ثَلَاثَةُ الأُصُولِ وَأَدِلَّتُهَا
Misingi Mitatu na Ushahidi Wake
لِلشَّيْخِ
مُحَمَّدٍ التَّمِيمِي رَحِمَهُ اللهُ
Cha Sheikh: Muhammad At-Tamiimiy
(Mwenyezi Mungu amrehemu)
بِسْمِ اللهِ الرَّحمَنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu
Tambua akurehemu MwenyeziMungu, yakwamba ni wajibu kwetu kujifunza mambo manne.
La kwanza: Ni Elimu:
Nayo ni kumfahamu Mwenyezi Mungu, na kumfahamu Nabii wake, na kuifahamu dini ya Uislamu kwa ushahidi.
La pili: Kuifanyia kazi.
La tatu: Kuifikisha kwa wengine.
La nne: Kuvumilia juu ya maudhi yapatikanayo katika kuilingania. Na ushahidi wa hayo ni kauli yake Mtukufu: “Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
﴿وَٱلۡعَصۡرِ1 إِنَّ ٱلۡإِنسَٰنَ لَفِي خُسۡرٍ2 إِلَّا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَعَمِلُواْ ٱلصَّٰلِحَٰتِ وَتَوَاصَوۡاْ بِٱلۡحَقِّ وَتَوَاصَوۡاْ بِٱلصَّبۡرِ3﴾
"Naapa kwa Zama! "Hakika binaadamu bila ya shaka yumo katika hasara, Ila wale walioamini, na wakatenda mema, na wakausiana kwa haki, na wakausiana kusubiri.” [Al-Asri: 1-3].
Na amesema Imamu Shafy, Mwenyezi Mungu amrehemu:
"Laiti asingeteremsha Mwenyezi Mungu hoja yoyote juu ya viumbe wake isipokuwa Sura hii basi ingeli watosha.
Na amesema Bukhari Mwenyezi
Mungu Mtukufu amrehemu: (Mlango wa) Elimu kabla ya kauli na matendo, na ushahidi ni kauli yake Mtukufu: “Basi jua ya kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, na uombe msamaha kwa dhambi yako...” [Muhammad: 9] hivyo akaanza kwa elimu kabla ya kauli na matendo.
(Tambua) Akuhurumie Mwenyezi Mungu, yakwamba ni lazima kwa Muislamu wa kiume na wa kike kujifunza mambo haya matatu na kuyafanyia kazi.
(La kwanza) Ni kuwa Mwenyezi Mungu ametuumba na akaturuzuku na wala hakutuacha hivi bure, bali alitutumia Mtume. Atakayemtii, ataingia Peponi. Na atakayemuasi, ataingia Motoni.
Na ushahidi wa hilo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّآ أَرۡسَلۡنَآ إِلَيۡكُمۡ رَسُولٗا شَٰهِدًا عَلَيۡكُمۡ كَمَآ أَرۡسَلۡنَآ إِلَىٰ فِرۡعَوۡنَ رَسُولٗا15 فَعَصَىٰ فِرۡعَوۡنُ ٱلرَّسُولَ فَأَخَذۡنَٰهُ أَخۡذٗا وَبِيلٗا16﴾
“Hakika Sisi tumemtuma kwenu Mtume aliye shahidi juu yenu, kama tulivyomtuma Mtume kwa Firauni. Lakini Firauni alimuasi huyo Mtume, basi tukamshika mshiko wa mateso.”[Al Muzzammil:15-16].
(La pili): Ni kuwa Mwenyezi Mungu haridhii kushirikishwa pamoja naye katika ibada zake yeyote, si Malaika aliyekaribu wala Nabii aliyetumwa, na ushahidi wa hilo ni kauli yake Mtukufu:
﴿وَأَنَّ ٱلۡمَسَٰجِدَ لِلَّهِ فَلَا تَدۡعُواْ مَعَ ٱللَّهِ أَحَدٗا18﴾
“Na hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu, basi msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu.” [Al-Jinn: 18].
