Namna ya Swala ya Mtume ﷺ (Kiswahili)

Mheshimiwa, Sheikh, Abdulaziz bin Baaz - Mwenyezi Mungu amrehemu - ameeleza ndani ya kitabu cha "Namna ya Swala ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake", kwa ufupi namna ya swala ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, kwa mbinu rahisi na njia nzuri kabisa, huku akitegemea ushahidi wa kimaandiko yaliyo sahihi; ili kiwe muongozo kwa Muislamu katika swala yake. Alibainisha ndani yake nguzo za swala na sunna zake na namna yake, kuanzia wudhu mpaka kutoa salamu ya kumaliza swala, akikusanya ndani yake kati ya ushahidi na upambanuzi, akilingania watu kumuiga kikamilifu Mtume, rehema na amani ziwe juu yake katika ibada hii kubwa zaidi.

  • earth Lugha
    (Kiswahili)
  • earth Mtunzi:
    الشيخ عبد العزيز بن باز

Tarjama zingine 52

ce شيشاني- нохчийн мотт sq ألباني- Shqip pt برتغالي- português as آسامي- অসমীয়া ms ملايو- Melayu uz أوزبكي- Ўзбек ar عربي- العربية ps بشتو- بشتو ur أردو- اردو en إنجليزي- English bn بنغالي- বাংলা ru روسي- Русский zh صيني- 中文 fa فارسي- فارسي fr فرنسي- Français hi هندي- हिन्दी sw سواحيلي- Kiswahili id إندونيسي- Indonesia ha هوسا- Hausa tl فلبيني تجالوج- Tagalog tr تركي- Türkçe gu غوجاراتية- ગુજરાતી te تلغو- తెలుగు si سنهالي- සිංහල ta تاميلي- தமிழ் mk مقدوني- македонски pl بولندي- polski it إيطالي- italiano hu هنجاري مجري- magyar ka جورجي- ქართული es إسباني- español kn كنادي- ಕನ್ನಡ or أورومو- afaan oromoo sr صربي- Српски az أذري- azərbaycanca lo لاو- ພາສາລາວ ml مليالم- മലയാളം tg طاجيكي- тоҷикӣ hy أرميني- Հայերէն bs بوسني- bosanski vi فيتنامي- Tiếng Việt dv ديفهي- ދިވެހި ky قرغيزي- Кыргызча st سوتي- Sesotho th تايلندي- ไทย ne نيبالي- नेपाली cs تشيكي- čeština fi فنلندي- suomi bg بلغاري- български mos موري- Mõõré mg ملاغاشي- Malagasy yo يوربا- Èdè Yorùbá
PHPWord

 

 

كَيْفِيَّةُ صَلَاةِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ

 

 

Namna ya Swala ya Mtume

 

 

لِفَضِيلَةِ الشَّيْخِ العَلَّامَةِ

عَبْدِ العَزِيزِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ بَازٍ

غَفَرَ اللَّهُ لَهُ وَلِوَالِدَيْهِ وَلِلْمُسْلِمِينَ

 

Mheshimiwa, Sheikh

Abdul-ʻAzīz bin Abdillah bin Baaz

 


بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Namna ya Swala ya Mtume

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

Kila sifa njema zinamstahiki Mwenyezi Mungu pekee, na rehema na amani ziwe juu ya mja wake na Mtume wake, Nabii wetu Muhammadi na watu wake na Maswahaba zake, ama baada hayo:-

Haya ni maneno mafupi katika kubainisha namna ya swala ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, nimetaka kuyaweka mbele ya kila Muislamu wa kiume na Muislamu wa kike, ili kila anayeisoma, ajitahidi kumuiga katika hilo, kwa mujibu wa kauli yake rehema na amani ziwe juu yake: "Swalini kama mlivyoniona mimi nikiswali."1 Na kwa msomaji, sasa huu ndio ufafanuzi wa hilo:

 

 

 

 

 

 

1. Ataeneza sawasawa maji ya udhu, na hilo ni mtu atawadhe kama alivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu; kwa kuifanyia kazi kauli yake aliyetakasika na kutukuka:

﴿يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓاْ إِذَا قُمۡتُمۡ إِلَى ٱلصَّلَوٰةِ فَٱغۡسِلُواْ وُجُوهَكُمۡ وَأَيۡدِيَكُمۡ إِلَى ٱلۡمَرَافِقِ وَٱمۡسَحُواْ بِرُءُوسِكُمۡ وَأَرۡجُلَكُمۡ إِلَى ٱلۡكَعۡبَيۡنِ...﴾.

