafunguwa na atalisha masikini kwa kila siku aliyoifunguwa, na wala haitamlazimu kuzilipa siku alizozifunguwa.
6. Mama mjamzito na mwanamke mwenye kunyonyesha ikiwa wataogopea nafsi zao au wakaogopea watoto wao kudhurika kutokana na kufunga, basi watafungua na watalipa. Na ikiwa kufungua kwao ni kwa sababu ya kuogopea watoto wao tu, basi watalipa siku walizozifunguwa na watawalisha masikini kwa kila siku waliyoifunguwa.
Sehemu ya Saba:
Mambo yenye kuharibu Funga:
(1) Kujamiiana
Mtu atakapofanya tendo la ndoa mchana wa Ramadhani, basi funga yake itakuwa imebatilika,na anawajibika kujizuia kwa muda uliobakia. Na ni wajibu juu yake kutubia na kutaka msamaha, na hii siku aliyofanya tendo la ndoa atailipa, na atatowa kafara. Na kafara yenyewe ni kumwacha huru mtumwa, ikiwa hatompata mtumwa atafunga miezi miwili mfululizo. Ikiwa hawezi kufunga miezi miwili mfululizo, atalisha masikini sitini, kila maskini atamlisha nusu ya kibaba cha chakula aina ya ngano au aina nyingine ya chakula kiliwacho katika mji huo.
(2) Kutokwa na manii, kwa sababu ya kubusu au kupapasa au kujitoa manii au kuendelea kutazama vyenye kusababisha matamanio
Basi ikiwa mfungaji atatokwa na manii ka sababu moja miongoni mwa hizi sababu, funga yake itakuwa imeharibika, na atalazimika kujizuia, na atailipa hii siku na hatowajibika kutoa kafara, lakini ni wajibu juu yake kutubia na kujuta pamoja na kutaka msamaha na kujiweka mbali na haya mambo ya kuamsha matamanio; kwa sababu yupo kwenye ibada tukufu.
(3) Kula na kunywa kwa kukusudia
(4) Kutoa damu kwa mfungaji kwa njia ya kupiga chuku (hijama) au kutoa damu chafu au kutoa damu kwa kutoa msaada
Na msingi wa haya ni maneno yake Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - kuhusu kupiga chuku (hijama): "Amefungua saumu mwenye kupiga chuku (hijama) na mwenye kupigwa chuku."13
Amesema Sheikhul-Islaam Ibnu Taimiyat, Mwenyezi Mungu amrehemu: "Na kauli ya kuwa kupiga chuku (hijama) inafunguza saumu, ni msimamo wa wataalamu wengi wa hadithi; kama vile Imamu Ahmad ibnu Hanbal, Is-haqa Ibnu Rahawaihy, Ibnu Khuzaimat, Ibnu Mundhir na wengineo."14
Ama kutokwa na damu pasina kukusudia kwa mfungaji kama vile kutokwa na damu za puani na damu zitokanazo kwenye jeraha, kung'oa jino na mfano wa hayo, basi kwa hakika haya hayaiathiri funga.
(5) Kujitapisha
Huku ni kukitoa kimakusudi chakula au kinywaji kilichopo tumboni kupitia mdomoni. Ama ikiwa matapishi yatamshinda na yakamtoka bila kutaka kwake, basi kutapika huko hakuiathiri funga yake; kwa maneno ya Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Yule ambaye yatamshinda matapishi, basi hawajibiki kulipa. Na atakayejitapisha, basi naalipe siku hiyo."15 Na maana ya neno (Dhara'ahu) katika hadithi hii ni hali ya matapishi kumshinda mtu na kutoka bila hiari yake.
Sehemu ya Nane:
Mambo yanayopendekezwa katika funga
(1) Kula daku; kwa ushahidi wa hadithi ya Anas Ibnu Maalik - radhi za Mwenyezi mungu ziwe juu yake - amesema: Amesema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Kuleni daku, kwani hakika kuna baraka katika chakula cha daku."16
(2) Kuchelewesha kula daku; ikiwa hakuogopei kuchomoza kwa alfajiri.