La tatu: Ni kuwa mwenye kumtii Mtume na akampwekesha Mwenyezi Mungu, haitakiwi kwake kumpenda mwenye kumpiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake hata kama atakuwa ndugu wa karibu. Na ushahidi wa hilo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿لَّا تَجِدُ قَوۡمٗا يُؤۡمِنُونَ بِٱللَّهِ وَٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِ يُوَآدُّونَ مَنۡ حَآدَّ ٱللَّهَ وَرَسُولَهُۥ وَلَوۡ كَانُوٓاْ ءَابَآءَهُمۡ أَوۡ أَبۡنَآءَهُمۡ أَوۡ إِخۡوَٰنَهُمۡ أَوۡ عَشِيرَتَهُمۡۚ أُوْلَٰٓئِكَ كَتَبَ فِي قُلُوبِهِمُ ٱلۡإِيمَٰنَ وَأَيَّدَهُم بِرُوحٖ مِّنۡهُۖ وَيُدۡخِلُهُمۡ جَنَّٰتٖ تَجۡرِي مِن تَحۡتِهَا ٱلۡأَنۡهَٰرُ خَٰلِدِينَ فِيهَاۚ رَضِيَ ٱللَّهُ عَنۡهُمۡ وَرَضُواْ عَنۡهُۚ أُوْلَٰٓئِكَ حِزۡبُ ٱللَّهِۚ أَلَآ إِنَّ حِزۡبَ ٱللَّهِ هُمُ ٱلۡمُفۡلِحُونَ22﴾
“Huwakuti watu wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kuwa wanawapenda wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao.
Hao ameandika katika nyoyo zao Imani, na amewapa nguvu kwa Roho itokayo kwake.
Na atawaingiza katika Mabustani yapitayo mito kati yake. Humo watakaa daima.
Mwenyezi Mungu awe radhi nao, na wao wawe radhi naye. Hao ndio Hizbullahi (Kundi la Mwenyezi Mungu). Juweni! Hakika Kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufanikiwa.” [Al-Mujadilah: 22].
Tambua, akuongoze Mwenyezi Mungu katika utiifu wake: Ya kuwa utakasifu ndiyo mila ya Ibrahim: Nao ni kumuabudu Mwenyezi Mungu, yeye pekee kwa kumtakasia dini, na kwa hilo amewaamrisha Mwenyezi Mungu viumbe wote, na akawaumba kwa ajili hiyo; kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَمَا خَلَقۡتُ ٱلۡجِنَّ وَٱلۡإِنسَ إِلَّا لِيَعۡبُدُونِ56﴾
“Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.” [Surat Adh-Dhariyaat: 56],
Na maana ya: Waniabudu: yaani: wanipwekeshe.
Na kubwa aliloliamrisha Mwenyezi Mungu ni tauhidi, nayo ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu kwa Ibada.
Na kubwa alilolikataza Mwenyezi Mungu ni Shirki: Nayo ni kumuomba asiyekuwa yeye pamoja naye.
Na ushahidi wa hilo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَٱعۡبُدُواْ ٱللَّهَ وَلَا تُشۡرِكُواْ بِهِۦ شَيۡـٔٗا...﴾
“Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote...” [An-Nisaa: 36].
(Utakapoambiwa): Ni ipi misingi mitatu ambayo ni wajibu kwa mwanadamu kuifahamu?
Basi sema: Ni mja kumjua Mola wake Mlezi, na Dini yake na Nabii wake Muhammadi - rehema na amani ziwe juu yake.
Msingi wa kwanza:
Utakapoulizwa: Nani Mola wako Mlezi?
Basi sema: Mola wangu Mlezi ni Mwenyezi Mungu aliyenilea na akawalea walimwengu wote kwa neema zake, na ndiye muabudiwa wangu sina mimi muabudiwa mwingine zaidi yake; na ushahidi ni: kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿ٱلۡحَمۡدُ لِلَّهِ رَبِّ ٱلۡعَٰلَمِينَ2﴾
“Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.” [Al-Fatiha: 2].
Na kila kisichokuwa Mwenyezi Mungu hicho ni kilimwengu, na mimi ni mmoja miongoni mwa walimwengu.
