PHPWord

 

 

 

حِرَاسَةُ التَّوحِيدِ

 

Ulinzi wa Tauhidi

 

 

لِسَمَاحَةِ الشَّيْخِ العَلَّامَةِ

عَبْدِ العَزِيزِ بْنِ عَبْدِ اللهِ بْنِ بَازٍ

رَحِمَهُ اللهُ

 

Mtunzi Mheshimiwa, Sheikh,

Abdulaziz bin Abdillah bin Baaz

 

 

 


بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Makala ya kwanza:

Itikadi sahihi na mambo yanayopingana nayo

Mtunzi Mheshimiwa, Sheikh,

Abdulaziz bin Abdillah bin Baaz

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu peke yake, na rehema na amani ziwe juu ya yule ambaye hakuna nabii atakayekuja baada yake, na ziwe juu ya watu wa familia yake na Maswahaba wake.

Ama baada ya kusema hayo: Kwa maana itikadi sahihi ndiyo asili ya dini ya Uislamu na msingi wa mila, nimeona kwamba ni muhimu nizungumzie maudhui haya, kuandika juu yake na kutunga makala katika kuyaeleza na kuyabainisha.

Na inavyofahamika kwa ushahidi wa kisheria utokanao na Qur'ani na Hadithi ni kuwa matendo na maneno yanakuwa sahihi na kukubaliwa ikiwa yatatokana na itikadi iliyo sahihi. Ama itikadi inapokuwa si sahihi, basi hubatilika kila kinachotokana nayo miongoni mwa matendo na maneno, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...وَمَن يَكۡفُرۡ بِٱلۡإِيمَٰنِ فَقَدۡ حَبِطَ عَمَلُهُۥ وَهُوَ فِي ٱلۡأٓخِرَةِ مِنَ ٱلۡخَٰسِرِينَ﴾

"Na anayekufuru kuamini, basi hakika matendo yake yameharibika, naye Akhera atakuwa miongoni mwa wenye hasara." [Al-Maidah: 5]

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَلَقَدۡ أُوحِيَ إِلَيۡكَ وَإِلَى ٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِكَ لَئِنۡ أَشۡرَكۡتَ لَيَحۡبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ ٱلۡخَٰسِرِينَ 65﴾

"Na kwa yakini yamefunuliwa kwako na kwa wale waliokuwa kabla yako: 'Bila ya shaka ukimshirikisha Mwenyezi Mungu, matendo yako yataanguka, na lazima utakuwa miongoni mwa wenye kupata hasara.'" [Az-Zumar: 65]

Na aya zenye maana hii ni nyingi sana. Na kwa hakika kitabu cha Mwenyezi Mungu kilicho wazi na sunna za Mtume wake muaminifu, ziwe juu yake kutoka kwa Mola wake Mlezi rehema na amani bora zaidi, vimeashiria kwamba itikadi sahihi kwa muhutasari ni mambo sita: Kumuamini Mwenyezi Mungu, Malaika wake, Vitabu vyake, Mitume wake na Siku ya Mwisho, na kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu ya heri na ya shari. Hivyo basi, mambo haya sita ndiyo msingi wa itikadi iliyo sahihi ambayo Kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu kiliteremka nayo, na Mwenyezi Mungu akamtuma nayo Mtume wake Muhammad - rehema na amani ziwe juu yake.

 

Na umekuja ushahidi mwingi wa kuhusu misingi hii sita katika Kitabu (cha Mwenyezi Mungu) na Sunna sahihi, na miongoni mwa ushahidi huo kwa mfano tu ni huu ufuatao:

Kwanza: Ushahidi kutoka katika Kitabu; Ikiwa ni pamoja na kauli ya Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mtukufu:

﴿لَّيۡسَ ٱلۡبِرَّ أَن تُوَلُّواْ وُجُوهَكُمۡ قِبَلَ ٱلۡمَشۡرِقِ وَٱلۡمَغۡرِبِ وَلَٰكِنَّ ٱلۡبِرَّ مَنۡ ءَامَنَ بِٱللَّهِ وَٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِ وَٱلۡمَلَٰٓئِكَةِ وَٱلۡكِتَٰبِ وَٱلنَّبِيِّـۧنَ...﴾

"Sio wema tu peke yake kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi katika kusali, bali wema hasa ni wale wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii." [Al-Baqara: 177]

Na kauli yake aliyetakasika na kutukuka:

﴿ءَامَنَ ٱلرَّسُولُ بِمَآ أُنزِلَ إِلَيۡهِ مِن رَّبِّهِۦ وَٱلۡمُؤۡمِنُونَۚ كُلٌّ ءَامَنَ بِٱللَّهِ وَمَلَٰٓئِكَتِهِۦ وَكُتُبِهِۦ وَرُسُلِهِۦ لَا نُفَرِّقُ بَيۡنَ أَحَدٖ مِّن رُّسُلِهِ...﴾

"Mtume ameamini yale yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake Mlezi, na Waumini vile vile. Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake na Mitume wake. (Wao husema) Hatutafautishi baina ya yeyote katika Mitume wake." [Al-Baqara: 285]

 

Na kauli yake Mtukufu:

﴿يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓاْ ءَامِنُواْ بِٱللَّهِ وَرَسُولِهِۦ وَٱلۡكِتَٰبِ ٱلَّذِي نَزَّلَ عَلَىٰ رَسُولِهِۦ وَٱلۡكِتَٰبِ ٱلَّذِيٓ أَنزَلَ مِن قَبۡلُۚ وَمَن يَكۡفُرۡ بِٱللَّهِ وَمَلَٰٓئِكَتِهِۦ وَكُتُبِهِۦ وَرُسُلِهِۦ وَٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِ فَقَدۡ ضَلَّ ضَلَٰلَۢا بَعِيدًا 136﴾

"Enyi mlioamini! Muaminini Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na Kitabu alichokiteremsha juu ya Mtume wake, na Kitabu alichokiteremsha kabla yake. Na anayemkataa Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Mwisho, basi huyo amekwishapotea kupotea kwa mbali." [An-Nisaa: 136].

Na kauli yake Mtukufu:

﴿أَلَمۡ تَعۡلَمۡ أَنَّ ٱللَّهَ يَعۡلَمُ مَا فِي ٱلسَّمَآءِ وَٱلۡأَرۡضِۚ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَٰبٍۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى ٱللَّهِ يَسِيرٞ 70﴾

"Je, hujui kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na katika ardhi? Hakika hayo yamo Kitabuni. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi." [Al-Hajj: 70]

Pili: Ushahidi kutoka katika Sunna: Miongoni mwake ni hadithi sahihi na maarufu aliyoipokea imamu Muslimu katika sahihi yake kutoka katika hadithi ya kiongozi wa Waumini Omar ibni Khatwab - radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - kuwa: Jibriil, amani iwe juu yake, alimuuliza Mtume - rehema na amani ziwe juu yake - kuhusu imani. Akamwambia: "Imani ni kumuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Mwisho, na kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu, kheri yake na shari yake."1 Hadi mwisho wa Hadithi hii, na imepokelewa na masheke wawili (Bukhari na Muslim) - pamoja na kuwepo tofauti ndogo - kutoka kwa Hadithi ya Abu Hurairah, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi.

Na hii misingi sita kinatokana nayo kila kitu kilicho lazima kwa Muislamu kukiamini kuhusiana na Mwenyezi Mungu Mtukufu na katika jambo la kurudishwa kwa Mwenyezi Mungu, na mengineyo katika mambo yasiyoonekana, miongoni mwa yale aliyojulisha juu yake Mwenyezi Mungu na Mtume wake, rehema na amani ziwe juu yake.

Ufafanuzi wa misingi hii sita ni kama ifuatavyo:

Msingi wa kwanza: Kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu. Inajumuisha mambo kadhaa; ikiwa ni pamoja na:

Na inajumuisha mambo kadhaa; miongoni mwayo: Kuamini kwamba Yeye ndiye Mungu wa kweli anayestahiki kuabudiwa mbali na kila kisichokuwa yeye, kwa kuwa yeye ndiye Muumba wa waja, Mwenye kuwatendea wema, Mwenye kusimamia riziki zao, Mwenye kujua mambo yao ya siri na ya wazi, Mwenye uwezo wa kumlipa thawabu mtiifu wao na kumuadhibu mwenye kuasi miongoni mwao.

Mwenyezi Mungu aliumba vizito viwili (majini na wanadamu) kwa ajili ya ibada hii na akawaamrisha kuifanya, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمَا خَلَقۡتُ ٱلۡجِنَّ وَٱلۡإِنسَ إِلَّا لِيَعۡبُدُونِ 56 مَآ أُرِيدُ مِنۡهُم مِّن رِّزۡقٖ وَمَآ أُرِيدُ أَن يُطۡعِمُونِ 57 إِنَّ ٱللَّهَ هُوَ ٱلرَّزَّاقُ ذُو ٱلۡقُوَّةِ ٱلۡمَتِينُ 58﴾

"Nami sikuwaumba majini na watu isipokuwa waniabudu Mimi.

Sitaki kutoka kwao riziki wala sitaki wanilishe.

Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti." [Adh-Dhariyat: 56-58].

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿يَٰٓأَيُّهَا ٱلنَّاسُ ٱعۡبُدُواْ رَبَّكُمُ ٱلَّذِي خَلَقَكُمۡ وَٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِكُمۡ لَعَلَّكُمۡ تَتَّقُونَ 21 ٱلَّذِي جَعَلَ لَكُمُ ٱلۡأَرۡضَ فِرَٰشٗا وَٱلسَّمَآءَ بِنَآءٗ وَأَنزَلَ مِنَ ٱلسَّمَآءِ مَآءٗ فَأَخۡرَجَ بِهِۦ مِنَ ٱلثَّمَرَٰتِ رِزۡقٗا لَّكُمۡۖ فَلَا تَجۡعَلُواْ لِلَّهِ أَندَادٗا وَأَنتُمۡ تَعۡلَمُونَ 22﴾

"Enyi watu! Muabuduni Mola wenu Mlezi aliye waumba nyinyi na wale wa kabla yenu, ili mpate kuwa wacha Mungu.

(Mwenyezi Mungu) ambaye amewafanyia hii ardhi kuwa kama tandiko, na mbingu kama paa, na akateremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo akatoa matunda yawe riziki zenu. Basi msimfanyie Mwenyezi Mungu washirika, na hali nyinyi mnajua." [Al-Baqara: 21-22].

Na kwa hakika Mwenyezi Mungu aliwatuma Mitume na akateremsha Vitabu kwa ajili ya kubainisha haki na kuilingania, na kutahadharisha yote yanayopingana nayo, kama alivyosema Mwenyezi Mungu aliyetakasika, Mtukufu:

﴿وَلَقَدۡ بَعَثۡنَا فِي كُلِّ أُمَّةٖ رَّسُولًا أَنِ ٱعۡبُدُواْ ٱللَّهَ وَٱجۡتَنِبُواْ ٱلطَّٰغُوتَ...﴾

"Na kwa hakika tulituma katika kila umma mtume, ya kuwa wamuabudu Mwenyezi Mungu na wajiepushe na kila kinachoabudiwa kinyume na Mwenyezi Mungu." [An-Nahli: 36].

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمَآ أَرۡسَلۡنَا مِن قَبۡلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِيٓ إِلَيۡهِ أَنَّهُۥ لَآ إِلَٰهَ إِلَّآ أَنَا۠ فَٱعۡبُدُونِ 25﴾

"Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hakuna mungu isipokuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu." [Al-Anbiya: 25].

Na amesema Mwenye nguvu na utukufu:

 

﴿الر كِتَابٌ أُحْكِمَتْ آيَاتُهُ ثُمَّ فُصِّلَتْ مِنْ لَدُنْ حَكِيمٍ خَبِيرٍ1 أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا اللَّهَ إِنَّنِي لَكُمْ مِنْهُ نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ2﴾

"Alif Lam Ra. Hiki ni Kitabu ambacho Aya zake zimewekwa wazi, kisha zikapambanuliwa, kilichotoka kwa Mwenye Hekima na Mwenye habari zote.

Ili msimuabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu. Hakika mimi kwenu ni muonyaji na mbashiri nitokae kwake." [Huud: 1-2].

Na uhakika wa ibada hii ni katika kumpwekesha Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka kwa mambo yote wanayotumia waja kuabudia miongoni mwa dua, hofu, kutaraji, kuswali, kufunga, kuchinja wanyama, kuweka nadhiri na mengineyo miongoni mwa ibada zinazofanywa kwa kumnyenyekea yeye, kumtaka Yeye tu na kumuogopa pamoja na kumpenda kikamilifu yeye aliyetakasika na kujishusha chini mbele ya ukuu wake.

Na mwenye kutafakari Qur'ani tukufu, atapata kwamba aya zake nyingi ziliteremka kuhusiana na misingi hii mitukufu, kama ilivyo katika maneno yake Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka:

﴿إِنَّآ أَنزَلۡنَآ إِلَيۡكَ ٱلۡكِتَٰبَ بِٱلۡحَقِّ فَٱعۡبُدِ ٱللَّهَ مُخۡلِصٗا لَّهُ ٱلدِّينَ فَاعْبُدِ اللَّهَ مُخْلِصًا لَهُ الدِّينَ 2 أَلَا لِلَّهِ الدِّينُ الْخَالِصُ وَٱلَّذِينَ ٱتَّخَذُواْ مِن دُونِهِۦٓ أَوۡلِيَآءَ مَا نَعۡبُدُهُمۡ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَآ إِلَى ٱللَّهِ زُلۡفَىٰٓ إِنَّ ٱللَّهَ يَحۡكُمُ بَيۡنَهُمۡ فِي مَا هُمۡ فِيهِ يَخۡتَلِفُونَۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَهۡدِي مَنۡ هُوَ كَٰذِبٞ كَفَّارٞ3﴾

"Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa Haki. Basi muabudu Mwenyezi Mungu ukimsafia Dini Yeye tu.

Sikilizeni. Hakika Dini Safi ni ya Mwenyezi Mungu tu. Na wale wanaowafanya wenginewe kuwa ni walinzi wakisema: 'Sisi hatuwaabudu ila wapate kutujongeza tu kumkaribia Mwenyezi Mungu', hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao katika yale wanayo hitilafiana. Hakika Mwenyezi Mungu hamuongoi aliye muongo kafiri." [Az-Zumar: 3-2]

Na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعۡبُدُوٓاْ إِلَّآ إِيَّاهُ...﴾

"Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote isipokuwa Yeye." [Al Israai: 23].

Na amesema Mwenye nguvu, Mtukufu:

﴿فَٱدۡعُواْ ٱللَّهَ مُخۡلِصِينَ لَهُ ٱلدِّينَ وَلَوۡ كَرِهَ ٱلۡكَٰفِرُونَ14﴾

"Basi muombeni Mwenyezi Mungu mkimsafia Dini Yeye tu, hata kama watachukia makafiri." [Ghaafir: 14]

Vile vile, mwenye kutafakari Sunna ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, atapata kwamba msingi huu mkubwa pia umepewa kipaumbele. Miongoni mwa hayo ni yale yaliyosimuliwa katika Sahihi mbili kutoka kwa Mua'adh - radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - kwamba Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alisema: "Haki ya Mwenyezi Mungu juu ya waja wake, ni wamuabudu yeye na wala wasimshirikishe na kitu chochote."2

Na huingia vilevile katika kumuamini Mwenyezi Mungu: Kuyaamini mambo yote aliyoyawajibisha Mwenyezi Mungu kwa waja wake, na akawalazimisha kuyafanya, miongoni mwayo ni nguzo tano za Uislamu zilizo maarufu.

Na hizo nguzo tano ni: Kushuhudia kuwa hapana mungu apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na kusimamisha swala, na kutowa Zaka, na kufunga Ramadhani, na kuhiji Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu kwa yule awezaye njia ya kuiendea, na mambo mengine yasiyokuwa hayo miongoni mwa mambo yaliyolazimishwa ambayo yamekuja katika sheria iliyo nzuri.

Na nguzo muhimu zaidi na tukufu katika hizi nguzo ni: Kushuhudia kuwa hapana mungu apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Tamko hili la shahada linahitajia kuifanya ibada kwa ajili ya Mwenyezi Mungu peke yake na kumkataa asiyekuwa yeye, na hii ndiyo maana ya (Laailaha illallahu). Kwani maana yake -kama walivyosema wanazuoni Mwenyezi Mungu awarehemu- ni: Hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake. Na kwa mujibu wa maana hiyo, basi kila kinachoabudiwa kinyume na Mwenyezi Mungu - awe ni mwanadamu au Malaika au jini au au yoyote asiyekuwa hao - ni muabudiwa batili, na mwenye kuabudiwa kwa haki ni Mwenyezi Mungu peke yake hana mshirika wake kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿ذَٰلِكَ بِأَنَّ ٱللَّهَ هُوَ ٱلۡحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدۡعُونَ مِن دُونِهِۦ هُوَ ٱلۡبَٰطِلُ...﴾

"Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye wa haki, na kwamba kila wanachokiabudu kinyume na yeye ni batili." [Al-Hajj: 62].

Na imeshatangulia kuwekwa wazi kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwaumba majini na watu kwa ajili ya msingi huu wa asili, na akawaamrisha kushikamana na msingi huo, na akatuma kwa ajili hiyo Mitume wake, na akateremsha kwa ajili hiyo Vitabu vyake. Hivyo basi ni wajibu kwa mja kulifikiria hilo vizuri na kulizingatia sana; ili ikuwiye wazi namna gani walivyo tumbukia Waislamu wengi katika ujinga mkubwa wa kutojuwa msingi huu; mpaka wakafikia kiwango cha kuabudu wengineo pamoja na Mwenyezi Mungu, na wakawafanyia wengineo haki yake ya kipekee. Basi Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuombwa msaada.

Na miongoni mwa kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kuamini kuwa Yeye ndiye Muumba wa ulimwengu, Mwenye kupanga mambo yao na Mwenye kuwaendesha kwa elimu yake na uwezo wake kama anavyotaka Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kwamba Yeye ndiye Mmiliki wa dunia na akhera, na ndiye Mola Mlezi wa walimwengu wote, hakuna muumba asiye kuwa Yeye wala hakuna Mola Mlezi asiyekuwa Yeye. Na kwamba yeye alituma Mitume na akateremsha Vitabu ili kuwafanya waja kuwa wema na kuwalingania kwenye mambo yenye wokovu wao na kutengenea kwao duniani na akhera. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu hana mshirika yeyote katika hayo yote. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿ٱللَّهُ خَٰلِقُ كُلِّ شَيۡءٖۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيۡءٖ وَكِيلٞ 62﴾

"Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu, na Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu." [Az-Zumar: 62].

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿إِنَّ رَبَّكُمُ ٱللَّهُ ٱلَّذِي خَلَقَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٖ ثُمَّ ٱسۡتَوَىٰ عَلَى ٱلۡعَرۡشِۖ يُغۡشِي ٱلَّيۡلَ ٱلنَّهَارَ يَطۡلُبُهُۥ حَثِيثٗا وَٱلشَّمۡسَ وَٱلۡقَمَرَ وَٱلنُّجُومَ مُسَخَّرَٰتِۭ بِأَمۡرِهِۦٓۗ أَلَا لَهُ ٱلۡخَلۡقُ وَٱلۡأَمۡرُۗ تَبَارَكَ ٱللَّهُ رَبُّ ٱلۡعَٰلَمِينَ54﴾

"Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwenyezi Mungu aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akainuka juu ya Kiti cha Enzi. Huufunika usiku kwa mchana, ufuatao upesi upesi. Na jua, na mwezi, na nyota zilizotiishwa kwa amri yake. Fahamuni! Kuumba ni kwake, na amri (ni yake). Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote." [Al-A'araf: 54]

Na vilevile miongoni mwa kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu: Ni kuyaamini majina yake mazuri na sifa zake tukufu zilizokuja katika Kitabu chake kitukufu, na zilizothibiti kutoka kwa Mtume wake muaminifu, pasina kubadilisha, kupinga, kutafuta kujua namna zilivyo haswa wala kufananisha.

﴿...لَيۡسَ كَمِثۡلِهِۦ شَيۡءٞۖ وَهُوَ ٱلسَّمِيعُ ٱلۡبَصِيرُ﴾

"Hakuna kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona." [Ash-Shuraa: 11].

Hivyo, ni wajibu kuyapitisha kama yalivyokuja bila kutafuta

kujua namna yalivyo haswa, pamoja na kuamini maana tukufu ambazo yaliashiria, ambazo ni sifa za Mwenyezi Mungu mwenye nguvu na utukufu, na ni wajibu kumuelezea Yeye Mtukufu kwa sifa hizo kwa namna inayomfailia pasina ya kumfananisha na kiumbe chake chochote kama sifa zake zozote. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Na amesema Mwenye nguvu na utukufu:

﴿فَلَا تَضۡرِبُواْ لِلَّهِ ٱلۡأَمۡثَالَۚ إِنَّ ٱللَّهَ يَعۡلَمُ وَأَنتُمۡ لَا تَعۡلَمُونَ74﴾

"Basi msimpigie Mwenyezi Mungu mifano. Kwa hakika yeye anajuwa, na nyinyi hamjui kitu chochote." [An-Nahli: 74].

Na hii ndiyo itikadi sahihi ya Ahlussunna waljamaa miongoni mwa Maswahaba wa Mtume - rehema na amani ziwe juu yake - na wale waliofuata baada yao kwa wema, na ndiyo itikadi aliyoinukuu imamu Abul Hasani Al-ash-'ariy katika kitabu chake, Mwenyezi Mungu amrehemu, kitabu kiitwacho "Makala mbalimbali" kutoka kwa watu wa hadithi na sunna" na pia waliinukuu wengineo miongoni mwa watu wenye elimu na imani.

Alisema Al-Awzaaiy Mwenyezi Mungu amrehemu: Aliulizwa imamu Zuhriy na Maq-huul kuhusu aya zinazohusiana na sifa za Mwenyezi Mungu, wakasema: "Zipitisheni kama zilivyokuja."3

 

 

 

 

 

Na akasema Al-Awzaaiy vilevile - Mwenyezi Mungu amrehemu: Tulikuwa tukisema ilhali wale waliokuja baada ya Maswahaba bado wako hai: 'Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu yupo juu ya Kiti chake cha Enzi, na tunaamini sifa zote zilizopokewa katika hadithi (za Mtume)."4

Na alisema Al-Waliid bin Muslim -Mwenyezi mungu amrehemu- "Aliulizwa Imamu Maalik, Auzaaiy, Al-laithiy ibnu Saad na Sufiani Al-thauriy -Mwenyezi Mungu awarehemu- kuhusu habari zilizopokelewa kuhusu sifa za Mwenyezi Mungu wakasema wote kuwa: 'Zipitisheni kama zilivyokuja bila ya kutafuta kujua namna zilivyo haswa.'"5

Na alipoulizwa Rabii'a ibn Abdurahmani, sheikh wa imamu Maalik, Mwenyezi Mungu amrehemu yeye na sheikh wake, kuhusu kuwa juu kwa Mwenyezi Mungu, akasema: 'Kuwa juu kwake kuna fahamika, na namna yake hasa haifahamiki, na lililo kwa Mwenyezi Mungu ni kutuma ujumbe, nao ni wajibu wa Mtume ni kufikisha kwa uwazi, na wajibu wetu sisi ni kusadiki.'6 Na alipoulizwa imamu Maalik -Mwenyezi Mungu amrehemu- kuhusu hilo alisema: "Kuwa juu kwake kunafahamika, na namna yake hasa haifahamiki, na kuamini jambo hilo ni wajibu, na kuuliza namna yake ni uzushi." Kisha akamwambia muulizaji: "Ninakuona kuwa wewe ni mtu muovu!" Kisha akatoa amri na akatolewa mahali pale.7 Na imepokelewa maana hii vilevile kutoka kwa mama wa waumini Ummu Salama - radhi za Mwenyezi Mungu - zimfikie.8

Na amesema imamu Abuu Abdurahman ibnu Mubaaraka -rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- kuwa: "Tunamjua Mola wetu Mlezi Mtukufu kuwa Yeye yupo juu ya mbingu zake na yupo juu ya Kiti chake cha Enzi hali yakujitenga na viumbe wake."9

Na maneno ya maulamaa kwenye mlango huu ni mengi sana hatuwezi kuyanukuu yote katika muhadhara huu. Mwenye kutaka kulifuatilia hilo zaidi, basi ayarejelee yaliyoandikwa na maulamaa wa sunna katika mlango huu, mfano kitabu kiitwacho "As-Sunnah" cha mtunzi aitwaye Abdullah ibn imamu Ahmad, na pia kitabu kiitwacho "At-Tauhiid" cha mtunzi aitwaye Al-imamu al-jaliil Muhammad ibn Khuzaimata, na kitabu kiitwacho "As-Sunna" cha mtunzi aitwaye Abulqaasim Al-lalkaaiy At-twabariy, na kitabu kiitwacho "As-Sunna" cha mtunzi aitwaye Abuubakar ibn Aaswim, na majibu ya sheikhul -islaam ibn Taimiya kujibu watu wa Hamaat, nalo ni jibu zuri lenye faida kubwa. Ameweka wazi humo -Mwenyezi Mungu amrehemu- itikadi ya Ahlusunnah, na akanukuu humo mengi ya maneno yao, na ushahidi wa kisheria na wa kiakili juu ya usahihi wa yale waliyoyasema Ahlusunnah, na ubatili wa yale waliyo yasema wagomvi wao.

Na hivi ndivyo ilivyokuwa risala yake iliyoitwa Tadmuuriyya. Kwani kwa hakika alieleza humo kwa undani na akaweka wazi itikadi ya ahlusunnah waljamaa kwa kutumia ushahidi ulionukuliwa kutoka katika Kitabu na Sunna na pia ushahidi wa kiakili na kujibu hoja za wapinzani majibu yenye kuweka wazi haki na kuibomoa batili kwa kila mwenye kulitazama hilo miongoni mwa wenye elimu kwa lengo zuri na kutaka kuijuwa haki. Na kwa ufupi ni kwamba: Itikadi ya Ahlusunnah wal-jamaa katika mlango wa majina ya Mwenyezi Mungu na sifa zake, ni kwamba wame mthibitishia Mwenyezi Mungu Mtukufu kile alicho kithibitisha yeye mwenyewe katika Kitabu chake, au kamthibitishia katika sunna zake Mtume wake Muhammad rehema na amani ziwe juu yake. Walimthibitishia bila ya kumfananisha, na wakamtakasa Mwenyezi Mungu Mtukufu kutokana na kufanana na viumbe wake utakaso ulio mbali na kuzikataa sifa zake. Kwa hivyo, wakafanikiwa kwa kusalimika kutokana na mgongano. Waliufanyia kazi ushahidi wote kwa kuwezeshwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa sababu ni katika sunna na kawaida ya Mwenyezi Mungu kumuwezesha mtu aliyekamatana na haki ambayo amewatuma nayo Mitume wake, na katowa kwa ajili ya hilo bidii zake, na akamkusudia Mwenyezi Mungu tu katika kutafuta kwake, kwamba Mwenyezi Mungu humuwezesha kuipata haki na kudhihiri ushahidi wake kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿بَلۡ نَقۡذِفُ بِٱلۡحَقِّ عَلَى ٱلۡبَٰطِلِ فَيَدۡمَغُهُۥ فَإِذَا هُوَ زَاهِقٞ...﴾

"Bali (tulifanyalo ni hili) tunaitupa kweli juu ya batili; ikaivunjilia mbali, na mara ikatoweka." [Surat Al-Anbiyaa: 18].

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَلَا يَأۡتُونَكَ بِمَثَلٍ إِلَّا جِئۡنَٰكَ بِٱلۡحَقِّ وَأَحۡسَنَ تَفۡسِيرًا33﴾

"Na hawakujii, ewe Mtume, hawa washirikina na hoja yoyote au utata wowote isipokuwa tutakuletea majibu ya ukweli na ufafanuzi wake mzuri zaidi." [Surat Al-Furqan: 33]

 

 

Na ama yule ambaye amekwenda kinyume na itikali ya Ahlusunnah kwa namna wanavyoitakidi katika mlango wa majina na sifa, huyo hapana shaka ni lazima atakuwa amekwenda kinyume na ushahidi wa Qur'ani na Sunna na ushahidi wa kiakili; na atakuwa ni mwenye kukinzana waziwazi na kila anachokithibitisha na kukikataa. Na ametaja Al-haafidh ibnu Kathiir -Mwenyezi Mungu amrehemu- katika tafsiri yake maarufu, kataja maneno mazuri katika maudhui hii, pale aliposema kuhusu maneno ya Mwenyezi Mungu -Mwenye nguvu na utukufu:

﴿إِنَّ رَبَّكُمُ ٱللَّهُ ٱلَّذِي خَلَقَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٖ ثُمَّ ٱسۡتَوَىٰ عَلَى ٱلۡعَرۡشِ...﴾

"Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwenyezi Mungu aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akainuka juu ya Kiti cha Enzi." [Al-A'araf: 54]

Na inapendeza kuyanukuu maneno hayo hapa kutokana na faida zake kubwa. Amesema ibnu Kathiir -Mwenyezi Mungu amrehemu- maneno ambayo maandishi yake yanasema hivi:

Watu kwenye suala hili wana maneno mengi sana, na hapa siyo mahala sahihi pa kuyakunjua maneno hayo. Sisi katika suala hili tunafuata madhehebu ya wema waliotangulia: Maaliki, Auzaaiy, At-Thauriy, Al-laithiy ibnu Saad, Ash-Shaafiiy, Ahmad ibnu Hanbal na Is-haqa ibnu Rahawaihi na wengineo miongoni mwa maimamu wa Waislamu wazamani na wa sasa. Nao ni msimamo wa kuyapitisha kama yalivyokuja pasina kutafuta kujua namna yalivyo haswa wala kuyafananisha wala kuyakataa. Na maana ya dhahiri inayotokea kwenye akili za wenye kuyafananisha haiingiliani na Mwenyezi Mungu.

Kwa hakika Mwenyezi Mungu hafanani na chochote katika viumbe wake.

﴿...لَيۡسَ كَمِثۡلِهِۦ شَيۡءٞۖ وَهُوَ ٱلسَّمِيعُ ٱلۡبَصِيرُ﴾

"Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona." [Ash-Shuraa: 11]. Bali uhakika wa jambo hilo ni kama walivyokwisha sema maimamu - miongoni mwao ni Nu'aimu ibnu Hammad Al-khuzaaiy, sheikh wa imamu Bukhariy alisema: "Yeyote atakaye mfananisha Mwenyezi Mungu na viumbe vyake, basi amekufuru. Na mwenye kupinga sifa aliyojisifu kwayo Mwenyezi Mungu, basi hakika amekufuru.10 Na hakuna kufananisha kokote katika sifa ambazo Mwenyezi Mungu alijisifia mwenyewe wala sifa ambazo amesifiwa kwazo na Mtume wake. Kwa hivyo, mwenye kumthibitishia Mwenyezi Mungu Mtukufu sifa zilizopokelewa katika aya zilizo waziwazi na hadithi sahihi kwa njia inayo endana na utukufu wa Mwenyezi Mungu, na aka mkanushia Mwenyezi Mungu mapungufu, basi hakika huyo atakuwa amefuata njia ya uongofu."11 mwisho wa kunukuu maneno ya Ibnu Kathiir Mwenyezi Mungu amrehemu.

Na huingia vilevile katika imani ya kumuamini Mwenyezi Mungu: kuwa na itikadi kwamba imani sahihi inakusanya maneno na vitendo. Imani hiyo inazidi kwa kutii maamrisho, na hupunguwa kwa kufanya madhambi. Na haifai kumkufurisha Muislamu kwa kufanya kitu katika madhambi ambayo siyo ushirikina wala kufuru, kama vile kufanya zinaa, kuiba, kula riba, kunywa pombe, kutowatendea wema wazazi wawili na mengineyo katika madhambi makubwa ikiwa hakuyafanya kuwa ni halali. Hili ni kwa mujibu maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَغۡفِرُ أَن يُشۡرَكَ بِهِۦ وَيَغۡفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَآءُ...﴾

"Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kushirikishwa, na husamehe madhambi yasiyokuwa shirki kwa amtakaye." [An-Nisaa: 48] Na kwa uthibitisho wa hadithi zilizopokelewa na wengi kutoka kwa Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- miongoni mwazo ni maneno yake: "Hakika Mwenyezi Mungu atamtoa Motoni yeyote atakayekuwa katika moyo wake na imani yenye uzito sawa na punje ya haradali."12

 

Msingi wa pili: Kuwaamini Malaika, na imani hii inakusanya mambo mawili:

Na inakusanya mambo mawili: Jambo la kwanza: kuwaamini Malaika kwa ujumla; nako ni kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ana Malaika amewaumba ili wamtii na akawasifia kuwa wao:

﴿وَقَالُواْ ٱتَّخَذَ ٱلرَّحۡمَٰنُ وَلَدٗاۗ سُبۡحَٰنَهُۥۚ بَلۡ عِبَادٞ مُّكۡرَمُونَ 26 لَا يَسۡبِقُونَهُۥ بِٱلۡقَوۡلِ وَهُم بِأَمۡرِهِۦ يَعۡمَلُونَ27 يَعۡلَمُ مَا بَيۡنَ أَيۡدِيهِمۡ وَمَا خَلۡفَهُمۡ وَلَا يَشۡفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ٱرۡتَضَىٰ وَهُم مِّنۡ خَشۡيَتِهِۦ مُشۡفِقُونَ28﴾

"Na wanasema: 'Arrahman (Mwingi wa rehema), ana mwana!' Subhanahu (ametakasika mbali na hayo)! Bali hao (wanaowaita wana) ni waja waliotukuzwa.

"Hawamtangulii kwa neno nao wanafanya kwa amri zake.

"Mwenyezi Mungu anayajuwa yaliyo mbele yao (hao Malaika) na yaliyo nyuma yao (hao Malaika) wala hawamuombei yeyote ila yule anayemridhia Mwenyezi Mungu, nao kwa sababu ya kumuogopa wananyeyekea." [Surat Al-Anbiyaa: 26-28]

Na wao wapo aina nyingi. Miongoni mwao kuna wale waliopewa jukumu la kubeba Kiti cha Enzi, na wengine ni walinzi wa Pepo na Moto, na wengine wamepewa jukumu la kuyahifadhi matendo ya waja. Jambo la pili: Kuwaamini Malaika mmoja mmoja kwa kina. Na hilo ni kwa kuamini jina la Malaika aliloitwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kama vile jina la Jibril aliyepewa jukumu la kubeba Ufunuo wa Mwenyezi Mungu (wahyi), na Mikaili aliyepewa jukumu la kunyesheleza mvua, na Malik mlinzi wa Moto, na Israfiil aliyepewa jukumu la kupuliza parapanda. Kama ulivyokuja utajo wao katika Hadithi sahihi, miongoni mwa hizo hadithi ni hadithi iliyothibiti katika sahihi kutoka kwa Aisha -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- kuwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, amesema: "Wameumbwa Malaika kutokana na nuru, na wameumbwa majini kutokana moto halisi, na ameumbwa Adam kutokana na udongo kama mlivyoelezewa."13 Ameipokea Imamu Muslim katika Sahihi yake.