"Enyi mlioamini, pindi mtakaposimama kutaka kuswali, basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka katika viwiko, na pakeni maji vichwa vyenu, (na muoshe) miguu yenu mpaka katika fundo mbili." [Al-Maida: 6] Mpaka mwisho wa Aya.

Na kauli ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Haikubaliki swala pasina twahara.".2

Na kauli yake Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alipokuwa anamwambia aliyekosea katika swala yake: "Utakaposimama katika swala, basi eneza vizuri maji ya udhu (katika viungo)."3

2. Mwenye kuswali ataelekea Kibla, nayo ni Al-Kaaba, mahala popote atakapokuwa kwa mwili wake wote akiwa amekusudia kwa moyo wake kuitekeleza swala anayoitaka, sawa sawa iwe ya faradhi au sunna, na wala asiitamke nia kwa ulimi wake; kwa sababu kutamka nia si katika sheria. Bali ni uzushi; kwa sababu Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, hakuitamka nia wala Maswahaba zake, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao. Ataweka kizuizi (sutra) atakayoswali akiielekea endapo atakuwa imamu au anaswali peke yake. Kuelekea kibla ni sharti katika swala, isipokuwa katika baadhi ya hali zilizoondolewa katika hilo, zina julikana na zimewekwa wazi katika vitabu vya wana zuoni.

3. Atatoa takbira ya kuhirimia swala kwa kusema: Allaahu Akbaru, huku macho yake yakitazama mahala pake pa kusujudu.

4. Atanyanyua mikono yake wakati wa takbira mpaka usawa wa mabega yake au usawa wa masikio yake.

5. Ataweka mikono yake juu ya kifua chake, kulia juu ya kiganja chake cha kushoto. Pia anaweza kuuweka juu ya kiwiko au muundi wa mkono; kwa sababu hayo yalithibiti kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake.

6. Ni sunna mtu asome dua ya ufunguzi wa swala, nayo ni: "Allaahumma baa'id bainii wa baina khatwaa yaaya, kamaa baa'atta bainal mashriqi wal maghribi. Allaahumma naqinii min khatwaayaaya, kamaa yunaqqath- thaubul abyadhwu minad-danasi. Allaahuma gh-silnii bil maai wath-thalji wal baradi." Yaani: Ewe Mwenyezi Mungu, weka mbali kati yangu mimi na makosa yangu, kama ulivyoweka mbali baini ya Mashariki na Magharibi. Ewe Mwenyezi Mungu, nitakase kutokana na makosa kama inavyotakaswa nguo nyeupe kutokana na uchafu. Ewe Mwenyezi Mungu, nioshe kutokana na makosa yangu kwa maji, theluji na barafu."4

Na akitaka, anaweza kusema badala ya hilo:

"Sub-haanaka llaahumma wabihamdika, watabaaraka smuka, wa ta'alaa jadduka, walaa ilaaha ghairuka." Yaani: Umetakasika ewe Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zako. Jina lako ni lenye baraka, na utukufu wako ni wa juu sana, wala hakuna mungu mwingine isipokuwa Wewe.5 Na akisoma dua zingine zisizokuwa hizo, miongoni mwa zile zilizothibiti kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, pia hakuna ubaya. Na kilicho bora zaidi ni asome dua hii wakati mwingine na dua hii wakati mwingine, kwa sababu hilo ndilo linamtia katika ukamilifu zaidi wa kumfuata Mtume. Kisha atasema: "A'udhu billahi minashshaitwaanir-rajiim." Maana yake: Ninajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na Shetani aliyelaaniwa. Kisha aseme: "Bismillahir-rahmanir-rahiim." Maana yake: Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Kisha asome suratul-Faatiha, kwa mujibu wa kauli yake Mtume: "Hana swala yeyote ambaye hakusoma kifunguzi cha Kitabu (Suratul Faatiha)."6 Na atasema: "Aaamiiin" baada yake, yaani: 'Ewe Mwenyezi Mungu pokea dua', kwa sauti kubwa katika swala za sauti kubwa, na kwa siri katika swala za siri. Kisha atasoma kiasi anachokiweza katika Qur'ani. Kilicho bora zaidi ni asome sura fupi za kati na kati baada ya Suratul-Faatiha, katika swala ya Adhuhuri, Laasiri na Ishaa. Na katika swala ya Al-fajiri asome sura ndefu. Na katika swala ya Maghribi, wakati mingine asome sura ndefu, na wakati mwingine sura fupi; kwa kuzifanyia kazi hadithi zilizokuja kulieleza hilo.

7. Atanyanyuka huku akitoa takbira, na huku aki nyanyua mikono yake mpaka usawa wa mabega yake au masikio yake. Atakiweka kichwa chake usawa wa mgongo wake na huku ameweka mikono yake juu ya magoti yake kwa kuvisambaza vidole vyake. Atulizane katika rukuu yake na aseme:Sub-haana Rabbiyal-Adhwiim (Ametakasika Mola wangu Mlezi Mtukufu). Na bora zaidi ni airudie dua hii mara tatu au zaidi. Pia inapendekezwa kusema pamoja na hivyo: "Sub-haanaka llaahumma wabihamdika. Allaahumma ghfirlii." Maana yake: Umetakasika ewe Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zako. Ewe Mwenyezi Mungu, nisamehe.7

8. Atanyanyua kichwa chake kutoka katika rukuu huku amenyanyua mikono yake mpaka usawa wa mabega yake au masikio yake huku akisema: Sami'a llaahu liman hamidah (Amemsikia Mwenyezi Mungu mwenye kumsifu). Na hili ni endapo atakuwa imamu au wakati anaswali peke yake. Na atasema wakati wa kunyanyuka kwake: "Rabbanaa walakal-hamdu, hamdan kathiiran twayyiban mubaarakan fiihi, mil-as samaawaati wamil-al Ardhwi, wamil-amaa shi ita min shaiin baad." Yaani: Mola wetu Mlezi, sifa njema ni zako, sifa (shukurani) nyingi nzuri zenye baraka ndani yake, kwa ujazo wa mbingu na ujazo wa ardhi, na ujazo wa chochote ukitakacho baada yake.8

Ama akiwa nyuma ya imamu (maamuma), basi atatakiwa kusema wakati wa kunyanyuka: 'Rabbanaa walakal-hamdu', yaani (Ewe Mola wetu Mlezi, ni zako sifa njema zote), mpaka mwisho wa maneno yaliyo tangulia. Na endapo atazidisha kila mmoja wao, nina kusudia imamu na maamuma na anayeswali peke yake: "Ahluth'thanaa walmajd, ahaqqu maaqaalal 'abdu, wakulluna laka 'abdu. Allahumma laa maani'a limaa a'atwaita, walaa mu'utwiya limaa mana'ata, walaa yanfa'u dhaljaddi minkal jaddu." Yaani: 'Unastahiki zaidi sifa njema na utukufu, haya ni maneno ya haki zaidi aliyoyasema mja, nasi sote ni waja wako. Ewe Mwenyezi Mungu, hakuna wa kuzuia uliyoyatoa, wala wa kuyatoa uliyoyazuia, wala hawezi kunufaisha mwenye utukufu (yeyote) kuliko wewe ewe Mtukufu.'9 Basi itakuwa vizuri, kwa sabubu hilo lilithibiti kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake.

Na inapendekezwa waweke wote wawili, yaani: Imamu na anayeswali peke yake mikono yake juu ya kifua chake kama alivyofanya wakati wa kusimama kwake kabla ya kurukuu, kwa sababu yamethibiti yanayoonyesha hilo kutoka katika hadithi za Wail bin Hujri na Sahli bin Sa'adi, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao.