Utakapoulizwa: Ni kwa kitu gani umemjua Mola wako Mlezi?
Basi sema: Nimemjua kwa alama zake na viumbe vyake. Na miongoni mwa viumbe vyake ni mbingu saba na ardhi saba na vyote vilivyomo na vilivyo kati yake.
Na ushahidi ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَمِنۡ ءَايَٰتِهِ ٱلَّيۡلُ وَٱلنَّهَارُ وَٱلشَّمۡسُ وَٱلۡقَمَرُۚ لَا تَسۡجُدُواْ لِلشَّمۡسِ وَلَا لِلۡقَمَرِ وَٱسۡجُدُواْۤ لِلَّهِۤ ٱلَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمۡ إِيَّاهُ تَعۡبُدُونَ37﴾
"Na katika Ishara zake ni usiku na mchana, na jua na mwezi. Basi msilisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Mwenyezi Mungu aliyeviumba, ikiwa nyinyi mnamuabudu Yeye tu."[Fusswilat: 37].
Na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّ رَبَّكُمُ ٱللَّهُ ٱلَّذِي خَلَقَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٖ ثُمَّ ٱسۡتَوَىٰ عَلَى ٱلۡعَرۡشِۖ يُغۡشِي ٱلَّيۡلَ ٱلنَّهَارَ يَطۡلُبُهُۥ حَثِيثٗا وَٱلشَّمۡسَ وَٱلۡقَمَرَ وَٱلنُّجُومَ مُسَخَّرَٰتِۭ بِأَمۡرِهِۦٓۗ أَلَا لَهُ ٱلۡخَلۡقُ وَٱلۡأَمۡرُۗ تَبَارَكَ ٱللَّهُ رَبُّ ٱلۡعَٰلَمِينَ54﴾
“Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwenyezi Mungu aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akainuka akawa juu ya Kiti cha Enzi. Huufunika usiku kwa mchana, ufuatao upesi upesi. Na jua, na mwezi, na nyota zinazotumika kwa amri yake. Fahamuni! Kuumba na amri ni zake. Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.” [Surat Al-A'araf: 54]
Na Mola Mlezi ndiye muabudiwa wa kweli; na ushahidi wa hilo ni kauli yake Mtukufu:
﴿يَٰٓأَيُّهَا ٱلنَّاسُ ٱعۡبُدُواْ رَبَّكُمُ ٱلَّذِي خَلَقَكُمۡ وَٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِكُمۡ لَعَلَّكُمۡ تَتَّقُونَ21 ٱلَّذِي جَعَلَ لَكُمُ ٱلۡأَرۡضَ فِرَٰشٗا وَٱلسَّمَآءَ بِنَآءٗ وَأَنزَلَ مِنَ ٱلسَّمَآءِ مَآءٗ فَأَخۡرَجَ بِهِۦ مِنَ ٱلثَّمَرَٰتِ رِزۡقٗا لَّكُمۡۖ فَلَا تَجۡعَلُواْ لِلَّهِ أَندَادٗا وَأَنتُمۡ تَعۡلَمُونَ22﴾
"Enyi watu! Muabuduni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni nyinyi na wale wa kabla yenu, ili mpate kuokoka.
(Mwenyezi Mungu) ambaye amekufanyieni hii ardhi kuwa kama tandiko, na mbingu kama paa, na akateremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo akatoa matunda yawe riziki zenu. Basi msimfanyie Mwenyezi Mungu washirika, na hali nyinyi mnajua." [Al-Baqara: 21-22].
Amesema Imamu Ibni Kathiir, Mwenyezi Mungu Mtukufu amrehemu: "Muumba wa vitu hivi ndiye anayestahiki kuabudiwa".