(3) Kufanya haraka kufungua ikiwa itathibitika kuzama kwa jua. Amesema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Hautowacha umma wangu kuwa kwenye heri ikiwa watachelewesha kula daku na kuharakisha kufungua saumu."17
(4) Inapendekezwa aanze kufungua kwa tende mbichi. Na ikiwa hatopata, basi na afungue kwa tende kavu. Na ikiwa hatopata, basi na afungue kwa maji; kwa ushahidi wa maneno ya Anas - radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: Alikuwa Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - akifungua kwa tende mbichi kabla ya kuswali. Ikiwa hangefungua kwa tende mbichi, basi angefungua kwa tende kavu. Na ikiwa siyo tende kavu, basi angekunywa funda za maji."18
(5) Inapendekezwa kwa mwenye kufunga aombe dua aipendayo wakati wa kufungua. Amesema Mtume - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Hakika mfungaji wakati wa kufungua kwake ana maombi yasiyokataliwa."19
(6) Kuzidisha ibada za aina mbalimbali, kama vile kusoma Qur'ani na kumtaja Mwenyezi Mungu, na kisimamo cha usiku, na swala ya Tarawehe, na kuswali swala za sunna zenye mpangilio maalumu, na kutoa sadaka, na kutoa katika njia za kheri; kwani kwa hakika mema hufuta maovu.
Sehemu ya Tisa:
Tanabahisho:
• Inampasa mfungaji ajiepushe na kusema uongo, kusengenya na kutukana. Na ikiwa yeyote atamtukana au kumtolea maneno machafu, basi na aseme, "Hakika mimi nimefunga."
Amesema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Funga ni ngao. Basi na asifanye mfungaji uchafu wala ujinga. Na ikiwa mtu atampiga au atamtukana, basi na aseme mara mbili: "Hakika mimi nimefunga."20
• Miongoni mwa mambo anayokatazwa mwenye kufunga ni kuyapandisha maji sana wakati wa kusukutua au wakati wa kuyapandisha puani. Haya ni kwa sababu inahofiwa kwamba huenda maji yakaingia ndani ya mwili wake.
Alisema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Na fikisha sana maji wakati wa kuyapandisha puani isipokuwa utakapokua umefunga."21
• Kupiga mswaki hakuharibu funga. Bali ni sunna na inapendekezwa kwa mwenye kufunga na asiyefunga kupiga mswaki mwanzo wa mchana na mwisho wake, kwa mujibu wa kauli iliyo sahihi.
Sehemu ya Kumi:
Kulipa funga ya Ramadhani
Atakayefungua katika mwezi wa Ramadhani kwa sababu inayoruhusika kama vile kupata udhuru za kisheria ambazo zinamruhusu kufungua, au kwa sababu iliyo haramu kama vile mwenye kuharibu funga yake kwa kufanya tendo la ndoa au kitendo chochote kingine, basi inamlazimu kuilipa siku hiyo; kwa ushahidi wa maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...فَعِدَّةٞ مِّنۡ أَيَّامٍ أُخَرَ...﴾
"Basi atimize hisabu katika siku nyenginezo." (Al-Baqara: 183) Na inapendekezwa kwa mwenye deni la funga kufanya haraka kulilipa, ili kujiweka mbali na deni lake. Na inapendekezwa ulipaji huo uwe ni wa kufuatanisha; kwa sababu kulipa deni kunachukuliwa kama kutekeleza. Hata hivyo, mwenye deni la funga anaruhusiwa kuchelewesha kulilipa kwa sababu muda wa kufanya hivyo ni mpana.
Vile vile anaruhusiwa kuzilipa tofauti tofauti, lakini ikiwa mwezi wa Shaaban haukubakia isipokuwa kiasi ambacho kitamtosheleza kulipa deni lake, basi atafunga mfululizo; kutokana na ufinyu wa muda, na hairuhusiki kulichelewesha hilo mpaka baada ya Ramadhani nyingine pasina udhuru.
• Na yeyote atakayechelewesha kulipa mpaka ikafika Ramadhani nyingine, mtu huyo ana hali za aina mbili:
Awe amechelewesha kwa udhuru wa kisheria, mfano aendelee kuugua mpaka akafikiwa na Ramadhani nyingine, basi mtu huyu analazimika kulipa tu.
Awe amechelewesha bila kuwa na udhuru, basi huyu inamlazimu kulipa na kulisha masikini kwa kila siku alizowacha kufunga, nusu kibaba ya chakula kinacholiwa katika mji huo.