9. Atasujudu huku akitoa takbira, kwa kuweka magoti yake kabla ya mikono yake ikiwa itakuwa rahisi kwake kufanya hivyo. Lakini ikiwa ni vigumu kwake, basi atatanguliza mikono yake kabla ya magoti yake, akiwa kaelekea Kibla kwa vidole vya miguu yake na mikono yake, akiwa kavifungamanisha vidole vya mikono yake huku kavinyoosha, na atakuwa juu ya viungo vyake saba: Paji la uso pamoja na pua, mikono miwili, magoti mawili na tumbo za vidole vya miguu miwili. Atasema: "Sub-haana rabbiyal-A'alaa." Yaani: 'Ametakasika Mola wangu Mlezi aliye juu zaidi.' Ni sunna aseme hivyo mara tatu au zaidi, na inapendekezwa aseme pia pamoja na hivyo: "Sub-haanaka llaahumma rabbanaa wabihamdika. Allaahumma ghfirli." Yaani: Umetakasika ewe Mwenyezi Mungu, Mola wetu Mlezi, na sifa njema zote ni zako. Ewe Mwenyezi Mungu, nisamehe. Na anatakiwa azidishe kuomba dua kwa kauli ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake: "Ama katika rukuu, mtukuzeni sana Mola Mlezi. Na ama katika sijida, jitahidini sana kuomba dua kwa wingi. Kwani hapo ni mahala bora zaidi kwenu nyinyi pa kujibiwa dua."10

Na amuombe Mola wake Mlezi katika kheri za dunia na akhera, sawa sawa Swala iwe ya faradhi au ya sunna, na aweke mbali miundi yake ya mkono na mbavu zake, na tumbo lake mbali na mapaja yake, na mapaja yake mbali na miundi yake ya miguu, na anyanyue dhiraa (mikono) yake kutoka katika ardhi, kwa mujibu wa kauli ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake: "Linganeni sawa katika sijida, na asitandaze mmoja wenu mikono yake kama anavyoitandaza mbwa."11

 

10. Atanyanyua kichwa chake huku akitoa takbira, na atatandika mguu wake wa kushoto na kuukalia, na atasimamisha mguu wake wa kulia na ataweka mikono yake juu ya mapaja yake na magoti yake, na atasema: "Rabbighfirlii war-hamnii wahdinii warzuqunii wa'afinii waj-burnii." Maana yake: 'Ewe Mola wangu Mlezi, nisamehe na unirehemu, na uniongoze, na uniruzuku, na unipe salama na uniunge.'12 Na atatulizana katika kikao hiki.

 

11. Atasujudu sijida ya pili huku akitoa takbira na atafanya ndani yake kama alivyofanya katika sijida ya kwanza.

12. Atanyanyua kichwa chake huku akitoa takbira, na atakaa kikao kifupi kama kikao cha kati ya sijida mbili. Kikao hiki kinaitwa kikao cha mapumziko. Nacho si cha lazima, bali kinapendekezwa tu, na hata akikiacha, basi hakuna ubaya juu yake. Kikao hiki hakina dhikri wala dua yoyote. Kisha atanyanyuka juu kwa ajili ya rakaa ya pili kwa kuegemea magoti yake ikiwa hilo litakuwa jepesi kwake. Na kama litakuwa gumu kwake, basi atajitegemeza kwenye Ardhi. Kisha atasoma Faatiha na chochote kilicho chepesi kwake katika Qur'ani baada ya Faatiha. Kisha atafanya kama alivyofanya katika rakaa ya kwanza.