Na aina za Ibada alizoziamrisha Mwenyezi Mungu: - mfano kama Uislamu, na Imani, na Wema; na miongoni mwazo ni: Dua, na Hofu, na Kutaraji, na Kumtegemea Mwenyezi Mungu, na kuwa na Shauku, na Woga, na Unyenyekevu, na Kumcha, na Kutubia, na Kutaka msaada, na Kuomba kinga, na Mvua, na Kuchinja, na Kuweka Nadhiri, na mengineyo miongoni mwa aina za Ibada alizoziamrisha Mwenyezi Mungu - zote hizo ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; na ushahidi ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَأَنَّ ٱلۡمَسَٰجِدَ لِلَّهِ فَلَا تَدۡعُواْ مَعَ ٱللَّهِ أَحَدٗا18﴾
"Na hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu, basi msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu." [Al-Jinn: 18].
Atakayekielekeza chochote miongoni mwa Ibada hizo kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu basi huyo ni Mshirikina, na ushahidi ni kauli yake Mtukufu:
﴿وَمَن يَدۡعُ مَعَ ٱللَّهِ إِلَٰهًا ءَاخَرَ لَا بُرۡهَٰنَ لَهُۥ بِهِۦ فَإِنَّمَا حِسَابُهُۥ عِندَ رَبِّهِۦٓۚ إِنَّهُۥ لَا يُفۡلِحُ ٱلۡكَٰفِرُونَ117﴾
"Na anayemuomba - pamoja na Mwenyezi Mungu - mungu mwingine, hana ushahidi wa hili; basi bila ya shaka hesabu yake iko kwa Mola wake Mlezi. Kwa hakika makafiri hawafanikiwi." [Al-Mu’minun: 117]. Na imekuja katika Hadithi: "Dua ndiyo kiini cha ibada." Na ushahidi wake ni kauli yake Mtukufu:
﴿وَقَالَ رَبُّكُمُ ٱدۡعُونِيٓ أَسۡتَجِبۡ لَكُمۡۚ إِنَّ ٱلَّذِينَ يَسۡتَكۡبِرُونَ عَنۡ عِبَادَتِي سَيَدۡخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ60﴾
"Na Mola wenu Mlezi anasema: Niombeni, nitakuitikieni. Kwa hakika wale ambao wanajivuna wakaacha kuniabudu Mimi wataingia Jahannamu wadhalilike." [Ghafir: 60].
Na ushahidi wa kuwa na hofu, ni kauli yake Mtukufu:
﴿...فَلَا تَخَافُوهُمۡ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤۡمِنِينَ﴾
"...basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi ikiwa nyinyi ni Waumini." [Al-Imran: 175].
Na ushahidi wa kutaraji, ni kauli yake Mtukufu:
﴿...فَمَن كَانَ يَرۡجُواْ لِقَآءَ رَبِّهِۦ فَلۡيَعۡمَلۡ عَمَلٗا صَٰلِحٗا وَلَا يُشۡرِكۡ بِعِبَادَةِ رَبِّهِۦٓ أَحَدَۢا﴾
"Kwa hivyo, mwenye kutaraji kukutana na Mola wake Mlezi, basi na atende vitendo vyema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake Mlezi." [Al-Kahf: 110].
Na ushahidi wa kutegemea kwa Mwenyezi Mungu, ni kauli yake Mtukufu:
﴿...وَعَلَى ٱللَّهِ فَتَوَكَّلُوٓاْ إِن كُنتُم مُّؤۡمِنِينَ﴾
"Na mtegemeeni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini." [Al-Maidah: 23],
Na kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿...وَمَن يَتَوَكَّلۡ عَلَى ٱللَّهِ فَهُوَ حَسۡبُهُ...﴾
"Na anayemtegemea Mwenyezi Mungu, basi Yeye humtosha." [At-Talaq: 3].
Na ushahidi wa kuwa na shauku na hofu na unyenyekevu, ni kauli yake Mtukufu:
﴿...إِنَّهُمۡ كَانُواْ يُسَٰرِعُونَ فِي ٱلۡخَيۡرَٰتِ وَيَدۡعُونَنَا رَغَبٗا وَرَهَبٗاۖ وَكَانُواْ لَنَا خَٰشِعِينَ﴾
"Kwa hakika walikuwa wakiharakisha katika mambo mema na wakituomba kwa kutaraji na kwa kuogopa. Na walikuwa wanyenyekevu kwetu." [Al-Anbiya: 90]
Na ushahidi wa kuwa na woga, ni kauli yake Mtukufu:
﴿...فَلَا تَخۡشَوۡهُمۡ وَٱخۡشَوۡنِ...﴾
"..basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi." [Maida: 3].