 

 

 

 

Msingi wa tatu: Kuamini Vitabu. Na hili linakusanya vile vile mambo mawili:

Jmabo la kwanza: Kuviamini Vitabu kwa ujumla. Hilo ni kwa kuamini kwamba Mwenyezi Mungu aliteremsha Vitabu kwa Manabii na Mitume wake; ili kuweka wazi haki yake, na kulingania hiyo haki kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿لَقَدۡ أَرۡسَلۡنَا رُسُلَنَا بِٱلۡبَيِّنَٰتِ وَأَنزَلۡنَا مَعَهُمُ ٱلۡكِتَٰبَ وَٱلۡمِيزَانَ لِيَقُومَ ٱلنَّاسُ بِٱلۡقِسۡطِ...﴾

"Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa hoja za waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu." [Al Hadid: 25]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿كَانَ ٱلنَّاسُ أُمَّةٗ وَٰحِدَةٗ فَبَعَثَ ٱللَّهُ ٱلنَّبِيِّـۧنَ مُبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ وَأَنزَلَ مَعَهُمُ ٱلۡكِتَٰبَ بِٱلۡحَقِّ لِيَحۡكُمَ بَيۡنَ ٱلنَّاسِ فِيمَا ٱخۡتَلَفُواْ فِيهِ...﴾

"Watu wote walikuwa ni umma mmoja. Basi Mwenyezi Mungu akatuma Manabii wabashiri na waonyaji. Na pamoja nao akateremsha Kitabu kwa Haki, ili kihukumu baina ya watu katika yale waliyohitilafiana. Na wala hawakuhitalifiana ndani yake ila wale waliopewa Kitabu hicho..." [Al-Baqara: 213]

 

 

Jambo la pili: Kuviamini Vitabu kimoja kimoja; nako ni kuamini vitabu alivyoviita Mwenyezi Mungu kwa majina yake, kama vile Taurati, Injili, Zaburi, na Qur'ani. Na tunaitakidi kwamba Qur'ani ndiyo kitabu bora zaidi na cha mwisho. Nayo Qur'ani ndiyo yenye kuvihukumu vitabu vyote na yenye kuvisadikisha. Na Qur'ani ndicho kitabu ambacho yaupasa umma wote kukifuata na kuhukumu kwacho; pamoja na kuhukumu kwa habari sahihi zilizopokelewa kutoka kwa Mtume - rehema na amani ziwe juu yake. Kwa sababu, Mwenyezi Mungu Mtukufu alimtuma Mtume wake Muhammad -rehema na mani ziwe juu yake- kwa majini na watu, na akamteremshia hii Qur'ani ili awahukumu kwayo, na kaifanya hii Qur'ani kuwa ni ponyo ya maradhi ya nyoyo, na ubainisho wa kila kitu, na ni muongozo na rehema kwa Waumini, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَهَٰذَا كِتَٰبٌ أَنزَلۡنَٰهُ مُبَارَكٞ فَٱتَّبِعُوهُ وَٱتَّقُواْ لَعَلَّكُمۡ تُرۡحَمُونَ155﴾

"Na hiki ni Kitabu tulichokiteremsha, kilichobarikiwa. Basi kifuateni, na mcheni Mungu, ili mrehemewe." [Al-An'aam: 155]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...وَنَزَّلۡنَا عَلَيۡكَ ٱلۡكِتَٰبَ تِبۡيَٰنٗا لِّكُلِّ شَيۡءٖ وَهُدٗى وَرَحۡمَةٗ وَبُشۡرَىٰ لِلۡمُسۡلِمِينَ﴾

 

"Na tumeteremsha kwako Kitabu, kiwe ni upambanuzi wa kila kitu, na muongozo na rehema, na bishara njema kwa Waislamu." [An-Nahli: 89]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿قُلۡ يَٰٓأَيُّهَا ٱلنَّاسُ إِنِّي رَسُولُ ٱللَّهِ إِلَيۡكُمۡ جَمِيعًا ٱلَّذِي لَهُۥ مُلۡكُ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضِۖ لَآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ يُحۡيِۦ وَيُمِيتُۖ فَـَٔامِنُواْ بِٱللَّهِ وَرَسُولِهِ ٱلنَّبِيِّ ٱلۡأُمِّيِّ ٱلَّذِي يُؤۡمِنُ بِٱللَّهِ وَكَلِمَٰتِهِۦ وَٱتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمۡ تَهۡتَدُونَ158﴾

"Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume kwenu nyinyi nyote, niliyetumwa na Mwenyezi Mungu Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Hakuna mungu ila Yeye anayehuisha na anayefisha. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake asiyejua kusoma na kuandika, ambaye anamuamini Mwenyezi Mungu na maneno yake. Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka." Na aya zenye maana hii ni nyingi.

Nguzo ya nne: Kuwaamini Mitume

Na inakusanya mambo mawili: Jambo la kwanza: Kuwaamini Mitume kwa ujumla. Nako ni kuamini kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwatumia waja wake Mitume kutoka miongoni mwao, ili watoe habari njema na waonye, na walinganizi wa haki. Kwa hivyo, yeyote atakayewakubali, atafaulu kwa kuwa na furaha. Na atakayewapinga, atastahiki hasara na majuto. Na wa mwisho wao na mbora wao zaidi ni Mtume Muhammad ibnu Abdillah -rehema na amani ziwe juu yake- kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَلَقَدۡ بَعَثۡنَا فِي كُلِّ أُمَّةٖ رَّسُولًا أَنِ ٱعۡبُدُواْ ٱللَّهَ وَٱجۡتَنِبُواْ ٱلطَّٰغُوتَ...﴾

"Na kwa hakika tulituma katika kila umma Mtume, ya kuwa muabuduni Mwenyezi Mungu na jiepusheni na kila kinachoabudiwa kinyume na Mwenyezi Mungu." [An-Nahli: 36]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿رُّسُلٗا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى ٱللَّهِ حُجَّةُۢ بَعۡدَ ٱلرُّسُلِ...﴾

"Mitume hao ni wabashiri na waonyaji, ili watu wasiwe na hoja juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kuletewa Mitume." [An-Nisaa: 165] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَآ أَحَدٖ مِّن رِّجَالِكُمۡ وَلَٰكِن رَّسُولَ ٱللَّهِ وَخَاتَمَ ٱلنَّبِيِّـۧنَ...﴾

"Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na mwisho wa Manabii." [Al-Ahzab: 40].

Jambo la pili: Kuwaamini Mitume mmoja mmoja. Nako ni kuwaamini Mitume mmoja mmoja na kuwaita kwa majina yao kama alivyowaita Mwenyezi Mungu au kama yalivyothibiti majina yao kutoka kwa Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake; Kama vile Nuuh, Huud, Swaaleh, Ibrahim, na wengineo rehema na amani za Mwenyezi na Mungu ziwe juu yao na juu watu wa familia zao na wafuasi wao.

Msingi wa tano: Kuamini siku ya Mwisho

Msingi huu unajumuisha:

Kuamini kila kitu ambacho Mwenyezi Mungu na Mtume wake rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake walifahamisha kuwa kitatokea baada ya kufa, kama vile mtihani wa kaburini, adhabu na neema zake, na yale yatakayokuwa siku ya Kiyama miongoni mwa mambo ya kutisha na ya shida, na kutakuwepo na Njia (Swiraat), mizani, kuhesabiwa, kulipwa na kusambazwa vitabu vya matendo kwa watu. Basi kutakuwa na mwenye kukichukuwa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia na mwenye kukichukuwa kwa mkono wake wa kushoto au kwa nyuma ya mgongo wake.

Na inaingia vilevile katika imani, kuamini uwepo hodhi ya kunywa maji ya Mtume wetu Muhammad rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ambayo watu watakwenda kunywa maji humo, na kuamini uwepo wa Pepo na Moto, Waumini kumuona Mola wao Mlezi Mtukufu na kuwasemesha wao, na kuamini mengineyo yaliyokuja katika Qur'ani na hadithi sahihi kutoka kwa Mtume rehema amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Ni wajibu kuamini hayo yote na kuyasadikisha kwa namna alivyoweka wazi Mwenyezi Mungu na Mtume wake rehema na mani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.

Msingi wa sita: Kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu

Na inaingia ndani yake kuyaamini mambo manne:

Jambo la kwanza: Kuamini kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu, hakika alikwishajuwa yaliyokuwepo na yaliyopo sasa. Na alijua hali za waja wake, riziki zao, vifo vyao, matendo yao na mengineyo katika mambo yao. Kwa hivyo, hakifichikani kitu chochote kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...وَٱعۡلَمُوٓاْ أَنَّ ٱللَّهَ بِكُلِّ شَيۡءٍ عَلِيمٞ﴾

"Na jueni ya kuwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua zaidi kila kitu." [Al-Baqara: 231] Na amesema Mwenye Nguvu na utukufu:

﴿...لِتَعۡلَمُوٓاْ أَنَّ ٱللَّهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيۡءٖ قَدِيرٞ وَأَنَّ ٱللَّهَ قَدۡ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيۡءٍ عِلۡمَۢا﴾

"Ili mjue kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu, na kwamba Mwenyezi Mungu amekizingira kila kitu kukijua vilivyo kwa elimu yake." [At-Talaq: 12].

 

 

Jambo la pili: Kuamini kwamba Mwenyezi Mungu alikwishaandika kila alilolipanga na kulipitisha; kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿قَدۡ عَلِمۡنَا مَا تَنقُصُ ٱلۡأَرۡضُ مِنۡهُمۡۖ وَعِندَنَا كِتَٰبٌ حَفِيظُۢ 4﴾

"Hakika Sisi tunajua kiasi cha kila kinachopunguzwa na ardhi kutokana nao. Na kwetu kipo Kitabu kinachohifadhi yote." [Qaaf: 4]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...وَكُلَّ شَيۡءٍ أَحۡصَيۡنَٰهُ فِيٓ إِمَامٖ مُّبِينٖ﴾

"Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asili lenye kubainisha." [Yasin: 12]

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿أَلَمۡ تَعۡلَمۡ أَنَّ ٱللَّهَ يَعۡلَمُ مَا فِي ٱلسَّمَآءِ وَٱلۡأَرۡضِۚ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَٰبٍۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى ٱللَّهِ يَسِيرٞ70﴾

"Je, hujui kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na katika ardhi? Hakika hayo yamo Kitabuni. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi." [Al-Hajj: 70]

Jambo la tatu: Kuamini matashi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu anayoyapitisha. Alitakalo liwe, linakuwa. Na asilolitaka lisiwe, basi haliwi. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...إِنَّ ٱللَّهَ يَفۡعَلُ مَا يَشَآءُ﴾

"Hakika Mwenyezi Mungu hufanya atakalo." [Al-Hajj: 18]. Na amesema Mwenye Nguvu na utukufu:

﴿إِنَّمَآ أَمۡرُهُۥٓ إِذَآ أَرَادَ شَيۡـًٔا أَن يَقُولَ لَهُۥ كُن فَيَكُونُ82﴾

"Hakika amri yake anapotaka kitu kiwe, ni kukiambia, "Kuwa!" Na kikawa." [Yasin: 82]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمَا تَشَآءُونَ إِلَّآ أَن يَشَآءَ ٱللَّهُ رَبُّ ٱلۡعَٰلَمِينَ29﴾

"Wala nyinyi hamtataka isipokuwa atake Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote."

[At-Takwir: 29].

Jambo la Nne: Kuamini uumbaji wa Mwenyezi Mungu Mtukufu wa viumbe vyote vilivyopo. Hivyo basi, hakuna muumba zaidi yake Yeye, na wala hakuna mola mlezi asiyekuwa Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿ٱللَّهُ خَٰلِقُ كُلِّ شَيۡءٖۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيۡءٖ وَكِيلٞ62﴾

"Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu, na Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu." [Az-Zumar: 62] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿يَٰٓأَيُّهَا ٱلنَّاسُ ٱذۡكُرُواْ نِعۡمَتَ ٱللَّهِ عَلَيۡكُمۡۚ هَلۡ مِنۡ خَٰلِقٍ غَيۡرُ ٱللَّهِ يَرۡزُقُكُم مِّنَ ٱلسَّمَآءِ وَٱلۡأَرۡضِۚ لَآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَۖ فَأَنَّىٰ تُؤۡفَكُونَ3﴾

"Enyi watu, kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu. Ati yupo muumba mwengine asiyekuwa Mwenyezi Mungu anayekupeni riziki kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Hapana mungu ila Yeye tu. Basi wapi mnakogeuzwa?" [Faatir: 3]

Basi kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu kuna jumuisha kuamini haya mambo manne yote kama ilivyo katika itikadi ya Ahlussunnah waljamaa; tofauti na wenye kupinga baadhi ya hayo mambo katika watu wa uzushi (Bidaa).

Na miongoni mwa mambo muhimu katika itikadi sahihi ambayo wanayaitakidi Ahlussunnah waljamaa ni kupenda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kuchukia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kuwafanya vipenzi na kusaidiana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kuwafanya uadui kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo itikadi inayoitwa kupenda na kuchukia, na itikadi hii ni katika kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Hivyo basi, Muumini huwapenda Waumini wenzake na huwafanya ni vipenzi, na huwachukia makafiri na kuwafanyia uadui. Na Waumini wakuu sana katika umma huu ni Maswahaba wa Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake kama ilivyopitishwa kwa Ahlussunna waljamaa. Wao wanawapenda na wanawafanya kuwa ni vipenzi vyao, na wanaitakidi kuwa hao Maswahaba ndio watu bora zaidi baada ya Mitume, kwa maneno ya Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Karne iliyo bora zaidi ni karne yangu, kisha karne ya waliofuata, kisha waliofuata."14 Wanachuoni wamekubaliana kwamba hadithi hii ni sahihi.

Na wanaitakidi kuwa mbora wao zaidi ni Abubakari As-Swiddiq, kisha Umar Al-Faaruuq, kisha Uthman Dhunnurain, kisha Ali Al-murtadhwa radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote. Kisha wanafuatia baada yao waliosalia miongoni mwa wale kumi waliobashiriwa Pepo, kisha Maswahaba wote radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao. Wananyamazia ugomvi uliokuwa kati ya Maswahaba, na wanaitakidi kuwa wao katika ugomvi huo walikuwa ni wenye kujitahidi. Yeyote aliyefikia usahihi, ana malipo mara mbili. Na aliyekosea, basi atapata malipo mara moja.

Na wanawapenda watu wa nyumba ya bwana Mtume -rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- wenye kumuamini Mtume na ni vipenzi vyao, na wanawapenda wake za Mtume wa Mwenyezi Mungu -rehema na amani ziwe juu yake- na wake hao ni mama wa Waumini na wanawaombea radhi wote. Na wanajiweka mbali na njia za Mashia ambao wanawachukia Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu -rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- na wanawatukana, na kuwasifia watu wa nyumba ya Mtume (Ahlul baiti) zaidi kupita kiasi, na kuwainua juu zaidi ya nafasi yao aliyowaweka Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu na utukufu. Vile vile, wanajiweka mbali na kundi la Nawaaswib, kundi ambalo linawaudhi watu wa nyumba ya Mtume (Ahlul baiti) kwa maneno na vitendo.

Na haya yote tuliyoyataja yanaingia kwenye itikadi sahihi ambayo Mwenyezi Mungu amemtuma Mtume wake Muhammad -rehema na mani ziwe juu yake- kwayo. Nayo ni itikadi ambayo ni wajibu kuiamini, kushikamana nayo, kunyooka juu yake na kujihadhari na itikadi zenye kupingana nayo. nayo pia ndiyo itikadi ya kundi lililofaulu la Ahlussunna waljamaa, kundi ambalo ameliongelea Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- kwa kusema: "Halitowacha kundi moja katika umma wangu kuwa washindi kwenye haki. Hawadhuriki na mwenye kuwaachilia mbali (bila usaidizi) mpaka ije amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu wakiwa vivyo hivyo."15 Na katika riwaya, ilikuja hadithi hii hivi: "Halitowacha kundi katika umma kunusuriwa kwenye haki."16 Na amesema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Wamegawanyika Mayahudi katika makundi sabini na moja, nao Wakristo wamegawanyika katika makundi sabini na mbili. Na utagawanyika umma huu katika makundi sabini na tatu. Makundi hayo yote yataingia Motoni isipokuwa kundi moja." Tukasema: 'Ni la akina nani ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?' Akasema: "Yeyote atakayekuwa katika mfano wa yale niliyo nayo mimi na Maswahaba zangu."17

 

Itikadi zinazopingana na itikadi sahihi

Wenye kuipinga hii itikadi, na wenye kwenda kinyume nayo; ni makundi mengi. Miongoni mwao kuna wenye kuabudu Masanamu, Malaika, Mawalii, majini, miti, mawe na vinginevyo. Haya makundi yote hayakukubali wito wa Mitume, bali waliwapinga na hawakuwajali, kama ambavyo Makuraishi na makundi ya Waarabu walivyomfanyia Mtume wetu Muhammad - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Walikuwa wakiiomba miungu yao kuwakidhia haja zao, kuwaponya wagonjwa wao na kuwakinga kutokana na maadui zao. Pia walikuwa wakichinja kwa ajili yao na wakiweka nadhiri kwa ajili yao. Alipowakataza hayo Mtume -rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- na akawaamrisha kumfanyia ibada Mwenyezi Mungu peke yake, walishangaa jambo hilo na wakampinga na wakasema:

﴿أَجَعَلَ ٱلۡأٓلِهَةَ إِلَٰهٗا وَٰحِدًاۖ إِنَّ هَٰذَا لَشَيۡءٌ عُجَابٞ5﴾

"Amewafanya miungu wote kuwa ni Mungu Mmoja tu? Hakika hili ni jambo la ajabu sana." [Swad: 5]

Basi Mtume -rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- hakuwacha kuwalingania kuelekea kwa Mwenyezi Mungu, kuwatahadharisha na ushirikina na kuwawekea wazi uhakika wa yale wanayoyalingania, mpaka Mwenyezi Mungu akawaongoza wale walioongoka miongoni mwao, kisha wakaingia baada ya hapo katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi kwa makundi na ikadhihiri dini ya Mwenyezi Mungu na kuzishinda dini zingine zote baada ya wito endelevu na Jihadi ndefu ya Mtume -rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- na Maswahaba zake, Mwenyezi Mungu awaridhie, na wale waliofuata baada yao kwa wema. Kisha hali ikabadilika, na viumbe wengi wakagubikwa na ujinga; na wengi wakarudi kwenye dini za zama za ujinga, kwa kuvuka mipaka kuhusiana na Manabii na mawalii, na kuwaomba na kuwataka msaada, na aina zingine za ushirikina. Na hawakujuwa maana ya neno "Laailaha ilallahu (hakuna mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu)" kama walivyojua maana yake makafiri wa Kiarabu. Basi Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuombwa msaada.

Ushirikina huu haujaacha kuendelea kuenea miongoni mwa watu hadi wakati wetu. Kwa sababu ya kuenea kwa ujinga na kuwepo kwa kipindi kirefu kutokea zama za unabii.

Na tuhuma zenye utata za hawa washirikina wa zamani ndizo tuhuma za utata za washirikina wa sasa, nazo ni kauli zao:

﴿...هَٰٓؤُلَآءِ شُفَعَٰٓؤُنَا عِندَ ٱللَّهِ...﴾

"Hawa ni waombezi wetu kwa Mwenyezi Mungu." [Yunus: 18], Na maneno yao waliposema:

﴿...مَا نَعۡبُدُهُمۡ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَآ إِلَى ٱللَّهِ زُلۡفَىٰٓ...﴾

"Sisi hatuwaabudu wao isipokuwa ili wapate kutujongeza tu kumkaribia Mwenyezi Mungu." [Az-Zumar: 3]. Na hakika Mwenyezi Mungu alibatilisha utata huu, na akaweka wazi kuwa atakayemuabudu asiyekuwa Yeye awe atakavyokuwa, atakuwa ame mshirikisha Mwenyezi Mungu na amemkufuru, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَيَعۡبُدُونَ مِن دُونِ ٱللَّهِ مَا لَا يَضُرُّهُمۡ وَلَا يَنفَعُهُمۡ وَيَقُولُونَ هَٰٓؤُلَآءِ شُفَعَٰٓؤُنَا عِندَ ٱللَّهِ...﴾

"Nao, badala ya Mwenyezi Mungu, wanaabudu wasiowadhuru wala kuwanufaisha, na wanasema: 'Hawa ndio waombezi wetu kwa Mwenyezi Mungu!" [Yunus: 18] Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu akawajibu kwa maneno yake:

﴿قُلۡ أَتُنَبِّـُٔونَ ٱللَّهَ بِمَا لَا يَعۡلَمُ فِي ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَلَا فِي ٱلۡأَرۡضِۚ سُبۡحَٰنَهُۥ وَتَعَٰلَىٰ عَمَّا يُشۡرِكُونَ18﴾

"Sema: 'Je, mnamwambia Mwenyezi Mungu asiyoyajua yaliyoko katika mbingu wala katika ardhi? Sub-hanahu wa Taa'la (ametakasika na ametukuka) mbali na hao wanaomshirikisha naye.'" [Yunus: 18]

Basi Mwenyezi Mungu Mtukufu akaweka wazi katika aya hii kuwa kumuabudu asiyekuwa Yeye miongoni mwa Manabii na Mawalii au wengineo ni ushirikina ulio mkubwa hata wakiuita wenye kufanya hivyo kwa jina lingine. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...وَٱلَّذِينَ ٱتَّخَذُواْ مِن دُونِهِۦٓ أَوۡلِيَآءَ مَا نَعۡبُدُهُمۡ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَآ إِلَى ٱللَّهِ زُلۡفَىٰٓ...﴾

"Na wale waliowafanya walinzi wengine badala yake Yeye, Mwenyezi Mungu ni Mwangalizi bora juu yao. Wala wewe si wakili juu yao." [Az-Zumar: 3]. Kisha Mwenyezi Mungu akawajibu kwa kauli yake:

﴿...إِنَّ ٱللَّهَ يَحۡكُمُ بَيۡنَهُمۡ فِي مَا هُمۡ فِيهِ يَخۡتَلِفُونَۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَهۡدِي مَنۡ هُوَ كَٰذِبٞ كَفَّارٞ﴾

"Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao katika yale wanayohitilafiana. Hakika Mwenyezi Mungu hamuongoi aliye muongo kafiri mno." [Az-Zumar: 3].

Basi Mwenyezi Mungu Mtukufu akaweka wazi kwa hayo kuwa kumuabudu kwao asiyekuwa Yeye kwa kuomba, kuhofu, kutaraji na mfano wa hayo ni kumkufuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, na akaweka wazi kuwa kauli yao ni ya uongo waliposema kwamba miungu yao inawaweka karibu zaidi na Mwenyezi Mungu.

Na miongoni mwa itikadi za kikafiri ambazo zinapingana na itikadi iliyo sahihi, na zenye kwenda kinyume na waliyokuja nayo Mitume -rehema na amani ziwe juu yao- ni kile wanachoitakidi wenye kupinga uwepo wa Muumba wanaoishi katika zama hizi miongoni mwa wafuasi wa Marx, Lenin na wasiokuwa hao miongoni mwa walinganizi wa kutokuwepo kwa Muumba na walinganiao ukafiri. Ni sawa waliite hilo kwa jina la Ujamaa au Ukomunisti au Uamsho au yasiyokuwa hayo miongoni mwa majina mengine, hakuna tofauti. Kwani, msingi mkuu wa hawa wanao pinga uwepo wa Mwenyezi Mungu ni kuwa hakuna mungu na kuwa maisha yalipatikana kwa nyenzo tu.

Na miongoni mwa misingi yao ni kupinga kufufuliwa baada ya kufa, na kupinga uwepo wa Pepo na Moto na kupinga dini zote. Na atakayetazama kwenye vitabu vyao na kayasoma waliyokuwa nayo, atayafahamu hayo kwa yakini, na hapana shaka kuwa hizi itikadi zinapingana na dini zote za mbinguni, huwafikisha watu wake kwenye mwisho mbaya hapa duniani na akhera.

Na amiongoni mwa hizo itikadi zenye kupingana na haki, ni kile wanachoitakidi baadhi ya Masufi kwamba baadhi ya wanaowaita Mawalii wanashirikiana na Mwenyezi Mungu kupanga na kuendesha mambo ya ulimwengu, na wanawaita kwa majina ya Aq-twaab (viongozi wakubwa) na Autaad (vigogo) na Al-aghwaath (wasidizi na watoa huduma) na majina mengine ambayo wameyazusha kwa ajili ya miungu wao. Huu ni ushirikina katika umola, nao ndio aina mbaya sana ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Na yeyote atakayefuatilia ushirikina wa washirikina wa zama za ujinga, na akaufananisha na wa washirikina wa zama hizi, atakuta kuwa ushirikina wa zama hizi ni mkubwa zaidi na wa hali ya juu, na kuliweka wazi hilo ni kama hivi: Ni kuwa makafiri wa Kiarabu katika zama za ujinga walijulikana kwa mambo mawili: Jambo la kwanza: Washirikina wa zamani hawakuwa wakishirikisha kwenye umola. Bali ushirikina wao ulikuwa kwenye ibada tu. Kwa maana walikuwa wakiukubali umola wa Mwenyezi Mungu peke yake -Mwenye nguvu na utukufu- kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَلَئِن سَأَلۡتَهُم مَّنۡ خَلَقَهُمۡ لَيَقُولُنَّ ٱللَّهُ...﴾

"Na ukiwauliza ni nani aliyewaumba? Bila ya shaka watasema: "Mwenyezi Mungu!'" [Az-Zukhruf: 87] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿قُلۡ مَن يَرۡزُقُكُم مِّنَ ٱلسَّمَآءِ وَٱلۡأَرۡضِ أَمَّن يَمۡلِكُ ٱلسَّمۡعَ وَٱلۡأَبۡصَٰرَ وَمَن يُخۡرِجُ ٱلۡحَيَّ مِنَ ٱلۡمَيِّتِ وَيُخۡرِجُ ٱلۡمَيِّتَ مِنَ ٱلۡحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ ٱلۡأَمۡرَۚ فَسَيَقُولُونَ ٱللَّهُۚ فَقُلۡ أَفَلَا تَتَّقُونَ31﴾

"Sema: Ni nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Au ni nani anayemiliki kusikia na kuona? Na ni nani amtoaye hai kutoka kwenye maiti, na akamtoa maiti kutoka kwa aliye hai? Na ni nani anayeyaendesha mambo yote? Watasema: Allah (Mwenyezi Mungu). Basi sema: Je, hamumchi?" [Yunus: 31]. Na Aya zenye maana hii ni nyingi sana.

Jambo la pili: Ushirikina wao katika ibada haukuwa ni wa muda wote, bali ulikuwa ukitokea wakati wa raha. Ama wakati wa shida, walikuwa wakimtakasia ibada Mwenyezi Mungu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿فَإِذَا رَكِبُواْ فِي ٱلۡفُلۡكِ دَعَوُاْ ٱللَّهَ مُخۡلِصِينَ لَهُ ٱلدِّينَ فَلَمَّا نَجَّىٰهُمۡ إِلَى ٱلۡبَرِّ إِذَا هُمۡ يُشۡرِكُونَ65﴾

"Na wanapopanda makafiri kwenye majahazi baharini, na wakaogopa kuzama, wanampwekesha Mwenyezi Mungu na kumtakasia dua wakati wa shida yao. Na Anapowaokoa akawafikisha kwenye nchi kavu, na shida ikawaondokea, wanarudi kwenye ushirikina wao." [Al-Ankabut: 65].

Ama washirikina wa sasa, ushurikina wao umezidi zaidi ule wa wale wa mwanzo kwa sehemu mbili: Sehemu ya kwanza: Ushirikina wa baadhi yao kwenye umola Sehemu ya pili: Ushirikina wao wakati wa raha na shida, kama linavyofahamika hilo kwa aliyeishi nao na akawafutalia hali zao, na akayaona wanayoyafanya kwenye kaburi la Hussein na Badawiy na wengineo katika nchi ya Misri, na kwenye kaburi la Al'aidaruus huko Aden, na Al-Haadiy katika nchi ya Yemen, na Ibnu 'Arabiy huko Sham, na sheikh Abdulqadir Al-Jailaaniy katika nchi ya Iraq, na makaburi mengine yaliyo mashuhuri ambayo watu wengi wanayatukuza, na wakayaelekezea haki nyingi za Mwenyezi Mungu - Mwenye nguvu na utukufu. Hata hivyo, ni mara chache sana kupata wenye kuwakataza hayo na kuwabainishia ukweli wa Tauhiid ambayo Mwenyezi Mungu alimtuma nayo Mtume wake, rehema na amani ziwe juu yake, na Mitume waliokuwa kabla yake amani iwe juu yao. Basi sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake Yeye tutarejea.

Na miongoni mwa itikadi potofu zinazopingana na itikadi sahihi katika mlango wa majina na sifa za Mwenyezi Mungu, ni itikadi ya wazushi miongoni mwa kundi liitwalo Jahmiayyah na Muutazila na wenye kufuata njia zao katika kupinga sifa za Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu na utukufu, na kuzikataa sifa zake Mwenyezi Mungu Mtukufu zenye ukamilifu, na badala yake wakamsifia kwa sifa za vitu visivyokuwepo, na visivyokuwa na uhai na visivyowezekana. Ametakasika Mwenyezi Mungu kuwa na sifa wanazomsifia utakasifu mkubwa wa hali ya juu.

Na anaingia katika itikadi potofu kila mwenye kupinga baadhi ya sifa na kukubali baadhi yake, kama vile kundi la Ashaaira. Kwa hakika, inawalazimu katika baadhi ya sifa walizozikubali waende sambamba na zile sifa ambazo walizikimbia na kuzikataa na wakabadilisha maana zake na wakawa ni wenye kwenda kinyume na ushahidi wa Kitabu na sunnah na ushahidi wa kiakili, na wakajitia katika mgongano ulio wazi kabisa kwenye suala hilo.

Ama Ahlussunna waljamaa, wao kwa hakika walimthibitishia Mwenyezi Mungu kile alichojithibitishia mwenyewe au kile alichomthibitishia Mtume wake Muhammad -rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- miongoni mwa majina na sifa kwa ukamilifu, na wakamuweka mbali na kumtakasa kwa kutomfananisha na viumbe wake, utakaso ambao uko mbali na uchafu wa kukataa kwamba Mwenyezi Mungu ana majina na sifa, na wakaufanyia kazi ushahidi wote na hawakuubadilisha wala kuukataa, na wakasalimika kutokana na mgongano ambao ulitokea kwa wengine kama ilivyotangulia kuwekwa wazi jambo hilo.

 

Na hii ndiyo njia ya mafanikio, na maisha mazuri duniani na akhera, na ndiyo njia iliyonyooka waliyoifuata watu wema waliotangulia katika umma huu na viongizi wake. Hawawezi kuwa wema watu wa mwisho wa umma huu, isipokuwa kwa kufuata kile kilichowafanya wa mwanzo wao kuwa wema, nacho ni kufuata Kitabu na Sunna, na kuacha kila kinachokwenda tofauti na viwili hivyo. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aurudishe umma huu kwenye uongofu wake, na wawe wengi walingazi wa uongofu, na awawezeshe viongozi wake na wanawazuoni wake kuupiga vita ushirikina, na kuumaliza kabisa na kutahadharisha dhidi ya njia zake... hakika Yeye ni Mwenye kusikia, aliye karibu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuwezesha, naye ndiye Mwenye kututosheleza na Msimamizi mzuri zaidi, hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu. Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Nabii wetu Muhammad, na familia yake na Maswahaba wake.

***

 


بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Makala ya Pili: Kuhusu hukumu ya kuomba kuokolewa kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, na watu wa familia yake, Maswahaba wake na wote wanaofuata uongofu wake.

Ama baada ya hayo: Gazeti la Al-Mujtama' Al-Kuwaiti katika toleo lake la kumi na tano, lililotokea tarehe 19/4/1390 Hijria, lilichapisha beti kwa anuani ya: (Katika Maadhimisho ya Kuzaliwa Mtume Mtukufu), ambazo zilijumuisha kuomba kuokolewa kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, na kutafuta nusura kutoka kwake kwamba auokoe Umma na kuunusuru na kuukomboa kutoka katika mgawanyiko na kutofautiana ambako uliingia ndani yake. Beti hizo zimetungwa na aliyejiita Amina. Na hizi ndizo beti zenyewe tulizoziashiria hapo juu:

Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, uokoe ulimwengu... unaowaka vita na kuungua kwa miale yake.

Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, uokoe Umma... kutoka katika giza la shaka, ambalo limekuwa refu sana

 

Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, uokoe Umma... uliopoteza maono yake katika michanganyiko ya huzuni

Mpaka aliposema:

Harakisha kuleta ushindi kama ulivyouharakisha... siku ya Badri ulipomuomba Mola Mlezi

Kwa hivyo, udhalili ukageuka kuwa ushindi wa ajabu... hakika Mwenyezi Mungu ana majeshi usiyoyaona

Hivi ndivyo mwandishi huyu anavyoelekeza wito na kuomba kwake kuokolewa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, akimuomba auokoe Umma kwa kuleta nusura haraka, huku akiwa amesahau au hajui kwamba nusura iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu peke yake, si mikononi mwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, wala yeyote mwingine miongoni mwa viumbe, kama alivyoeleza Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Kitabu chake kilicho wazi:

﴿...وَمَا النَّصْرُ إِلَّا مِنْ عِنْدِ اللَّهِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ﴾

"Na msaada hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Mwenye nguvu na Mwenye hekima." [Al-Imran: 126] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿إِنْ يَنْصُرْكُمُ اللَّهُ فَلَا غَالِبَ لَكُمْ وَإِنْ يَخْذُلْكُمْ فَمَنْ ذَا الَّذِي يَنْصُرُكُمْ مِنْ بَعْدِهِ...﴾

 

"Akikunusuruni Mwenyezi Mungu, hapana wa kukushindeni. Na akikutupeni, ni nani basi baada yake Yeye atayekunusuruni?" [Al-Imran: 160]

Kitendo hiki cha kuomba dua na kutafuta kuokolewa ni kuelekeza aina ya ibada kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na imeshajulikana kwa maandiko (ya Qur'ani na Sunna) na kwa makubaliano ya wanazuoni kwamba hilo haliruhusiwi, na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwaumba viumbe ili wamuabudu, na akatuma Mitume na kuteremsha Vitabu ili kufafanua ibada hiyo na kuwaita watu kwayo, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنْسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ56﴾

"Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi." [Surat Adh-Dhariyaat: 56].

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ...﴾

"Na kwa hakika, kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni Twaghuut (Shetani na vyote vinavyoabudiwa kinyume na Mwenyezi Mungu." [Surat An-Nahl: 36]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمَا أَرْسَلْنَا مِنْ قَبْلِكَ مِنْ رَسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ 25﴾

"Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipokuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu." [Surat Al-Anbiya: 25], Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿الر كِتَابٌ أُحْكِمَتْ آيَاتُهُ ثُمَّ فُصِّلَتْ مِنْ لَدُنْ حَكِيمٍ خَبِيرٍ1 أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا اللَّهَ إِنَّنِي لَكُمْ مِنْهُ نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ2﴾

"Alif Lam Raa. Hiki ni kitabu ambacho Aya zake zimewekwa wazi kisha zikapambanuliwa vizuri, kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye hekima, Mwenye habari za kila kitu.

(Imefanywa hivyo) ili msiabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu. Hakika mimi kwenu ni muonyaji na mbashiri nitokae kwake." [Surat Hud: 1-2]

Basi Mwenyezi Mungu Mtukufu akabainisha katika aya hizi zilizo wazi kwamba hakuwaumba wale viumbe wawili wazito (wanadamu na majini) isipokuwa wamu abudu Yeye peke yake, asiye na mshirika, na akaeleza kuwa alituma Mitume –rehema na amani ziwe juu yao- ili waamrishe ibada hii na kukataza kinyume chake, na akaeleza kuwa aliziweka wazi aya za Kitabu chake na kuzipambanua ili kisiabudiwe chochote kisichokuwa Yeye Mtukufu.

Inajulikana kuwa kuabudu maana yake ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtii, kwa kutii maamrisho yake na kuacha makatazo yake. Mwenyezi Mungu ameyaamrisha hayo na kujulisha juu yake katika Aya nyingi, zikiwemo kauli yake aliyetakasika:

﴿وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ...﴾

"Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu." [Surat Al-Bayyina: 5] Na kauli yake Mwenye nguvu, Mtukufu:

﴿وَقَضَى رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ...﴾

"Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu." [Surat Al-Israai: 23] Na kauli yake Mtukufu:

﴿إِنَّآ أَنزَلۡنَآ إِلَيۡكَ ٱلۡكِتَٰبَ بِٱلۡحَقِّ فَٱعۡبُدِ ٱللَّهَ مُخۡلِصٗا لَّهُ ٱلدِّينَ2 أَلَا لِلَّهِ ٱلدِّينُ ٱلۡخَالِصُۚ وَٱلَّذِينَ ٱتَّخَذُواْ مِن دُونِهِۦٓ أَوۡلِيَآءَ مَا نَعۡبُدُهُمۡ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَآ إِلَى ٱللَّهِ زُلۡفَىٰٓ إِنَّ ٱللَّهَ يَحۡكُمُ بَيۡنَهُمۡ فِي مَا هُمۡ فِيهِ يَخۡتَلِفُونَۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَهۡدِي مَنۡ هُوَ كَٰذِبٞ كَفَّارٞ3﴾

"Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa Haki. Basi muabudu Mwenyezi Mungu ukimsafia Dini Yeye tu." Sikilizeni. Hakika Dini Safi ni ya Mwenyezi Mungu tu. Na wale wanaowafanya wenginewe kuwa ni walinzi wakisema: Sisi hatuwaabudu ila wapate kutujongeza tu kumkaribia Mwenyezi Mungu - Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao katika yale wanayohitilafiana. Hakika Mwenyezi Mungu hamuongoi aliye muongo kafiri." [Az-Zumar: 2-3].

Na aya zenye maana hii ni nyingi. Zote zinaonyesha ulazima wa kufanya ibada kwa ajili ya Mwenyezi Mungu peke yake, na kuacha kumuabudu mwingine yeyote, sawa sawa wawe ni Manabii au wengineo.

Hakuna shaka kwamba dua ni miongoni mwa aina ya ibada iliyo muhimu na kamili zaidi. Kwa hivyo, ni lazima kuifanya kwa ajili ya Mwenyezi Mungu peke yake, kama alivyosema Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mtukufu:

﴿فَادْعُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ14﴾

"Basi muombeni Mwenyezi Mungu mkimsafia Dini Yeye tu, hata kama watachukia makafiri." [Surat Ghafir: 14] Na akasema Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mtukufu:

﴿وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّهِ أَحَدًا18﴾

"Na kwamba kwa hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu. Basi msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu" [Surat Al-Jinn: 18] Agizo hili la kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika dua, linawaenea viumbe wote, hata Manabii na wengineo. Na kauli yake:

﴿وَلَا تَدْعُ مِنْ دُونِ اللَّهِ مَا لَا يَنْفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ فَإِن فَعَلۡتَ فَإِنَّكَ إِذٗا مِّنَ ٱلظَّٰلِمِينَ106﴾

"Na wala usiombe badala ya Mwenyezi Mungu wale ambao hawakufai kitu wala hawakudhuru. Na ukifanya hivyo, basi wewe hakika ni miongoni mwa madhalimu." [Surat Yunus: 106] Haya maneno anaambiwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na inajulikana kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu alimkinga kutokana na ushirikina, lakini lengo la haya ni kuwaonya wasiokuwa yeye. Kisha akasema Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu mkubwa:

﴿وَلَا تَدۡعُ مِن دُونِ ٱللَّهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ فَإِنْ فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِنَ الظَّالِمِينَ106﴾

"Na wala usiombe badala ya Mwenyezi Mungu wale ambao hawakufai kitu wala hawakudhuru. Na ukifanya hivyo, basi wewe hakika ni miongoni mwa madhalimu." [Surat Yunus: 106] Maneno haya anaambiwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na kinachokusudiwa kwayo ni kuwaonya wengineo. Kwa sababu inajulikana kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu alimlinda Mtume wake kutokana na ushirikina. Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu akawa mkali katika kukataza na kuonya. Akasema:

﴿...فَإِنْ فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِنَ الظَّالِمِينَ﴾

"Ukifanya hivyo, basi hakika utakuwa miongoni mwa waliodhulumu." Wakati neno dhuluma linatumika kwa maneno ya ujumla, huwa linamaanisha ushirikina mkubwa, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...وَالْكَافِرُونَ هُمُ الظَّالِمُونَ﴾

"Na makafiri ndio madhalimu." [Al-Baqara: 254]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ﴾

"Kwani hakika ushirikina bila ya shaka ni dhuluma kubwa." [Luqman: 13]. Lau bwana wa watoto wa Adam, Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake, angemuomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu, angekuwa miongoni mwa madhalimu, basi itakuwa vipi kuhusu mwingine?!