13. Swala itakapokuwa ni ya rakaa mbili, kama swala ya Alfajiri au Ijumaa na Idi mbili, atakaa baada ya kunyanyuka kwake kutoka katika sijida ya pili akiwa amesimamisha mguu wake wa kulia, na ameulaza chini mguu wake wa kushoto, akiwa ameweka mkono wake wa kulia juu ya paja lake la kulia, akiwa amevi kunja vidole vyake vyote isipokuwa kidole cha shahada. Hicho ataashiria kwacho kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Na kama atakikunja kidole cha mwisho na kile kinacho fuatia katika mkono wake wa kulia, akatengeneza duara kwa kidole gumba chake na kidole cha kati, na akaashiria kwa kidole cha shahada, basi ni vizuri; kwa sababu namna zote mbili hizo zilithibiti kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake. Na kilicho bora ni afanye wakati mwingine hii na wakati mwingine hii. Ataweka mkono wake wa kushoto juu ya paja lake la kushoto na goti lake, kisha atasoma tahiyatu katika kikao hiki, nayo ni: "Attahiyyaatu lillaahi, wasswalawaatu wattwayyibaatu. Assalaamu a'laika ayyuhan nabiyyu, warahmatullaahi wabarakaatuh. Assalaamu 'alainaa wa 'alaa 'ibaadillaahi sswaalihiin. Ash-hadu anlaa ilaaha illa llaahu, wa ash-hadu anna Muhammadan 'abduhu warasuuluhu." Tafsiri yake: Maamkizi (amani) ni ya Mwenyezi Mungu, na swala na vile vilivyo vizuri. Amani iwe juu yako, ewe Nabii na rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake. Amani iwe juu yetu na juu ya waja wema wa Mwenyezi Mungu. Ninashuhudia kuwa hapana mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu, na nina shuhudia kuwa Muhammadi ni mja wake na ni Mtume wake. Kisha aseme: "Allahumma swalli 'alaa Muhammad wa 'alaa aali Muhammad, kamaa swallaita 'alaa Ibraahima wa 'alaa aali Ibraahim, innaka hamiidum-majid. Wabaarik 'alaa Muhammad wa 'alaa aali Muhammad, kamaa barakta 'alaa Ibraahima wa 'alaa aali Ibraahim, innaka hamiidum-majid." Yaani: Ewe Mwenyezi Mungu, mshushie rehema Muhammad, na jamaa zake Muhammad, kama ulivyomshushia rehema Ibrahim na jamaa za Ibrahim. Hakika Wewe ni Msifiwa, Mtukufu. Na mbariki Muhammad na jamaa zake Muhammad, kama ulivyo mbariki Ibrahim na jamaa zake Ibrahim. Hakika Wewe ni Msifiwa, Mtukufu.13

Na atajikinga kwa Mwenyezi Mungu kutokana na mambo manne, atasema: "Allaahumma inni a'udhubika min 'adhaabi jahannama, wa min 'adhaabil qabri, wamin fitnatil mahyaa wal mamaati, wamin sharri fitnatil masiihiddajjaali." Yaani: Ewe Mwenyezi Mungu, hakika mimi ninajilinda kwako kutokana na adhabu za Jahanamu, na majaribu ya uhai na ya kifo, na kutokana na majaribu ya Masihi Dajali.14

Kisha ataomba lolote alitakalo katika kheri za dunia na akhera, na akiwaombea wazazi wake au wengineo miongoni mwa Waislamu pia hakuna ubaya, sawa sawa swala iwe ni ya faradhi au ya sunna; kwa ujumla wa kauli ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, katika hadithi ya bin Masudi, radhi za Allah ziwe juu yake, wakati alimpomfundisha tahiyatu: "Kisha naachague katika dua inayompendeza zaidi, basi na aombe."15 Na katika tamko jingine: "Kisha naachague katika maombi anayoyataka."16

 

 

Na hii inakusanya yote yanayomnufaisha mja katika dunia na akhera. Kisha atatoa salamu kuliani kwake na kushotoni kwake kwa kusema: Assalaam alaikum warahmatullahi. Assalaam alaikum warahmatullahi.