Na ushahidi wa kutubia; ni kauli yake Mtukufu:
﴿وَأَنِيبُوٓاْ إِلَىٰ رَبِّكُمۡ وَأَسۡلِمُواْ لَهُ...﴾
"Na rejeeni kwa Mola wenu Mlezi, na silimuni kwake..." [Az-Zumar: 54].
Na ushahidi wa kuomba msaada, ni kauli yake Mtukufu:
﴿إِيَّاكَ نَعۡبُدُ وَإِيَّاكَ نَسۡتَعِينُ5﴾
"Wewe tu tunakuabudu, na wewe tu tunakuomba msaada." [Al-Fatiha: 5] Na imekuja katika Hadithi: "Utakapotaka msaada, basi taka msaada kwa Mwenyezi Mungu."
Na ushahidi wa kuomba kinga, ni kauli yake Mtukufu:
﴿قُلۡ أَعُوذُ بِرَبِّ ٱلۡفَلَقِ1﴾
"Sema: Najikinga kwa Mola Mlezi wa mapambazuko." [Surat Al-Falaq: 1], na
﴿قُلۡ أَعُوذُ بِرَبِّ ٱلنَّاسِ1﴾
"Sema: Ninajikinga kwa Mola Mlezi wa wanaadamu." [An-Nas: 1].
Na ushahidi wa kuomba mvua, ni kauli yake Mtukufu:
﴿إِذۡ تَسۡتَغِيثُونَ رَبَّكُمۡ فَٱسۡتَجَابَ لَكُمۡ...﴾
"Mlipokuwa mkimuomba msaada Mola wenu Mlezi, naye akakuitikieni..." [Al-Anfal: 9].
Na ushahidi wa kuchinja, ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿قُلۡ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحۡيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّهِ رَبِّ ٱلۡعَٰلَمِينَ162 لَا شَرِيكَ لَهُ...﴾
"Sema: Hakika Sala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote. Hana mshirika wake..." [Al-An'am: 162-163] Na katika mafundisho ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake: "Mwenyezi Mungu amemlaani anayechinja kwa ajili ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu."
Na ushahidi wa kuweka Nadhiri ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿يُوفُونَ بِٱلنَّذۡرِ وَيَخَافُونَ يَوۡمٗا كَانَ شَرُّهُۥ مُسۡتَطِيرٗا7﴾
"Wanatimiza nadhiri, na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea sana." [Al In saan:7]
Msingi wa pili:
Kujua Dini ya Uislamu kwa ushahidi. Na Uislamu ni kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kumpwekesha, na kunyenyekea kwake kwa kumtii, na kujitenga mbali na ushirikina na washirikina.
Uislamu una daraja tatu: Uislamu, Imani na Ihsani.
Na kila daraja lina nguzo zake.
Nguzo za Uislamu ni tano: Kushuhudia kuwa hapana mungu apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na kusimamisha Swala, na kutoa Zaka, na kufunga Ramadhani, na kuhiji katika Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu.
Basi ushahidi wa shahada (kushuhudia kuwa hapana mungu apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu) ni kauli yake Mungu Mtukufu:
﴿شَهِدَ ٱللَّهُ أَنَّهُۥ لَآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ وَٱلۡمَلَٰٓئِكَةُ وَأُوْلُواْ ٱلۡعِلۡمِ قَآئِمَۢا بِٱلۡقِسۡطِۚ لَآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ٱلۡعَزِيزُ ٱلۡحَكِيمُ18﴾
"Mwenyezi Mungu, na Malaika, na wenye elimu, wameshuhudia kuwa hakika hapana mungu ila Yeye, ndiye Mwenye kusimamisha uadilifu; hapana mungu ila Yeye Mwenye nguvu na Mwenye hekima." [Al-Imran: 18].
Na maana yake ni kwamba hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu.