• Funga za Sunna kwa mwenye deni la funga ya faradhi. Mwenye kudaiwa deni la funga ya Ramadhani, ni bora kufanya haraka kulipa kabla ya kufunga funga za sunna, lakini ikiwa funga za sunna muda wake ni mfinyu kama vile kufunga funga ya Arafa, na Ashuura, basi atazifunga kabla ya kulipa deni la Ramadhani; kwa sababu deni wakati wake ni mpana. Ama funga ya Ashura na Arafa, hizo muda wake ni mfinyu. Lakini asifunge siku sita za mwezi wa Shawwali isipokuwa baada ya kulipa deni la funga ya Ramadhani.
Haya ndiyo tuliyoweza kuyakusanya, na rehema na amani nyingi za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad na jamaa zake na Maswahaba wake.
***
Yaliyomo
Sehemu ya Kwanza: 2
Maana ya Funga, na ulazima wa kufunga Ramadhani 2
Sehemu ya pili: 4
Ubora wa kufunga Mwezi mtukufu wa Ramadhani 4
Sehemu ya tatu: 7
Kinachothibitisha kuingia kwa Mwezi wa Ramadhani 7
Sehemu ya Nne: 8
Nia katika kufunga: 8
Sehemu ya Tano: 8
Ni wajibu kwa nani kufunga? 8
Sehemu ya Sita: 9
Ni nani anayeruhusiwa kuwacha kufunga? 9
Sehemu ya Saba: 11
Mambo yenye kuharibu Funga: 11
Sehemu ya Nane: 13
Mambo yanayopendekezwa katika funga 13
Sehemu ya Tisa: 15
Tanabahisho: 15
Sehemu ya Kumi: 16
Kulipa funga ya Ramadhani 16
***
sw419v1.0 - 22/02/2026
Wamekubaliana Bukhari na Muslimu juu yake. Ameipokea Bukhari kwa namba 1898 (3/25) na akaipokea Muslimu kwa namba 1079 (2/758).
Ameipokea An-Nasaai katika kitabu kiitwacho Al-Kubra kwa namba (2536) (3/131).
Tazama upokeaji uliopita.
Ameipokea ibnu Maajah kwa namba 1753 (1/775).
Wamekubaliana Imamu Bukhari na Muslim juu yake. Imamu Bukhari ameipokea kwa namba 38 (1/16) na Imamu Muslimu kwa namba 760 (1/523).
Ameipokea Imamu Ahmad katika Musnad kwa namba 6323 (10/402), na An-Nasaai katika Al-Kubra kwa namba 2446 (3/102).
Wamekubaliana Bukhari na Muslimu juu yake. Ameipokea Bukhari kwa namba 1906 (3/27) na akaipokea Muslimu kwa namba 1080 (2/759).
Wamekubaliana Bukhari na Muslimu juu ya usahihi wake. Ameipokea Bukhari kwa namba 1907 (3/27) na akaipokea Muslimu kwa namba 1051 (2/762).
Ameipokea An-Nasaai katika kitabu kiitwacho Al-Kubra (2652)(3/170)
Al-Fataawaa Al-Kubra (2/469).
Ameipokea Imamu Muslimu katika sahihi yake kwa namba 335 (1/265)
Ameipokea Imamu Bukhari kwa namba 1937 (3/33), na Imamu Ahmad akaipokea kwenye Musnadi wake kwa namba 26217 (43/278).
Tazama: Majmu'ul-Fataawa, uk. (25/252).
Ameipokea Imamu Ahmad katika Musnadi wake kwa namba 10463 (16/283), na Tirmidhiy ameipokea katika kitabu kiitwacho Al-Jaami'ul-Kabiir kwa namba 720 (2/91).
Wamekubaliana Bukhari na Muslimu juu ya usahihi wake. Ameipokea Bukhari kwa namba 1923 (3/29), na akaipokea Muslimu kwa namba 1095 (2/770).
Ameipokea Imamu Ahmad katika Musnadi yake kwa namba 12507 (35/399).
Ameipokea Abu Daudi kwa namba 2356 (2/306).
Ameipokea ibnu Maajah kwa namba 1753 (1/775).
Ameipokea Imamu Bukhari kwa namaba 1894 (3/24).
Ameipokea Abu Daudi kwa namba 2366 (2/308), na Tirmidhiy katika Al-Jaami'ul-Kabiir kwa namba 788 (2/147).
Wamekubaliana Bukhari na Muslimu juu yake. Ameipokea Bukhari kwa namba 8 (1/11) na Muslimu kwa namba 16 (1/34).