14. Ikiwa swala ni ya rakaa tatu kama Magharibi, au ya rakaa nne kama Adhuhuri, Laasiri na Ishaa, basi atasoma tahiyatu iliyotajwa hivi punde pamoja na swala ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake. Kisha atasimama wima kwa kutegemea magoti yake, huku akinyanyua mikono yake usawa wa mabega yake au masikio yake huku akisema: Allaahu Akbaru, na ataiweka, yaani mikono yake juu ya kifua chake kama ilivyo tangulia, na atasoma suratul-Faatiha pekee. Na akisoma katika rakaa ya tatu na ya nne katika swala ya Adhuhuri zaidi ya Faatiha katika baadhi ya nyakati, basi hakuna ubaya; kwa sababu yalithibiti yanayoonyesha hilo kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, katika hadithi ya Abuu Saidi, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Na akiacha kumswalia Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, katika tahiyatu ya kwanza, pia hakuna ubaya; kwa sababu hilo ni sunna na si wajibu katika tahiyatu ya kwanza. Kisha atakaa tahiyatu baada ya rakaa ya tatu katika swala ya Magharibi na baada ya rakaa ya nne katika swala ya Adhuhuri, Laasiri na Ishaa, kama ilivyotangulia katika swala za rakaa mbili. Kisha atatoa salamu kuliani kwake na kushotoni kwake, na ataomba msamaha mara tatu, kisha atasema: "Allahumma antassalaam, waminkassalaam, tabaarakta yaa dhaljalaali wal ikraam." Tafsiri: 'Ewe Mwenyezi Mungu, hakika wewe ndiye amani, na amani hutoka kwako. Umetukuka ewe Mwenye utukufu na ukarimu.'17 Hili ni kabla ya kuwageukia watu kama atakuwa ni imamu. Kisha atasema: "Laa ilaaha illa llaahu wahdahuu laa shariika lahu, lahul-mulku walahul-hamdu, wahuwa 'alaa kulli shai-in qadiir. Allaahumma laa maani'a limaa a'atwaita, walaa mu'utwiya limaa mana'ata, walaa yanfa'u dhal-jaddi minkal-jaddu. Laa haulaa walaa quwwata illaa billaah. Laa ilaaha illa llaahu walaa na'abudu illaa iyyahu, lahun-niimatu, walahul-fadhlu walahuth-thanaaul-hasan. Laa ilaaha illa llaahu mukh liswiina lahuddiin walau karihal kaafiruun." Tafsiri: 'Hapana mungu apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, yeye pekee asiye na mshirika. Ufalme ni wake, na sifa njema zote ni zake, naye ni Muweza mno wa kila kitu. Ewe Mwenyezi Mungu, hakuna wa kuyazuia uliyoyatoa, wala wa kuyatoa uliyoyazuia, na wala hawezi kunufaisha mwenye utukufu kukuliko wewe ewe Mtukufu. Hapana uwezo wala nguvu isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu. Hapana mungu apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na wala hatu muabudu yeyote ila Yeye. Yeye ndiye Mwenye neema, na fadhila zote ni zake, na Yeye ndiye Mwenye sifa nzuri. Hapana mungu apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, hali ya kuwa tunamtakasia dini (matendo) hata kama makafiri watachukia.'18

Na atamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kusema: "Sub-haanallaah" mara thelathini na tatu, na amsifu kwa kusema: "Alhamdulillaah" mfano wa idadi hiyo, na amtukuze kwa kusema: "Allaahu Akbaru" kwa idadi hiyo. Kisha atasema ili kukamilisha mia moja: "Laa ilaaha illa llaahu wahdahuu laa shariika lahu, lahulmulku walahul-hamdu wahuwa 'alaa kulli shai-in qadiir." Maana yake: ‘Hapana mungu apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, yeye pekee asiye na mshirika. Ufalme ni wake, na sifa njema zote ni zake, naye ni Muweza mno wa kila kitu.’ Kisha atasoma ayatul Kursiy, Qul-huwallaahu ahad, Qul-a'udhubirabbil-falaq na Qul-a'udhubirabbin naasi, baada ya kila swala. Ni sunna kuzikariri sura hizi mara tatu tatu baada ya swala ya Alfajiri na swala ya Magharibi; kwa sababu kuna hadithi zilizosimulia hilo kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake. Nyiradi hizi zote ni sunna wala si faradhi.