Neno "Laa ilaaha -Hapana mungu" linakanusha yote yenye kuabudiwa kinyume na Mwenyezi Mungu.
Na "illa llaah" linathibitisha ibada kwa ajili ya Mwenyezi Mungu peke yake.
Hana mshirika katika ibada zake, kama vile asivyo na mshirika katika ufalme wake.
Na Tafsiri yake inayoliweka wazi ni kauli yake Mtukufu:
﴿وَإِذۡ قَالَ إِبۡرَٰهِيمُ لِأَبِيهِ وَقَوۡمِهِۦٓ إِنَّنِي بَرَآءٞ مِّمَّا تَعۡبُدُونَ26 إِلَّا ٱلَّذِي فَطَرَنِي..﴾
"Na pale Ibrahim alipomwambia baba yake na kaumu yake: Hakika mimi ninajitenga mbali na hayo mnayoyaabudu, Isipokuwa yule aliyeniumba.." [Az-Zukhruf: 26-27] Na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿قُلۡ يَٰٓأَهۡلَ ٱلۡكِتَٰبِ تَعَالَوۡاْ إِلَىٰ كَلِمَةٖ سَوَآءِۭ بَيۡنَنَا وَبَيۡنَكُمۡ أَلَّا نَعۡبُدَ إِلَّا ٱللَّهَ وَلَا نُشۡرِكَ بِهِۦ شَيۡـٔٗا وَلَا يَتَّخِذَ بَعۡضُنَا بَعۡضًا أَرۡبَابٗا مِّن دُونِ ٱللَّهِۚ فَإِن تَوَلَّوۡاْ فَقُولُواْ ٱشۡهَدُواْ بِأَنَّا مُسۡلِمُونَ64﴾
"Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa miungu Walezi badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka, basi semeni: Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu." [Al-Imran: 64].
Na ushahidi wa kushuhudia kuwa Muhammadi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ni kauli yake Mtukufu:
﴿لَقَدۡ جَآءَكُمۡ رَسُولٞ مِّنۡ أَنفُسِكُمۡ عَزِيزٌ عَلَيۡهِ مَا عَنِتُّمۡ حَرِيصٌ عَلَيۡكُم بِٱلۡمُؤۡمِنِينَ رَءُوفٞ رَّحِيمٞ128﴾
"Hakika amekwishakujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayokutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma." [At-Tauba:128]
Na maana ya kushuhudia kuwa "Muhammad ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu": Ni kumtii Mtume katika yale alioyaamrisha, na kumsadikisha kwa yale aliyoyaeleza, na kujiepusha na yale aliyoyakataza na kuyakemea, na asiabudiwe Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa namna alivyoelekeza.
Na ushahidi wa swala na zaka na tafsiri ya tauhidi ni kauli yake Mtukufu:
﴿وَمَآ أُمِرُوٓاْ إِلَّا لِيَعۡبُدُواْ ٱللَّهَ مُخۡلِصِينَ لَهُ ٱلدِّينَ حُنَفَآءَ وَيُقِيمُواْ ٱلصَّلَوٰةَ وَيُؤۡتُواْ ٱلزَّكَوٰةَۚ وَذَٰلِكَ دِينُ ٱلۡقَيِّمَةِ5﴾
"Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu, na washike Swala, na watoe Zaka. Na hiyo ndiyo Dini madhubuti." [Al-Bayyina: 5].
Na ushahidi wa Swaumu, ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ كُتِبَ عَلَيۡكُمُ ٱلصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى ٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِكُمۡ لَعَلَّكُمۡ تَتَّقُونَ183﴾
"Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyoandikiwa wale waliokuwa kabla yenu ili mpate kucha Mungu." [Al Baqara: 183].
Na ushahidi wa kuhiji, ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَلِلَّهِ عَلَى ٱلنَّاسِ حِجُّ ٱلۡبَيۡتِ مَنِ ٱسۡتَطَاعَ إِلَيۡهِ سَبِيلٗاۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ ٱللَّهَ غَنِيٌّ عَنِ ٱلۡعَٰلَمِينَ97﴾
"Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezaye njia ya kuiendea. Na atakayekanusha, basi Mwenyezi Mungu si mhitaji kwa walimwengu." [Al-Imran: 97].