Ikajulikana kutokana na aya hizi na nyinginezo kwamba kumuomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu miongoni mwa wafu, miti, masanamu na vinginevyo ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kunapingana na kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika ibada, ambayo ndiyo makusudio ya Mwenyezi Mungu kuumba vitu viwili vikubwa (majini na watu), kutuma Mitume, na kuteremsha Vitabu, na kunapingana na maana ya: Hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu. Ambayo hukanusha kuabudiwa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na kumthibitishia Mwenyezi Mungu peke yake ibada, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿ذَٰلِكَ بِأَنَّ ٱللَّهَ هُوَ ٱلۡحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدۡعُونَ مِن دُونِهِۦ هُوَ ٱلۡبَٰطِلُ وَأَنَّ ٱللَّهَ هُوَ ٱلۡعَلِيُّ ٱلۡكَبِيرُ62﴾

"Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye wa Kweli, na kwamba wale wanaowaomba badala yake, ni batili, na kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye Aliye Juu na ndiye Mkubwa" [Al-Hajj: 62].

Na huu ndio msingi wa dini na mila ya Kiislamu, na wala ibada haziwezi kuwa sahihi isipokuwa baada ya asili hii kuwa sahihi, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِنْ قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ65﴾

"Na kwa yakini yamefunuliwa kwako na kwa wale waliokuwa kabla yako: Bila ya shaka ukimshirikisha Mwenyezi Mungu, matendo yako yataanguka, na lazima utakuwa miongoni mwa wenye kupata hasara." [Surat Az-Zumar: 65] Na amesema Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka:

﴿...وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُمْ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴾

"Na lau wangelimshirikisha, yangeliwaharibikia yale waliyokuwa wakiyatenda." [Surat Al-An'am: 88].

Kutokana na yaliyotangulia hapo juu, inadhihirika kuwa Dini ya Uislamu na kushuhudia kwamba: (Hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu) vina misingi miwili mikuu:

 

 

Wa kwanza: Asiabudiwe ila Mwenyezi Mungu peke yake, asiye na mshirika. Kwa hivyo, mwenye kuwaomba wafu miongoni mwa Manabii na wengineo, au akawaomba masanamu, au miti, au mawe, au viumbe vingine, au akaomba kuokolewa nao, au akajikurubisha kwao kwa kuchinja na kuwawekea nadhiri, au akaswali kwa ajili yao, au akasujudu kwa ajili yao; basi hakika atakuwa amewafanya waola badala ya Mwenyezi Mungu, na akawafanya sawa na Mwenyezi Mungu Mtukufu, na akapinga na akakanusha maana ya hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu.

Wa pili: Mwenyezi Mungu Mtukufu hapaswi kuabudiwa isipokuwa kwa mujibu wa sheria ya Nabii na Mtume wake, rehema na amani ziwe juu yake. Kwa hivyo, mwenye kuzua katika Dini yale ambayo Mwenyezi Mungu hakuruhusu, basi hatakuwa ametekeleza maana ya kushuhudia kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na matendo yake hayatamnufaisha wala hayakubaliwa kutoka kwake. Amesema Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu mkubwa:

﴿وَقَدِمْنَا إِلَى مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَنْثُورًا23﴾

"Na tutayaendea yale waliyoyatenda katika vitendo vyao, tuvifanye kama mavumbi yaliyotawanywa." [Surat Al-Furqaan: 23].

 

 

Kilichokusudiwa na matendo yaliyotajwa katika aya hii ni matendo ya mtu aliyekufa huku bado anamshirikisha Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mtukufu.

Pia yanaingia katika hilo matendo yaliyobuniwa ambayo Mwenyezi Mungu hakuyaidhinisha. Hayo yatakuwa siku ya Kiyama kama mavumbi yaliyotawanywa, kwa sababu hayakulingana na sheria yake iliyotakaswa. Kama alivyosema Mtume rehema na amani ziwe juu yake: "Yeyote atakayezua (kitu) katika jambo letu hili (dini) ambalo si miongoni mwake, basi hilo litakataliwa." Wanachuoni wamekubaliana kwamba hadithi hii ni sahihi.

Na muhtasari wa maneno ni kwamba mwandishi huyu ameelekeza kuomba kwake kuokolewa na dua yake kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na akampuuza Mola Mlezi wa walimwengu wote, ambaye nusura, madhara na manufaa, vyote viko mikononi mwake, na hakuna chochote katika hivi kilicho katika mikono ya asiyekuwa Yeye.

Hakuna shaka kwamba jambo hili ni dhuluma kubwa na yenye matokeo mabaya sana. Na Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mtukufu aliamuru watu wamuombe Yeye peke yake, akawaahidi wenye kumuomba kwamba atawaitikia dua yao, na akawaonya wale wanaojivuna kufanya hivyo kwamba wataingia Jahannam, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mtukufu:

﴿وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ 60﴾

"Na Mola wenu Mlezi amesema: Niombeni, nita kuitikieni. Kwa hakika wale wanaojivuna kuniabudu Mimi, wataingia Jahannamu wadhalilike." [Surat Ghafir: 60] Yaani, watakuwa duni na wadhalilifu. Basi aya hii tukufu ikaonyesha kwamba dua ni ibada, na kwamba yeyote atakayejivuna kumuomba Mwenyezi Mungu, basi makazi yake yatakuwa Jahannam. Kwa hivyo, ikiwa hali ya anayejivuna kumuomba Mwenyezi Mungu ni hivyo, basi itakuwaje hali ya yule anayeomba asiyekuwa Yeye na akapuuza kumuomba Mwenyezi Mungu, ambaye Yeye – Mtukufu – ndiye wa karibu zaidi, Mwenye kumiliki kila kitu, na Mwenye uwezo juu ya kila kitu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ 186﴾

"Na waja wangu watakapokuuliza habari zangu, basi Mimi niko karibu. Naitikia maombi ya muombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka." [Surat Al-Baqara: 186], Na Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alieleza katika hadithi sahihi kwamba dua ndiyo ibada, na akamwambia mpwa wake, Abdullah bin Abbas - radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wawili: "Muhifadhi Mwenyezi Mungu, atakuhifadhi. Muhifadhi Mwenyezi Mungu, utamkuta mbele yako. Unapoomba, basi muombe Mwenyezi Mungu. Na unapotaka msaada, basi taka msaada kwa Mwenyezi Mungu." Imesimuliwa na Tirmidhii na wengineo.

Alisema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Yeyote atakayekufa huku ana muomba mwenza pamoja na Mwenyezi Mungu, ataingia Motoni." Imesimuliwa na Bukhari. Na imesimuliwa katika vitabu viwili (Sahihi Bukhari na Sahihi Muslim), kwamba Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake aliulizwa: Ni dhambi ipi kubwa zaidi? Akasema: "Kumfanyia Mwenyezi Mungu mwenza (mshirika) ilhali Yeye ndiye aliyekuumba." Kwa hivyo, kila anayemuomba mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu, au akaomba msaada kwa hicho, au akakiwekea nadhiri, au akakichijia, au akakifanyia ibada ya namna yoyote ile kando na hizi zilizotajwa, basi bila shaka atakuwa amekifanya kuwa mwenza wa Mwenyezi Mungu, sawa awe Nabii, au mtu mtakatifu, au Malaika, au jini, au sanamu, au kiumbe chochote kinginecho.

Hapa mtu anaweza kusema: Ni ipi hukumu ya kumuuliza mtu aliye hai kwa kile anachoweza kufanya, na kutafuta kuokolewa naye katika mambo ya kihisia anayoweza kuyafanya? Jibu ni kwamba hilo sio ushirikina, bali ni jambo la kawaida linaloruhusiwa miongoni mwa Waislamu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kisa cha Musa:

﴿...فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِنْ شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ...﴾

"Basi yule mwenzake akamtaka msaada kumpiga adui yake." [Al-Qasas: 15] Na kama alivyosemwa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kisa cha Musa pia:

﴿فَخَرَجَ مِنْهَا خَائِفًا يَتَرَقَّبُ...﴾

"Basi akatoka humo naye ana hofu, akiangalia huku na huku." [Al-Qaswas: 21] Na kama vile mtu anavyotafuta kuokolewa kutoka kwa marafiki zake katika vita na mambo mengine yanayowatokea watu na ambayo wanahitajiana ndani yake.

Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kuujulisha umma wake kwamba yeye hana uwezo wa kumnufaisha wala kumdhuru yeyote. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿قُلْ إِنَّمَا أَدْعُو رَبِّي وَلَا أُشْرِكُ بِهِ أَحَدًا21 قُلْ إِنِّي لَا أَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا رَشَدًا22﴾

"Sema: 'Hakika mimi ninamuomba Mola wangu Mlezi, wala simshirikishi Yeye na yeyote.' Sema: 'Hakika mimi sina mamlaka ya kukudhuruni wala kukuongozeni.'"

Sema: Mimi sina mamlaka ya kukudhuruni wala kukuongozeni. [Surat Al-Jinn: 21-22] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿قُلْ لَا أَمْلِكُ لِنَفْسِي نَفْعًا وَلَا ضَرًّا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّهُ وَلَوْ كُنْتُ أَعْلَمُ الْغَيْبَ لَاسْتَكْثَرْتُ مِنَ الْخَيْرِ وَمَا مَسَّنِيَ السُّوءُ إِنْ أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ188﴾

"Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara, ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa ninayajua ya ghaibu, ningejizidishia mema mengi, wala ovu lisingenigusa. Mimi si chochote ila ni muonyaji na mbashiri kwa watu wanaoamini." [Surat Al-A'raaf: 188] Na aya zenye maana hii ni nyingi sana.

Na inavyojulikana ni kwamba Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, haombi isipokuwa Mola wake Mlezi, kama ilivyothibiti kutoka kwake kwamba siku ya Badri alikuwa anaomba aokolewe na Mwenyezi Mungu na kumuomba nusura dhidi ya maadui zake, na alikuwa akisisitiza juu ya hilo na kusema: “Ewe Mola Mlezi! Nitimizie yale uliyoniahidi." mpaka yule mwenye kusadikisha mkubwa zaidi, Abubakari, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, akasema: "Imetosha ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwani hakika Mwenyezi Mungu atakutimizia yale aliyokuahidi." Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu akateremsha kauli hii kuhusiana na hilo:

 

﴿إِذۡ تَسۡتَغِيثُونَ رَبَّكُمۡ فَٱسۡتَجَابَ لَكُمۡ أَنِّي مُمِدُّكُم بِأَلۡفٖ مِّنَ ٱلۡمَلَٰٓئِكَةِ مُرۡدِفِينَ9﴾

"Mlipokuwa mkimuomba msaada Mola wenu Mlezi, naye akakujibuni kuwa: Kwa yakini Mimi nitakusaidieni kwa Malaika elfu (moja) wanaofuatana mfululizo." [Surat Al-Anfaal: 9] Basi, Yeye aliyetakasika, akawa kumbusha katika Aya hizi kuomba kwao kuokolewa, na akawaambia kuwa aliwaitikia na akawasaidia kwa Malaika; ili wapate habari njema ya ushindi na utulivu, na Yeye - utukufu ni wake - akabainisha kuwa ushindi hautokani na Malaika, bali ushindi hutoka kwake. Akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمَا النَّصْرُ إِلَّا مِنْ عِنْدِ اللَّهِ...﴾

"Na msaada hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu." [Al-Imran: 126] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَلَقَدْ نَصَرَكُمُ اللَّهُ بِبَدْرٍ وَأَنْتُمْ أَذِلَّةٌ فَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ123﴾

"Na hakika Mwenyezi Mungu alikwishakunusuruni katika Badri nanyi mlikuwa wanyonge. Basi mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kushukuru." [Al-Imran: 123]. Basi Yeye Mtukufu akabainisha katika Aya hii kwamba Yeye ndiye aliyewapa nusura Siku ya Badri. Kwa hivyo, ikajulikana kwa hilo kwamba alichowapa cha silaha na nguvu, na Malaika aliowateremshia ili wawasaidie, hivyo vyote ni visababu vya ushindi, habari njema na utulivu, lakini ushindi huo haukutokana na hayo, bali ulitoka kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Basi ni vipi anafanya ujasiri mwandishi huyu - au mtu mwingine yeyote - kuelekeza kilio chake cha kuomba kuokolewa na kuomba kwake ushindi kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na kumuacha Mola Mlezi wa walimwengu wote, Mmiliki wa kila kitu na Muweza wa kila kitu?!

Hapana shaka kwamba hili ni miongoni mwa ujinga mbaya zaidi, bali ni katika ushirikina mkubwa zaidi. Basi la wajibu kwa mwandishi huyu ni atubu kwa Mwenyezi Mungu aliyetakasika, kwa toba ya kweli. Na toba ya kweli ni ile inayohusisha mambo kadhaa, ambayo ni: Kwanza: Kujutia yale aliyofanya. Pili: Kuachana na aliyoyafanya. Tatu: Kuazimia kutorejea katika aliyofanya; ili kumpa Mwenyezi Mungu taadhima na kumkusudia Yeye peke yake, kufuata amri yake, na kutahadhari yale aliyokataza. Hii ndiyo toba ya kweli. Na kuna jambo la nne mahsusi iwapo kosa lake hilo linahusiana na haki za viumbe, basi naarudishe haki hiyo kwa mwenyewe, au amuombe amuondolee haki hiyo. Hili ndilo sharti la nne.

Mwenyezi Mungu amewaamrisha waja wake kufanya toba na akaahidi kuikubali, kama alivyosema Mtukufu:

﴿وَتُوبُوا إِلَى اللَّهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ31﴾

 

"Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa." [Surat An-Nur: 31] Na alisema kuhusu Wakristo:

﴿أَفَلَا يَتُوبُونَ إِلَى اللَّهِ وَيَسْتَغْفِرُونَهُ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَحِيمٌ74﴾

"Je, hawatubu kwa Mwenyezi Mungu na waka muomba msamaha? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghufira (msamaha) na Mwenye kurehemu" [Al-Maaida: 74] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّهِ إِلَهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ وَمَنْ يَفْعَلْ ذَلِكَ يَلْقَ أَثَامًا68 يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا69 إِلَّا مَنْ تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَئِكَ يُبَدِّلُ اللَّهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَحِيمًا70﴾

"Na wale wasiomuomba mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa haki, wala hawazini. Na atakayefanya hayo, atapata madhara.

Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo akifedheheshwa.

Isipokuwa atakayetubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu." [Al-Furqaan: 68-70] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَهُوَ الَّذِي يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَعْفُو عَنِ السَّيِّئَاتِ وَيَعْلَمُ مَا تَفْعَلُونَ25﴾

"Naye ndiye anayepokea toba kwa waja wake, na anasamehe makosa, na anayajua mnayoyatenda." [Ash-Shuura: 25]

Ilithibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake kwamba alisema: "Uislamu unabomoa yale yaliyokuwa kabla yake, na toba inafuta yale yaliyokuwa kabla yake."

Nimeyaandika maneno haya mafupi kwa sababu ya hatari kubwa ya ushirikina, na kwa sababu ndio dhambi kubwa zaidi, na kwa sababu ya hofu ya watu kudanganywa na yale yaliyoandikwa na mwandishi huyu, na kwa sababu ya ulazima wa kunasihi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kuwanasihi waja wake. Na ninamuomba Mwenyezi Mungu mwenye utukufu mkubwa atunufaishe kwayo, aziboreshe hali zetu na hali za Waislamu wote, atujaalie sisi sote ufahamu wa dini na kuwa imara juu yake, na atulinde sisi na Waislamu wote kutokana na shari za nafsi zetu na ubaya wa matendo yetu. Kwani, Yeye ndiye Msimamizi wa hayo na Mwenye uwezo wa kuyafanya.

 

 

Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Nabii wetu Muhammad, na familia yake na Maswahaba wake.

 

***

 


بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Makala ya Tatu

Kuhusu hukumu ya kutafuta msaada kutoka kwa majini na mashetani, na kuweka nadhiri kwa ajili yao.

Kutoka kwa Abdul-Aziz bin Abdullah bin Baaz kwenda kwa yeyote anayeuona (ujumbe huu) miongoni mwa Waislamu, Mwenyezi Mungu aniwezeshe mimi na wao tushikamane na dini yake na kubaki imara juu yake, aamiin.

Assalaam alaikum Warahmatullaahi Wabarakaatuh

Ama baada ya hayo: Baadhi ya ndugu zangu waliniuliza kuhusu kile ambacho baadhi ya watu wajinga hufanya cha kumuomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na kutafuta msaada wake katika mambo mazito muhimu; kama vile kuwaomba dua majini, kuwataka kuokolewa, kuwawekea nadhiri na kuchinja kwa ajili yao. Na katika hayo pia ni kauli ya baadhi yao: "Enyi saba", na saba ni katika viongozi wa majini, "mchukueni", "mvunjeni mifupa yake", na "kunyweni damu yake", "mkatakateni vipande", "enyi saba, mfanyieni fulani hivi." Au kauli ya baadhi yao: “Mchukueni, enyi majini wa mchana, enyi pepo wa Alasiri.” Haya mara nyingi hupatikana katika baadhi ya maeneo ya kusini (mwa nchi hii). Na mengine yanayohusiana na jambo hili ni kuwaomba dua wafu, wakiwemo Manabii, watu wema na wengineo, na kuwaomba dua Malaika na kuwataka wawaokoe. Yote haya na yanayofanana nayo yanatokea kwa wengi miongoni mwa wale wanaojinasibisha na Uislamu, kwa kutojua na kuwaiga wale waliokuwa kabla yao, na pengine baadhi yao hurahisisha hilo sana na kutumia hoja ya kusema: 'Hili ni jambo linalopita tu juu ya ulimi, na hatulikusudii wala hatuliitakidi.'

Vile vile, akaniuliza kuhusu hukumu ya kuolewa na mtu anayejulikana kwa vitendo hivi, na vichinjwa vyao, na kuwaswalia, na kuswali nyuma yao, na kuhusu kuwasadikisha wachawi na wapiga ramli. Kama mtu anayedai kujua ugonjwa fulani na sababu zake kwa kuangalia tu kitu kilichougusa mwili wa mgonjwa; kama vile kilemba, suruali, kitambaa na mfano wa hivyo.

Jibu: Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu peke yake, na rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie yule ambaye hakuna Nabii baada yake, na juu ya jamaa zake na Maswahaba wake na wote walioongoka kupitia wao mpaka Siku ya Kiyama.

Ama baada ya hayo: Hakika Mwenyezi Mungu Aliyetakasika na kutukuka, aliumba viumbe viwili vizito (majini na wanadamu) ili wamuabudu, na sio kitu kingine chochote, na ili wamuombe Yeye pekee na kumtaka msaada, na kumchinjia, na kumuwekea nadhiri na ibada nyingine zote. Aliwatuma Mitume kuyaleta haya, na akawaamrisha kufanya hivyo, na akateremsha vitabu vya mbinguni, ambavyo kikubwa chake kabisa ni Qur’ani Tukufu, ili kueleza hayo, na kulingania kwayo, na kuwaonya watu dhidi ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kuabudu asiyekuwa Yeye. Hii ndiyo asili ya asili zote na msingi wa dini na mila ya Kiislamu, na ndiyo maana ya kushuhudia kwamba hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu, na uhakika wa hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu. Kwani, inakanusha asifanyiwe uungu na ibada yeyote asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na inamthibitishia - yaani ibada - Mwenyezi Mungu peke yake, mbali na chochote miongoni mwa viumbe. Ushahidi wa hayo kutoka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunnah za Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ni mwingi sana, ikiwa ni pamoja na: Maneno ya Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu mkubwa:

﴿وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنْسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ56﴾

"Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi." [Surat Adh-Dhariyaat: 56]. Na kauli yake Mtukufu:

﴿وَقَضَى رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ...﴾

"Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu." [Surat Al-Israai: 23] Na kauli yake Mtukufu:

﴿وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ...﴾

"Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu." [Surat Al-Bayyina: 5] Na kauli yake Mtukufu:

﴿وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ60﴾

"Na Mola wenu Mlezi amesema: Niombeni, nitakuitikieni. Kwa hakika wale wanaojivuna kuniabudu Mimi, wataingia Jahannamu wadhalilike." [Surat Ghafir: 60] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ...﴾

"Na waja wangu watakapokuuliza kuhusu Mimi, basi Mimi nipo karibu. Naitika maombi ya muombaji anaponiomba." [Al-Baqarah: 186].

Basi Yeye aliyetakasika akabainisha katika Aya hizi kwamba aliumba vitu viwili vizito (majini na watu) ili vimwabudu, na kwamba aliamuru na kuusia waja wake katika Qur’ani iliyo wazi, na kwa ulimi wa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, kwamba asiabudiwe isipokuwa Mola wao Mlezi.

Mwenyezi Mungu Mtukufu alibainisha kuwa dua ni ibada kubwa, na mwenye kutakabari akaiacha, ataingia Motoni. Na akawaamrisha waja wake kumuomba dua Yeye peke yake, na akaeleza kuwa yuko karibu na anajibu dua zao. Basi ikawa ni wajibu kwa waja wote kumkusudia Mola wao Mlezi tu katika dua. Kwa sababu hiyo ni aina ya ibada ambayo wameumbwa kwa ajili yake na wakaamrishwa kuifanya, na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ162 لَا شَرِيكَ لَهُ وَبِذَلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ163﴾

"Sema: 'Hakika Sala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.'"

Hana mshirika yeyote. Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu." [Al-An'am: 162-163]

Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu akamuamrisha Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kuwajulisha watu kwamba sala yake na ibada zake za kuchinja, na uhai wake na kifo chake ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote, asiye na mshirika. Na kwa mujibu wa hayo, mwenye kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu, atakuwa amemshirikisha Mwenyezi Mungu, kama vile akiswali kwa ajili ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu Mwenyezi Mungu -aliyetakasika- aliifanya swala na kuchinja kuwa vitu viwili vinavyo kwenda kwa pamoja, na akajulisha kwamba viwili hivyo ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu peke yake, asiye na mshirika yeyote. Kwa hivyo, mwenye kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu, kama vile majini, Malaika, wafu na wengineo kwa kutaka kujiweka karibu nao kwa kufanya hivyo, basi ni sawa na anayeswali kwa ajili ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Imekuja katika Hadithi sahihi kwamba Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alisema: "Mwenyezi Mungu amemlaani mwenye kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu." Na amesimulia Imaam Ahmad kwa Isnadi Hasan (mlolongo mzuri wa wasimulizi) kutoka kwa Twariq bin Shihab, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba alisema: "Wanaume wawili walipita karibu na watu waliokuwa na sanamu ambalo hakuna mtu angeweza kupita hapo mpaka alitolee kitu. Mmoja wao akaambiwa: Toa kitu kwa ajili yake. Akasema: Sina kitu cha kulitolea. Wakasema: Toa hata kama ni nzi. Kwa hivyo, akalitolea nzi, basi wakamwachilia aende zake na akaingia Motoni. Kisha wakamwambia mwenzake: Litolee kitu. Akasema: Siwezi kumtolea kitu yeyote (kwa njia ya ibada) ila Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa hivyo wakampiga shingo yake (akafa), na akaingia Peponi."

Hivyo basi, ikiwa mwenye kufanya ibada ya kujiweka karibu na sanamu na mfano wake kwa kutoa nzi au mfano wake ni mshirikina anayestahiki kuingia Motoni, basi atakuwa vipi mwenye kuwaomba majini, Malaika na watu wema? Na atakuwa vipi mwenye kuwaomba wamuokoe, akawawekea nadhiri na akajisogeza karibu nao kwa vichinjwa, kwa kutaraji kuhifadhi mali yake kwa kufanya hivyo, au kumponya mgonjwa wake, au kuwafanya wanyama wake na mazao yake kuwa salama? Na atakuwa vipi mwenye kufanya hivyo kwa kuhofu shari za majini, au kitu kama hicho?! Hakuna shaka kwamba mwenye kufanya hivyo na wengine kama yeye, wanastahiki zaidi kuwa washirikina, wanaostahiki kuingia Motoni kuliko mtu huyu aliyelipa sanamu nzi kwa njia ya ibada.

Miongoni mwa yaliyokuja katika suala hili - pia - ni kauli ya Mola Mtukufu:

﴿إِنَّآ أَنزَلۡنَآ إِلَيۡكَ ٱلۡكِتَٰبَ بِٱلۡحَقِّ فَٱعۡبُدِ ٱللَّهَ مُخۡلِصٗا لَّهُ ٱلدِّينَ2 أَلَا لِلَّهِ ٱلدِّينُ ٱلۡخَالِصُۚ وَٱلَّذِينَ ٱتَّخَذُواْ مِن دُونِهِۦٓ أَوۡلِيَآءَ مَا نَعۡبُدُهُمۡ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَآ إِلَى ٱللَّهِ زُلۡفَىٰٓ إِنَّ ٱللَّهَ يَحۡكُمُ بَيۡنَهُمۡ فِي مَا هُمۡ فِيهِ يَخۡتَلِفُونَۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَهۡدِي مَنۡ هُوَ كَٰذِبٞ كَفَّارٞ3﴾

"Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa Haki. Basi muabudu Mwenyezi Mungu ukimsafia Dini Yeye tu."

Sikilizeni. Hakika Dini Safi ni ya Mwenyezi Mungu tu. Na wale wanaowafanya wenginewe kuwa ni walinzi wakisema: Sisi hatuwaabudu ila wapate kutujongeza tu kumkaribia Mwenyezi Mungu - Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao katika yale wanayohitilafiana. Hakika Mwenyezi Mungu hamuongoi aliye muongo kafiri." [Az-zumar: 1-3] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَيَعْبُدُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنْفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِنْدَ اللَّهِ قُلْ أَتُنَبِّئُونَ اللَّهَ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَى عَمَّا يُشْرِكُونَ18﴾

"Nao, badala ya Mwenyezi Mungu, wanaabudu wasiowadhuru wala kuwanufaisha, na wanasema: Hawa ndio waombezi wetu kwa Mwenyezi Mungu! Sema: Je, mnamwambia Mwenyezi Mungu asiyoyajua yaliyoko katika mbingu wala katika ardhi? Sub-hanahu wa Taala (Ametakasika na ametukuka) mbali na hao wanaomshirikisha naye." [Yunus: 18]

Basi Mwenyezi Mungu Mtukufu akajulisha katika Aya hizi mbili kwamba washirikina walichukua kinyume na Mwenyezi Mungu walinzi miongoni mwa viumbe, wakiwaabudu pamoja naye kwa kuwahofu, kuwatumaini, kuwachinjia, kuwawekea nadhiri, kuwaomba dua na mfano wa hayo, wakidai kuwa walinzi hao wanawaweka wale wanaowaabudu karibu na Mwenyezi Mungu na wanawafanyia uombezi kwake. Basi Mwenyezi Mungu aliyetakasika akawakadhibisha na akabainisha batili zao hizo, na akawaita waongo, makafiri na washirikina, na akajitakasa mbali na ushirikina wao huo.

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...سُبْحَانَهُ وَتَعَالَى عَمَّا يُشْرِكُونَ﴾

"Ametakasika na ametukuka mbali na hao wanao mshirikisha naye." [An-Nahli: 1]. Basi ikajulikana kutokana na hayo kwamba mwenye kumchukua Malaika, au Nabii, au jini, au mti au jiwe na akaviomba pamoja na Mwenyezi Mungu, na akavitaka msaada, na akajikurubisha kwavyo kwa nadhiri na kuchinja kwa kutaraji uombezi wake kwa Mwenyezi Mungu, na kumjongeza kwake, au kutaraji kuponya wagonjwa, au kuhifadhi mali, au usalama wa asiyekuwapo, au mengineyo, basi hakika atakuwa ameanguka katika ushirikina huu mkubwa na balaa la kutisha, ambalo Mwenyezi Mungu alisema juu yake:

﴿إِنَّ اللَّهَ لَا يَغْفِرُ أَنْ يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَلِكَ لِمَنْ يَشَاءُ وَمَنْ يُشْرِكْ بِاللَّهِ فَقَدِ افْتَرَى إِثْمًا عَظِيمًا48﴾

"Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kushirikishwa, na husamehe yaliyo chini ya hilo kwa amtakaye. Na anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, basi hakika amezua dhambi kubwa." [An-Nisaa: 48]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿إِنَّهُ مَنْ يُشْرِكْ بِاللَّهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنْصَارٍ72﴾

 

"Kwani anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu atamharamishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na waliodhulumu hawatakuwa na wa kuwanusuru." [Al-Ma’idah: 72].

Uombezi Siku ya Kiyama utatolewa tu kwa ajili ya watu wa tauhidi na ikhlasi, si kwa watu wa ushirikina, kama alivyosema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alipoulizwa: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni nani kati ya watu wote atakaye furahia uombezi wako? Akasema: "Atakayesema: 'Laa ilaaha illa llaahu (Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu)' likiwa limetoka moyoni mwake kwa utakasifu kabisa." Alisema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Kila Nabii ana dua inayojibiwa. Basi kila Nabii akaharakisha kuomba dua yake. Nami nimeihifadhi dua yangu iwe ni uombezi kwa ajili ya umma wangu Siku ya Kiyama, nayo itampata -Mwenyezi Mungu akipenda- kila atakayekufa katika umma wangu huku hamshirikishi Mwenyezi Mungu na chochote."

Washirikina wa mwanzo walikuwa wakiamini kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mola wao Mlezi, Muumba na Mruzuku wao. Walitegemea tu Mitume, na watu wema, na Malaika, na miti, na mawe na mfano wa hivyo wakitarajia uombezi wao kwa Mwenyezi Mungu na kuwakurubisha kwake, kama ilivyotajwa hapo awali kwenye aya mbali mbali. Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu hakuwapa udhuru kwa hilo. Bali aliwakanusha katika hilo kwenye Kitabu chake kitukufu, na akawaita makafiri na washirikina, na akawakadhibisha katika kudai kwao kwamba miungu hao wanawaombea na kuwakurubisha kwa Mwenyezi Mungu wawe karibu zaidi. Pia Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake hakuwapa udhuru. Bali aliwapiga vita juu ya ushirikina huu mpaka wamfanyie Mwenyezi Mungu peke yake ibada, na kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu aliyetakasika:

﴿وَقَاتِلُوهُمْ حَتَّى لَا تَكُونَ فِتْنَةٌ وَيَكُونَ الدِّينُ لِلَّهِ...﴾

"Na piganeni nao mpaka pasiwepo fitina, na Dini iwe ya Mwenyezi Mungu tu." [Al-Baqara: 193]. Na amesema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Nimeamrishwa nipigane vita na watu mpaka washuhudie kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kuwa Muhammadi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na wadumishe swala, na watoe zaka. Basi pindi watakapofanya hivyo, watakuwa wamezikinga kutokana nami damu zao na mali zao isipokuwa kwa haki ya Uislamu, na hesabu yao itakuwa juu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu." Maana ya kauli ya Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Mpaka washuhudie kuwa hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu"

Yaani: Mpaka wamkusudie Mwenyezi Mungu peke yake katika ibada, pasina kila kitu kisichokuwa Yeye.

Washirikina walikuwa wakiwaogopa majini na wana jikinga kwao. Basi Mwenyezi Mungu Mtukufu akateremsha maneno yake haya kuhusu hilo:

﴿وَأَنَّهُ كَانَ رِجَالٌ مِنَ الْإِنْسِ يَعُوذُونَ بِرِجَالٍ مِنَ الْجِنِّ فَزَادُوهُمْ رَهَقًا6﴾

"Na hakika walikuwako wanaume katika watu waliokuwa wakitafuta kujikinga kwa wanaume wa kijini; kwa hivyo wakawazidishia madhambi." [Al-Jin: 6]. Wafasiri walisema kuhusu Aya hii tukufu: Maana ya kauli yake:

﴿...فَزَادُوهُمْ رَهَقًا﴾

"Kwa hivyo wakawazidishia madhambi." Yaani: Uoga na hofu; kwa sababu majini hujiona wakubwa na wanatakabari wanapowaona watu wanakimbilia kwao, na hapo wanawaongezea hofu na uoga ili wawaabudu kwa wingi na kutafuta kimbilio kwao.

Na Mwenyezi Mungu aliwageuzia Waislamu badala ya hilo kutafuta kimbilio kwake Yeye aliyetakasika, na kwa maneno yake makamilifu, na akateremsha kuhusiana na hilo kauli yake Mtukufu:

﴿وَإِمَّا يَنْزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّهِ إِنَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ200﴾

 

 

"Na uchochezi wa Shetani ukikuchochea, basi omba ulinzi wa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Msikivu, Mjuzi." [Al-A'araf: 200]. Na kauli yake Mtukufu:

﴿قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ1﴾

"Sema: Ninajikinga kwa Mola Mlezi wa mapambazuko" Na imepokelewa kwa njia sahihi kwamba Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alisema: "Atakayeshuka mahala popote kisha akasema: 'A'udhu bikalimaati-llaahit-taammaati min sharri maa khalaqa: Tafsiri: Najilinda kwa maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyotimia, kutokana na uovu wa vile alivyo viumba, hakitomdhuru chochote mpaka atakapoondoka mahala pake hapo."

Kutokana na Aya na Hadithi zilizotangulia, mtafutaji wa uokovu, na mwenye kutaka kuihifadhi dini yake na kusalimika kutokana na ushirikina uliofichikana na ulio wazi atajua kwamba kujifungamanisha na wafu, Malaika, na majini na viumbe wengineo, na kuwaomba dua, na kujikinga kwao na mengineyo, ni miongoni mwa matendo ya washirikina wa enzi ya ujahilia (ujinga), na ni miongoni mwa aina mbaya kabisa za kumshirikisha Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa hivyo, la wajibu ni kuyaacha, kujihadhari nayo, na watu kuusiana kuyaacha na kumkemea yeyote anayeyafanya.

Na ama anayejulikana miongoni mwa watu kwa vitendo hivi vya kishirikina, basi hairuhusiwi kumuoa, wala kula kichinjwa chake, wala kumswalia, wala kuswali nyuma yake, mpaka atangaze toba kutokana na hayo kwa Mwenyezi Mungu aliyetakasika, na amkusudie Mwenyezi Mungu peke yake katika dua na ibada. Kwani dua ndiyo ibada, bali ndio kiini chake, kama alivyosema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Dua ndiyo ibada." Na imepokelewa kutoka kwake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika maneno mengine kwamba alisema: "Dua ndiyo kiini cha ibada." Ama kuwaowa washirikina, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَلَا تَنْكِحُوا الْمُشْرِكَاتِ حَتَّى يُؤْمِنَّ وَلَأَمَةٌ مُؤْمِنَةٌ خَيْرٌ مِنْ مُشْرِكَةٍ وَلَوْ أَعْجَبَتْكُمْ وَلَا تُنْكِحُوا الْمُشْرِكِينَ حَتَّى يُؤْمِنُوا وَلَعَبْدٌ مُؤْمِنٌ خَيْرٌ مِنْ مُشْرِكٍ وَلَوْ أَعْجَبَكُمْ أُولَئِكَ يَدْعُونَ إِلَى النَّارِ وَاللَّهُ يَدْعُو إِلَى الْجَنَّةِ وَالْمَغْفِرَةِ بِإِذْنِهِ وَيُبَيِّنُ آيَاتِهِ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ221﴾

"Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa mwanamume Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Hao wanaitia kwenye Moto, na Mwenyezi Mungu anaitia kwenye Pepo na maghufira (msamaha) kwa idhini yake. Naye huzibainisha Aya zake kwa watu ili wapate kukumbuka." [Al-Baqarah: 221]. Hapa, Mwenyezi Mungu Mtukufu amekataza Waislamu kuoa wanawake washirikina, wanoabudu masanamu, majini, Malaika na vinginevyo, mpaka waamini kwa kumkusudia Mwenyezi Mungu pekee katika ibada, na kumsadikisha Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, katika yale aliyokuja nayo na kufuata njia yake. Na pia akakataza kuwaozesha wanaume washirikina wanawake wa Kiislamu, mpaka waamini kwa kumkusudia Mwenyezi Mungu pekee katika ibada, na kumsadikisha Mtume, rehema na amani ziwe juu yake na kufuata njia yake.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu alieleza kuwa mjakazi Muumini ni bora kuliko mwanamke mshirikina aliye huru, hata kama atampendeza anayemtazama na kusikia maneno yake kwa urembo wake na uzuri wa maneno yake, na kwamba mtumwa Muumini ni bora kuliko mwanamume mshirikina aliye huru, hata kama atampendeza msikilizaji na mtazamaji wake kwa uzuri wake, ufasaha wake na ujasiri na mambo mengine. Kisha akaeleza sababu za ubora huu kwa kauli yake aliyetakasika:

﴿...أُولَئِكَ يَدْعُونَ إِلَى النَّارِ...﴾

"Hao wanaitia kwenye Moto." [Al-Baqara: 221]. Akimaanisha washirikina wanaume na wanawake. Kwa sababu wao ni walinganizi wa kwenda Motoni kwa kauli zao, vitendo vyao, mwenendo wao na maadili yao. Ama Waumini wanaume na Waumini wanawake, hao ni katika walinganizi wa kwenda Peponi kwa maadili yao, matendo yao na mwenendo wao. Basi vipi hawa na hao watakuwa sawa?