Na inaruhusiwa katika sheria kwa kila Muislamu wa kiume na wa kike kuswali kabla ya swala ya Adhuhuri rakaa nne, na baada yake rakaa mbili. Na rakaa mbili baada ya swala ya Magharibi na Ishaa, na rakaa mbili kabla ya swala ya Alfajiri. Hizi zote ni jumla ya rakaa kumi na mbili. Rakaa hizi huitwa rawaatib (sunna zilizopangiliwa na zenye malipo maalumu) kwa sababu Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alikuwa akidumu kuziswali anapokuwa nyumbani. Ama safarini, alikuwa akiziacha isipokuwa sunna ya kabla ya Alfajiri na swala ya witiri; kwani hizo, yeye rehema na amani ziwe juu yake, alikuwa akizidumisha anapokuwa nyumbani na safarini. Na kilicho bora zaidi ni ziswaliwe sunna hizi ndani ya nyumba. Lakini ikiwa ataziswalia msikitini, basi hakuna ubaya; kwa mujibu wa kauli ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake: "Swala bora zaidi kwa mtu ni ile ya nyumbani kwake isipokuwa swala ya faradhi."19

Na kudumu na rakaa hizi ni miongoni mwa sababu za kuingia Peponi; kwa kauli ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake: "Atakayeswali rakaa kumi na mbili mchana na usiku, atajengewa nyumba ndani ya Pepo kwa sababu ya rakaa hizo."20

Na akiswali rakaa nne kabla ya Laasiri, na rakaa mbili kabla ya swala ya Magharibi, na rakaa mbili kabla ya swala ya Ishaa, basi ni vizuri; kwa sababu yamethibiti kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, yanayoonyesha hivyo. Na akiswali rakaa nne baada ya Adhuhuri au nne kabla yake, pia ni vizuri; kwa kauli yake rehema na amani ziwe juu yake: "Atakayehifadhi rakaa nne kabla ya Adhuhuri na rakaa nne baada yake, basi Mwenyezi Mungu atamharamishia kuingia Motoni."21 Na maana yake ni kwamba azidishe rakaa mbili baada ya Adhuhuri juu ya sunna zilizopangiliwa; kwa sababu sunna zilizopangiliwa ni nne kabla yake na mbili baada yake. Akizidisha mbili baada yake, itakuwa imefanyika kama ilivyokuja katika hadithi ya Ummu Habiba, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.

Na Mwenyezi Mungu ndiye msimamizi bora katika kuyawezesha mambo, na rehema na amani ziwe juu ya Nabii wetu Muhammadi bin Abdillah na juu ya watu wa familia yake, Maswahaba zake na wote wana omfuata kwa wema mpaka siku ya Malipo.

 

 

 

***

 


Kaipokea Muslim, kwa nambari (224).

Kaipokea Bukhari, kwa nambari (5782).

Kaipokea Bukhari, kwa nambari 744, na Muslim, kwa nambari 598.

Kaipokea Muslim, kwa nambari (399).

Kaipokea Bukhari, kwa nambari (756).

Bukhari kwa nambari: 817, na Muslim kwa nambari: 484.

Kaipokea Bukhari nambari: 711, na Muslim kwa nambari: 598.

Kaipokea Muslim, kwa nambari (477).

Kaipokea Muslim, kwa nambari (479).

Kaipokea Bukhari kwa nambari: 788, na Muslim kwa nambari: 493.

Kaipokea Tirmidhi, kwa nambari (284), na Abuu Daudi, kwa nambari (850), na Ibnu Maajah, kwa nambari (898).

Kaipokea Bukhari kwa nambari: 797, na Muslim kwa nambari: 402.

Kaipokea Bukhari kwa nambari: 1311, na Muslim kwa nambari: 588.

Kaipokea An-Nasai, kwa nambari 1298.

Kaipokea Muslim, kwa nambari (402).

Kaipokea Muslim, kwa nambari (591).

Kaipokea Muslim, kwa nambari (402).

Kaipokea Bukhari, kwa nambari (6860).

Kaipokea Muslim, kwa nambari (728).

Kaipokea Ahmad, kwa nambari (25547), na Tirmidhi, kwa nambari (393), na Abuu Daudi, kwa nambari (1077).

Kaipokea Bukhari, kwa nambari (605).