Ngazi ya pili: Imani; nayo iko zaidi ya sehemu sabini, ya juu yake zaidi ni kauli ya: Laa ilaaha illa llaahu -Hapana mungu anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu-, na ya chini yake zaidi ni kuondoa udhia njiani, na staha ni sehemu katika imani.
Na nguzo zake ni Sita: Ni kumuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Mwisho, na kuamini Mipango ya Mwenyezi Mungu, ya kheri yake na ya shari yake.
Na ushahidi juu ya nguzo hizi sita ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿لَّيۡسَ ٱلۡبِرَّ أَن تُوَلُّواْ وُجُوهَكُمۡ قِبَلَ ٱلۡمَشۡرِقِ وَٱلۡمَغۡرِبِ وَلَٰكِنَّ ٱلۡبِرَّ مَنۡ ءَامَنَ بِٱللَّهِ وَٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأٓخِرِ وَٱلۡمَلَٰٓئِكَةِ وَٱلۡكِتَٰبِ وَٱلنَّبِيِّـۧنَ...﴾
"Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii..." [Al Baqara: 177].
Na ushahidi wa Kadari (Mipango ya Mwenyezi Mungu), ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّا كُلَّ شَيۡءٍ خَلَقۡنَٰهُ بِقَدَرٖ49﴾
"Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo." [Al-Qamar: 49].
Daraja ya tatu: Ihsan – ina nguzo moja – nayo ni kumwabudu Mwenyezi Mungu kana kwamba unamuona, na ikiwa humuoni, basi Yeye anakuona.
Na ushahidi ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّ ٱللَّهَ مَعَ ٱلَّذِينَ ٱتَّقَواْ وَّٱلَّذِينَ هُم مُّحۡسِنُونَ128﴾
"Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kumcha, na watendao mema."[An-Nahli: 128].
Na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَتَوَكَّلۡ عَلَى ٱلۡعَزِيزِ ٱلرَّحِيمِ217 ٱلَّذِي يَرَىٰكَ حِينَ تَقُومُ218 وَتَقَلُّبَكَ فِي ٱلسَّٰجِدِينَ219﴾
"Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. [217] Ambaye anakuona unaposimama [218] Na mageuko yako kati ya wanaosujudu." [Ash-Shu'ara: 217-219] Na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَمَا تَكُونُ فِي شَأۡنٖ وَمَا تَتۡلُواْ مِنۡهُ مِن قُرۡءَانٖ وَلَا تَعۡمَلُونَ مِنۡ عَمَلٍ إِلَّا كُنَّا عَلَيۡكُمۡ شُهُودًا إِذۡ تُفِيضُونَ فِيهِ...﴾
"Na huwi katika jambo lolote, wala husomi sehemu yoyote katika Qur'ani, wala hamtendi kitendo chochote ila Sisi huwa ni mashahidi juu yenu mnaposhughulika nayo..." [Yunus: 61] Mpaka mwisho wa Aya.
Na ushahidi kutoka katika maneno ya Mtume: Ni Hadithi Mashuhuri ya Jibrili kutoka kwa Omari -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake -kwamba alisema: "Tulikuwa tumekaa kwa Mtume - rehema na amani ziwe juu yake - siku moja, ghafla akatokeza mwanaume mmoja, mwenye nguo nyeupe sana, mwenye nywele nyeusi sana, hazionekani kwake athari za safari, na wala hakuna anayemfahamu yeyote katika sisi, mpaka akakaa kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, akashikanisha magoti yake katika magoti ya Mtume, rehema na amani ziwe juu yake (mfano wa kikao cha tahiyatu) na akaweka mikono yake juu ya mapaja yake, na akasema: Ewe Muhammadi!
"Hebu nieleze kuhusu Uislamu?"
Basi Mtume - rehema na amani ziwe juu yake - akasema: “Uislamu ni kushuhudia ya kwamba hapana mungu apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na kwamba Muhammad ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na kusimamisha Swala, na kutoa Zaka, na kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani, na kwenda kuhiji Makkah kwa mwenye uwezo wa kwenda huko.” Akasema: “Umesema ukweli” -Tukastaajabu kwake-; anamuuliza na kumsadikisha.