Na ama kuhusu kuwaswalia washirikina, Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu mkubwa amesema kuhusu wanafiki:

﴿وَلَا تُصَلِّ عَلَى أَحَدٍ مِنْهُمْ مَاتَ أَبَدًا وَلَا تَقُمْ عَلَى قَبْرِهِ إِنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ وَمَاتُوا وَهُمْ فَاسِقُونَ84﴾

"Wala usimsalie kabisa yeyote katika wao akifa, wala usisimame kaburini kwake. Hakika hao wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakafa na hali ni wapotofu." [At-Tauba: 84] Kwa hivyo Yeye Mtukufu akabainisha katika Aya hii tukufu kwamba mnafiki na kafiri hawafai kuswaliwa. Kwa sababu wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi vile vile haifai kuswali nyuma yao, wala wasifanywe viongozi wa Waislamu. Kwa sababu ya ukafiri wao na kukosa kwao uaminifu, na kwa sababu ya uadui mkubwa ulio baina yao na Waislamu, na kwa sababu wao si katika watu wa kuswali na kuabudu. Kwa sababu hakuna tendo linalosalia pamoja na ukafiri na ushirikina. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atusalimishe kutokana na hayo. Na ama kuhusu kula vichinjo vya washirikina, Mwenyezi Mungu Mtukufu Mwenye utukufu mkubwa alisema, akieleza kuharamishwa kwa wanyama waliokufa wenyewe na vichinjo vya washirikina:

﴿وَلَا تَأْكُلُوا مِمَّا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللَّهِ عَلَيْهِ وَإِنَّهُ لَفِسْقٌ وَإِنَّ الشَّيَاطِينَ لَيُوحُونَ إِلَى أَوْلِيَائِهِمْ لِيُجَادِلُوكُمْ وَإِنْ أَطَعْتُمُوهُمْ إِنَّكُمْ لَمُشْرِكُونَ121﴾

"Wala msile katika wale ambao hawakusomewa jina la Mwenyezi Mungu. Kwani huo ni upotofu. Na kwa yakini mashetani wanawafunza marafiki zao kubishana nanyi. Na mkiwafuata, basi hapana shaka nyinyi mtakuwa washirikina." [Al-An'am: 121]. Basi Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwakataza Waislamu kula wanyama waliokufa bila ya kuchinjwa kisheria na vichinjo vya washirikina. Kwa sababu hivyo ni najisi, kwani vichinjo vyao vina hukumu ya wanyama waliokufa bila ya kuchinjwa kisheria hata kama jina la Mwenyezi Mungu litatajwa juu yake. Kwa sababu kuwatajia jina la Mwenyezi Mungu ni batili na halina athari yoyote juu yake. Kwa sababu hii ni ibada, na ushirikina unavunjilia mbali na kubatilisha ibada, mpaka mshirikina atubie kwa Mwenyezi Mungu aliyetakasika. Mwenyezi Mungu Mtukufu ameruhusu tu chakula cha Watu wa Kitabu katika kauli yake:

﴿...وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حِلٌّ لَكُمْ وَطَعَامُكُمْ حِلٌّ لَهُمْ...﴾

"Na chakula cha wale waliopewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao." [Al-Maidah: 5] Kwa sababu wanajinasibisha na dini ya mbinguni, na wanadai kuwa wao ni wafuasi wa Musa na Isa, ijapokuwa wanasema uongo katika hilo. Mwenyezi Mungu aliifuta dini yao na kuibatilisha kwa kumtuma Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake kwa watu wote, lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu, alituhalalishia chakula na wanawake wa Watu wa Kitabu kwa sababu ya hekima ya kina, na siri zilizozingatiwa, ambazo wanazuoni wamezieleza, tofauti na washirikina wanaoabudu masanamu na wafu miongoni mwa manabii na mawalii na wengineo. Kwa sababu dini yao haina msingi, wala hata shaka juu yake. Bali ni ya batili tokea msingi wake. Ndiyo maana vichinjwa vya watu wake ni nyamafu na hairuhusiwi kuvila.

Ama mtu kumwambia mwingine: "Jini amekusibu" “Jini amekuchukua”, “Shetani amepeperuka nawe” na mfano wake, hayo ni aina ya matusi na hayaruhusiwi kati ya Waislamu, kama aina nyingine zote za matusi. Hayo hayazingatiwi kuwa ni ushirikina, isipokuwa ikiwa mwenye kusema hivi anaamini kwamba majini wana watawala watu bila ya idhini ya Mwenyezi Mungu na mapenzi yake, kwa hivyo, mwenye kuamini haya kuhusu majini au viumbe wengineo, anakuwa kafiri kwa sababu ya imani hii. Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliyetakasika ndiye Mwenye kumiliki kila kitu, na Muweza wa kila kitu, na Yeye ndiye mwenye kunufaisha na kudhuru, na hakuna kitu kinachoweza kupatikana isipokuwa kwa idhini yake, na kwa kutaka kwake, na mipango yake iliyotangulia, kama alivyosema Mtukufu akimuamrisha Mtume wake, rehema na amani ziwe juu yake kwamba awaambie watu juu ya msingi huu mkuu:

﴿قُلْ لَا أَمْلِكُ لِنَفْسِي نَفْعًا وَلَا ضَرًّا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّهُ وَلَوْ كُنْتُ أَعْلَمُ الْغَيْبَ لَاسْتَكْثَرْتُ مِنَ الْخَيْرِ وَمَا مَسَّنِيَ السُّوءُ إِنْ أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ188﴾

"Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara, ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa ninayajua ya ghaibu, ningejizidishia mema mengi, wala ovu lisingenigusa. Mimi si chochote ila ni muonyaji na mbashiri kwa watu wanaoamini." [Al-A'araf: 188] Kwa hivyo, ikiwa bwana wa viumbe na mbora wao -rehema na amani ziwe juu yake- hajimilikii manufaa wala madhara isipokuwa apendavyo Mwenyezi Mungu, basi itakuwa vipi kuhusu viumbe vingineo? Na kuna aya nyingi katika maana hii.

Ama kuwauliza wapiga ramli, na wachawi, na wanajimu, na mfano wao miongoni mwa wale wanao shughulika na habari za ghaibu, huu ni uovu na wala hauruhusiwi, na tena kuwasadikisha ni kubaya zaidi na ni uovu mno. Bali ni katika matawi ya ukafiri; kama alivyosema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Atakayemuendea mpiga ramli na akamuuliza kuhusu lolote, basi hatakubaliwa swala yoyote siku arobaini." Imepokelewa na Imamu Muslim katika Sahihi yake. Na katika Sahihi yake – pia – kutoka kwa Muawia bin Al-Hakam As-Sulami, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi kwamba: "Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alikataza kumwendea mpiga ramli na kumuuliza kitu."

Watu wa vitabu vya Sunna wamepokea kutoka kwa Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake kwamba alisema: "Atakayemuendea kuhani na akamsadikisha kwa yale anayoyasema, basi hakika atakuwa amekufuru yale yaliyoteremshwa kwa Muhammad rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake." Na kuna hadithi nyingi zenye maana hii. Kwa hivyo ni wajibu kwa Waislamu kutahadhari kuwauliza makuhani na wapiga ramli, na wachawi na wengineo wote ambao wanashughulika na kusimulia mambo ya ghaibu na ya kuwahadaa na kuwachanganya Waislamu, sawa iwe kwa jina la utabibu au mengineyo, kwa sababu ya yale yaliyotangulia kutajwa kuhusu katazo la Mtume rehema na amani ziwe juu yake juu ya hayo na onyo lake dhidi yake. Na yanaingia katika hayo yale wanayodai baadhi ya watu kwa jina la utabibu miongoni mwa mambo ya ghaibu anaponusa harufu ya kilemba cha mgonjwa, au kitambaa cha mgonjwa, au kitu kama hicho, anasema: 'Mgonjwa huyu wa kiume au wa kike alifanya hivi na vile', akitaja mambo ya ghaibu ambayo hakuna ushahidi wake katika kilemba cha mgonjwa huyo. Bali makusudio ya hayo ni kuwahadaa na kuuchanganya umma, ili waseme kuwa yeye ni mjuzi wa matibabu na aina za maradhi na sababu zake, na pengine akawapa baadhi ya madawa, na huenda kwa bahati wakaponywa kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, basi wakadhani kuwa ni kwa sababu ya dawa zake hizo. Na huenda maradhi hayo yakawa yamesababishwa na baadhi ya majini na mashetani wanaomtumikia mdai huyo katika utabibu wake na wanamwambia baadhi ya mambo ya ghaibu wanayoyajua, basi yeye akategemea hayo na akawaridhisha majini hao na mashetani kwa yale yanayowafaa katika ibada, hivyo basi wakamuondoka mgonjwa huyo na kuachana na madhara waliyomfanyia, na hili ni jambo linalojulikana kuhusu majini na mashetani na wale wanaowatumia.

Hivyo basi, la wajibu pia kwa Waislamu ni kujihadhari na jambo hili, na kuusiana kuachana nalo, na kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu katika mambo yote. Na hakuna ubaya kutumia ruqya ya kisheria na dawa zinazozuhusika na kutafuta tiba kwa madaktari ambao humchunguza mgonjwa na kuthibitisha maradhi yake kwa kutumia njia zinazoonekana na za kihisia za kueleweka. Imepokelewa kwa usahihi kwamba Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alisema: "Mwenyezi Mungu hakuteremsha ugonjwa isipokuwa aliuteremshia tiba yake. Aliijua aliyeijua na akakosa kuijia yule aliyekosa kuijua." Na alisema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Kila ugonjwa una dawa. Kwa hivyo, ikiwa ugonjwa utapatwa na dawa, basi utapona kwa idhini ya Mwenyezi Mungu." Na alisema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Enyi waja wa Mwenyezi Mungu, tafuteni matibabu, lakini msitafute matibabu kwa yale yaliyoharamishwa." Na kuna hadithi nyingi zenye maana hii.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aziboreshe hali za Waislamu wote, aziponye nyoyo na miili yao kutokana na maovu yote, awaunganishe juu ya uongofu, na atuepushe sisi na wao kutokana na majaribu ya kupotosha na kumtii Shetani na wafuasi wake. Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu, na hakuna uwezo wala nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu aliye juu, Mtukufu.

Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Nabii wetu Muhammad, na familia yake na Maswahaba wake.

 

***

 


بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Makala ya Nne:

Kuhusu hukumu ya kuabudu kwa kutumia nyiradi za kiuzushi na za kishirikina

Kutoka kwa Abdul-Aziz bin Abdullah bin Baaz kwenda kwa ndugu yetu mtukufu (.....), Mwenyezi Mungu amuwezeshe kufikia kila la heri, Amin.

Assalaam alaikum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Sasa basi: Imenifikia barua yako tukufu, Mwenyezi Mungu akuongoze, na habari zilizomo ndani yake kwamba wako watu katika nchi yako wanaoshikamana na nyiradi ambazo Mwenyezi Mungu hakuziteremshia uthibitisho wowote, baadhi yake ni za kizushi na baadhi yake ni za kishirikina, na wananasibisha hilo kwa amiri wa waumini Ali bin Abi Twalib, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, na wengineo. Dua hizo wanazisoma katika mikusanyiko ya dhikiri, au misikitini baada ya swala ya Magharibi, wakidai kuwa ni kitendo cha kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, kama vile kusema: Kwa haki ya Mwenyezi Mungu, enyi watu wa Mwenyezi Mungu, tusaidieni kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, na kuweni wasaidizi wetu kupitia kwa Mwenyezi Mungu. Na kama wasemavyo: Enyi miti mitukufu, enyi mabwana, itikieni enyi mlio na usaidizi miongoni mwetu, na muombeeni kwa Mwenyezi Mungu, huyu ni mja wenu amesimama, na amejitolea kukaa mlangoni kwenu, na anaogopa mapungufu yake, tusaidie ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, na mimi sina wa kwenda kwake asiyekuwa nyinyi, na kutoka kwenu maombi yanapatikana, na nyinyi ni watu wa Mwenyezi Mungu, kupitia kwa Hamza, bwana wa mashahidi, na ni nani asiyekuwa nyinyi anayeweza kutunusuru sisi, tusaidie ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na kama wanavyosema: Ewe Mwenyezi Mungu mpe rehema yule uliyemfanya kuwa sababu ya kugawanyika kwa siri zako kuu na kufichuka kwa nuru zako za rehema, hivyo akawa mwakilishi wa uwepo wa Mola Mlezi, na mrithi wa siri zako za dhati.

Na kutaka kwenu kubainishiwa ni yapi ya uzushi na yapi ni ya ushirikina, na je ni sahihi kuswalia nyuma ya imamu anayeomba dua hii, ikiwa hayo yote yanajulikana?

Jibu: Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu peke yake, na rehema na amani zimshukie yule ambaye hakuna Nabii baada yake, na juu ya jamaa zake na Maswahaba wake, na wanaofuata uongofu wake mpaka Siku ya Kiyama.

Ama baada ya hayo: Basi jua -Mwenyezi Mungu akuongoze- kwamba Mwenyezi Mungu aliyetakasika aliumba viumbe na akatuma Mitume -rehema na amani ziwe juu yao- ili Yeye peke yake aabudiwe, bila ya mshirika mbali na chochote kisichokuwa Yeye, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنْسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ56﴾

"Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi." [Dhariyat: 56].

Na ibada kama ilivyotangulia kubainishwa ni kumtii Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kumtii Mtume wake Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwa kufanya yale aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na kuyaacha aliyoyakataza Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kwa sababu ya kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na kumtakasia Mwenyezi Mungu vitendo, pamoja na kumpenda sana Mwenyezi Mungu, na kujidhalilisha kikamilifu kwake peke yake. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَقَضَى رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ...﴾

"Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu." [Al-Israa: 23]. Yaani aliamrisha na kuusia kwamba aabudiwe Yeye peke yake tu. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ2 الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ3 مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ4 إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ5﴾

"Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.

Mwingi wa rehema, Mwingi wa kurehemu.

Mwenye kumiliki Siku ya Malipo."

5. Ni Wewe tu tunayekuabudu na ni Wewe tu tunayekuomba msaada." [Al-Fatiha 2-5] Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka akaweka wazi katika aya hizi kwamba Yeye pekee ndiye anayestahiki kuabudiwa na kuombwa msaada. Na akasema Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu mkubwa:

﴿إِنَّآ أَنزَلۡنَآ إِلَيۡكَ ٱلۡكِتَٰبَ بِٱلۡحَقِّ فَٱعۡبُدِ ٱللَّهَ مُخۡلِصٗا لَّهُ ٱلدِّينَ2 أَلَا لِلَّهِ ٱلدِّينُ ٱلۡخَالِصُۚ...﴾

"Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa Haki. Basi muabudu Mwenyezi Mungu ukimsafia Dini Yeye tu. Hakika Dini Safi ni ya Mwenyezi Mungu tu."

Hakika Dini Safi ni ya Mwenyezi Mungu tu... [Az-Zumar: 2-3]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿فَادْعُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ14﴾

"Basi muombeni Mwenyezi Mungu mkimsafia Dini Yeye tu, hata kama watachukia makafiri." [Surat Ghafir: 14] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّهِ أَحَدًا18﴾

"Na kwamba kwa hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu. Basi msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu." [Surat Al-Jinn: 18]

 

Kuna aya nyingi katika maana hii, na zote zinaonyesha ulazima wa kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika ibada.

Inajulikana kuwa dua kwa aina zake zote ni ibada, na hairuhusiwi kwa mtu yeyote kumuomba yeyote isipokuwa Mola wake Mlezi, wala kuomba msaada na kuokolewa kwa yeyote isipokuwa kutoka kwake, kwa kufanyia kazi Aya hizi tukufu na yale yaliyokuja na maana hii hii. Haya ni kuhusiana na mambo ya kawaida na sababu za kihisia ambazo kiumbe kilicho hai, kilichopo sasa kinayaweza, kwa kuwa hizo si katika ibada. Bali inajuzu kwa maandiko na makubaliano ya wanazuoni kwamba mtu anaweza kutafuta msaada kutoka kwa mtu aliye hai, mwenye uwezo, katika mambo ya kawaida ambayo ana uwezo nayo. Kama vile kutafuta msaada wake ili kuepusha maovu ya mwanawe, au mtumishi, au mbwa, au mfano wa hayo. Na pia kama vile mtu kutafuta msaada kutoka kwa mtu aliye hai, aliyepo, mwenye uwezo, au mtu asiyekuwepo, kupitia njia za kihisia kama vile kuandikiana na mfano wake, katika kujenga nyumba yake, au kutengeneza gari lake au mambo kama hayo. Na katika hayo ni mtu kutafuta kuokolewa kutoka kwa ndugu zake katika jihadi, vita na mfano wa hayo. Na pia katika mlango huu, ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kisa cha Musa, rehema na amani ziwe juu yake:

﴿...فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِنْ شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ...﴾

"Basi yule mwenzake akamtaka msaada kumpiga adui yake." [Al-Qasas: 15].

Ama kutafuta kuokolewa na wafu, majini, Malaika, miti na mawe, haya ni katika ushirikina mkubwa, na ni aina moja na matendo waliyokuwa washirikina wa mwanzo wakiwafanyia miungu wao, kama vile al-Uzza, al-Lata na wengineo. Na vile vile kutafuta kuokolewa na kusaidiwa na wale anaoamini kwamba wana ulinzi kati ya walio hai, katika mambo ambayo Mwenyezi Mungu pekee ndiye mwenye uwezo juu yake kama vile kuponya wagonjwa, kuongoa nyoyo, kuingia Peponi, kuokoka na Moto na mfano wa hayo.

Aya zilizotangulia na Aya na Hadithi zilizokuja na maana zinazofanana nazo, zote zinaashiria ulazima wa kuelekeza nyoyo kwa Mwenyezi Mungu katika mambo yote, na kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake. Kwa sababu waja wameumbwa kwa ajili ya hili, na waliamrishwa kufanya hivyo, kama ilivyotajwa hapo awali katika Aya mbalimbali, na kama vile katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَاعْبُدُوا اللَّهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا...﴾

"Na muabuduni Mwenyezi Mungu na msimshirikishe na chochote." [An-Nisaai: 36] Na kauli yake Mtukufu:

 

﴿وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ...﴾

"Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini." [Surat Al-Bayyina: 5] Na maneno ya Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake katika hadithi ya Muadhi Mwenyezi Mungu amuwiye radhi: “Haki ya Mwenyezi Mungu juu ya waja wake ni kwamba wamuabudu wala wasimshirikishe na chochote.” Wanachuoni wamekubaliana kwamba hadithi hii ni sahihi. Na kauli yake Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika hadithi ya bin Masudi, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi: "Yeyote atakayekufa huku anamuomba mwenza pamoja na Mwenyezi Mungu, ataingia Motoni." Imepokelewa na Bukhari. Katika Sahihi mbili, kutoka kwa bin Abbas, Mwenyezi Mungu awawie radhi wote wawili, ya kwamba Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alipomtuma Muadhi kwenda Yemen, alimwambia: “Hakika wewe unawajia watu wa Kitabu, basi na liwe la kwanza utakalowalingania ni kushuhudia kwamba hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu." Na katika tamko lingine: “Waite katika kushuhudia kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, na kwamba hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu." Na katika mapokezi ya Bukhari: "Basi na liwe jambo la kwanza unalowalingania ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu." Na katika Sahihi Muslim, kutoka kwa Tariq bin Ushaim Al-Ashja’i, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, ya kwamba Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: "Atakayesema: Laa ilaaha illa llaah, na akakufuru vyote vinavyoabudiwa kinyume na Mwenyezi Mungu, itakuwa haramu mali yake na damu yake, na hesabu yake itakuwa juu ya Mwenyezi Mungu, Mwenye utukufu mkubwa." Na kuna hadithi nyingi zenye maana hii.

Tauhidi hii ndiyo chimbuko la Dini ya Uislamu, nayo ndiyo msingi wa mila hii, na ndiyo kichwa cha jambo hili, na ndiyo wajibu muhimu zaidi, nayo ndiyo hekima katika kuumbwa kwa vizito viwili (wanadamu na majini), na ndiyo hekima ya kuwatuma Mitume wote, rehema na amani ziwe juu yao, kama ilivyotangulia katika aya zilizoonyesha hayo. Miongoni mwake ni maneno ya Mola Mtukufu:

﴿وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنْسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ56﴾

"Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi." [Surat Adh-Dhariyaat: 56]. Na miongoni mwa ushahidi wa hayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَسُولًا أَنِ ااعْبُدُوا اللَّهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ...﴾

"Na kwa hakika, kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni Twaghuut (Shetani na vyote vinavyoabudiwa kando na Mwenyezi Mungu." [Surat An-Nahl: 36]. Na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمَا أَرْسَلْنَا مِنْ قَبْلِكَ مِنْ رَسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ25﴾

"Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipokuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu." [Al-Anbiya: 25]. Na Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu mkubwa amesema kuhusu Nuhu, Hud, Saleh na Shuaib -rehema na amani ziwe juu yao- kwamba waliwaambia watu wao:

﴿...اعْبُدُوا اللَّهَ مَا لَكُمْ مِنْ إِلَهٍ غَيْرُهُ...﴾

"Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye." [Al-A'araf: 59]. Na huu ndio wito wa Mitume wote, kama ilivyoashiriwa na zile Aya mbili zilizotangulia. Na maadui wa Mitume walikiri kwamba Mitume waliwaamrisha kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake na kuwakataa waungu wanaoabudiwa badala yake, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu mkubwa katika kisa cha 'Adi, kwamba walimwambia Hudi, rehema na amani ziwe juu yake:

﴿...أَجِئْتَنَا لِنَعْبُدَ اللَّهَ وَحْدَهُ وَنَذَرَ مَا كَانَ يَعْبُدُ آبَاؤُنَا...﴾

"Je, umetujia ili tumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na tuyaache waliyo kuwa wakiyaabudu baba zetu?" [Al-A'araf: 70], Na alisema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu Makuraishi pale Mtume wetu Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alipowalingania kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake na kuyaacha waliyokuwa wakiyaabudu badala yake miongoni mwa Malaika, watakatifu, masanamu, miti na vinginevyo:

﴿أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَهًا وَاحِدًا إِنَّ هَذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ5﴾

"Amewafanya miungu wote kuwa ni Mungu Mmoja tu? Hakika hili ni jambo la ajabu sana." [Swad: 5] Na amesema Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka kuhusu wao:

﴿إِنَّهُمْ كَانُوا إِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ يَسْتَكْبِرُونَ35 وَيَقُولُونَ أَئِنَّا لَتَارِكُوٓاْ ءَالِهَتِنَا لِشَاعِرٖ مَّجۡنُونِۭ36﴾

"Hakika wao walikuwa wanapoambiwa: 'Laa ilaaha illallahu (Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu tu)', wanajivuna."

Na wanasema: Hivyo sisi tuiache miungu yetu kwa ajili ya huyu mtunga mashairi mwendawazimu?" [As-Saffat: 35, 36]. Na kuna aya nyingi zinazoonyesha maana hii.

Kutokana na Aya na hadithi tulizozitaja, inakubainikia -Mwenyezi Mungu aniwezeshe mimi na wewe kuifahamu dini na kutambua sawasawa haki ya Mola Mlezi wa walimwengu wote - kwamba dua hizi na aina mbalimbali za kutafuta kuokolewa ulizozitaja katika swali lako, zote ni katika aina za ushirikina mkubwa. Kwa sababu ni kuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na kuomba mambo asiyoweza kuyafanya asiyekuwa Yeye, kutoka kwa wafu na wasiokuwepo, na hilo linachukiza zaidi kuliko ushirikina wa watu wa mwanzo; Kwa sababu wale wa mwanzo walikuwa wakishirikisha tu wakati wa raha na mafanikio. Ama katika nyakati za magumu, walikuwa wakimsafia Mwenyezi Mungu ibada. Kwa sababu walijua kwamba Yeye Mtukufu ndiye Muweza wa kuwaepusha mbali na dhiki, na si mwingine, kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika kitabu chake kilicho wazi kuhusu washirikina hao.

﴿فَإِذَا رَكِبُواْ فِي ٱلۡفُلۡكِ دَعَوُاْ ٱللَّهَ مُخۡلِصِينَ لَهُ ٱلدِّينَ فَلَمَّا نَجَّىٰهُمۡ إِلَى ٱلۡبَرِّ إِذَا هُمۡ يُشۡرِكُونَ65﴾

"Na wanapopanda katika merikebu, humuomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafia utiifu. Lakini anapo wavusha wakafika nchi kavu, mara wanamshirikisha." [Al-Ankabut: 65] Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema akiwaongelesha katika Aya nyingine:

﴿وَإِذَا مَسَّكُمُ ٱلضُّرُّ فِي ٱلۡبَحۡرِ ضَلَّ مَن تَدۡعُونَ إِلَّآ إِيَّاهُۖ فَلَمَّا نَجَّىٰكُمۡ إِلَى ٱلۡبَرِّ أَعۡرَضۡتُمۡۚ وَكَانَ ٱلۡإِنسَٰنُ كَفُورًا67﴾

"Na inapokufikieni tabu katika bahari, hao mnao waomba wanapotea, isipokuwa Yeye tu. Na anapo kuvusheni mkafika nchi kavu, mnageuka. Ama (kweli) mwanadamu ni mwingi wa kukufuru." [Al-Israa: 67].

Iwapo mwenye kusema katika washirikina hawa wa nyuma atasema: 'Hakika sisi hatumaanishi kwamba hao wanaweza kufaidi wenyewe, au wanaponya wagonjwa wetu wenyewe, au wanaweza kutunufaisha wenyewe au kutudhuru wenyewe. Bali tunamaanisha (na kutafuta) uombezi wao kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika hayo?'

Jibu ni aambiwe: Hakika hili ndilo lengo na makusudio ya makafiri wa mwanzo, na hawakumaanisha ya kwamba miungu yao inaumba au kutoa riziki, au inanufaisha au inadhuru yenyewe. Kwa sababu, hayo yanabatilika kwa yale aliyoyataja Mwenyezi Mungu kuwahusu ndani ya Qur'ani, na kwamba walikusudia uombezi wao na heshima yao, na kuwakurubisha kwa Mwenyezi Mungu wawe karibu zaidi, kama alivyosema Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka:

﴿وَيَعۡبُدُونَ مِن دُونِ ٱللَّهِ مَا لَا يَضُرُّهُمۡ وَلَا يَنفَعُهُمۡ وَيَقُولُونَ هَٰٓؤُلَآءِ شُفَعَٰٓؤُنَا عِندَ ٱللَّهِ...﴾

"Nao, badala ya Mwenyezi Mungu, wanaabudu wasiowadhuru wala kuwanufaisha, na wanasema: 'Hawa ndio waombezi wetu kwa Mwenyezi Mungu!" [Yunus: 18] Mwenyezi Mungu akawapinga katika hilo kwa kauli yake:

 

﴿...قُلۡ أَتُنَبِّـُٔونَ ٱللَّهَ بِمَا لَا يَعۡلَمُ فِي ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَلَا فِي ٱلۡأَرۡضِۚ سُبۡحَٰنَهُۥ وَتَعَٰلَىٰ عَمَّا يُشۡرِكُونَ﴾

"Sema: Je, mnamwambia Mwenyezi Mungu asiyoyajua yaliyoko katika mbingu wala katika ardhi? Sub-hanahu wa Taa'la (ametakasika na ametukuka) mbali na hao wanaomshirikisha naye." [Yunus: 18] Basi, Yeye aliyetakasika akabainisha kuwa hamjui muombezi yeyote mbele yake mbinguni au ardhini kwa namna iliyokusudiwa na washirikina. Na kile ambacho Mwenyezi Mungu hajui uwepo wake, basi hicho hakipo. Kwa sababu Yeye aliyetakasika hakuna kinachofichikana kwake. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿تَنزِيلُ ٱلۡكِتَٰبِ مِنَ ٱللَّهِ ٱلۡعَزِيزِ ٱلۡحَكِيمِ 1 إِنَّآ أَنزَلۡنَآ إِلَيۡكَ ٱلۡكِتَٰبَ بِٱلۡحَقِّ فَٱعۡبُدِ ٱللَّهَ مُخۡلِصٗا لَّهُ ٱلدِّينَ2 أَلَا لِلَّهِ ٱلدِّينُ ٱلۡخَالِصُۚ وَٱلَّذِينَ ٱتَّخَذُواْ مِن دُونِهِۦٓ أَوۡلِيَآءَ مَا نَعۡبُدُهُمۡ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَآ إِلَى ٱللَّهِ زُلۡفَىٰٓ إِنَّ ٱللَّهَ يَحۡكُمُ بَيۡنَهُمۡ فِي مَا هُمۡ فِيهِ يَخۡتَلِفُونَۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَهۡدِي مَنۡ هُوَ كَٰذِبٞ كَفَّارٞ3﴾

"Uteremsho wa Kitabu hiki umetokana na Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa Haki. Basi muabudu Mwenyezi Mungu ukimsafia Dini Yeye tu.

Sikilizeni. Hakika Dini Safi ni ya Mwenyezi Mungu tu. Na wale wanaowafanya wenginewe kuwa ni walinzi wakisema: 'Sisi hatuwaabudu ila wapate kutujongeza tu kumkaribia Mwenyezi Mungu', hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao katika yale wanayohitilafiana. Hakika Mwenyezi Mungu hamuongoi aliye muongo kafiri." [Az-Zumar: 1-3]

Maana ya dini hapa ni ibada. Nayo ni kumtii Mwenyezi Mungu na kumtii Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kama ilivyotangulia kutajwa. Na inaingia ndani yake dua, kuomba kuokolewa, hofu, matumaini, kuchinja na nadhiri. Pia inaingia ndani yake swala, saumu na mengineyo aliyoamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kwa hivyo, Yeye aliyetakasika akabainisha kwamba ibada ni yake peke yake, na kwamba ni wajibu kwa waja kumkusudia Yeye Mwenye utukufu mkubwa pekee ndani yake. Kwa sababu kumuamrisha kwake Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kumkusudia Yeye tu katika ibada pia ni kuwaamrisha wana wote wa umma huu.

Kisha Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu mkubwa akaeleza baada ya hayo kuhusu makafiri. Akasema:

﴿وَٱلَّذِينَ ٱتَّخَذُواْ مِن دُونِهِۦٓ أَوۡلِيَآءَ مَا نَعۡبُدُهُمۡ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَآ إِلَى ٱللَّهِ زُلۡفَىٰٓ﴾

"Na wale wanaowafanya wenginewe kuwa ni walinzi wakisema: Sisi hatuwaabudu ila wapate kutujongeza tu kumkaribia Mwenyezi Mungu." [Az-Zumar: 3]. Mwenyezi Mungu aliyetakasika akawajibu kwa kusema:

﴿...إِنَّ ٱللَّهَ يَحۡكُمُ بَيۡنَهُمۡ فِي مَا هُمۡ فِيهِ يَخۡتَلِفُونَۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَهۡدِي مَنۡ هُوَ كَٰذِبٞ كَفَّارٞ﴾

"Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao katika yale wanayohitilafiana. Hakika Mwenyezi Mungu hamuongoi aliye muongo kafiri." [Az-Zumar: 3]. Basi Yeye Mtukufu, akabainisha katika Aya hii tukufu ya kwamba makafiri hawakuwaabudu mawalii badala yake isipokuwa ili kuwakurubisha kwa Mwenyezi Mungu, wawe karibu zaidi. Na haya ndiyo makusudio ya makafiri wa zamani na wa sasa, na Mwenyezi Mungu alilibatilisha hilo kwa kusema:

﴿...إِنَّ ٱللَّهَ يَحۡكُمُ بَيۡنَهُمۡ فِي مَا هُمۡ فِيهِ يَخۡتَلِفُونَۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَهۡدِي مَنۡ هُوَ كَٰذِبٞ كَفَّارٞ﴾

"Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao katika yale wanayohitilafiana. Hakika Mwenyezi Mungu hamuongoi aliye muongo kafiri." [Az-Zumar: 3]. Basi Mwenyezi Mungu aliyetakasika akauweka wazi uongo wao katika madai yao ya kwamba miungu yao inawakurubisha kwa Mwenyezi Mungu, wakawa karibu zaidi, na kufuru yao kwa sababu ya ibada walizofanya kwa ajili yao. Basi kwa hilo, kila mwenye utambuzi hata mdogo tu atajua kwamba makafiri wa mwanzo ulikuwa ukafiri wao ni kuwachukua Mitume, mawalii, miti, mawe na viumbe vingine kuwa waombezi baina yao na Mwenyezi Mungu. Waliitakidi kwamba wanaweza kutimiza haja zao bila idhini Yake Mtukufu na kuridhia kwake, sawa na vile mawaziri wanavyofanya uombezi mbele ya wafalme. Hapo wakawa wamempima Yeye Mtukufu na wafalme na viongozi. Wakasema: Kama vile mtu ambaye ana haja kwa mfalme au kiongozi anafanyiwa uombezi kwake kupitia wasiri wake na mawaziri wake, basi ndivyo tunavyojikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwaabudu Manabii wake na mawalii wake. Hili ni katika batili kubwa zaidi. Kwa sababu Yeye Mtukufu, hana wa kufanana naye na wala halinganishwi na viumbe vyake, na hakuna awezaye kufanya uombezi kwake isipokuwa kwa idhini yake, na Yeye hawapi idhini isipokuwa watu wa Tauhidi tu. Yeye aliyetakasika na kutukuka ni Muweza wa kila kitu, na ni Mjuzi wa kila kitu, na Yeye ni Mwingi wa kurehemu kuliko wote wanaorehemu, wala hamuogopi yeyote, wala hamhofu. Kwa sababu Yeye Mtukufu, ni Mshindi juu ya waja wake, na huwaendesha apendavyo. Mwenyezi Mungu ni tofauti na wafalme na viongozi. Wao hawana uwezo wa kufanya kila kitu, ndiyo maana wanahitaji mtu wa kuwasaidia katika yale ambayo hawawezi kuyafanya, kama mawaziri wao, na wasiri wao na askari wao, kama vile wanavyo hitaji kujulishwa mahitaji ya wale ambao hawayajui mahitaji yao, kwa hivyo wanahitaji mtu miongoni mwa mawaziri wao na wasiri wao wa kuwafanyia huruma na kuwaridhisha. Ama Mola Mlezi Mwenye utukufu mkubwa, Yeye aliyetakasika ni Mkwasi asiyewahitaji viumbe wake wote, na ni mwenye huruma kwao sana kuliko mama zao, ndiye hakimu muadilifu, anayeweka vitu mahali pake kulingana na hekima yake, elimu yake na uwezo wake. Kwa hivyo hairuhusiwi kumlinganisha na viumbe wake kwa njia yoyote ile. Ndiyo maana, Yeye aliyetakasika akabainisha katika Kitabu chake kwamba washirikina walikiri kwamba Yeye ndiye Muumba, Mwenye kuruzuku na Mwendeshaji mambo, na kwamba Yeye ndiye Mwenye kujibu wenye dhiki kubwa, anayeondoa maovu, anayehuisha na anayefisha na mengineyo miongoni mwa vitendo vyake Yeye aliyetakasika. Mzozo baina ya washirikina na Mitume ulikuwa juu ya kumkusudia Mwenyezi Mungu peke yake katika ibada, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu mkubwa:

﴿َوَلَئِن سَأَلۡتَهُم مَّنۡ خَلَقَهُمۡ لَيَقُولُنَّ ٱللَّهُ...﴾

"Na ukiwauliza ni nani aliyewaumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu!" [Az-Zukhruf: 87] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿قُلۡ مَن يَرۡزُقُكُم مِّنَ ٱلسَّمَآءِ وَٱلۡأَرۡضِ أَمَّن يَمۡلِكُ ٱلسَّمۡعَ وَٱلۡأَبۡصَٰرَ وَمَن يُخۡرِجُ ٱلۡحَيَّ مِنَ ٱلۡمَيِّتِ وَيُخۡرِجُ ٱلۡمَيِّتَ مِنَ ٱلۡحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ ٱلۡأَمۡرَۚ فَسَيَقُولُونَ ٱللَّهُۚ فَقُلۡ أَفَلَا تَتَّقُونَ31﴾

"Sema: Ni nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Au ni nani anayemiliki kusikia na kuona? Na ni nani amtoaye hai kutoka kwenye maiti, na akamtoa maiti kutoka kwa aliye hai? Na ni nani anayeyaendesha mambo yote? Watasema: Allah (Mwenyezi Mungu). Basi sema: Je, hamumchi?" [Yunus: 31] Na aya zenye maana hii ni nyingi sana.

Zilishatangulia kutajwa Aya zinazoonyesha kwamba mzozo uliokuwa baina ya Mitume na umma wao ni juu ya kumkusudia Mwenyezi Mungu pekee katika ibada, kama vile kauli yake Mtukufu:

﴿وَلَقَدۡ بَعَثۡنَا فِي كُلِّ أُمَّةٖ رَّسُولًا أَنِ ٱعۡبُدُواْ ٱللَّهَ وَٱجۡتَنِبُواْ ٱلطَّٰغُوتَ...﴾

"Na kwa hakika, kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni Twaghuut (Shetani na vyote vinavyoabudiwa kinyume na Mwenyezi Mungu." [Surat An-Nahl: 36]. Na kuna aya nyingi sana zilizokuja katika maana hii. Na Yeye aliyetakasika ameeleza katika sehemu nyingi katika Kitabu chake kitukufu suala la uombezi. Akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿َ...مَن ذَا ٱلَّذِي يَشۡفَعُ عِندَهُۥٓ إِلَّا بِإِذۡنِهِ...﴾

"Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake isipokuwa kwa idhini yake?" [Al-Baqara: 255]. Na akasema Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mtukufu:

﴿وَكَم مِّن مَّلَكٖ فِي ٱلسَّمَٰوَٰتِ لَا تُغۡنِي شَفَٰعَتُهُمۡ شَيۡـًٔا إِلَّا مِنۢ بَعۡدِ أَن يَأۡذَنَ ٱللَّهُ لِمَن يَشَآءُ وَيَرۡضَىٰٓ26﴾

"Na wako Malaika wangapi mbinguni, ambao uombezi wao hautafaa chochote isipokuwa baada ya Mwenyezi Mungu kutoa idhini kwa amtakaye na kumridhia." [An-Najm: 26].

Na akasema katika kuwaelezea Malaika:

﴿...وَلَا يَشۡفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ٱرۡتَضَىٰ وَهُم مِّنۡ خَشۡيَتِهِۦ مُشۡفِقُونَ﴾

"Wala hawamuombei yeyote ila yule anayemridhia Yeye, nao kwa sababu ya kumuogopa wananyenyekea." [Al-Anbiya: 28].

Na akajulisha kuwa haridhii ukafiri kutoka kwa waja wake. Bali anaridhia shukurani kutoka kwao. Nayo shukurani ni kumpwekesha na kufanya matendo ya kumtii. Amesema Mtukufu:

﴿إِن تَكۡفُرُواْ فَإِنَّ ٱللَّهَ غَنِيٌّ عَنكُمۡۖ وَلَا يَرۡضَىٰ لِعِبَادِهِ ٱلۡكُفۡرَۖ وَإِن تَشۡكُرُواْ يَرۡضَهُ لَكُمۡ...﴾

"Mkikufuru, basi Mwenyezi Mungu si mwenye haja nanyi, lakini hafurahii kufuru kwa waja wake. Na mkishukuru, Yeye hufurahika nanyi." [Az-Zumar: 7]

Na imepokelewa na Bukhari katika Sahihi yake kutoka kwa Abuu Huraira, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba alisema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni nani mwenye furaha zaidi ya kupata uombezi wako?" Akasema: "Atakayesema: 'Laa ilaaha illa llaahu (Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu) likiwa limetoka moyoni mwake kwa utakasifu kabisa." Au alisema: "Kutoka katika nafsi yake."

Na katika Sahihi tena, kutoka kwa Anas, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: "Kila Nabii ana dua inayojibiwa. Basi kila Nabii akaharakisha kuomba dua yake. Nami nimeihifadhi dua yangu iwe ni uombezi kwa ajili ya umma wangu Siku ya Kiyama, nayo itampata - Mwenyezi Mungu akipenda - kila atakayekufa katika umma wangu huku hamshirikishi Mwenyezi Mungu na chochote." Na kuna hadithi nyingi zenye maana hii.

Aya na hadithi zote tulizozitaja zinaashiria kuwa ibada ni haki ya Mwenyezi Mungu peke yake, na kwamba hairuhusiwi kufanya chochote miongoni mwake kwa ajili ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu, si kwa ajili ya Manabii wala wengineo, na kwamba uombezi ni miliki ya Mwenyezi Mungu, kama alivyosema Mtukufu:

﴿قُل لِّلَّهِ ٱلشَّفَٰعَةُ جَمِيعٗا...﴾

"Sema: Uombezi wote uko kwa Mwenyezi Mungu." [Az-Zumar: 44] Hakuna anayeustahiki uombezi isipokuwa baada kumpa muombezi idhini na kumridhia yule anayefanyiwa uombezi. Naye aliyetakasika haridhii chochote isipokuwa kumpwekesha Yeye, kama ilivyotajwa hapo awali. Basi kwa mujibu wa hayo, washirikina hawana fungu lolote katika uombezi, na Mwenyezi Mungu alikwishabainisha haya katika kauli yake Mtukufu:

﴿فَمَا تَنفَعُهُمۡ شَفَٰعَةُ ٱلشَّٰفِعِينَ 48﴾

"Basi hautawafaa kitu uombezi wa waombezi." [Al-Muddaththir: 48] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...مَا لِلظَّٰلِمِينَ مِنۡ حَمِيمٖ وَلَا شَفِيعٖ يُطَاعُ 18﴾

"Madhalimu hawatakuwa na rafiki, wala muombezi wa kuitikiwa." [Ghaafir: 18].

Inajulikana kuwa dhuluma kwa ujumla ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...وَٱلۡكَٰفِرُونَ هُمُ ٱلظَّٰلِمُونَ﴾

"Na makafiri ndio madhalimu." [Al-Baqara: 254], Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...إِنَّ ٱلشِّرۡكَ لَظُلۡمٌ عَظِيمٞ﴾

"Kwani hakika ushirikina bila ya shaka ni dhuluma kubwa." [Luqman: 13].

 

 

 

 

Ama uliyoyataja katika swali lako katika kauli za baadhi ya Masufi misikitini na kwingineko: "Ewe Mwenyezi Mungu, mrehemu yule uliyemfanya sababu ya kugawanyika kwa siri zako kuu, na kuzuka kwa nuru zako za rehema, basi akawa ni mwakilishi wa uwepo wa Mola Mlezi, na mrithi wa siri zako za ndani ... n.k.

Jibu ni kwamba: Maneno haya na kauli zinazofanana nayo ni katika kujisumbua bure na kuwa na msimamo mkali ambao Mtume wetu Muhammad, rehema na amani zimshukie, alionya dhidi yake katika yale aliyoyasimulia Muslim ndani ya Sahihi yake kutoka kwa Abdullah bin Masudi, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, kuwa alisema kwamba: Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani zimshukie, alisema: "Watu wenye msimamo mkali wameangamia," aliyasema mara tatu.

Amesema Imam Khattwabi, Mwenyezi Mungu amrehemu: Mwenye msimamo mkali ni yule anayezama katika jambo fulani na kujisumbua kulipekua akifuata njia ya watu wa theolojia (wana falsafa), wanaoingia katika yale yasiyowahusu, wanaozama katika yale ambayo akili zao haziwezi kuyafikia.

Na alisema Abuu Sa'adaat binil-Athiir: Hao ndio wanaozama na kuingia ndani katika mazungumzo, ambao huzungumza kwa mapafu yao (Yaani: Kwa kujikalifisha wasiyoyaweza).

Na kwa yale waliyoyataja maimamu hawa wawili miongoni mwa maimamu wa lugha, inakudhihirikia wewe na kila mwenye ufahamu hata mdogo kwamba namna hii ya kumuombea rehema na amani Nabii wetu na Mtume wetu na bwana wetu, Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ni miongoni mwa kujisumbua na kushika msimamo mkali ambako kulikatazwa. Katika mlango huu, Muislamu anafaa kutafuta njia iliyothibiti ya kumuombea rehema na amani Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na hiyo itamtoshelezaa asihitaji njia nyingine yoyote.

Katika hizo ni ile iliyopokelewa na Bukhari na Muslim katika Sahihi zao mbili, kutoka kwa Ka'ab bin Ujrah, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, kwamba Maswahaba, Mwenyezi Mungu awawie radhi walisema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu alituamrisha kukuombea rehema, basi tunakuombea vipi rehema?" Akasema: Semeni: Ewe Mwenyezi Mungu, shusha rehema juu ya Muhammad na aali zake Muhammad, kama ulivyoshusha rehema juu ya Ibrahim na aali za Ibrahim. Hakika Wewe ni Msifiwa mno, Mtukufu. Na shusha baraka juu ya Muhammad na aali za Muhammad, kama ulivyoshusha baraka juu ya Ibrahim na aali za Ibrahim. Hakika Wewe ni Msifiwa mno, Mtukufu.

 

Na katika Sahihi mbili, kutoka kwa Abuu Humaidi As-Sa’idi, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, kwamba walisema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, tuna kuombea vipi rehema?" Akasema: “Semeni: Ewe Mwenyezi Mungu, shusha rehema juu ya Muhammad na wake zake na dhuriya wake, kama ulivyoshusha rehema juu ya aali za Ibrahim. Na mbariki Muhammad na wake zake na dhuriya wake, kama ulivyowabariki aali za Ibrahimu. Hakika Wewe ni Msifiwa mno, Mtukufu.”

Na katika Sahihi Muslim, kutoka kwa Abuu Masud Al-Ansari, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, alisema: Bashir bin Sa'ad alisema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu ametuamrisha kukuombea rehema, basi tunakuombea vipi rehema?" Akanyamaza, kisha akasema: “Semeni: 'Ewe Mwenyezi Mungu, shusha rehema juu ya Muhammad na aali za Muhammad, kama ulivyoshusha rehema juu ya aali za Ibrahimu. Na mbariki Muhammad na aali za Muhammad kama ulivyowabariki aali za Ibrahim. Hakika wewe katika walimwengu ni Msifiwa, Mtukufu.' Na kutoa salamu ni kama mlivyokwishajua."

Maneno haya na maneno yanayofanana na hayo miongoni mwa yale yaliyothibiti kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, ndiyo mambo ambayo Muislamu anapaswa kuyatumia katika kumuombea rehema na amani Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake. Kwa sababu Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, ndiye mjuzi zaidi kuliko watu wote kuhusu yale yanayostahiki kutumika kuhusiana naye, kama vile yeye ndiye mjuzi zaidi kuliko watu wote kuhusu maneno yanayofaa kutumika kuhusiana na Mola wake Mlezi.

Ama maneno yaliyotungwa tu na ya kizushi, na maneno yanayoweza kuwa na maana isiyo sahihi; kama maneno yaliyotajwa katika swali lako, hayo hayapaswi kutumiwa. Kwa sababu ni ya kujisumbua tu, na kwa sababu yanaweza kufasiriwa kwa maana batili, pamoja na kwamba hayo ni kinyume na maneno aliyoyachagua Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe juu yake na akauongoza umma wake kuyatumia, naye ndiye mjuzi zaidi ya viumbe vyote na anayewanasihi zaidi na aliye mbali zaidi ya mambo ya kujisumbua bure, rehema na amani bora zaidi ziwe juu yake kutoka kwa Mola wake Mlezi.

Ni hayo tu, na ninatumai kwamba kuna utoshelevu na manufaa kwa mwenye kutafuta haki katika yale tuliyoyataja ya ushahidi wa kueleza uhakika wa Tauhidi, uhakika wa ushirikina, na tofauti baina ya walivyokuwa wakifanya washirikina wa mwanzo na washirikina wa baadaye katika suala hili, na katika kueleza jinsi ya kumuombea Mtume rehema kwa njia ya kisheria. Ama yule asiyetaka kujua haki, basi huyo anafuata tu matamanio yake. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿فَإِن لَّمۡ يَسۡتَجِيبُواْ لَكَ فَٱعۡلَمۡ أَنَّمَا يَتَّبِعُونَ أَهۡوَآءَهُمۡۚ وَمَنۡ أَضَلُّ مِمَّنِ ٱتَّبَعَ هَوَىٰهُ بِغَيۡرِ هُدٗى مِّنَ ٱللَّهِۚ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَهۡدِي ٱلۡقَوۡمَ ٱلظَّٰلِمِينَ50﴾

"Na ikiwa hawakuitikii, basi jua kuwa wanafuata pumbao lao tu. Na ni nani aliyepotea zaidi kumshinda anayefuata pumbao lake bila ya uongofu utokao kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wenye kudhulumu." [Al-Qasas: 50]

Basi Yeye Mtukufu, akabainisha katika Aya hii tukufu kwamba; watu kuhusiana na yale ambayo Mwenyezi Mungu aliyomtuma nayo Mtume wake Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie ya uongofu na Dini ya haki wako aina mbili:

Ya kwanza: Mwenye kumuitikia Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Ya pili: Mwenye kufuata matamanio yake, kisha Yeye Mtukufu akaeleza kuwa hakuna mpotevu zaidi kuliko yule anayefuata matamanio yake bila ya uongofu utokao kwa Mwenyezi Mungu.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu -Aliyetukuka- atujaalie salama kutokana na kufuata matamanio, na kwamba atujaalie sisi na nyinyi na ndugu zetu wote miongoni mwa wale wenye kumuitikia Mwenyezi Mungu na Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, wale wanaoiheshimu sheria yake na wanaojitahadhari dhidi ya kila kitu kinachokwenda kinyume na sheria yake, kama uzushi na matamanio. Kwani Yeye ndiye Mpaji, Mkarimu zaidi.

Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wake na Mtume wake, Nabii wetu Muhammad, na aali zake, Maswahaba wake na wafuasi wake wanaomfuata kwa wema mpaka Siku ya Malipo.

***

 


بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Makala ya Tano:

Hukumu ya kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume na kuzaliwa kwa wengineo

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, na watu wa familia yake, Maswahaba wake na wote wanaofuata uongofu wake.

Ama baada ya hayo: Swali lilirudiwa kutoka kwa wengi kuhusu hukumu ya kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, na kumsimamia, na kumtolea salamu na mambo mengine yanayofanywa katika sherehe hizi za kuzaliwa.

Jibu ni kusema: Hairuhusiwi kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake au kuzaliwa kwa mtu mwingine yeyote, kwa sababu hili ni miongoni mwa uzushi uliozushwa katika dini, kwa sababu Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, hakufanya hivyo, wala makhalifa wake waongofu, wala wasiokuwa hao miongoni mwa Maswahaba, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, wala wale waliowafuata kwa wema katika karne zote bora, na wao ndio wajuzi zaidi wa Sunna, na wenye upendo kamili kabisa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, na wenye kufuata zaidi sheria yake kuliko wale waliokuja baada yao. Na amesema Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka katika Kitabu chake kilicho wazi:

﴿...وَمَآ ءَاتَىٰكُمُ ٱلرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَىٰكُمۡ عَنۡهُ فَٱنتَهُواْ...﴾

"Na anachokupeni Mtume, chukuenii. Na anacho kukatazeni, jiepusheni nacho."

[Al-Hashr: 7] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...فَلۡيَحۡذَرِ ٱلَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنۡ أَمۡرِهِۦٓ أَن تُصِيبَهُمۡ فِتۡنَةٌ أَوۡ يُصِيبَهُمۡ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴾

"Basi nawatahadhari wanaokhalifu (kwenda kinyume na) amri yake, usijeukawapata msiba au ikawapata adhabu chungu. [An-Nur: 63] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿لَّقَدۡ كَانَ لَكُمۡ فِي رَسُولِ ٱللَّهِ أُسۡوَةٌ حَسَنَةٞ لِّمَن كَانَ يَرۡجُواْ ٱللَّهَ وَٱلۡيَوۡمَ ٱلۡأٓخِرَ وَذَكَرَ ٱللَّهَ كَثِيرٗا21﴾

"Hakika nyinyi mnayo ruwaza (kiigizo) chema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana". [Al-Ahzab: 21]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 

 

﴿وَٱلسَّٰبِقُونَ ٱلۡأَوَّلُونَ مِنَ ٱلۡمُهَٰجِرِينَ وَٱلۡأَنصَارِ وَٱلَّذِينَ ٱتَّبَعُوهُم بِإِحۡسَٰنٖ رَّضِيَ ٱللَّهُ عَنۡهُمۡ وَرَضُواْ عَنۡهُ وَأَعَدَّ لَهُمۡ جَنَّٰتٖ تَجۡرِي تَحۡتَهَا ٱلۡأَنۡهَٰرُ خَٰلِدِينَ فِيهَآ أَبَدٗاۚ ذَٰلِكَ ٱلۡفَوۡزُ ٱلۡعَظِيمُ100﴾

"Na wa wale waliotangulia, wa kwanza, miongoni mwa walio hama, na Answari (waliowapokea), na walio wafuata kwa wema, Mwenyezi Mungu ameridhika nao, na wao wameridhika naye, na amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa." [At-Tauba: 100]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...ٱلۡيَوۡمَ أَكۡمَلۡتُ لَكُمۡ دِينَكُمۡ وَأَتۡمَمۡتُ عَلَيۡكُمۡ نِعۡمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ ٱلۡإِسۡلَٰمَ دِينٗا...﴾

"Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini." [Al-Maidah: 3] Na aya zenye maana hii ni nyingi sana. Na imethibiti kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba alisema: "Yeyote atakayezua katika jambo letu hili kitu ambacho hakimo, basi hicho kitakataliwa." Yaani atarudishiwa yeye mwenyewe. Na alisema katika hadithi nyingine: "Shikamaneni na Sunna zangu na Sunna za makhalifa wanyoofu waongofu wa baada yangu. Zikamateni na kuzing'ata kwa magego. Na jihadharini na mambo mapya (katika dini). Kwani kila jambo jipya ni uzushi, na kila uzushi ni upotofu." Katika Hadithi hizi mbili kuna onyo kali dhidi ya kuanzisha uzushi na kuufanyia kazi. Na kuzua mfano wa sherehe hizi za kuzaliwa inafahamika kwa jambo hilo kwamba Mwenyezi Mungu aliyetakasika hakuukamilishia umma huu dini, na kwamba Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, hakufikisha yale ambayo umma huu unapaswa kuyafanyia kazi, mpaka hawa wa nyuma walipokuja, wakazua katika sheria yale ambayo Mwenyezi Mungu hakuyaidhinisha, wakidai kuwa haya ndiyo yanayowaleta karibu na Mwenyezi Mungu. Bila shaka kuna hatari kubwa ndani yake, na nikuweka pingamizi kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, rehema na amani ziwe juu yake, na Mwenyezi Mungu amewatimizia waja wake dini, na akatimiza neema zake juu yao. Na Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alifikisha ujumbe ulio wazi, na wala hakuacha njia inayomfikisha mtu Peponi, na kumuweka mbali na Moto isipokuwa aliubainishia umma huu, kama ilivyothibiti katika hadithi sahihi kutoka kwa Abdullah bin Amri, Mwenyezi Mungu awe radhi naye kwamba alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, alisema: "Mwenyezi Mungu hakumtuma Nabii yeyote ila ilikuwa ni haki juu yake kuwaonyesha umma wake heri anayoijua kwao, na kuwaonya dhidi ya uovu anaoujua kwao." Imesimuliwa na Muslim katika Sahihi yake.

 

 

Inajulikana kuwa Mtume wetu, rehema na amani ziwe juu yake, ndiye mbora wa Manabii na wa mwisho wao, na mkamilifu wao zaidi katika kufikisha na kunasihi. Kwa hivyo, kama maadhimisho ya kuzaliwa kwake yangekuwa katika dini ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu anairidhia, Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, angewaelezea umma wake, au angeyafanya katika maisha yake, au wangeyafanya Maswahaba wake, Mwenyezi Mungu awe radhi nao. Basi pindi hakuna lolote katika haya lililotokea, ikajulikana kwamba huo sio chochote katika Uislamu. Bali ni miongoni mwa uzushi ambao Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, aliuonya umma wake dhidi yake, kama lilivyotangulia kutajwa hilo katika Hadithi mbalimbali. Na Aya na hadithi katika mlango huu ni nyingi.

Na limekemea wazi kundi la wanachuoni suala la kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake na kutahadharisha dhidi yake, kwa mujibu wa ushahidi uliotajwa hapo juu na ushahidi mwingineo. Lakini baadhi ya watu waliokuja baadaye walikwenda kinyume kwa hivyo wakaruhusu hilo ikiwa halitajumuisha uovu wowote, kama vile kupita kiasi katika kumsifu Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, na kama vile kuchanganyika wanawake na wanaume, kutumia ala za burudani, na mambo mengineyo ambayo yanakatazwa na Sheria tukufu, na wakaona kwamba ni katika uzushi mzuri.

Lakini kanuni ya kisheria ni kurudisha chochote ambacho watu wanazozana ndani yake katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓاْ أَطِيعُواْ ٱللَّهَ وَأَطِيعُواْ ٱلرَّسُولَ وَأُوْلِي ٱلۡأَمۡرِ مِنكُمۡۖ فَإِن تَنَٰزَعۡتُمۡ فِي شَيۡءٖ فَرُدُّوهُ إِلَى ٱللَّهِ وَٱلرَّسُولِ إِن كُنتُمۡ تُؤۡمِنُونَ بِٱللَّهِ وَٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِۚ ذَٰلِكَ خَيۡرٞ وَأَحۡسَنُ تَأۡوِيلًا59﴾

"Enyi mlio amini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo, basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema". [An-Nisaa: 59] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمَا ٱخۡتَلَفۡتُمۡ فِيهِ مِن شَيۡءٖ فَحُكۡمُهُۥٓ إِلَى ٱللَّهِ ...﴾

"Na mkihitilafiana katika jambo lolote, basi hukumu yake iko kwa Mwenyezi Mungu." [Ash-Shuraa: 10].

Basi tumelirejesha suala hili, ambalo ni: kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu, na tukakikuta kinatuamrisha kumfuata Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, katika yale aliyokuja nayo, na kutuonya juu ya yale aliyoyakataza, na kinatujulisha kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ameukamilishia umma huu dini yake, na sherehe hii sio katika yale aliyokuja nayo Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, kwa hivyo linakuwa si katika dini ambayo Mwenyezi Mungu ametukamilishia na akatuamrisha kumfuata Mtume ndani yake.

Pia tumelirudisha hilo katika Sunna ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake; na hatukupata ndani yake kwamba alifanya hivyo, wala hata hakuamrisha hivyo, wala Maswahaba wake Mwenyezi Mungu awe radhi nao hawakufanya hivyo, kwa hivyo tukajua kwa hayo kwamba hilo si katika dini, bali ni katika uzushi uliozushwa, na ni katika kuwaiga watu wa Kitabu miongoni mwa Mayahudi na Wakristo katika sikukuu zao.

Basi kwa hayo, inakuwa wazi kwa kila mtu ambaye ana ufahamu hata mdogo tu na hamu ya kujua haki na uadilifu katika kutafuta kwake haki, kwamba kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, si katika dini ya Uislamu, bali ni katika uzushi uliozushwa, ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume wake, rehema na amani ziwe juu yake, wameamrisha kuuwacha na kujitahadhari nao. Na kwamba mwenye akili timamu hafai kudanganyika na wingi wa watu wanaofanya hivyo katika pande zote za Dunia, kwa sababu haki haijulikani kwa wingi wa watendaji wake.

 

Bali inajulikana kwa ushahidi wa kisheria, kama alivyosema Mwenyezi Mungu kuhusu Mayahudi na Wakristo:

﴿وَقَالُواْ لَن يَدۡخُلَ ٱلۡجَنَّةَ إِلَّا مَن كَانَ هُودًا أَوۡ نَصَٰرَىٰۗ تِلۡكَ أَمَانِيُّهُمۡۗ قُلۡ هَاتُواْ بُرۡهَٰنَكُمۡ إِن كُنتُمۡ صَٰدِقِينَ111﴾

"Na walisema: Hataingia Peponi ila aliyekuwa Yahudi au Mkristo. Hayo ni matamanio yao. Sema: Leteni ushahidi wenu kama nyinyi ni wasema kweli." [Al-Baqarah: 111] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَإِنْ تُطِعْ أَكْثَرَ مَنْ فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ...﴾

“Na ukiwatii wengi katika hawa waliomo duniani, watakupoteza mbali na Njia ya Mwenyezi Mungu." [Al-An'am: 116]

Zaidi ya hayo, nyingi ya sherehe hizi za kuzaliwa, licha ya kwamba ni uzushi, hazikosi maovu mengine, kama vile kuchanganyika wanawake na wanaume, matumizi ya nyimbo na muziki, kunywa vileo na dawa za kulevya, na maovu mengineyo. Na kunaweza kutokea ndani yake kitu kikubwa zaidi kuliko hayo, ambacho ni ushirikina mkubwa, na hilo huwa kwa kupitiliza mipaka kuhusiana na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, au wengineo katika Mawalii (wachamungu), na kumuomba dua na kumlilia, na kumuomba usaidizi, na kuamini kwamba anajua mambo ya ghaibu, na mfano wa hayo miongoni mwa mambo ya kufuru ambayo watu wengi huyafanya wakati wa kusherehekea sherehe hizi za kuzaliwa kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, na wengineo miongoni mwa wale wanaowaita Mawalii. Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, kwamba alisema: "Jiepusheni na kupitiliza kiasi katika dini, kwani wale waliotangulia kabla yenu waliangamizwa na kupitiliza kiasi katika dini." Na amesema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Msinisifu sana kama Wakristo walivyomsifu sana mwana wa Mariamu. Hakika mimi ni mja tu. Basi semeni: Mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake." Imepokelewa na Bukhari, katika Sahihi yake kutoka katika Hadithi ya Omari, Mwenyezi Mungu awe radhi naye.

Na katika maajabu na mambo yasiyo ya kawaida ni kwamba watu wengi wanakuwa wakakamavu na wanajitahidi katika kuhudhuria sherehe hizi za uzushi, na kuzitetea, na anakosa kufanya kile ambacho Mwenyezi Mungu amemuwajibisha kama vile kuhudhuria swala za jamaa na tena hata hajali hilo na wala haoni kwamba amefanya ovu kubwa, na hakuna shaka kwamba hili ni katika udhaifu wa imani, uchache wa ufahamu, na kutu nyingi ya madhambi na maasi iliyo mioyoni mwao. Tunamuomba Mwenyezi Mungu salama, sisi pamoja na Waislamu wote.

 

Na katika hayo ni kwamba baadhi yao wanadhani kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, anahudhuria katika sherehe za kuzaliwa kwake, na hii ndiyo sababu wanasimama kwa ajili yake wakimsalimia na kumkaribisha. Na hili ni katika batili kubwa zaidi na ujinga mbaya kabisa. Kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, hawezi kutoka kaburini kwake kabla ya Siku ya Kiyama, na wala hawasiliani na yeyote katika watu, wala hahudhurii mkutano wao. Bali yuko kaburini mwake mpaka Siku ya Kiyama, na roho yake iko juu ya walio juu kabisa kwa Mola wake katika nyumba ya utukufu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿ثُمَّ إِنَّكُمْ بَعْدَ ذَلِكَ لَمَيِّتُونَ15 ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ تُبْعَثُونَ16﴾

"Kisha hakika nyinyi baada ya hayo mtakufa".

Kisha hakika nyinyi Siku ya Kiyama mtafufuliwa". [Al-Muminun: 15-16]

Na amesema Mtume rehema na amani zimshukie: "Mimi ndiye wa kwanza ambaye kaburi lake litafunguka siku ya Kiyama, na mimi ndiye muombezi wa kwanza na wa kwanza atakayekubaliwa uombezi wake." Rehema na amani bora zaidi ziwe juu yake kutoka kwa Mola wake Mlezi.

 

 

Basi Aya hizi mbili tukufu na Hadithi hii tukufu, na Aya na Hadithi zilizokuja na maana yake, zote zinaashiria kwamba Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, na watu wengineo waliokufa watatoka makaburini mwao Siku ya Kiyama tu. Hili ni jambo ambalo kuna maafikiano juu yake miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu, na hakuna mvutano wowote juu yake baina yao. Kwa hivyo kila Muislamu anapaswa kuwa na ufahamu wa mambo haya, na kutahadhari na yale waliyozua wajinga na mfano wao miongoni mwa mambo ya uzushi na uchawi ambayo Mwenyezi Mungu hakuyateremshia ushahidi wowote. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye ombwa msaada, naye ndiye Mtegemewa, na wala hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa Yeye.

Ama kumuombea Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, hayo ni miongoni mwa ibada bora za kujiweka kwazo karibu na Mwenyezi Mungu, na ni miongoni mwa matendo mema, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿إِنَّ ٱللَّهَ وَمَلَٰٓئِكَتَهُۥ يُصَلُّونَ عَلَى ٱلنَّبِيِّۚ يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ صَلُّواْ عَلَيۡهِ وَسَلِّمُواْ تَسۡلِيمًا56﴾

"Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamsalia Nabii. Enyi mlio amini! Msalieni na mumsalimu kwa salamu." [Al-Ahzab: 56] Na amesema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie: "Yeyote atakayeniswalia mara moja, Mwenyezi Mungu atamswalia mara kumi kwa hilo." Hilo linaruhusiwa katika wakati wote, na linasisitizwa mwishoni mwa kila swala. Bali ni wajibu kwa mujibu wa kundi la wanachuoni katika Tahiyatu ya mwisho katika kila sala. Hali yake ya kuwa sunna inasisitizwa katika sehemu nyingi; ikiwa ni pamoja na baada ya adhana, wakati anapotajwa yeye rehema na amani ziwe juu yake, siku ya Ijumaa na usiku wake, kama zilivyo onyesha hilo hadithi nyingi.

Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuombwa atuongoze sisi na Waislamu wengine wote katika kuifahamu dini yake na kuwa imara juu yake, na amneemeshe kila mtu kushikamana na Sunna, na kujihadhari na uzushi. Hakika Yeye ndiye Mpaji, Mkarimu mno.

Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad na familia yake na Maswahaba zake.

***

 


بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Makala ya Sita:

Hukumu ya kusherehekea usiku wa Al-Israa na Mi'raj

Sifa njema zote anastahiki Mwenyezi Mungu, na rehema na amani zimfikie Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake na Maswahaba wake.

Ama baada ya hayo: Hakuna shaka kwamba Al-Israa na Mi'raj ni miongoni mwa alama kubwa za Mwenyezi Mungu, zinazoashiria ukweli wa Mtume wake Muhammad, rehema na amani zimshukie, na ukuu wa hadhi yake mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama vile ni ushahidi wa uwezo mkubwa wa Mwenyezi Mungu na kuwa kwake juu ya viumbe vyake vyote. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:

﴿سُبۡحَٰنَ ٱلَّذِيٓ أَسۡرَىٰ بِعَبۡدِهِۦ لَيۡلٗا مِّنَ ٱلۡمَسۡجِدِ ٱلۡحَرَامِ إِلَى ٱلۡمَسۡجِدِ ٱلۡأَقۡصَا ٱلَّذِي بَٰرَكۡنَا حَوۡلَهُۥ لِنُرِيَهُۥ مِنۡ ءَايَٰتِنَآۚ إِنَّهُۥ هُوَ ٱلسَّمِيعُ ٱلۡبَصِيرُ1﴾

"Ametakasika Yule aliyemchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyouzunguka, ili tumu onyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona". [Al-Israa: 1].

 

 

Imesimuliwa kwa wingi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe juu yake kwamba alipanda mbinguni, na akafunguliwa milango yake mpaka akapita mbingu ya saba, na Mola wake Mlezi Mtukufu akamsemesha akamwambia kile alichotaka, na akamfaradhishia swala tano. Hapo awali Mwenyezi Mungu Mtukufu alikuwa amemfaradhishia swala hamsini, lakini Nabii Muhammad rehema na amani ziwe juu yake hakuacha kumrudia na kumuomba azipunguze, mpaka akazifanya kuwa tano. Basi ni tano katika wajibu, na ni hamsini katika malipo; kwa sababu jema moja linalipwa mfano wake mara kumi. Kwa hivyo sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu na shukrani kwa neema zake zote.

Usiku huu ambao ilifanyika Isra na Mi’raj ndani yake, haukubainishwa haswa ulikuwa upi katika Hadithi sahihi, si katika Rajab wala katika mwezi wowote ule. Kila kilichokuja katika kuteua muda wake haswa, hicho hakikuthibiti kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwa mujibu wa wanazuoni wa elimu ya Hadithi. Na Mwenyezi Mungu anayo hekima kubwa zaidi ya kuwasahaulisha watu usiku huo. Na hata kama ingejulikana kwamba yalitokea katika usiku fulani unaojulikana, basi wasinge ruhusiwa kuuadhimisha. Kwa sababu Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na Maswahaba zake, Mwenyezi Mungu awawie radhi, hawakuuadhimisha, wala hawakuuwekea kitu chochote maalumu. Na kama kuuadhimisha kungekuwa jambo lililoko katika sheria, basi Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, angeliuelezea umma wake hilo; ima kwa kauli au kwa vitendo. Na kama lingetokea jambo kama hilo, basi lingejulikana na kuwa maarufu, na Maswahaba, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, wangelitufikishia sisi. Kwani wao walisimulia kutoka kwa Mtume wao, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kila kitu ambacho umma unakihitaji, na hawakupuuza chochote katika Dini. Bali wao ndio waliokuwa wa kwanza kuiendea kila heri. Kwa hivyo, kungekuwa kuadhimisha usiku huu kuko katika sheria, basi wangekuwa watu wa kwanza kufanya hivyo. Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ndiye mwenye kunasihi zaidi kuliko watu wote, na alikwishafikisha ujumbe kufikisha kwa hali ya juu zaidi, na akatekeleza amana. Kwa hivyo, kungekuwa kuuadhimisha usiku huu na kuusherehekea kunatoka kwa Mwenyezi Mungu, basi Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, hangekosa kujua hilo, na hangelificha. Na pindi hakuna chochote kilichotokea katika hayo, ikajulikana kuwa kuusherehekea na kuuadhimisha si katika Uislamu hata kidogo. Na tayari Mwenyezi Mungu alishaukamilishia umma huu dini yake, akautimizia neema zake, na akawakanusha wale wanaotunga sheria katika dini yale ambayo Mwenyezi Mungu haku yaruhusu. Amesema Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka katika Kitabu chake kilicho wazi:

﴿...ٱلۡيَوۡمَ أَكۡمَلۡتُ لَكُمۡ دِينَكُمۡ وَأَتۡمَمۡتُ عَلَيۡكُمۡ نِعۡمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ ٱلۡإِسۡلَٰمَ دِينٗا...﴾

"Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini." [Al-Maidah: 3] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿أَمۡ لَهُمۡ شُرَكَٰٓؤُاْ شَرَعُواْ لَهُم مِّنَ ٱلدِّينِ مَا لَمۡ يَأۡذَنۢ بِهِ ٱللَّهُۚ وَلَوۡلَا كَلِمَةُ ٱلۡفَصۡلِ لَقُضِيَ بَيۡنَهُمۡۗ وَإِنَّ ٱلظَّٰلِمِينَ لَهُمۡ عَذَابٌ أَلِيمٞ21﴾

"Au hao wana miungu ya kishirikina iliyowatungia dini asiyoitolea idhini Mwenyezi Mungu? Na lau lisingekuwako neno la kupambanua, basi wangelikatiwa hukumu baina yao. Na hakika wenye kudhulumu watapata adhabu chungu). [Ash-Shura: 21].

Na ilithibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika Hadithi sahihi kwamba alitahadharisha dhidi ya uzushi na akatangaza wazi kwamba ni upotofu ili kutanabahisha umma wake juu ya ukubwa wa hatari yake, na kuwaweka mbali na kuufanya, ikiwa ni pamoja na yale yaliyothibiti katika Sahihi mbili kutoka kwa Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, kwamba alisema: "Yeyote atakayezua katika jambo letu hili kitu ambacho hakimo, basi hicho kitakataliwai." Katika simulizi ya Muslim: "Mwenye kufanya amali ambayo hatukuiamrisha, basi amali hiyo itakataliwa." Na katika Sahihi Muslim, kutoka kwa Jabir Mwenyezi Mungu awe radhi naye alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe juu yake alikuwa akisema katika hotuba yake siku ya Ijumaa: "Ama baada ya hayo. Hakika mazungumzo bora ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Na muongozo bora ni muongozo wa Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Na mambo mabaya zaidi ni mambo ya kuzushwa. Na kila uzushi ni upotevu." Aliongeza Imam Nasai kwa mlolongo mzuri wa wasimulizi kwamba: "Na kila upotofu ni Motoni." Na katika Sunan, imesimuliwa kutoka kwa Al-'Irbat bin Sariyah, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, kwamba alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alituaidhi mawaidha makali sana. Nyoyo zikajaa hofu kwa sababu yake, na macho yakamiminika machozi kwa sababu yake, basi tukasema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni kama kwamba ni mawaidha ya anayeaga. Basi tuusie." Akasema: "Ninawausia kumcha Mwenyezi Mungu, na kusikia na utii, hata kama atakutawaleni mtumwa. Kwani hakika yeyote kati yenu atakayeishi, ataona tofauti nyingi. Kwa hivyo shikamaneni na Sunna yangu na Sunna ya makhalifa wanyoofu waongofu baada yangu. Zikamateni na kuzing'ata kwa magego. Na jihadharini na mambo ya kuzushwa. Kwani kila jambo jipya (katika dini) ni uzushi, na kila uzushi ni upotofu." Na kuna hadithi nyingi zenye maana hii.

Ilithibiti kutoka kwa Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, na kutoka kwa watangulizi wema wa baada yao, kutahadharisha dhidi ya uzushi na kutisha kutokana nao. Hili si isipokuwa kwa sababu tu ni kuongeza katika dini na kutunga sheria ambayo Mwenyezi Mungu hakuidhinisha, na ni kujifananisha na maadui wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa Mayahudi na Wakristo katika kuongeza katika dini yao, na katika kuzua kwao ndani yake kile ambacho Mwenyezi Mungu hakuidhinisha, na kwa sababu hilo linamaanisha kwamba kuna upungufu katika dini ya Kiislamu, kuishutuhumu kwamba si kamilifu, lakini hili linajulikana kwamba ni uharibifu mkubwa, uovu mbaya sana, na kugongana na maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...ٱلۡيَوۡمَ أَكۡمَلۡتُ لَكُمۡ دِينَكُمۡ...﴾

"Leo nimekukamilishieni dini yenu." [Al-Maidah: 3] Na kwenda kinyume wazi wazi na hadithi za Mtume, rehema na amani ziwe juu yake zinazoonya dhidi ya uzushi na zinazomuweka mtu mbali na hilo.

 

Ni hayo, na ninatumai kwamba ushahidi tulioutaja utamtosha na kumridhisha mtafutaji haki katika kukataza uzushi huu. Ninamaanisha uzushi wa kusherehekea usiku wa Israai na Mi'raj, na kuonya dhidi yake, na kwamba hauhusiani na dini ya Kiislamu hata kidogo.

Na kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwajibisha kuwapa Waislamu nasaha, na kubainisha yale ambayo Mwenyezi Mungu amewawekea sheria yake katika dini, na kuharamisha kuficha elimu, niliona niwatanabahishe ndugu zangu Waislamu juu ya uzushi huu, ambao umeenea katika sehemu nyingi, mpaka baadhi ya watu wakadhani kwamba hilo ni katika dini.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu arekebishe hali za Waislamu wote, awape ufahamu wa dini na atuwezeshe sisi na wao kushikamana na haki na kuwa imara juu yake, na kuacha yenye kwenda kinyume. Hakika Yeye ndiye Msimamizi wa hayo na Mwenye uwezo juu yake.

Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Nabii wetu Muhammad, na familia yake na Maswahaba wake.

***

 


بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Makala ya Saba:

Hukumu ya kusherehekea usiku wa nusu ya Shaaban

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye tukamilishia Dini, na akatutimizia neema, na rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimfikie Nabii wake na Mtume wake Muhammad, Nabii wa toba na rehema.

Ama baada ya hayo: Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:

﴿...ٱلۡيَوۡمَ أَكۡمَلۡتُ لَكُمۡ دِينَكُمۡ وَأَتۡمَمۡتُ عَلَيۡكُمۡ نِعۡمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ ٱلۡإِسۡلَٰمَ دِينٗا...﴾

"Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini." [Al-Maidah: 3] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿أَمۡ لَهُمۡ شُرَكَٰٓؤُاْ شَرَعُواْ لَهُم مِّنَ ٱلدِّينِ مَا لَمۡ يَأۡذَنۢ بِهِ ٱللَّهُ...﴾

"Au hao wana miungu ya kishirikina iliyowatungia dini asiyoitolea idhini Mwenyezi Mungu?" [Ash-Shura: 21]. Na katika Sahihi mbili kutoka kwa Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, ya kwamba Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alisema: "Yeyote atakayezua katika jambo letu hili kitu ambacho hakimo, basi kitu hicho kitakataliwai." Na katika Sahihi Muslim, kutoka kwa Jabir Mwenyezi Mungu amridhie, ya kwamba Mtume rehema na amani juu yake alikuwa akisema katika hotuba ya Ijumaa: "Ama baada ya hayo: Hakika mazungumzo bora ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Na muongozo bora ni muongozo wa Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Na mambo mabaya zaidi ni mambo ya kuzushwa. Na kila uzushi ni upotevu." Kuna Aya na Hadithi nyingi zenye maana hii, nazo ninaonyesha wazi kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ameukamilishia umma huu dini, na ameutimizia neema yake, na hakumfisha Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, isipokuwa baada ya Mtume kufikisha kufikisha kwa wazi, na akauelezea umma huu maneno na matendo yote ambayo Mwenyezi Mungu ameuwekea katika sheria yake. Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alieleza wazi kwamba kila kitu ambacho watu watazusha baada yake na kukinasibisha na dini ya Kiislamu, sawa kiwe ni maneno au vitendo, hivyo vyote ni uzushi utakaokataliwa na na arudishiwe aliyeuanzisha, hata kama nia yake ilikuwa njema. Maswahaba wa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, walilijua jambo hili, na vile vile wanavyuoni wa Kiislamu wa baada yao. Kwa hivyo, wakaukemea uzushi huo na kuonya dhidi yake, kama alivyotaja hilo kila aliyeandika juu ya kuheshimu Sunna na kukataza uzushi; kama vile Ibn Wadhwaah, At-Twartuushii, Abu Shaama na wengineo.

Na hakika miongoni mwa uzushi ambao baadhi ya watu wameuanzisha ni uzushi wa kusherehekea usiku wa nusu ya Sha’ban na kuiteua siku hiyo kwa ajili ya saumu. Hakuna ushahidi wowote unaoweza kutegemewa kwa hili. Ila kuna Hadithi dhaifu ambazo zimeripotiwa kuhusu ubora wake, ambazo hairuhusiwi kuzitegemea.

Ama kuhusu kile kilichokuja kuhusiana na fadhila za kuswali ndani yake, hizo zote ni za kutungwa na watu, kama wasomi wengi walivyotanabahisha juu ya hilo, na tutataja baadhi ya maneno yao baadaye, Mwenyezi Mungu akipenda.

Pia kuna simulizi zinazohusiana na hilo zilizosimuliwa kutoka kwa watangulizi wema miongoni mwa wanazuoni wa Sham na wengineo.

Wanavyuoni walio wengi wamekubaliana kwamba kusherehekea hilo ni uzushi, na kwamba Hadithi zilizosimuliwa kuhusu fadhila zake, zote ni dhaifu, na baadhi yake ni za kutungwa na watu. Miongoni mwa wale waliotanabahisha juu ya hilo ni Al-Hafidh Ibn Rajab katika kitabu chake "Latwa’if Al-Ma’arif" na wengineo. Na inajulikana kuwa Hadithi dhaifu zinaweza kutumika tu katika matendo ya ibada ambazo asili yake ilithibiti kwa ushahidi sahihi.

Ama kuhusu kusherehekea usiku wa nusu ya Sha'aban, hilo halina msingi sahihi; ndiyo utumike pamoja na hadithi dhaifu. Kanuni hii utukufu ilitajwa na Imam Abu Al-Abbas, Sheikh Al-Islam Ibn Taymiyyah, Mwenyezi Mungu amrehemu.

Nami ninakufikishia, ewe msomaji kile ambacho baadhi ya wasomi walisema katika suala hili, ili uweze kulifahamu vyema.

Wanavyuoni -Mwenyezi Mungu awarehemu- wame afikiana kwamba jambo la wajibu ni kurejesha mambo ambayo watu wanabishana ndani yake kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu mkubwa, na kwenye Sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Hapo, chochote kinachopingana na viwili hivyo, inakuwa ni lazima kukitupilia mbali. Na ibada yoyote ambayo haikuja katika viwili hviyo, basi hiyo ni uzushi ambao hauruhusiwi kuutenda, achilia mbali kuulingania na kuwahimiza watu juu yake. Amesema Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka:

﴿يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓاْ أَطِيعُواْ ٱللَّهَ وَأَطِيعُواْ ٱلرَّسُولَ وَأُوْلِي ٱلۡأَمۡرِ مِنكُمۡۖ فَإِن تَنَٰزَعۡتُمۡ فِي شَيۡءٖ فَرُدُّوهُ إِلَى ٱللَّهِ وَٱلرَّسُولِ إِن كُنتُمۡ تُؤۡمِنُونَ بِٱللَّهِ وَٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِۚ ذَٰلِكَ خَيۡرٞ وَأَحۡسَنُ تَأۡوِيلًا59﴾

 

 

"Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo, basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema". [An-Nisaa: 59] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿َمَا ٱخۡتَلَفۡتُمۡ فِيهِ مِن شَيۡءٖ فَحُكۡمُهُۥٓ إِلَى ٱللَّهِ...﴾

"Na mkihitilafiana katika jambo lolote, basi hukumu yake iko kwa Mwenyezi Mungu." [Ash-Shuraa: 10]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿قُلۡ إِن كُنتُمۡ تُحِبُّونَ ٱللَّهَ فَٱتَّبِعُونِي يُحۡبِبۡكُمُ ٱللَّهُ وَيَغۡفِرۡ لَكُمۡ ذُنُوبَكُمۡ...﴾

"Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu". [Al-Imran: 31] Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤۡمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيۡنَهُمۡ ثُمَّ لَا يَجِدُواْ فِيٓ أَنفُسِهِمۡ حَرَجٗا مِّمَّا قَضَيۡتَ وَيُسَلِّمُواْ تَسۡلِيمٗا65﴾

"La! Ninaapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayohitilafiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utakayotoa, na wanyenyekee kabisa". [An-Nisaa: 65] Na Aya zenye maana hii ni nyingi, nazo zinataja moja kwa moja kuwa ni wajibu kurudisha masuala ya hitilafu kwenye Kitabu na Sunna, na kwamba ni lazima kuridhia hukumu ya viwili hivyo, na kwamba hili ndilo hitaji la imani, na ndilo bora kwa waja duniani na akhera, na ndiyo yenye mwisho mwema.

Al-Hafith Ibn Rajab, Mwenyezi Mungu amrehemu, alisema katika kitabu chake: (Latwaif Al-Maarif) katika suala hili, baada ya maneno yaliyotangulia. Alisema hivi:

"Na usiku wa nusu ya Shaaban, wafuasi wa Masahaba waliokuwa huko Sham kama vile Khalid bin Ma'daan, Mak-huul, na Luqman bin Amir na wengineo, walikuwa wakiutukuza na kujibibiisha ndani yake kufanya ibada, na kutoka kwao ndio watu walichukua ubora wake na kuutukuza. Ilisemekana kuwa simulizi za Kiisraeli ziliwafikia katika suala hili, na wakati hili lilipojulikana kuhusiana nao katika nchi, watu wakatofautiana katika hilo. Basi baadhi yao wakalikubali kutoka kwao na wakaafikiana nao kuhusiana na kuutukuza, katika hao ni kikundi miongoni mwa wale wafanyao ibada sana katika watu wa Basra na wengineo. Hilo lilikataliwa na wanachuoni wengi wa Hijazi, ikiwa ni pamoja na Atwaa, na bin Abi Mulaika, na lilinukuliwa na 'Abdur-Rahman ibn Zaid ibn Aslam kutoka kwa wanazuoni wa watu wa Madina, nayo ndiyo kauli ya wafuasi wa Malik na wengineo, nao wote walisema: Huo wote ni uzushi.

Wanachuoni wa watu wa Sham walitofautiana katika njia ya kufanya ibada ndani yake kwa kauli mbili:

Ya kwanza: Kwamba inapendekezwa kufanya ibada ndani yake kwa kikundi ndani ya misikiti. Khalid bin Madan, na Luqman bin Amir na wengineo walikuwa wakivaa nguo zao bora, wakijifukizia moshi wa manukato na kupaka wanja, na kusimama msikitini usiku huo, na pia Ishaq bin Rahawaihi alikubaliana nao katika hayo. Alisema kuhusiana na kusimama kwa ajili ya swala misikitini katika jamaa: Huu si uzushi. Hili lilinukuliwa na Harb Al-Karmaani katika masuala yake.

Ya pili: Kwamba inachukiza kukutana ndani yake katika misikiti kwa ajili ya sala, kusimulia visa na kuomba dua, lakini haichukizi mtu kusali ndani yake yeye mwenyewe, na hivi ndivyo alivyosema Al-Awza'i, imamu wa watu wa Sham, faqihi wao na mwanachuoni wao, na hii ndiyo kauli iliyokaribu zaidi na usahihi, Mwenyezi Mungu akipenda." Hadi aliposema: “Na haijulikani Imam Ahmad alisema nini kuhusu usiku wa nusu ya Sha'aban, lakini zinaweza kutolewa riwaya mbili kutoka kwake zenye kupendekeza kuusimama kama zile riwaya mbili zilizopokelewa kutoka kwake zenye kupendekeza kusimama katika usiku wa Idi mbili. Katika masimulizi moja, hakupendekeza kusimama usiku wa Idi mbili katika jamaa; kwa sababu hilo halikupokelewa kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie na maswahaba wake. Na alipendekeza hilo (katika simulizi nyingine), kwa sababu Abdur-Rahman bin Yazid bin Al-Aswad alifanya hivyo, naye ni miongoni mwa wale waliokuja baada ya Maswahaba. Na vile vile kusimama kwa ajili ya ibada usiku wa nusu ya Shaban hakuna kilichothibiti kuhusiana na hilo kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, wala kutoka kwa Maswahaba wake. Na hilo lilithibiti tu kutoka kwa kundi la watu binafsi waliokuja baada ya Maswahaba miongoni mwa wanachuoni wa watu wa Sham.

Yamekwisha yaliyokusudiwa katika maneno ya Al-Hafidh Ibn Rajab, Mwenyezi Mungu amrehemu, na ndani yake ameeleza kwa uwazi kabisa kwamba hakuna chochote kilichothibiti kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, wala kutoka kwa Maswahaba zake kuhusu usiku wa katikati ya Sha’ban.

Ama kuhusu kile ambacho Al-Auza'i alichagua -Mwenyezi Mungu amrehemu- kupendekeza mtu binafsi kusimama kwa ajili ya ibada na kuchagua kwake Al-Hafidh Ibn Rajab kauli hii, hilo ni geni na dhaifu. Kwa sababu kila kitu ambacho hakikuthibiti kwa ushahidi wa kisheria kwamba ni katika sheria, hairuhusiwi kwa Muislamu kukizua katika dini ya Mwenyezi Mungu, sawa akifanye peke yake au katika jamaa, na sawa akifanye kwa siri au wazi wazi; kwa ujumla wa kauli ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake: "Mwenye kufanya tendo ambalo hatukuliamrisha, basi hilo litakataliwa." Na ushahidi mwingine wa kukanusha na kuonya dhidi ya uzushi.

Imam Abu Bakar at-Tartushi, Mwenyezi Mungu amrehemu, alisema katika kitabu chake Al-Hawaadith wal-Bida'u:

"Na amesimulia bin Wadhwaah kutoka kwa Zaid bin Aslam, ya kuwa, alisema: Hatukuwahi kuona yeyote kati ya Mashekhe wetu au wanasheria wetu akizingatia (suala la kusimama usiku wa) nusu ya Sha'baan, wala kuzingatia hadithi ya Mak-hul, wala hata hawakuwa wakiona kuwa kuna ubora wowote kuliko usiku mwingineo."

Na aliambiwa bin Abi Mulaikah: Ziadi An-Numairi anasema: "Hakika malipo ya usiku wa nusu ya Sha'baan ni kama malipo ya usiku wa Cheo (Lailatul-Qadr)." Akasema: "Laiti ningemsikia huku nikiwa na fimbo mkononi, basi ningempiga nayo." Na Ziadi alikuwa msimuliaji wa visa. Yamekamilika makusudio.

Na amesema Ash-Shaukani –Mwenyezi Mungu amrehemu– katika kitabu “Al-Fawa’id Al-Majmu’ah” yafuatayo:

Hadithi ya: “Ewe Ally, mwenye kusali rakaa mia katika usiku wa nusu ya Shaaban akisoma Al-Fatiha katika kila rakaa na Qul huwallahu ahad mara kumi, Mwenyezi Mungu atamtimizia kila haja yake." n.k. Ni hadithi waliyoitunga watu, na mtu hawezi kuwa na shaka yoyote kuhusu maneno yake yanayosema wazi wazi juu ya thawabu zake kwamba hayo yalitungwa tu na watu, na hata wasimulizi wake hawajulikani vyema, na pia ilisimuliwa katika njia ya pili na ya tatu, ambazo zote zimetungwa tu na watu na wasimulizi wake hawajulikani. Na alisema katika "Al-Mukhtaswar": Hadithi ya kuswali katika nusu ya Sha'ban ni batili. Ibn Hibban alisimulia hadithi ya Ali: "Unapokuwa usiku wa nusu ya Sha'ban, simameni usiku wake, na fungeni saumu mchana wake." ni dhaifu. Alisema katika "Alla-alii": (Kuswali) Rakaa mia moja katika nusu ya Shaaban kwa ikhlas ni (kama rakaa) elfu moja." pamoja na urefu wa fadhila yake. Hii imepokelewa na Ad-Dailami na wengineo, lakini ni ya kutungwa tu na watu, wengi wa wasimulizi wake katika njia zake tatu hawajulikani na ni madhaifu. Na akasema: "Na rakaa kumi na mbili kwa ikhlas ni (kama rakaa) mia tatu na sitini". Nayo pia ni hadithi ya kutungwa na watu. Alisema: "Na rakaa kumi na nne" Pia ni hadithi ya kutungwa na watu.

Kuna kundi la mafaqihi (wanachuoni) lililoizingatia hadithi hii, kama vile mwandishi wa (Al-Ihyaa) na wengineo, vile vile wengineo miongoni mwa wafasiri. Na imepokelewa swala ya usiku huu - ninamaanisha: Usiku wa nusu ya Sha'ban - kwa njia tofauti toafauti, ambazo zote ni batili. Hili halipingani na riwaya ya At-Tirmidhi kutoka kwa Hadithi ya Aisha, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, kuhusu kwenda kwake Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, huko Al-Baqi’, na kushuka kwa Mola Mlezi katika usiku wa katikati ya Sha'ban hadi mbingu ya chini kabisa, na kwamba Yeye husamehe zaidi ya idadi ya nywele za kondoo wa kabila la Kalb. Kwani hapa suala linahusiana na swala hii iliyotungwa na watu katika usiku huu. Hata hivyo, hadithi hii ya Aisha ina udhaifu na usimulizi wake haufiki kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kama vile hadithi ya Ali, ambayo imetajwa hapo awali kuhusu kusimama kwa ajili ya swala katika usiku wa nusu ya Shaban haipingani na hali ya kwamba swala hii imetungwa na watu, pamoja na udhaifu wake, kama tulivyotaja.

Al-Hafidh Al-Iraqi alisema: "Hadithi ya Swala ya usiku wa nusu ya Shaban imetungwa na watu na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, hakuisema na ni kumzulia uongo juu yake." Imam An-Nawawi alisema katika kitabu cha "Al-Majmu" kwamba: Swala inayo julikana kama swala ya arraghaaib, ambayo ni rakaaa kumi na mbili kati ya Maghrib na Isha, usiku wa Ijumaa ya kwanza ya Rajab, na swala ya usiku wa nusu ya Shaaban ambayo ni rakaa mia moja, sala hizi mbili ni uzushi unaopingwa, na mtu asidanganyike na kutajwa kwake katika kitabu cha "Quut Al-Quluub" na "Ihayaa 'Uluumud-Diin" wala katika hadithi yoyote ambayo zilitajwa ndani yake. Zote hizo ni batili, na wala mtu asidanganyike na baadhi ya maimamu waliotatizika kuhusiana na hukumu yake, kwa hivyo wakaandika makaratasi kuhusu kuzipendekeza, kwa sababu walikosea katika hilo."

Sheikh, Imamu, Abu Muhammad Abdul-Rahman bin Ismail al-Maqdisii aliandika kitabu chenye thamani kubwa katika kukanusha hayo, na akafanya kazi nzuri sana ndani yake. Na maneno ya wanazuoni katika suala hili ni mengi sana, na lau tungenukuu kila kitu tulichokiona katika maneno yaliyosemwa juu ya suala hili, basi maneno hayo yangekuwa marefu sana, na pengine tuliyoyataja yatamtosha na kumridhisha mtafutaji haki.

Kupitia Aya, Hadithi na maneno ya wanachuoni yaliyotangulia hapo juu, inadhihirika kwa mtafutaji haki kwamba kusherehekea usiku wa katikati ya Sha’ban kwa swala au mambo mengineyo, na kuuteua mchana wake kwa ajili ya saumu, ni uzushi unaokataliwa na wanavyuoni wengi, na hayo hayana msingi wowote katika Sheria safi. Bali ni miongoni mwa mambo mapya yaliyotokea katika Uislamu baada ya zama za Maswahaba, Mwenyezi Mungu awe radhi nao. Inamtosha mtafutaji haki katika mlango huu na wingineyo kauli ya Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu mkubwa:

﴿...ٱلۡيَوۡمَ أَكۡمَلۡتُ لَكُمۡ دِينَكُمۡ...﴾

"Leo nimekukamilishieni dini yenu." [Al-Maidah: 3] Na aya nyingizeno zilizokuja na maana yake, na maneno ya Mtume rehema na amani ziwe juu yake: "Yeyote atakayezua katika jambo letu hili kitu ambacho hakimo, basi hicho kitakataliwai." Na hadithi zilizokuja na maana yake.

Na katika Sahihi Muslim, kutoka kwa Abuu Huraira, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Msiuteuwe usiku wa Ijumaa kwa ajili ya kusimama katika usiku, na wala msiiteuwe siku yoyote ile kwa ajili ya kufunga saumu ndani yake, isipokuwa ikiwa ni katika kufanga saumu ambako mmoja wenu hufunga." Kama kungekuwa kuuteuwa usiku fulani kwa ajili ya ibada fulani kunaruhusiwa, basi usiku wa Ijumaa ungekuwa bora zaidi ya usiku mwingineo, kwa sababu mchana wake ndio mchana bora zaidi ambao jua limewahi kuuchomozea, kwa mujibu wa andiko la Hadithi sahihi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake. Basi pindi Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alipoonya dhidi ya kuuteuwa usiku huu kwa ajili ya ibada, hilo likaonyesha kwamba usiku mwingineo haufai zaidi, hairuhusiwi kuuteuwa kwa ajili ya ibada yoyote ile isipokuwa kwa ushahidi sahihi unaoonyesha uteuzi huo.

Kwa kuwa usiku wa Cheo (Lailatul-Qadr) na siku zote za Ramadhan tumeamrishwa kusimama kwa ajili ya ibada na kufanya bidii ndani yake, Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alitanabahisha dhidi ya hili, na akauhimiza umma kusimama ndani yake kwa ajili ya ibada, na mwenyewe akafanya hivyo, kama ilivyo katika Sahihi mbili kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ya kwamba alisema: "Atakayefunga Ramadhani kwa imani na kutarajia malipo (ya Mwenyezi Mungu), atasamehewa dhambi zake zilizotangulia. Na atakayesimama katika Lailatul-Qadri kwa ajili ya ibada kwa imani na kutarajia malipo, atasamehewa dhambi zake zilizotangulia." Basi kama usiku wa nusu ya Shaaban, au usiku wa kwanza wa Ijumaa katika mwezi wa Rajab, au usiku wa Al-Israa na Mi'raj, ungelikuwa ni katika sheria kuuteuwa kwa ajili ya sherehe au ibada fulani, basi Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, angeliuongoza umma kwake katika hayo, au angeyafanya yeye mwenyewe, na kama kingelitokea kitu kama hicho, basi Masahaba -Mwenyezi Mungu awe radhi nao- wangekifikisha kwa umma, na wasingekificha umma usikijue, na wao ndio watu bora kabisa, na na ndio wenye kunasihi zaidi watu baada ya Manabii, rehema na amani ziwe juu yao, na Mwenyezi Mungu aliwaradhia Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake na akawafanya kuridhia.

Umekwishajua hivi karibuni kutokana na maneno ya wanachuoni kwamba hakuna chochote kilichothibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, wala kutoka kwa Maswahaba zake, Mwenyezi Mungu awawie radhi, kuhusu fadhila za usiku wa Ijumaa ya kwanza katika Rajab, wala usiku wa katikati ya Sha’ban, kwa hivyo ikajulikana kuwa kuzisherehekea ni uzushi ulioingizwa katika Uislamu, na vile vile kuziteua kwa ajili ya ibada fulani ni uzushi unaokatazwa. Vivyo hivyo, usiku wa ishirini na saba wa Rajab, ambao baadhi ya watu wanaamini kuwa ndio usiku wa Al-Israa na Mi'raj, hairuhusiwi kuuteuwa kwa ajili ya kitu chochote cha ibada, wala kuusherehekea; kwa sababu ya ushahidi uliotangulia. Lau hilo lingejulikana. Basi itakuwa vipi na ukweli katika kauli za wanachuoni ni kwamba halijulikani. Na kauli ya yule aliyesema: Ni usiku wa ishirini na saba wa Rajab, ni kauli batili na haina msingi wowote katika hadithi sahihi, na alisema vizuri sana aliyesema:

Na mambo bora zaidi ni yale yanayotokana na uongofu... na mambo mabaya zaidi ni mambo ya uzushi, na ya kubumbwa.

Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuombwa atuwezeshe sisi na Waislamu wote kushikamana na Sunna na kuwa imara juu yake na kuyatahadhari yale yaliyokwenda kinyume nayo. Hakika Yeye ni Mpaji, Mkarimu.

Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wake na Mtume wake, Mtume wetu Muhammad, na juu ya familia yake na Maswahaba wake wote.

 

***

 


بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Makala ya Nane:

Tanbihi muhimu juu ya uongo wa wosia ulionasibishwa na

Sheikh Ahmad, mtumishi wa Msikiti mtukufu wa Mtume

Kutoka kwa Abdulaziz bin Abdullah bin Baz hadi kwa Waislamu watakaousoma, Mwenyezi Mungu awalinde kwa Uislamu, na atuepushe sisi na wao na uzushi mbaya wa wajinga na madhalimu. Amiin.

Assalaam alaikum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Ama baada ya hayo: Niliona ujumbe unaohusishwa na Sheikh Ahmad, mtumishi wa Msikiti mtukufu wa Mtume, wenye kichwa cha habari: "Huu ni wosia kutoka Madina kutoka kwa Sheikh Ahmad, mtumishi wa Msikiti mtukufu wa Mtume," ambapo alisema:

"Nilikuwa ninakesha usiku wa Ijumaa nikisoma Qur'ani Tukufu, na baada ya kusoma usomaji wa Majina Mazuri ya Mwenyezi Mungu, nilipomaliza hilo, nilijiandaa kwa ajili ya kulala, na nikamuona mtu mwenye muonekano mzuri, Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, aliyekuja na Aya za Qur'ani na hukumu tukufu; viwe rehema kwa walimwengu wote, bwana wetu Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Akasema: Ewe Sheikh Ahmad. Nikasema: Nimekuitikia ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mtukufu wa viumbe vyote. Akaniambia: "Nimeaibika kwa matendo mabaya ya watu, na sikuweza kukutana na Mola wangu Mlezi wala Malaika; kwa sababu kuanzia Ijumaa hadi Ijumaa watu elfu mia moja na sitini walikufa mbali na dini ya Uislamu." Na kisha akataja baadhi ya dhambi ambazo watu waliingia ndani yake. Kisha akasema: "Huu hapa wasia ambao ni rehema kwao kutoka kwa Mwenye nguvu, atendaye atakavyo." Kisha akataja baadhi ya alama za Saa ya Kiyama, hadi aliposema: "Basi Sheikh Ahmad, waambie wasia huu, kwa sababu umenukuliwa kwa kalamu ya mipango ya Mwenyezi Mungu kutoka katika ubao uliohifadhiwa. Na yeyote anayeuandika na kupeleka kutoka nchi hadi nchi, na mahali hadi mahali, atajengewa kasri Peponi. Na yeyote asiyeuandika na kuutuma, atanyimwa uombezi wangu Siku ya Kiyama." Na yeyote atakayeuandika na alikuwa maskini, basi Mwenyezi Mungu atamajirisha, au ikiwa alikuwa na deni, Mwenyezi Mungu atamlipia deni lake, au alikuwa na dhambi, Mwenyezi Mungu atamsamehe yeye na wazazi wake kwa baraka ya wosia huu. Na yeyote ambaye hatauandika katika waja wa Mwenyezi Mungu, uso wake utakuwa mweusi duniani na Akhera. Na akasema: "Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu", mara tatu, "huu ni ukweli, na ikiwa mimi ni muongo, basi nitoke duniani nikiwa mimi si Muislamu. Na atakayeuamini, ataokoka na adhabu ya Moto. Na atakayeukanusha, atakuwa amekufuru."

Huu ndio muhtasari wa yale yaliyo katika wosia aliozuliwa uongo Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake. Na tumeshawahi kuusikia wosia huu wa uongo mara nyingi miaka mingi iliyopita, ukienezwa miongoni mwa watu mara kwa mara, na kusambazwa miongoni mwa watu wengi wa kawaida, na kuna tofauti katika maneno yake yenyewe. Na muongo wake anasema: Alimuona Mtume rehema na amani ziwe juu yake usingizini, kwa hivyo akambebesha wosia huu. Na katika chapa hii ya mwisho tuliyokutajia ewe msomaji, huyo mzushi alidai ndani yake kwamba alimuona Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alipokuwa anajitayarisha kulala, kwa hivyo maana yake ni kwamba alimuona akiwa macho!

Katika wasia huu, huyu mzushi alidai mambo mengi, ambayo ni uongo ulio wazi, na batili iliyo wazi mno. Nitakutanabahisha juu yake hivi karibuni katika neno hili, Mwenyezi Mungu akipenda. Na tayari nilikwisha tanabahisha juu yake katika miaka iliyopita, na nikawaelezea watu kwamba ni uongo ulio wazi, na batili iliyo wazi kabisa. Basi pindi niliposoma chapa hii ya mwisho, nilisita kuandika juu yake, kwa sababu ya kuonekana wazi kwa ubatili wake, na ujasiri mkubwa wa mzushi huyu kusema uongo, na sikudhani kwamba ubatili wake utamshawishi yeyote mwenye ufahamu hata mdogo tu, au maumbile sahihi ya kawaida. Hata hivyo, ndugu wengi waliniambia kwamba umesambazwa miongoni mwa watu wengi, na wanaupokezana na baadhi yao wakausadiki. Basi kwa sababu hii, niliona kwamba ni lazima juu ya watu kama mimi kuandika juu yake ili kuelezea ubatili wake, na kwamba umetungwa dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ili mtu yeyote asidanganyike nao. Na mwenye kuutafakari miongoni mwa wale wenye elimu na imani, au wenye maumbile sahihi na ya kawaida, na akili timamu, atajua kwamba ni uongo na uzushi kwa njia nyingi.

Na niliuliza baadhi ya jamaa wa Sheikh Ahmad, ambaye anahusishwa uzushi huu, kuhusu wosia huu, na wakanijibu kwamba ni uongo juu ya Sheikh Ahmad, na kwamba hata hakuusema. Sheikh Ahmad aliyetajwa hapo juu alikufa kitambo, na hata kama tutachukulia kwamba Sheikh Ahmad aliyetajwa hapo juu, au yeyote yule aliyemzidi umri, alidai kuwa amemuona Mtume rehema na amani ziwe juu yake akiwa usingizini au akiwa macho, na akamuusia wosia huu, tungejua kwa hakika kwamba yeye ni muongo, au aliyemwambia hayo ni shetani, si Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, kwa njia nyingi, miongoni mwake zikiwa ni:

Kwanza: Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, hamuonekanii mtu akiwa macho baada ya kufa kwake. Kwa hivyo, mwenye kudai miongoni mwa Masufi wajinga kwamba anaweza kumuona Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akiwa macho, au kwamba anahudhuria katika sherehe za kuzaliwa kwake, au mambo mfano wa hayo, basi amekosea kosa baya zaidi, akachanganyikiwa sana, akaingia katika kosa kubwa, na akahalifu Kitabu, Sunnah na makubaliano ya wanachuoni. Kwa sababu, wafu watatoka makaburini mwao Siku ya Kiyama tu, si katika dunia hii. Na yeyote atakayesema kinyume na hivi, basi huyo ni muongo uongo ulio wazi, au amekosea na amechanganyikiwa, hakuijua haki ambayo wema waliotangulia waliijua, na wakaifuata Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na wale waliokuja baada yao na wale walio wafuata kwa wema. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:

﴿ثُمَّ إِنَّكُم بَعۡدَ ذَٰلِكَ لَمَيِّتُونَ15 ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ تُبْعَثُونَ16﴾

"Kisha hakika nyinyi baada ya hayo mtakufa."

Kisha hakika nyinyi Siku ya Kiyama mtafufuliwa. [Al-Muminun: 15-16] Na alisema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie: "Mimi ndiye wa kwanza ambaye kaburi lake litafunguka siku ya Kiyama, na mimi ndiye muombezi wa kwanza na wa kwanza atakayekubaliwa uombezi wake." Na kuna hadithi nyingi zenye maana hii.

Pili: Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, hasemi chochote kinyume na haki, si wakati wa uhai wake wala baada ya kifo chake. Na wasia huu unapingana kwa uwazi na Sheria yake, na hilo ni kwa mambo mengi yatakayokuja. Lakini Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, anaweza kuonekana usingizini. Na mwenye kumuona katika usingizi kama alivyo katika muonekano wake wa heshima, basi amemuona; kwa sababu Shetani hawezi kuchukua sura yake, kama lilivyoelezwa hilo katika hadithi sahihi tukufu, lakini jambo kubwa hapa ni juu ya imani ya muonaji, ukweli wake, uadilifu wake, uelewa wake mzuri, dini yake na uaminifu wake, na je alimuona Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake katika sura yake au katika sura nyingine.

Kama kungekuwa na Hadithi kutoka kwa Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake ambayo aliisema maishani mwake, kupitia njia ya wasimulizi waaminifu, waadilifu, wenye uelewa mzuri, hiyo isingewezakutegemewa, na wala haingetumiwa kama hoja, au ikiwa ingekuja kupitia njia ya wasimulizi waaminifu, wenye uelewa mzuri lakini ikawa inapingana na simulizi ya yule ambaye aliihifadhi bora kuliko wao, na ikawa na ukiukaji mkubwa ambao haiwezekani kuunganisha baina ya simulizi hizi mbiili, basi moja yake angechukuliwa kwama ilifutiliwa mbali ambayo haiwezi kufanyiwa kazi, nayo ya pili inakuwa ndiyo iliyofuta na ambayo inafaa kufanyiwa kazi, ikiwa hilo linawezekana kwa masharti yake. Lakini kama haiwezekani kuunganisha wala hakuna moja iliyofutilia mbali nyingine, inakuwa ni lazima kutupilia mbali simulizi ya yule ambaye ana uwezo mdogo wa kuhifadhi, na uadilifu mchache, na inahukumiwa kwamba imekengeuka na haifanyiwi kazi.

Basi utakuwa vipi wasia usiojulikana aliyeusimulia kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na hata haujulikani uadilifu wake? Katika hali hii, ni haki zaidi kuutupilia mbali na kutouangalia, hata kama hauna kitu ndani yake kinachohalifu Sheria. Basi itakuwaje ikiwa wasia huo unajumuisha mambo mengi yanayoashiria ubatili wake, na kwamba amesingiziwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, na unajumuisha kutunga sheria ya dini ambayo Mwenyezi Mungu hakuiidhinisha?

Na alisema Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Yeyote atakayesema juu yangu yale ambayo sikuyasema, basi na ajiandalie makazi yake Motoni." Na mzushi wa wasia huu alisema juu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, yale ambayo hakuyasema na akamdanganyishia uongo ulio wazi na hatari. Basi anafailia namna gani onyo hili kubwa la adhabu, na analistahiki namna gani; ikiwa hataharakisha kutubu, na kueneza kwa watu kwamba yaliyo katika wasia huu ni uongo dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake; kwa sababu yeyote anayeeneza batili miongoni mwa watu na kuuhusisha na dini; toba yake haitakuwa sahihi isipokuwa kwa kutangaza na kudhihirisha kinyume chake, ili watu wajue kwamba aliachana na uongo wake huo, na akabainisha kwamba yeye ni muongo, kwa mujibu wa maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿إِنَّ ٱلَّذِينَ يَكۡتُمُونَ مَآ أَنزَلۡنَا مِنَ ٱلۡبَيِّنَٰتِ وَٱلۡهُدَىٰ مِنۢ بَعۡدِ مَا بَيَّنَّٰهُ لِلنَّاسِ فِي ٱلۡكِتَٰبِ أُوْلَٰٓئِكَ يَلۡعَنُهُمُ ٱللَّهُ وَيَلۡعَنُهُمُ ٱللَّٰعِنُونَ159 إِلَّا ٱلَّذِينَ تَابُواْ وَأَصۡلَحُواْ وَبَيَّنُواْ فَأُوْلَٰٓئِكَ أَتُوبُ عَلَيۡهِمۡ وَأَنَا ٱلتَّوَّابُ ٱلرَّحِيمُ160﴾

"Hakika wale wanaoficha tuliyoyateremsha, nazo ni hoja zilizo wazi na uongofu baada ya Sisi kuzibainisha kwa watu Kitabuni, hao anawalaani Mwenyezi Mungu, na wanawalaani kila wenye kulaani."

Isipokuwa wale waliotubu na wakatengeneza na wakabainisha, basi hao nitapokea toba yao, na Mimi ni Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu." [Al-Baqarah: 159, 160] Katika aya hii tukufu, Mwenyezi Mungu Mtukufu akaweka wazi kwamba yeyote anayeficha chochote katika haki, toba yake juu ya hilo haitakuwa sahihi isipokuwa baada ya kurekebisha na kubainisha. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu alisha wakamilishia waja wake dini, na akawatimizia neema kwa kumtuma Mtume wake Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na Mwenyezi Mungu akamfunulia sheria kamili, na wala hakumfisha isipokuwa baada ya kuikamilisha na kuibainisha, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...ٱلۡيَوۡمَ أَكۡمَلۡتُ لَكُمۡ دِينَكُمۡ وَأَتۡمَمۡتُ عَلَيۡكُمۡ نِعۡمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ ٱلۡإِسۡلَٰمَ دِينٗا...﴾

"Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini." [Al-Maidah: 3]

Na yule aliyeuzua wosia huu alikuja katika karne ya kumi na nne, akitaka kuwavisha watu dini mpya, ambayo mwenye kuifuata sheria yake ndiye atakayeingia Peponi, na kunyimwa Pepo na kuingia Motoni kwa yule ambaye hatafuata sheria yake. Anataka kuufanya wosia huu aliouzua kuwa mkubwa na bora kuliko Qur'ani, ambapo alizua ndani yake kwamba: Yeyote atakayeuandika na kuutuma kutoka nchi hadi nchi, au kutoka mahali hadi mahali, atajengewa kasri Peponi. Na yeyote ambaye hatauandika na kuutuma, atanyimwa uombezi wa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, Siku ya Kiyama. Hilo ni katika uongo mbaya zaidi, na miongoni mwa dalili za wazi kabisa za uongo wa wosia huu, na uchache wa staha ya yule alieyuzua, na ukubwa wa ujasiri wake katika kusema uongo; kwa sababu mwenye kuandika Qur'ani Tukufu na kuituma kutoka nchi moja hadi nyingine, au kutoka sehemu moja hadi sehemu nyingine, hawezi kupata ubora huu ikiwa hataifanyia kazi Qur'ani Tukufu. Kwa hivyo anawezaje kumpata hilo mwandishi wa uzushi huu na mwenezaji wake kutoka nchi moja hadi nchi nyingine? Na asiyeiandika Qur'ani na kuituma kutoka nchi moja hadi nchi nyingine, hawezi kunyimwa uombezi wa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ikiwa ni Mumini anayefuata sheria yake. Uzushi huu mmoja katika wosia huu unatosha kuonyesha ubatili wake, uongo wa mchapishaji wake, upuuzi wake, na upumbavu wake, na umbali wake na suala la kujua yale aliyokuja nayo Mtume rehema na amani ziwe juu yake ya uongofu.

Na katika wasia huu, isipokuwa yale yaliyotajwa, kuna mambo mengine, ambayo yote yanaonyesha ubatili wake na uongo wake, hata kama mzushi wake ataapa viapo elfu moja au zaidi kwamba ni sahihi, na hata kama atadai kwamba atapata adhabu kubwa zaidi na mateso makali zaidi ili kuonyesha kwamba yeye ni mkweli, hawezi kuwa mkweli wala wasia huo hauwezi kuwa sahihi. Bali huo -ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, tena ninaapa kwa Mwenyezi Mungu- ni katika batili kubwa na mbaya zaidi. Nasi tunamshuhudisha Mwenyezi Mungu aliyetakasika na waliotuhudhuria miongoni mwa Malaika, na yeyote atakayeliona andiko hili miongoni mwa Waislamu -basi ni ushahidi ambao tutakutana nao mbele ya Mola wetu Mezi Mtukufu- kwamba wosia huu ni uongo na uzushi dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, Mwenyezi Mungu amfedheheshe huyu aliyeuzua na amtendee kile anachostahili.

Na kuna mambo mengi kando na haya tuliyotaja ambayo yanaonyesha uongo wa wasia huu na ubatili wake, ikiwa ni pamoja na:

Jambo la kwanza: Kauli yake ndani yake: "Kwa sababu kuanzia Ijumaa hadi Ijumaa, wamekufa watu laki moja na sitini si katika dini ya Kiislamu." Kwa sababu hili ni katika elimu ya ghaibu, na wahyi ulikatwa kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, baada ya kufa kwake, na tena hata katika uhai wake alikuwa hajui ghaibu, basi itakuwa vipi baada ya kufa kwake? Kama alivyosema Mwenyezi Mungu aliyetakasika:

﴿قُل لَّآ أَقُولُ لَكُمۡ عِندِي خَزَآئِنُ ٱللَّهِ وَلَآ أَعۡلَمُ ٱلۡغَيۡبَ...﴾

"Sema: Mimi sikwambiini kuwa ninazo hazina za Mwenyezi Mungu. Wala sijui mambo yaliyofichikana." [Al-An'am: 50] Na kauli yake Mtukufu:

﴿قُل لَّا يَعۡلَمُ مَن فِي ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضِ ٱلۡغَيۡبَ إِلَّا ٱللَّهُ...﴾

"Sema: Hapana katika mbingu na ardhi ajuaye ya ghaibu isipokuwa Mwenyezi Mungu." [An-Naml: 65] Na katika Hadithi sahihi kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: “Watu fulani watafukuzwa kwenye hodhi langu Siku ya Kiyama, kwa hivyo nitasema: 'Ewe Mola Mlezi! Ni Maswahaba wangu, ni Maswahaba wangu.' Nataambiwa: 'Hakika wewe hujui walichokizua baada yako.' Kwa hivyo, nitasema kama alivyosema mja mwema: "Na mimi nilikuwa shahidi juu yao nilipokuwa nao. Na uliponifisha, ukawa Wewe ndiye Mwangalizi juu yao. Na Wewe ni shahidi juu ya kila kitu." [Al-Ma'idah: 117].

Jambo la pili: Miongoni mwa mambo yanayoashiria ubatili wa wasia huu na kwamba ni uongo, ni kusema kwake ndani yake: "Atakayeuandika na alikuwa masikini, Mwenyezi Mungu atamtajirisha, au alikuwa na deni, Mwenyezi Mungu atamlipia deni lake, au alikuwa na dhambi, Mwenyezi Mungu atamsamehe yeye na wazazi wake kwa baraka ya wasia huu." hadi mwisho wake. Hili ni katika uongo mkubwa zaidi, na ushahidi wa wazi kabisa wa uongo wa mzushi wake, na uchache wa staha yake mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya waja wake. Kwa sababu mambo haya matatu hayatokei tu kwa kuandika Qur'ani Tukufu, kwa hivyo yanawezaje kutokea kwa mwenye kuandika wasia huu batili! Badala yake, mtu huyu muovu anataka kuwachanganya watu, na kuwafungamanisha na wosia huu, ili wauandike na wafungamane na fadhila hii inayodaiwa, na waache visababu ambavyo Mwenyezi Mungu aliwawekea waja wake katika sheria, na akavifanya kuwa njia ya kuwafikisha katika utajiri na kulipa madeni, na kupata msamaha wa dhambi. Basi tunajikinga kwa Mwenyezi Mungu kutokana na sababu za kuachiliwa mbali (na Mwenyezi Mungu) na kutii matamanio na Shetani.

Jambo la tatu: Katika mambo ambayo yanaonyesha ubatili wa wasia huo, ni kusema kwake ndani yake: "Na yeyote asiyeuandika katika waja wa Mwenyezi Mungu, uso wake utakuwa mweusi katika dunia hii na Akhera." Hili pia ni katika uongo mbaya zaidi, na katika ushahidi wa wazi kabisa wa ubatili wa wosia huo, na uongo wa mzushi wake. Inaruhusiwa vipi katika akili timamu ya mtu kuandika wosia huu uliotoka kwa mtu asiyejulikana katika karne ya kumi na nne, akiuzua dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake akidai kwamba yeyote asiyeuandika, uso wake utakuwa mweusi katika dunia hii na Akhera. Na yeyote atakayeuandika, atakuwa tajiri baada ya kuwa masikini, na atasalimika kutokana na deni baada ya kuwa na madeni mengi, na atasamehewa madhambi aliyotenda!!

Utakatifu ni wako (Mwenyezi Mungu)! Huu ni uzushi mkubwa!! Na hakika ushahidi na hali halisi vinashuhudia uongo wa mzushi huyu, na ukubwa wa ujasiri wake dhidi ya Mwenyezi Mungu, na uchache staha yake mbele ya Mwenyezu Mungu na mbele ya watu. Kwani kuna watu wengi sana ambao hawakuuandika, na nyuso zao hazikuwa nyeusi. Na kuna umati mkubwa wa watu ambao hakuna anayeweza kuwahesabu isipokuwa Mwenyezi Mungu tu waliuandika mara nyingi, lakini madeni yao hayakulipwa, na umaskini wao haukuisha. Kwa hivyo tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na ukengeufu wa mioyo na kutu ya madhambi. Sifa hizi na malipo haya (aliyoandika) hayakuja katika Sheria tukufu kwa mwenye kuandika kitabu bora na kitukufu zaidi ambacho ni Qur'ani Tukufu. Basi atayapataje mwenye kuandika wosia unaojumuisha aina mbalimbali za batili, na sentensi nyingi za aina za ukafiri. Mwenyezi Mungu ametakasika! Ni mstahamilivu namna gani kwa mwenye kumfanyia ujasiri wa kumzulia uongo!

Jambo la nne: Katika mambo ambayo yanaonyesha kwamba wasia huu ni batili kubwa zaidi na uongo ulio wazi zaidi ni kauli yake ndani yake: "Na yeyote atakaye uamini, ataokoka na adhabu ya Moto. Na yeyote atakayeukanusha, atakuwa amekufuru." Hili pia ni katika kufanya ujasiri sana katika kusema uongo, na ni katika batili mbaya zaidi. Mzushi huyu anawaita watu wote kuamini uzushi wake, na anadai kwamba kwa kufanya hivyo, wataepukana na adhabu ya Moto, na kwamba yeyote atakayeukanusha, atakuwa amekufuru. Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, hakika muongo huyu amemsingizia Mwenyezi Mungu vikubwa sana, na ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba alisema jambo ambalo si la kweli. Kwa sababu mwenye kuusadiki, yeye ndiye anayestahiki kuwa kafiri si mwenye kuu kadhibisha. Kwa sababu ni uzushi, batili na uongo usio na msingi sahihi. Tunamshuhudisha Mwenyezi Mungu kwamba ni uongo, na kwamba mzushi wake ni muongo ambaye anataka kuwawekea watu sheria ya yale ambayo Mwenyezi Mungu hakuyaruhusu, na kuingiza katika dini yao yale yasiyo ndani yake ilhali Mwenyezi Mungu ameshaukamilishilia umma huu dini kabla ya uzushi huu kwa karne kumi na nne. Basi kuweni macho enyi wasomaji na ndugu zangu, na jihadharini na kuamini mfano wa uzushi huu, na kuueneza baina yenu. Kwani haki ina nuru juu yake isiyomchanganya mwenye kuitafuta. Kwa hivyo, itafuteni haki kwa ushahidi wake, na waulizeni wenye elimu juu ya yale yenye kuwatatiza, wala msidanganyike na viapo vya waongo. Kwani Ibilisi aliyelaaniwa aliwaapia wazazi wenu wawili Adam na Hawa kwamba anawapa nasaha ya kweli, ihali yeye ndiye haini mkubwa zaidi na muongo wa waongo, kama alivyosimulia hilo Mwenyezi Mungu Mtukufu. Akasema Yeye aliyetakasika na kutukuka:

﴿وَقَاسَمَهُمَآ إِنِّي لَكُمَا لَمِنَ ٱلنَّٰصِحِينَ21﴾

"Naye akawaapia: Kwa yakini mimi ni miongoni wa wanaowashauri". [Al-A'raf: 21]

Basi jihadharini naye, na jihadharini na wafuasi wake miongoni mwa wazushi. Kwani wana viapo vingapi vya uongo, ahadi wanazohaini, na maneno yaliyopambwa ya kudanganya na kupotosha! Ama alichotaja mzushi huyu kuhusu kuibuka maovu. Hilo ni ukweli, na Qur’ani Tukufu na Sunna safi zimeonya dhidi yake vikali sana, na ndani yake kuna uongofu na utoshelevu.

Ama kuhusu yale yaliyotajwa kuhusu alama za Kiyama, Hadithi mbalimbali za kinabii zilishabainisha alama za Kiyama zitakazokuwa, na Qur’ani Tukufu pia ikaashiria baadhi yake . Kwa hivyo, anayetaka kuzijua, atazikuta katika mahali pake katika vitabu vya Sunna na maandiko ya watu wa elimu na imani. Watu hawana haja ya kuelezewa na mzushi kama huyo, kuwachanganya kwake na kuingiza kwake haki ndani ya uongo. Mwenyezi Mungu anilinde mimi, nyinyi na Waislamu wote kutokana na shari za mashetani, majaribu ya wapotoshaji, kukengeuka kwa waliokengeuka na kuchanganya kwa maadui wa Mwenyezi Mungu, wana batili wanaotaka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao na kuwachanganya watu kuhusiana na dini yao. Na Mwenyezi Mungu ataikamilisha nuru yake na kuinusuru dini yake, hata kama watachukia maadui wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa mashetani na wafuasi wao katika makafiri na wakataajimungu (wapagani).

Na tunamuomba Mwenyezi Mungu aziboreshe hali za Waislamu, na awaneemeshe kuifuata haki, kukaa imara juu yake na kutubia kwa Mwenyezi Mungu aliyetakasika kutokana na madhambi yote. Kwani Yeye ndiye Mwenye kupokea toba, Mwingi wa kurehemu na Muweza wa kila kitu. Mwenyezi Mungu ndiye anaye tutosha, naye ndiye Mtegemewa bora. Na hakuna uwezo wala nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu, aliye juu, Mkuu.

Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa viumbe vyote, na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wake na Mtume wake mkweli na mwaminifu, na juu ya familia yake, Maswahaba wake na wote wanaomfuata kwa wema mpaka Siku ya Malipo.

 

***

 


بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Makala ya tisa: Hukumu ya uchawi na ukuhani na yanayohusiana na mawili hayo18

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu peke yake, na rehema na amani ziwe juu ya yule ambaye hakuna Nabii baada yake. Ama baada ya hayo:

Kwa kuzingatia ongezeko la hivi karibuni la wachawi miongoni mwa wale wanaodai kuwa madaktari wanaotibu kwa njia ya uchawi au ukuhani, na kuenea kwao katika baadhi ya nchi, na kuwatumia kwao vibaya walio wajinga miongoni mwa watu ambao wengi wao mara nyingi hawana elimu, niliona, kama aina ya nasaha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na waja wake, kwamba nieleze hatari kubwa iliyo ndani ya hayo juu ya Uislamu na Waislamu, kwa sababu ya yale yaliyo ndani yake ya kujifungamanisha na asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kuhalifu amri yake na amri ya Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.

Kwa hivyo ninasema, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, kwamba inaruhusiwa kutafuta matibabu kulingana na makubaliano ya watu wote, na Muislamu anaweza kwenda kwa daktari wa magonjwa ya ndani, upasuaji, mishipa au mengineyo; ili ampime ugonjwa wake na kumtibu kwa dawa zinazofaa zinazoruhusiwa kwa mujibu wa sheria za Kiislamu, kulingana na anachojua katika elimu ya tiba. Kwa sababu hili linaingia katika mlango wa kuchukua visababu vya kawaida na wala halipingani na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu aliyetakasika, aliyetukuka aliteremsha ugonjwa na akateremsha dawa yake pamoja nao. Wanaijua wanaoijua (dawa hiyo) na hawaijui wasioijua. Hata hivyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu hakufanya ponya ya waja wake katika yale aliyo waharamishia.

Hivyo basi, mgonjwa haruhusiwi kwenda kwa wapiga ramli wanaodai kuwa wanajua mambo yaliyofichika ili kujua ugonjwa wake kutoka kwao, kama vile haruhusiwi kusadiki wanayomwambia, kwa sababu wanasema kwa kukisia tu mambo ya ghaibu, au wanawaleta majini ili wapate wanachotaka kwa msaada wao. Hawa hukumu yao ni kwamba wamekufuru na wamepotea ikiwa wanadai kuwa wanajua ghaibu.

Muslim amepokea katika Sahihi yake kwamba Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: "Atakayekwenda kwa mtabiri na akamuuliza jambo, swala zake hazitakubaliwa kwa siku arobaini."

 

 

"Atakayekwenda kwa kuhani (mchawi, mtabiri) na akasadiki anayoyasema, basi hakika ameshakufuru yale yaliyoteremshwa kwa Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake." Atakaye muendea kuhani na akamsadikisha kwa yale anayoyasema, basi hakika amekufuru yale yaliyoteremshwa kwa Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Imepokelewa na Abuu Daudi na pia wanazuoni wa vile Vitabu vinne vya Sunna, naye Al-Hakim akasema ni kwamba ni hadithi sahihi, kutoka kwa Nabii, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwa matamshi yafuatayo: “Atakayemuendea mpiga ramli au kuhani na akamsadikisha kwa yale anayoyasema, basi hakika ameshakufuru yale yaliyo teremshwa kwa Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.”

Na imesimuliwa kutoka kwa Imran bin Huswain, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, kwamba alisema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Si miongoni mwetu aathirikaye na vitu (kama vile ndege), au anaye fanyiwa hilo la kuathirika, au kuhani (mpiga ramli) au mwenye kupigiwa ramli, au mchawi, au mwenye kufanyiwa uchawi. Na atakayekwenda kwa kuhani na akasadiki anayosema, basi hakika ameshakufuru yale yaliyoteremshwa kwa Muhammad rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Imepokelewa na Al-Bazzaar kwa msururu mzuri wa wasimulizi.

Kwa hivyo, katika Hadithi hizi tukufu, kuna katazo la kwenda kwa wapiga ramli, makuhani, wachawi na mfano wao, na kuwauliza na kuwasadiki, na pia zina ahadi ya adhabu juu ya kufanya hivyo.

Kwa hivyo, hairuhusiwi kudanganyika na ukweli wao katika baadhi ya mambo, wala kwa wingi wa watu wanaowajia, kwani wao hawajui kitu na hairuhusiwi kwa watu kudanganyika nao. Kwa sababu Mtume -rehema na amani zimshukie- alikataza kuwaendea, kuwauliza na kuwasadikisha; kwa sababu katika hilo, kuna uovu mkubwa, hatari kubwa na matokeo mabaya zaidi, na kwa sababu wao ni waongo, waovu.

Hadithi hizi pia zina ushahidi wa kukufuru kwa kuhani (mtabiri) na mchawi, kwa sababu wanadai kuwa wanayajua mambo ya ghaibu, na hilo ni kufuru, na kwa sababu hawawezi kufikia lengo lao isipokuwa kwa kuwatumikia majini na kuwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, jambo ambalo ni kumkufuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumshirikisha. Na mwenye kuwasadiki katika yale wanayodai kwamba wanajua mambo ya ghaibu anakuwa kama wao. Na kila anayepokea mambo haya kutoka kwa mtu anaye yafanya, basi Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - yuko mbali sana naye.

Vile vile, Muislamu haruhusiwi kusalimu amri kwa wanachodai kuwa ni tiba, kama vile kuongea maneno yasiyoeleweka na kumimina risasi, na mengineyo miongoni mwa ushirikina wanaoufanya. Hayo yote ni katika ukuhani na kuwachanganya watu. Na mwenye kuyakubali hayo, basi hakika atakuwa amewasaidia katika batili yao na ukafiri wao.

Vile vile, hairuhusiwi kwa Muislamu yeyote kuwaendea ili kuwauliza kuhusu yule ambaye mtoto wake au jamaa yake atamuoa, au kuhusu mapenzi, uaminifu, uadui na utengano utakaokuwa baina ya wanandoa na familia yao, na mfano wa hayo. Kwa sababu hayo yote ni katika ghaibu ambayo haijui isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu tu.

Hivyo basi, la wajibu kwa watawala, watu wanao amrisha mema na kukataza maovu (Ahlul-Hisbah), na wengineo wenye uwezo na mamlaka, ni kukataza kwenda kwa wapiga ramli, watabiri na wengineo, na kumzuia yeyote anayejishughulisha na lolote katika hayo sokoni na kwingineko, na kuwakataza vikali zaidi, na kumkataza yeyote anayewaendea.

Vile vile uchawi. Kwani huo ni katika makatazo ya kikafiri, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mtukufu kuhusu wale Malaika wawili:

 

 

﴿...وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنۡ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَآ إِنَّمَا نَحۡنُ فِتۡنَةٞ فَلَا تَكۡفُرۡۖ فَيَتَعَلَّمُونَ مِنۡهُمَا مَا يُفَرِّقُونَ بِهِۦ بَيۡنَ ٱلۡمَرۡءِ وَزَوۡجِهِۦۚ وَمَا هُم بِضَآرِّينَ بِهِۦ مِنۡ أَحَدٍ إِلَّا بِإِذۡنِ ٱللَّهِۚ وَيَتَعَلَّمُونَ مَا يَضُرُّهُمۡ وَلَا يَنفَعُهُمۡۚ وَلَقَدۡ عَلِمُواْ لَمَنِ ٱشۡتَرَىٰهُ مَا لَهُۥ فِي ٱلۡأٓخِرَةِ مِنۡ خَلَٰقٖۚ وَلَبِئۡسَ مَا شَرَوۡاْ بِهِۦٓ أَنفُسَهُمۡۚ لَوۡ كَانُواْ يَعۡلَمُونَ﴾

"Wala hao hawakumfundisha yeyote mpaka wamwambie: "Hakika sisi ni mtihani; basi usikufuru." Wakajifunza kwa hao wawili yale ya kumtenganisha mtu na mkewe. Wala hawawezi kumdhuru mtu ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na wanajifunza yatakayo wadhuru wala hayawanufaishi. Na hakika wanajua kwamba aliyekhiari haya, hatakuwa na fungu lolote katika Akhera. Na hakika ni kiovu mno walichojiuzia nafsi zao laiti wangelijua." [Al-Baqara: 102].

Aya hizi tukufu zinaashiria kuwa uchawi ni ukafiri na kwamba wachawi wanamtenganisha mtu na mkewe. Pia zinaonyesha kwamba uchawi haufanyi kazi wenyewe tu, iwe ni kunufaisha au kudhuru. Bbali unafanya kazi kwa idhini ya Mwenyezi Mungu ya kiulimwengu na ya kimipango yake. Kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba heri na shari.

Aya hii tukufu pia inaashiria kwamba wale wanaoamiliana na uchawi wanaamiliana na yanayowadhuru na hayawanufaishi, na kwamba hawana fungu lolote kwa Mwenyezi Mungu. Na hii ni ahadi kubwa inayoashiria hasara yao kubwa hapa duniani na Akhera, na kwamba walijiuza wenyewe kwa thamani ya chini kabisa, na ndiyo maana Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka akawakashifu juu ya hilo kwa kauli yake:

﴿...وَلَبِئۡسَ مَا شَرَوۡاْ بِهِۦٓ أَنفُسَهُمۡۚ لَوۡ كَانُواْ يَعۡلَمُونَ﴾

"Na hakika ni kiovu mno walichojiuzia nafsi zao laiti wangelijua." [Al Baqara: 102] Neno 'shiraa' hapa linamaanisha kuuza.

Na hakika, madhara yamekuwa makubwa na hali imezidi kuwa mbaya kwa sababu ya hawa wazushi waliorithi elimu hizi kutoka kwa washirikina, na wakazitumia kuwachanganya wenye akili dhaifu. Basi sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake Yeye tutarejea. Na Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ndiye Mtegemewa bora zaidi.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuepushe na atupe salama kutokana na shari za wachawi, makuhani na walaghai wengineo wote. Pia tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awalinde Waislamu kutokana na uovu wao, na awawezeshe watawala wa Kiislamu kujihadhari nao na kutekeleza hukumu ya Mwenyezi Mungu juu yao; ili waja wapate nafuu kutokana na madhara yao na matendo yao machafu. Hakika, Yeye ndiye Mpaji, Mkarimu.

Na hakika, Mwenyezi Mungu Mtukufu amewawekea waja wake katika sheria, yale wanayoweza kujikinga kwayo shari ya uchawi kabla haujatokea, na akawaelezea cha kujitibu kwacho baada ya kutokea kwake, kama rehema yake na wema wake kwao na kuwakamilishia neema zake juu yao.

Yafuatayo ni maelezo ya mambo ambayo mtu anaweza kujikinga kwayo hatari ya uchawi kabla haujatokea na mambo anayoweza kujitibu kwayo baada ya kutokea kwake, miongoni mwa mambo yanayoruhusiwa kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu. Na maelezo yake ni kama ifuatavyo:

Kwanza: Yale yanayotumika katika kujilinda dhidi ya hatari ya uchawi kabla ya kutokea kwake. La muhimu na lenye manufaa zaidi katika hayo ni: Kujilinda kwa nyiradi za kisheria, dua mbalimbali, na mambo mbalimbali ya kujikinga kwayo, yaliyosimuliwa kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, ikiwa ni pamoja na kusoma Ayatul-Kursii - ambayo ndiyo aya kubwa zaidi katika Qur’ani Tukufu - baada ya kila swala iliyofaradhishwa baada ya salamu. Nayo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿ٱللَّهُ لَآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ٱلۡحَيُّ ٱلۡقَيُّومُۚ لَا تَأۡخُذُهُۥ سِنَةٞ وَلَا نَوۡمٞۚ لَّهُۥ مَا فِي ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَمَا فِي ٱلۡأَرۡضِۗ مَن ذَا ٱلَّذِي يَشۡفَعُ عِندَهُۥٓ إِلَّا بِإِذۡنِهِۦۚ يَعۡلَمُ مَا بَيۡنَ أَيۡدِيهِمۡ وَمَا خَلۡفَهُمۡۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيۡءٖ مِّنۡ عِلۡمِهِۦٓ إِلَّا بِمَا شَآءَۚ وَسِعَ كُرۡسِيُّهُ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَۖ وَلَا يَـُٔودُهُۥ حِفۡظُهُمَاۚ وَهُوَ ٱلۡعَلِيُّ ٱلۡعَظِيمُ255﴾

 

"Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye aliye Hai, Msimamia mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni vyake pekee vyote vilivyomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kufanya uombezi mbele yake bila ya idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui chochote katika vilivyo katika ujuzi wake, ila kwa atakalo mwenyewe. Mahali inapokanyaga miguu yake (Kursii) pametanda mbingu na dunia; na wala haemewi na kuvilinda viwili hivyo. Na Yeye ndiye aliye juu zaidi, Mkuu." [Al-Baqara: 255]. Na pia kuisoma wakati wa kulala. Kwani ilipokelewa kwa njia sahihi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani zimshukie, kwamba alisema: "Mwenye kusoma Ayatul-Kursi usiku, ataendelea kuwa na mlinzi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na hakuna shetani atakaye mkaribia mpaka afike asubuhi."

Na miongoni mwake ni kusoma:

﴿قُلۡ هُوَ ٱللَّهُ أَحَدٌ1﴾

"Sema: 'Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee'".

﴿قُلۡ أَعُوذُ بِرَبِّ ٱلۡفَلَقِ1﴾

"Sema: 'Ninajikinga kwa Mola Mlezi wa mapambazuko.'".

﴿قُلۡ أَعُوذُ بِرَبِّ ٱلنَّاسِ1﴾

"Sema: 'Ninajikinga kwa Mola Mlezi wa wanaadamu.'" [An-Nas: 1] Baada ya kila Swala ya lazima.

Pia azisome sura hizi tatu mara tatu tatu mwanzoni mwa mchana baada ya swala ya Alfajiri, na mwanzoni mwa usiku baada ya swala ya Maghrib.

Na miongoni mwake ni kusoma zile aya mbili za mwisho za Surat Al-Baqara mwanzoni mwa usiku, ambazo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿ءَامَنَ ٱلرَّسُولُ بِمَآ أُنزِلَ إِلَيۡهِ مِن رَّبِّهِۦ وَٱلۡمُؤۡمِنُونَۚ كُلٌّ ءَامَنَ بِٱللَّهِ وَمَلَٰٓئِكَتِهِۦ وَكُتُبِهِۦ وَرُسُلِهِۦ لَا نُفَرِّقُ بَيۡنَ أَحَدٖ مِّن رُّسُلِهِۦۚ وَقَالُواْ سَمِعۡنَا وَأَطَعۡنَاۖ غُفۡرَانَكَ رَبَّنَا وَإِلَيۡكَ ٱلۡمَصِيرُ285﴾

"Mtume ameamini yale yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake Mlezi, na Waumini vile vile. Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake na Mitume wake. Hatutofautishi baina ya yeyote katika Mitume wake, na (Waumini) husema: Tumesikia na tumetii. Tunakutaka maghfira Mola wetu Mlezi! Na marejeo ni kwako." Hadi mwisho wa sura.

Haya ni kwa sababu imepokelewa kwa njia sahihi kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba alisema: "Mwenye kusoma aya mbili za mwisho za Surat Al-Baqarah nyakati za usiku, zitamtosheleza." Maana yake - na Mwenyezi Mungu ndiye anayejua zaidi - ni kwamba zitamtosheleza kutokana na kila uovu. Na miongoni mwa hizo ni kujikinga kwa wingi kwa kusema: "Najilinda kwa maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyotimia kutokana na uovu wa alivyoviumba." usiku na mchana, na anapoingia katika mahali popote kama vile nyumbani, jangwani, hewani au baharini, kulingana na kauli ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Atakayeshuka mahala popote kisha akasema: 'A'udhu bikalimaati-llaahit-taammaati min sharri maa khalaqa (Ninajilinda kwa maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyotimia, kutokana na uovu wa vile alivyoviumba)', hakitomdhuru chochote mpaka atakapoondoka mahala pake hapo."

Na miongoni mwake ni Muislamu kusema mara tatu mwanzoni mwa mchana na mwanzo wa usiku: "Kwa jina la Mwenyezi Mungu ambaye hakuna chochote kinachoweza kudhuru pamoja na jina lake, ardhini wala mbinguni, naye ni Mwenye kusikia, ajuaye zaidi."

Kwa sababu kuna mahimizo sahihi juu ya hilo kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na kwamba hilo ni sababu ya kusalimika kutokana na madhara yote.

Pili: Yale yanayotumika kujitibu kwayo uchawi baada ya kutokea kwake. Hili pia linaweza kufanywa kwa mambo kadhaa:

 

 

La kwanza: Kuzidishia kumuomba Mwenyezi Mungu dua kwa unyenyekevu, na kumuomba Yeye aliyetakasika kuondoa madhara na dhiki hiyo.

Pili: Kufanya bidii kujua eneo la uchawi huo katika ardhi, mlima au sehemu nyingineyo. Basi utakapojulikana, ukatolewa na kuharibiwa, uchawi huo utabatilika. Hili ni miongoni mwa matibabu ya uchawi yenye manufaa zaidi.

Tatu: Kufanya ruqya pamoja na kusoma dhikri na nyiradi za kisheria ambazo ni nyingi. Miongoni mwa hizo ni:

Yale yaliyothibiti katika kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Ewe Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa watu, ondosha maumivu, na ponyesha. Wewe ndiye Mponyeshaji. Hakuna ponya ila ponya yako. Ponya isiyobakisha maradhi." Atayasema mara tatu.

Na miongoni mwake ni ruqya (dua mbalimbali) ambayo Jibril alimsomea Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Nazo ni kauli yake: "Kwa jina la Mwenyezi Mungu ninakusomea ruqya, kutokana na kila jambo linalokudhuru, na kutokana na kila nafsi au jicho la hasidi. Mwenyezi Mungu akuponye. Kwa jina la Mwenyezi Mungu, ninakusomea ruqya." Atayarudia haya mara tatu.

 

Na miongoni mwake - nayo ni tiba yenye manufaa kwa mwanamume aliyezuiliwa kumuingilia mke wake - ni kuchukua majani saba ya mkunazi wa kijani kibichi, kisha ayaponde kwa jiwe au kitu mfano wake, kisha ayaweke kwenye chombo na ayamiminie maji ya kumtosha kuoga, kisha asomee ndani yake:

Ayatul-Kursii

﴿قُلۡ يَٰٓأَيُّهَا ٱلۡكَٰفِرُونَ1﴾

"Sema: 'Enyi makafiri.'" [Al-Kaafiruun: 1], na

﴿قُلۡ هُوَ ٱللَّهُ أَحَدٌ1﴾

"Sema: 'Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee.'" [Al-Ikhlaas: 1], na

﴿قُلۡ أَعُوذُ بِرَبِّ ٱلۡفَلَقِ1﴾

"Sema: 'Ninajikinga kwa Mola Mlezi wa mapambazuko.'" [Al-Falaq: 1], na

﴿قُلۡ أَعُوذُ بِرَبِّ ٱلنَّاسِ1﴾

"Sema: 'Ninajikinga kwa Mola Mlezi wa wanadamu.'" [An-Nas: 1]

Na aya za uchawi zilizo katika Surat Al-A’raf. Nazo ni kauli ya Mwenyezi Mungu aliyetakasika:

﴿وَأَوۡحَيۡنَآ إِلَىٰ مُوسَىٰٓ أَنۡ أَلۡقِ عَصَاكَۖ فَإِذَا هِيَ تَلۡقَفُ مَا يَأۡفِكُونَ117 فَوَقَعَ ٱلۡحَقُّ وَبَطَلَ مَا كَانُواْ يَعۡمَلُونَ118 فَغُلِبُواْ هُنَالِكَ وَٱنقَلَبُواْ صَٰغِرِينَ119﴾

"Nasi tukamfunulia Musa kumwambia: Tupa fimbo yako. Mara ikavimeza vyote vile walivyovibuni. 117. Kweli ikathibiti na yakabatilika waliyokuwa wakiyatenda. 118. Kwa hivyo walishindwa hapo, na wakageuka kuwa wadogo."

Kweli ikathibiti na yakabat'ilika waliyo kuwa wakiyatenda.

Kwa hivyo walishindwa hapo, na wakageuka kuwa wadogo. [Al-A'raf: 117-119]

Na aya za Surat Yunus. Nazo ni maneno ya Mwenyezi Mungu aliyetakasika:

﴿وَقَالَ فِرۡعَوۡنُ ٱئۡتُونِي بِكُلِّ سَٰحِرٍ عَلِيمٖ79 فَلَمَّا جَآءَ ٱلسَّحَرَةُ قَالَ لَهُم مُّوسَىٰٓ أَلۡقُواْ مَآ أَنتُم مُّلۡقُونَ80 فَلَمَّآ أَلۡقَوۡاْ قَالَ مُوسَىٰ مَا جِئۡتُم بِهِ ٱلسِّحۡرُۖ إِنَّ ٱللَّهَ سَيُبۡطِلُهُۥٓ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يُصۡلِحُ عَمَلَ ٱلۡمُفۡسِدِينَ81 وَيُحِقُّ ٱللَّهُ ٱلۡحَقَّ بِكَلِمَٰتِهِۦ وَلَوۡ كَرِهَ ٱلۡمُجۡرِمُونَ82﴾

"Na Firauni akasema: Nileteeni kila mchawi mjuzi! 79. Basi walipokuja wachawi, Musa aliwaambia: Tupeni mnavyovitupa! 80. Walipotupa, Musa alisema: Mliyoleta ni uchawi. Hakika Mwenyezi Mungu haitengenezi kazi ya waharibifu. 81. Na Mwenyezi Mungu huhakikisha Haki kwa maneno yake, hata wangachukia wakosefu."

Basi walipo kuja wachawi, Musa aliwaambia: Tupeni mnavyo tupa! 80

Walipo tupa, Musa alisema: Mliyo leta ni uchawi. Hakika Mwenyezi Mungu haitengenezi kazi ya waharibifu.

Na Mwenyezi Mungu huhakikisha Haki kwa maneno yake, hata wanga chukia wakosefu [Yunus: 79-82],

Na aya zilizoko katika Surat Twaha:

﴿قَالُواْ يَٰمُوسَىٰٓ إِمَّآ أَن تُلۡقِيَ وَإِمَّآ أَن نَّكُونَ أَوَّلَ مَنۡ أَلۡقَىٰ65 قَالَ بَلۡ أَلۡقُواْۖ فَإِذَا حِبَالُهُمۡ وَعِصِيُّهُمۡ يُخَيَّلُ إِلَيۡهِ مِن سِحۡرِهِمۡ أَنَّهَا تَسۡعَىٰ66 فَأَوۡجَسَ فِي نَفۡسِهِۦ خِيفَةٗ مُّوسَىٰ67 قُلۡنَا لَا تَخَفۡ إِنَّكَ أَنتَ ٱلۡأَعۡلَىٰ68 وَأَلۡقِ مَا فِي يَمِينِكَ تَلۡقَفۡ مَا صَنَعُوٓاْۖ إِنَّمَا صَنَعُواْ كَيۡدُ سَٰحِرٖۖ وَلَا يُفۡلِحُ ٱلسَّاحِرُ حَيۡثُ أَتَىٰ69﴾

"Wakasema: 'Ewe Musa! Je, utatupa wewe, au tutakuwa sisi wa kwanza kutupa?' 65. Akasema: 'Bali tupeni nyinyi!' Tahamaki, kamba zao na fimbo zao zikaonekana mbele yake, kwa uchawi wao, kuwa zinakwenda mbio. 66. Basi Musa akaingia hofu nafsi yake. 67. Tukasema: 'Usihofu! Hakika wewe ndiwe utakayeshinda. 68. Na kitupe kilicho katika mkono wako wa kulia; kitavimeza walivyoviunda. Hakika walivyounda ni hila za mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote afikapo.'"

Akasema: Bali tupeni nyinyi! Tahamaki kamba zao na fimbo zao zikaonekana mbele yake, kwa uchawi wao, kuwa zinapiga mbio.

Basi Musa akaingia khofu nafsi yake.

Tukasema: Usikhofu! Hakika wewe ndiye utakaye shinda.

Na kitupe kilicho katika mkono wako wa kulia; kitavimeza walivyo viunda. Hakika walivyo unda ni hila za mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote afikapo. [Twaha: 65-69].

Baada ya kusomea ndani ya maji kile kilichotajwa, atakunywa kwayo midomo mitatu na aoge kwa yaliyosalia, na kwa hayo ugonjwa utaondoka, Mwenyezi Mungu akipenda. Ikiwa kuna haja ya kufanya hivyo mara mbili au zaidi, basi hakuna ubaya mpaka ugonjwa huo uishe.

Dhikri hizi, kijikinga huku na njia hizi, ni miongoni mwa sababu kubwa za kujiepusha na uovu wa uchawi na maovu mengineyo, na pia ni silaha kubwa zaidi ya kuondoa uchawi baada ya kutokea kwake; kwa wale wanaozidumisha kwa ukweli na imani, na kuwa na imani na Mweyezi Mungu, kumtegemea Yeye na kufunguka kwa kifua kwa yale ambayo mambo haya yanaashiria.

Haya ndiyo nimeweza kueleza miongoni mwa mambo yanayotumika kujilinda kwayo dhidi ya uchawi na kujitibu kwayo, na Mwenyezi Mungu ndiye Muwezeshaji.

Hapa linakuja suala muhimu, ambalo ni kutibu uchawi kwa mambo wanayofanya wachawi ambayo hutimia kwa njia ya kujikurubusha kwa majini kwa kuwachinjia au kitu kinginecho miongoni mwa mambo ya kujiweka karibu nao. Hili haliruhusiwi. Kwa sababu, ni katika matendo ya Shetani. Bali ni miongoni mwa ushirikina mkubwa. Pia hairuhusiwi kuutibu kwa kuwauliza makuhani, wapiga ramli na wachawi, na kutumia wanayoyasema. Na kwa sababu wao hawaamini, na kwa sababu ni waongo na waovu wanaodai kuwa wanayajua mambo ya ghaibu na huwahadaa watu. Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alionya dhidi ya kuwaendea, kuwauliza na kuwaamini, kama ilivyoelezwa hapo awali mwanzoni mwa makala hii. Kwa hivyo, la wajibu ni kujihadhari na hilo. Imepokelewa kwa njia sahihi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba aliulizwa kuhusu kutibu kwa kutumia uchawi. Akasema: "Hilo ni katika matendo ya Shetani." Imepokelewa na Imaam Ahmad na Abuu Daudi kwa msururu mzuri wa wasimulizi.

Annushra ni kuufungua uchawi kutoka kwa waliorogwa. Na annushra aliyomaanisha Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, hapa ni ile waliyokuwa wakifanya watu wa zama za ujinga, ambayo ni kumtaka mchawi kuufungua uchawi fulani, au kuufungua kwa uchawi mfano wake kutoka kwa mchawi mwingine.

Ama kuufungua uchawi kwa njia ya ruqya, kinga za kisheria na dawa zinazoruhusiwa, basi hakuna ubaya hakita hayo, kama ilivyotangulia kutajwa. Hayo yamesemwa moja kwa moja na mwanachuoni mkubwa Ibn al-Qayyim, na Sheikh Abdul-Rahman bin Hassan katika Fat-hul Majiid, Mwenyezi Mungu awarehemu wote wawili, na hili pia limesemwa moja kwa moja na wanachuoni wengineo.

Basi Mwenyezi Mungu ndiye aombwaye kuwawezesha Waislamu kufikia usalama kutokana na kila maovu, na kwamba awahifadhie dini yao, na awaruzuku kuifahamu na awaweke mbali na kila chenye kuhalifu sheria yake.

Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wake na Mtume wake, Mtume wetu Muhammad, na juu ya familia yake na Mawahaba wake wote.

 

***

 


بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Makala ya kumi: Kutahadharisha dhidi ya kujenga misikiti kwenye makaburi

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehema na amani ziwe juu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Ama baada ya hayo: Nimeona kile kilichochapishwa katika toleo la tatu la Jarida la Raabitwatul-Uluum Al-Islaamiyya katika mlango wa "Habari za Waislamu katika mwezi mmoja": 'Hakika Raabitwatul-Uluum Al-Islaamiyya katika Ufalme wa Kihashimi wa Yordani inakusudia kujenga msikiti kwenye pango jipya lililogunduliwa katika kijiji cha Ar-Rahiib, nalo ni pango ambalo linasemwa kuwa wale Watu wa pango waliotajwa katika Qur'ani Tukufu walilala humo.' Mwisho.

Kwa sababu ya wajibu wa kushauri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kuwashauri waja wake, niliona kwamba nielekeze neno katika jarida lenyewe la Raabitwatul-Uluum Al-Islaamiyya katika Ufalme wa Kihashimi wa Yordani likijumuisha nasaha kwa jumuiya hiyo dhidi ya kutekeleza kile ilichokusudia cha kujenga msikiti kwenye pango lililotajwa hapo juu. Na hilo si isipokuwa ni kwa sababu kujenga misikiti kwenye makaburi ya Manabii, watu wema na athari zao ni katika yale ambayo sheria kamili ya Kiislamu ilikuja kukataza na kuonya dhidi yake, na kumlaani mwenye kufanya hivyo; kwa sababu ni katika mambo ya ushirikina na kupitiliza kiasi kuhusiana na Manabii na watu wema. Hali halisi ya mambo ni ushahidi juu ya usahihi wa yale ambayo Sheria ilikuja nayo, na ni ushahidi kwamba yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, na ni uthibitisho wa wazi na hoja thabiti ya ukweli wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika yale aliyoyasema juu ya Mwenyezi Mungu na akaufikishia umma wake. Kila mtu anayezingatia hali ya ulimwengu wa Kiislamu na kile kilichotokea ndani yake cha ushirikina na kupitiliza kiasi kwa sababu ya kujenga misikiti juu ya makaburi na kuyatukuza, na kuyavika mavazi, kuyapamba, na kuyawekea wahudumu, kwa hakika atajua kwamba ni miongoni mwa njia za ushirikina, na kwamba katika mazuri ya sheria ya Kiislamu ni kuyazuia hayo na kuonya dhidi ya kuyajenga.

Na katika yale yaliyokuja kuhusiana na hilo ni yale yaliyosimuliwa na Masheikh wawili Bukhari na Muslim, Mwenyezi Mungu awarehemu, kutoka kwa Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, kwamba alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alisema: "Mwenyezi Mungu aliwalaani Mayahudi na Wakristo. Waliyafanya makaburi ya manabii wao kuwa misikiti." Aisha akasema, hapo alikuwa anaonya dhidi ya kile walichokifanya. Aisha akasema: Kama si kwa sababu ya hilo, basi wangeliweka wazi kaburi lake, lakini alihofia kwamba linaweza kufanywa msikiti. Na katika Sahihi mbili pia kuna kwamba "Ummu Salama na Ummu Habiba, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, walimueleza Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kanisa waliloliona katika ardhi ya Uhabeshi (Ethiopia), na picha zilizokuwa ndani yake. Basi Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake akasema: "Hao pindi mtu mwema miongoni mwao anapokufa, wanajenga msikiti juu ya kaburi lake, na kuchora picha hizo ndani yake. Hao ndio viumbe waovu mbele ya Mwenyezi Mungu."

Na katika Sahihi Muslim, Jundab bin Abdillah, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, alisema: Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, siku tano kabla ya kufa kwake, akisema: "Hakika mimi ninakimbilia kwa Mwenyezi Mungu kwamba nisijekuwa na rafiki mwendani miongoni mwenu. Kwani Mwenyezi Mungu amenifanya mimi kuwa mwendani kama alivyomfanya Ibrahim kuwa mwendani. Na lau kama ningekuwa wa kujifanyia mwendani katika umma wangu, basi ningemfanya Abubakari kuwa mwendani wangu. Fahamuni kuwa hakika wale waliokuwa kabla yenu walikuwa waki yafanya makaburi ya Manabii wao kuwa Misikiti. Tambueni kuwa, msiyafanye makaburi kuwa Misikiti, kwani hakika mimi ninakukatazeni hilo." Na Aya na hadithi katika mlango huu ni nyingi.

Na maimamu wengi miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu kutoka katika madhehebu yote manne na mengineyo walisema kwamba misikiti isijengwe juu ya makaburi, na wakaonya dhidi ya hili, kwa mujibu wa Sunnah ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na kwa njia ya kunasihi umma na kuuonya usije ukaanguka katika upotofu ambao wale waliokuwa kabla ya umma huu walianguka ndani yake miongoni mwa Wayahudi na Wakristo.

Kwa hivyo, la wajibu juu ya Jumuiya ya Al-Uluum Al-Islaamiyya ya huko Yordani, na Waislamu wengine wote ni kufuata Sunnah, kufuata njia ya Maimamu, na kutahadhari yale ambayo Mwenyezi Mungu na Mtume wake wametahadharisha. Kwani katika hilo kuna kutengenea kwa waja, furaha yao na kuokoka kwao duniani na akhera. Na baadhi ya watu katika mlango huu walishikamana na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kuhusiana na kisa cha wale Watu wa Pangoni:

﴿...قَالَ ٱلَّذِينَ غَلَبُواْ عَلَىٰٓ أَمۡرِهِمۡ لَنَتَّخِذَنَّ عَلَيۡهِم مَّسۡجِدٗا﴾

"Wakasema wale walioshinda katika shauri lao: Bila ya shaka tutawajengea msikiti juu yao." [Al-Kahf: 21]

 

 

Jibu la hilo ni kusema kwamba: Mwenyezi Mungu Mtukufu alieleza kuhusu viongozi na watu wenye udhibiti wa Mamlaka wakati huo kuwa walisema maneno haya, lakini hilo si kwamba Mwenyezi Mungu aliridhia maneno yao hayo na kuyakubali. Bali aliyasema kwa njia ya kashifa, kuonyesha kasoro yake, na kuwaweka watu mbali na kitendo chao hicho. Hili linathibitishwa na ukweli kwamba Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ambaye aya hii iliteremshwa juu yake, na ambaye ndiye mjuzi wa tafsiri yake zaidi ya watu wote alikataza umma wake kujenga misikiti juu ya makaburi, na akawaonya juu ya hili na kuwalaani na kuwakashifu wale wanaofanya hivyo.

Lau kuwa hilo lingekuwa linaruhusiwa, basi Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani zimshukie, asingekuwa mkali kiasi hicho kikubwa, na akakwenda mbali zaidi katika hilo hadi kumlaani anayefanya hivyo, na akajulisha kwamba wao ni miongoni mwa viumbe waovu mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na hili linamtosha na kumridhisha mtafutaji haki. Na hata kama tungekubali kwamba kujenga misikiti juu ya makaburi kuliruhusika kwa wale waliotangulia kabla yetu, hilo halingeruhusiwa kwetu kuwafuata katika suala hili. Kwa sababu, sheria yetu inafuta sheria zilizotangulia, na Mtume wetu, rehema na amani ziwe juu yake, ndiye mwisho wa Mitume, na sheria yake ni kamilifu na ya ujumla. Naye alitukataza kujenga misikiti juu ya makaburi. Kwa hivyo, haturuhusiwi kumhalifu, na tunalazimika kumfuata, kushikamana na kile alichokuja nacho, na kuacha kile kinachohalifu hilo katika sheria za zamani, na desturi zinazopendekezwa tu na wale wanaozifanya, kwa sababu hakuna kilicho kamili zaidi kuliko sheria ya Mwenyezi Mungu, wala hakuna muongozo mzuri zaidi kuliko muongozo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.

Na Mwenyezi Mungu ndiye aombwaye atuwezeshe sisi na Waislamu wote kuwa imara katika dini yake, na kushikamana na sheria ya Mtume wake Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake; katika maneno na vitendo, kwa nje na ndani, na katika mambo mengine yote mpaka tutakapokutana na Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Aliye karibu mno.

Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wake na Mtume wake Muhammad, jamaa zake na Maswahaba wake, na wale wanaofuata muongozo wake mpaka Siku ya Malipo.

 

***

 

 

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Makala ya kumi na moja: Kuzika wafu misikitini

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehema na amani zimshukie Mtume wa Mwenyezi Mungu, na ali zake, na wote wanaofuata muongozo wake. Ama baada ya hayo:

Nilisona gazeti la "Al-Khartum" lililotolewa mnamo 17/4/1415 Hijria, na nikapata yamechapishwa humo maelezo ya kumzika bwana Muhammad Al-Hasan Al-Idrisii karibu na baba yake katika msikiti wao katika mji wa Umdurman... n.k.

Mwenyezi Mungu alipowajibisha kuwapa nasaha Waislamu, na kuweka wazi kukanusha kwa mwenye kukanusha, niliona kwamba nitahadharishe ya kuwa kuwazika maiti katika misikiti ni jambo lisiloruhusiwa. Bali ni katika njia za ushirikina, na ni katika matendo ya Mayahudi na Wakristo ambayo Mwenyezi Mungu aliwakemea kwa sababu yake, na Mtume wake, rehema na amani ziwe juu yake, aliwalaani, kama ilivyokuja katika Sahihi mbili kutoka kwa Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, kwamba alisema: "Mwenyezi Mungu aliwalaani Mayahudi na Wakristo. Waliyafanya makaburi ya manabii wao kuwa misikiti." Na katika Sahihi Muslim, kutoka kwa Jundab bin Abdullah, kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alisema: "Sikilizeni! Hakika wale waliokuwa kabla yenu walikuwa wakifanya makaburi ya manabii wao na wema wao kuwa misikiti. Sikilizeni! Msiyafanye makaburi kuwa misikiti. Kwani ninakukatazeni hilo?" Na kuna hadithi nyingi zenye maana hii.

Basi la wajibu kwa Waislamu kila mahali -kuanzia serikali na raia -ni kumcha Mwenyezi Mungu, na kujihadhari na yale aliyoyakataza, na wawazike wafu wao nje ya misikiti, kama Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, na Maswahaba wake walivyokuwa wakiwazika wafu nje ya misikiti, na vile vile wale waliokuja baada yao na kuwafuata kwa wema.

Na ama kupatikana kwa kaburi la Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, katika msikiti wake, na pia kupatikana humo makaburi ya Maswahaba wake wawili, Abubakari na Omari, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao, hilo si hoja ya kuwazika maiti katika misikiti. Kwa sababu yeye, rehema na amani ziwe juu yake, alizikwa ndani ya nyumba yake - katika nyumba ya Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie - kisha Maswahaba wake hao wawili wakazikwa pamoja naye. Wakati Al-Walid bin 'Abdul-Malik alipoupanua msikiti wa Mtume, akaiingiza nyumba yake (Mtume) ndani ya msikiti baada ya miaka mia moja ya kwanza ya Hijiria. Wanazuoni walimpinga kwa hilo, lakini yeye aliona kuwa hilo haliwezi kuzuia upanuzi, na kwamba jambo hilo lilikuwa wazi na haliwezi kumchanganya yeyote.

Kwa hayo, inadhihirika wazi kwa kila Muislamu kwamba yeye, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na Maswahaba wake wawili, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, hawakuzikwa msikitini. Kuingizwa kwao humo kwa sababu ya upanuzi sio hoja ya kuruhusu kuzika katika misikiti; kwa sababu hawako msikitini, bali wako nyumbani kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake. Na kwa sababu matendo ya Al-Walid hayawezi kuwa hoja ya mtu yeyote katika hilo. Bali hoja iko katika Kitabu na Sunna, na katika makubaliano ya watangulizi wema wa umma huu, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, na atujaalie kuwa miongoni mwa wafuasi wao kwa wema.

Kwa ajili ya Nasaha na kuondoa dhima, imeandikwa barua hii mnamo: 14/5/1415 Hijiria.

Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuafikisha, na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad, jamaa zake, na Maswahaba wake, na wafuasi wao kwa wema.

 

***

 


بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Makala ya Kumi na Mbili: Kubainisha ukafiri na upotofu wa anayedai kuwa inaruhusiwa kwa yeyote kutoka katika Sheria ya Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote, na rehema na amani ziwe juu ya mwisho wa Manabii na Mitume, Nabii wetu Muhammad, na familia yake na Maswahaba wake wote.

Ama baada ya hayo: Nilisoma makala iliyochapishwa katika jarida la Ash-Sharq Al-Awsat nambari (5824) ya tarehe 5/6/1415 Hijria, ilioandikwa na anayejiita: Abdul-Fattah Al-Haaiki, kwa anwani: (Ufahamu usio sahihi).

Na muhtasari wa makala yenyewe ni kukataa kwake kile kinachojulikana katika dini ya Uislamu bila ya shaka yoyote, na kwa maandiko (matakatifu) na makubaliano ya wanazuoni; ambacho ndiyo ujumla wa ujumbe wa Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake, kwa watu wote, na madai yake kwamba yeyote ambaye hakumfuata Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na hakumtii, lakini akabakia katika Uyahudi au Ukristo, yuko katika dini ya haki, kisha akamfanyia kiburi Mola wa walimwengu wote -Aliyetakasika- kuhusiana na hekima yake katika kuwaadhibu makafiri na waasi, yeye akaona kwamba hilo ni mchezo mtupu.

Aliyapotosha maandiko ya dini, akayaweka katika sehemu zisizokuwa zake, na akayafasiri kama yanavyotaka matakwa yake, na akapuuza ushahidi wa kisheria na maandiko ya wazi yanayoonyesha ujumla wa utume wa Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake, na ukafiri wa anayesikia habari zake kisha asimfuate, na kwamba hakika Mwenyezi Mungu hatakubali dini nyingine isipokuwa Uislamu, na maandiko mengine ya wazi ambayo nimeyaacha. Alifanya hivi ili wajinga wadanganyike na maneno yake. Hiki alichokifanya ni ukafiri wa wazi, kutoka katika Uislamu, na kumkanusha Mwenyezi Mungu aliyetakasika, aliyetukuka, na pia Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kama anavyojua hayo anayesoma makala hiyo miongoni mwa watu wenye elimu na imani.

Basi la wajibu kwa kiongozi mkuu ni kumpeleka mahakamani, kumtaka atubu na kumhukumu kulingana na inavyotakiwa na Sheria safi.

Mwenyezi Mungu Mtukufu aliuweka wazi ujumbe wa ujumla wa Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake, na wajibu wa kumfuata kwa viumbe wazito wawili (majini na watu), na hili hakosi kulijua mtu yeyote mwenye elimu hata chache tu miongoni mwa Waislamu.

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿قُلۡ يَٰٓأَيُّهَا ٱلنَّاسُ إِنِّي رَسُولُ ٱللَّهِ إِلَيۡكُمۡ جَمِيعًا ٱلَّذِي لَهُۥ مُلۡكُ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضِۖ لَآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ يُحۡيِۦ وَيُمِيتُۖ فَـَٔامِنُواْ بِٱللَّهِ وَرَسُولِهِ ٱلنَّبِيِّ ٱلۡأُمِّيِّ ٱلَّذِي يُؤۡمِنُ بِٱللَّهِ وَكَلِمَٰتِهِۦ وَٱتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمۡ تَهۡتَدُونَ158﴾

"Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume kwenu nyinyi nyote, niliyetumwa na Mwenyezi Mungu Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Hapana mungu ila Yeye anayehuisha na anayefisha. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake asiyejua kusoma na kuandika, ambaye anamuamini Mwenyezi Mungu na maneno yake. Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka." [Al-A'raaf: 158] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...وَأُوحِيَ إِلَيَّ هَٰذَا ٱلۡقُرۡءَانُ لِأُنذِرَكُم بِهِۦ وَمَنۢ بَلَغَ...﴾

"Na nimefunuliwa Qur'ani hii ili kwayo nikuonyeni nyinyi na kila inayemfikia." [Al-An-aam: 19] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿قُلۡ إِن كُنتُمۡ تُحِبُّونَ ٱللَّهَ فَٱتَّبِعُونِي يُحۡبِبۡكُمُ ٱللَّهُ وَيَغۡفِرۡ لَكُمۡ ذُنُوبَكُمۡۚ وَٱللَّهُ غَفُورٞ رَّحِيمٞ31﴾

"Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu." [Al-'Imran: 31] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمَن يَبۡتَغِ غَيۡرَ ٱلۡإِسۡلَٰمِ دِينٗا فَلَن يُقۡبَلَ مِنۡهُ وَهُوَ فِي ٱلۡأٓخِرَةِ مِنَ ٱلۡخَٰسِرِينَ85﴾

"Na anayetafuta dini isiyokuwa Uislamu, haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa miongoni mwa wenye kupata hasara." [Al-Imran: 85] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمَآ أَرۡسَلۡنَٰكَ إِلَّا كَآفَّةٗ لِّلنَّاسِ بَشِيرٗا وَنَذِيرٗا...﴾

"Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mbashiri na muonyaji." [Saba: 28] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمَآ أَرۡسَلۡنَٰكَ إِلَّا رَحۡمَةٗ لِّلۡعَٰلَمِينَ107﴾

"Nasi hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu wote." [Al-Anbiya: 107]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...وَقُل لِّلَّذِينَ أُوتُواْ ٱلۡكِتَٰبَ وَٱلۡأُمِّيِّـۧنَ ءَأَسۡلَمۡتُمۡۚ فَإِنۡ أَسۡلَمُواْ فَقَدِ ٱهۡتَدَواْۖ وَّإِن تَوَلَّوۡاْ فَإِنَّمَا عَلَيۡكَ ٱلۡبَلَٰغُۗ وَٱللَّهُ بَصِيرُۢ بِٱلۡعِبَادِ﴾

"Na waambie wale waliopewa Kitabu na wale wasio na kisomo: 'Je, mmesilimu?' Wakisilimu, basi wameongoka. Na wakikengeuka, basi juu yako ni kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake." [Al-'Imran: 20]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 

﴿تَبَارَكَ ٱلَّذِي نَزَّلَ ٱلۡفُرۡقَانَ عَلَىٰ عَبۡدِهِۦ لِيَكُونَ لِلۡعَٰلَمِينَ نَذِيرًا1﴾

"Ametukuka aliyeteremsha Furqani (Qur'ani) kwa mja wake, ili awe muonyaji kwa walimwengu wote." [Al-Furqan: 1].

Na wamesimulia Bukhari na Muslim, kutoka kwa Jabir radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: "Nilipewa vitu vitano ambavyo hakuna mtu mwingine aliyepewa hivyo kabla yangu: Nimenusuriwa kwa hofu kwa safari ya mwezi mmoja. Na nilifanyiwa ardhi kuwa msikiti na safi, kwa hivyo mtu yeyote katika umma wangu atakayepatwa na wakati wa swala mahali popote, basi na aswali. Na nilihalalishiwa ngawira, na hakuna mtu yeyote aliye halalishiwa hizo kabla yangu. Na nimepewa uombezi (mkuu). Na Nabii alikuwa akitumwa kwa watu wake hasa, nami nilitumwa kwa watu kwa wote."

Huku ni kubainisha kwa wazi kwa ujumla wa utume wa Mtume wetu Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwa wanadamu wote, na kwamba ulifutilia mbali sheria zote zilizotangulia, na kwamba yeyote ambaye hamfuati Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na hamtii, basi yeye ni kafiri muasi, anayestahili kuadhibiwa. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 

﴿...وَمَن يَكۡفُرۡ بِهِۦ مِنَ ٱلۡأَحۡزَابِ فَٱلنَّارُ مَوۡعِدُهُۥ...﴾

"Na anayemkufuru katika makundi, basi Moto ndio pahala pa miadi yake." [Hud: 17]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...فَلۡيَحۡذَرِ ٱلَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنۡ أَمۡرِهِۦٓ أَن تُصِيبَهُمۡ فِتۡنَةٌ أَوۡ يُصِيبَهُمۡ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴾

"Basi na watahadhari wanaohalifu (kwenda kinyume na) amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu chungu). [An-Nur: 63] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمَن يَعۡصِ ٱللَّهَ وَرَسُولَهُۥ وَيَتَعَدَّ حُدُودَهُۥ يُدۡخِلۡهُ نَارًا خَٰلِدٗا فِيهَا وَلَهُۥ عَذَابٞ مُّهِينٞ14﴾

"Na anayemuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akaipindukia mipaka yake, (Mwenyezi Mungu) atamtia Motoni adumu humo, na atapata adhabu ya kudhalilisha." [An-Nisaa: 14] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...وَمَن يَتَبَدَّلِ ٱلۡكُفۡرَ بِٱلۡإِيمَٰنِ فَقَدۡ ضَلَّ سَوَآءَ ٱلسَّبِيلِ﴾

"Na anayebadilisha Imani kwa ukafiri, bila ya shaka huyo amepotea njia iliyo sawa). [Al-Baqarah: 108] Na aya zenye maana hii ni nyingi sana.

 

 

Mwenyezi Mungu Mtukufu ameunganisha kumtii Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, pamoja na kumtii Yeye, na akaeleza wazi kwamba yeyote anayeamini kinyume cha Uislamu, basi amepata hasara, na hatakubali kutoka kwake malipo yoyote wala fidia. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمَنْ يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَنْ يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ 85﴾

"Na anayetafuta dini isiyokuwa Uislamu, haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa miongoni mwa wenye kupata hasara." [Al-Imran: 85] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿مَنْ يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّهَ...﴾

"Mwenye kumtii Mtume, basi atakuwa amemtii Mwenyezi Mungu." [An-Nisaa: 80] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿قُلْ أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ فَإِنْ تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُمْ مَا حُمِّلْتُمْ وَإِنْ تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا...﴾

"Sema: Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume. Na mkigeuka, basi yaliyo juu yake ni aliyobebeshwa, na yaliyo juu yenu ni mliyobebeshwa nyinyi. Na mkimtii yeye, mtaongoka." [An-Nur: 54] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَالْمُشْرِكِينَ فِي نَارِ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا أُولَئِكَ هُمْ شَرُّ الْبَرِيَّةِ 6﴾

"Hakika wale waliokufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu na washirikina wataingia katika Moto wa Jahannamu wadumu milele humo. Hao ndio viumbe waovu kabisa." [Al-Bayyina: 6].

Na Muslim alipokea katika Sahihi yake kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: "Ninaapa kwa yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake. Hakuna yeyote katika umma huu atakayenisikia mimi sawa awe ni Myahudi au Mkristo, kisha akafa bila ya kuamini yale niliyotumwa nayo isipokuwa atakuwa katika watu wa Motoni."

Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe juu yake aliweka wazi kwa vitendo vyake na maneno yake ubatili wa dini ya wale ambao hawakuingia katika Uislamu; kwani alipigana vita na Mayahudi na Wakristo, kama vile alivyopigana na makafiri wengineo, na akachukua kodi ya ulinzi (jizia) kwa wale waliompa ili wasizuie wito wa Uislamu kuwafikia wengine zaidi yao, na ili miongoni mwao waingie katika Uislamu wale wanaotaka kufanya hivyo bila ya kuwaogopa watu wake kuwazuia au kuwaua.

 

Bukhari na Muslim walisimulia kutoka kwa Abuu Huraira, Mwenyezi Mungu amridhie, kwamba alisema: Tulipokuwa msikitini, Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alitoka nje na akasema: "Nendeni kwa Mayahudi." Basi tukatoka pamoja naye mpaka tukafika katika nyumba ya mafunzo (chuo cha mafunzo), na Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akasimama na kuwaita akisema: "Enyi kundi la Wayahudi, silimuni, mtasalimika." Wakasema: 'Umeshafikisha, ewe Abul-Qasim.' Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akawaambia: "Hicho ndicho ninachotaka, silimuni, mtasalimika." Wakasema: 'Umeshafikisha, ewe Abul-Qasim.' Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akawaambia: "Hicho ndicho ninachotaka." Kisha akayasema mara ya tatu..." hadi mwisho wa Hadithi.

Kinachokusudiwa ni kwamba Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alienda kwa watu wenye dini miongoni mwa Wayahudi katika nyumba yao ya mafunzo, kisha akawalingania kwenye Uislamu, na akawaambia: "Silimuni, mtasalimika." na akarudia kuwaambia hayo mara kadhaa.

Vile vile, alituma barua yake kwa Hiraqli huku akimuita kwenye Uislamu, na kumfahamisha kwamba akikataa, basi atabeba dhambi za wale walioukataa Uislamu kwa sababu ya kukataa kwake kusilimu. Bukhari na Muslim walisimulia katika Sahihi zao kwamba: Hiraqli aliitisha barua ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na akaisoma, na tazama, ndani yake kulikuwa: "Bismillahir Rahmanir Rahiim. Kutoka kwa Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwenda kwa Hiraqli, mkuu wa Warumi. Amani iwe juu ya mwenye kufuata uongofu. Ama baada ya kusema hayo: Kwa hakika, mimi ninakuita kwa wito wa Uislamu. Silimu, utasalimika. Na silimu, Mwenyezi Mungu atakupa malipo yako mara mbili. Na ikiwa utapeana mgongo, basi yatakuwa juu yako madhambi ya wakulima wa huko."

﴿يَٰٓأَهۡلَ ٱلۡكِتَٰبِ تَعَالَوۡاْ إِلَىٰ كَلِمَةٖ سَوَآءِۭ بَيۡنَنَا وَبَيۡنَكُمۡ أَلَّا نَعۡبُدَ إِلَّا ٱللَّهَ وَلَا نُشۡرِكَ بِهِۦ شَيۡـٔٗا وَلَا يَتَّخِذَ بَعۡضُنَا بَعۡضًا أَرۡبَابٗا مِّن دُونِ ٱللَّهِۚ فَإِن تَوَلَّوۡاْ فَقُولُواْ ٱشۡهَدُواْ بِأَنَّا مُسۡلِمُونَ64﴾

"Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lililo sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Miungu Walezi badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka, basi semeni: Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu." [Al-'Imran: 64].

 

 

Kisha, walipogeuka na wakakataa kuingia katika Uislamu, Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akawapiga vita yeye na Maswahaba wake, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, na akawatoza kodi (jizya).

Na ili kusisitiza upotovu wao na kwamba wako kwenye dini batili baada ya kufutwa na dini ya Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, Mwenyezi Mungu akamuamrisha Muislamu kumuomba Mwenyezi Mungu kila siku, katika kila swala na katika kila rakaa kwamba amuongoze kwenye njia iliyonyooka iliyo sahihi inayokubalika, ambayo ni Uislamu. Na kwamba amuokoe kutokana na njia ya wale aliowakasirikia, yaani Wayahudi na mfano wao ambao wanajua kwamba wako katika batili lakini wanasisitiza kusalia juu yake. Na kwamba amuepushe na njia ya wale waliopotea, wanaoabudu bila ya elimu, na wanadai kwamba wako kwenye njia ya uongofu ilhali wako kwenye njia ya upotofu, yaani Wakristo, na wengineo wanaofanana nao miongoni mwa umma mwingine ambao wanaabudu kwa upotofu na ujinga. Haya yote ni ili Muislamu ajue kwa uhakika kwamba kila dini isiyokuwa ya Kiislamu ni batili, na kwamba kila anayemuabudu Mwenyezi Mungu si kwa Uislamu, ni mpotofu. Na asiyeamini hivi, basi yeye si katika Waislamu. Na ushahidi katika mlango huu ni mwingi katika Kitabu na Sunna.

Basi la wajibu kwa mwandishi wa makala hayo 'Abdul-Fattaah, ni kuharakisha kutubu kisawasawa, na kwamba aandike makala ambayo atatangaza ndani yake toba yake, na mwenye kutubia kwa Mwenyezi Mungu kwa dhati, Mwenyezi Mungu atamsamehe; kwa kauli ya Mwenyezi Mungu aliyetakasika:

﴿...وَتُوبُوٓاْ إِلَى ٱللَّهِ جَمِيعًا أَيُّهَ ٱلۡمُؤۡمِنُونَ لَعَلَّكُمۡ تُفۡلِحُونَ﴾

"Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa". [Surat An-Nur: 31] Na kauli yake Mtukufu:

﴿وَٱلَّذِينَ لَا يَدۡعُونَ مَعَ ٱللَّهِ إِلَٰهًا ءَاخَرَ وَلَا يَقۡتُلُونَ ٱلنَّفۡسَ ٱلَّتِي حَرَّمَ ٱللَّهُ إِلَّا بِٱلۡحَقِّ وَلَا يَزۡنُونَۚ وَمَن يَفۡعَلۡ ذَٰلِكَ يَلۡقَ أَثَامٗا68 يُضَٰعَفۡ لَهُ ٱلۡعَذَابُ يَوۡمَ ٱلۡقِيَٰمَةِ وَيَخۡلُدۡ فِيهِۦ مُهَانًا69 إِلَّا مَن تَابَ وَءَامَنَ وَعَمِلَ عَمَلٗا صَٰلِحٗا فَأُوْلَٰٓئِكَ يُبَدِّلُ ٱللَّهُ سَيِّـَٔاتِهِمۡ حَسَنَٰتٖۗ وَكَانَ ٱللَّهُ غَفُورٗا رَّحِيمٗا70﴾

"Na wale wasiomuomba mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyoiharimisha Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa haki, wala hawazini. Na atakayefanya hayo, atapata madhara.

Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo akifedheheshwa."

Isipokuwa atakayetubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu". [Al-Furqan: 68-70].

Na kwa kauli ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Uislamu unabomoa yaliyokuwa kabla yake, na toba inabomoa yaliyokuwa kabla yake." Na kauli yake Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie: "Mwenye kutubia dhambi, ni kama asiyekuwa na dhambi."

Na kuna hadithi nyingi zenye maana hii.

Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atuonyeshe haki kuwa ni haki na atujaalie kuifuta, na atuonyeshe batili kuwa ni batili na atujaalie kujiepusha nayo. Na atuneemeshe sisi na mwandishi Abdul-Fattaah na Waislamu wote kutubu kisawasawa, na atuepushe sote na fitina za kupotosha, kutii matamanio na Shetani. Hakika yeye ndiye msimamizi wa hayo na Mwenye uwezo juu yake.

Na rehema na amani ziwe kwa Nabii wetu Muhammad, jamaa zake, na Maswahaba wake, na wote wanaowafuata kwa wema mpaka Siku ya Malipo.

 

***

 

***


Ameipokea Bukhari (2056) na Muslim (30).

Ameipokea Al-lalkaiy katika Ufafanuzi wa misingi ya itikadi (73 5), na Ibnu abdul barri katka Jaamiy al-ilmi wa fadh-luhu (1801), lakini kwa matamshi "hadithi mbalimbali" badaya ya "aya zenye sifa (za Mwenyezi Mungu)", na tamko lenyewe linasema hivi: "Zipokeeni hadithi hizi kama zilivyokuja wala msijadiliane kuhusiana nao."

Ameipokea Al-baihaqiy katika Al-asmaau wasswifaat (865), na Ibnu Taimiyat akasema kwamba hadithi hii ni sahihi katika kitabi kiitwacho Al-hamawiyyat (uk 269), na Adh-dhahabiy akasema katika kitabu kiitwacho Al-ir-dhwi (2/223): "Wapokezi wake ni maimamu waaminifu."

Ameipokea Al-Laalakaaiy katika Sharhi Usuulul Itikad (930), na Al-Baihaqiy katika Al-Asmaau wa swifaat (955).

Ameipokea Al-Laalakaaiy katika Sharhi Usuulul Itikad (665), na Al-Baihaqiy katika Al-Asmau was-Swifaat (868).

Ameipokea Al-Lalkaaiy katika Sharhi usuulul itikad (664), na Abuu Nu'aimu katika Hil-yatul auliyaa (6/325), na Baihaqiy katika Al-asmau wa swifaat (867)

Ameipokea Al-muzakkiy katika kitabu kiitwacho Al-muzakkiyat (29), na Ibnu Battwah katika Ibaanat (120), na Al-laalakaiy katika Sharh Usuululitiqad (663).

Ameipokea Al- daaramiy katika kuwajibu kundi la Jahamia (67) na Baihaqiy katika kitabu kiitwacho Al-asmaau wa swifaat (903).

Ameipokea Adh-Dhahabiy katika kitabu Al-Uluwwiy (464), na akasema Al-Albaniy katika Mukhtaswar Al-Uluwwiy (uk. 184): "Hii ni cheni sahihi, na wapokezi wake ni waaminifu na wanafahamika."

Tafsiri ya Ibnu Kathiir (3/426 427).

Ameipokea Al-Bukhariy (22) kutoka katika hadithi ya Abii Said Al-Khuduriy - radhi za Mwenyezi Mungu zimfikie.

Ameipokea hadithi hii Imamu Muslim (2996), kutoka katika hadithi ya Aisha, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.

Ameipokea Bukhariy (3651) na Muslimu (2533), kutoka katika hadithi ya Abdullahi ibnu Masud - Mwenyezi Mungu amridhie.

Ameipokea Imamu Muslimu (1920) kutoka katika hadithi ya Thauban, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.

Ameipokea Ibnu Maajah (3953) kutoka katika hadithi ya Thauban, Mwenyezi Mungu amridhie, na kaisahihisha ibnu Hibban (6753), na Al-Haakim (8653).

Ameipokea At-Tirmidhiy (2641) kutoka katika hadithi ya Abdullahi ibnu Umar, radhi za Mwenyezi Mungu zimfikie, na akasema Al-munaawiy katika kitabu cha Faidhul Qadiir (5/347): "Ndani yake kuna Abdurahman ibnu Ziyaad Al-ifriikiy. Amesema Adh-dhahabiy: 'Walisema kwamba ni dhaifu', naye Albaniy amesema kwamba ni sahihi katika Swahihul jaamiy (5343).

Ameipokea hadithi hii imamu Muslim (8)

Ameipokea Bukhari (2056) na Muslim (30).