Akasema: Basi nieleze kuhusu imani?
Akasema: Ni kumwamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Mwisho, na kuamini Mipango ya Mwenyezi Mungu (kadari) ya heri yake na ya shari yake." Akasema: Umesema ukweli.
Akasema: Basi nieleze kuhusu ihsan?
Akasema: Ni kumuabudu Mwenyezi Mungu kana kwamba unamuona na ikiwa humuoni basi Yeye anakuona.
Akasema: Nifahamishe kuhusu Saa (ya mwisho)?
Akasema: Muulizwaji kuhusu hilo si mjuzi zaidi kuliko muulizaji.
Akasema: Basi nieleze kuhusu alama zake?
Akasema: Kuwa mjakazi atamzaa bosi wake, na kwamba utaona walio peku, uchi, mafukara, wachunga kondoo, wakishindaniana kwa urefu wa majengo.
Kisha akaondoka, nikakaa muda mrefu kidogo, kisha Mtume akaniambia: “Ewe Omari, hivi unamjua ni nani muulizaji?” Nikasema: “Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wajuao zaidi.” Akasema: “Huyo ni Jibrili, alikuja kukufundisheni dini yenu.”
Msingi wa tatu:
Kumjua Mtume wenu Muhammadi - rehema na amani ziwe juu yake, naye ni Muhammadi bin Abdillah bin Abil Muttwalib bin Hashim, na Hashim ni katika Makuraishi, na Makuraishi ni katika Waarabu, na Waarabu wanatokana na kizazi cha Ismaili bin Ibrahim kipenzi wa Mwenyezi Mungu kwake na kwa Nabii wetu, amani iwe juu yao.
Na alikuwa na umri wa miaka sitini na tatu (63), katika hiyo, miaka Arobaini (40) ilikuwa kabla ya utume, na miaka ishirini na tatu (23) akiwa Nabii na Mtume.
Alipewa Unabii kwa neno (Iqraa) Yaani: Soma. Na akapewa Utume kwa neno (Muddathir) Yaani: Aliye jifunika. Na mji wake ni Makka.
Mwenyezi Mungu alimtuma ili kuwaonya watu na ushirikina, na awaite kuja katika kumpwekesha Mwenyezi Mungu (Tauhidi), na ushahidi ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿يَٰٓأَيُّهَا ٱلۡمُدَّثِّرُ1 قُمۡ فَأَنذِرۡ2 وَرَبَّكَ فَكَبِّرۡ3 وَثِيَابَكَ فَطَهِّرۡ4 وَٱلرُّجۡزَ فَٱهۡجُرۡ5 وَلَا تَمۡنُن تَسۡتَكۡثِرُ6 وَلِرَبِّكَ فَٱصۡبِرۡ7﴾
"Ewe uliyejigubika! Simama uonye! Na Mola wako Mlezi mtukuze! Na nguo zako, zisafishe. Na yaliyo machafu yahame! Wala usitoe kwa kutaraji kuzidishiwa. Na kwa ajili ya Mola wako Mlezi, subiri!" [Suratul Mudathir: 1-7]. Na maana ya:
﴿قُمۡ فَأَنذِرۡ﴾
"Simama Uonye" Aonye kutokana na ushirikina, na awaite katika kumpwekesha Mwenyezi Mungu (Tauhidi).
﴿وَرَبَّكَ فَكَبِّرۡ﴾
"Na Mola wako Mlezi mtukuze!"
Yaani: Mtukuze kwa kumpwekesha Yeye peke yake katika ibada.
﴿وَثِيَابَكَ فَطَهِّرۡ﴾
"Na nguo zako, zisafishe."
Yaani: Safisha matendo yako kutokana na ushirikina.
﴿وَٱلرُّجۡزَ فَٱهۡجُرۡ﴾
"Na yaliyo machafu yahame!"
Machafu: Yaani Masanamu. Na kuyahama kwake ni kuyaacha na kuwaacha wafanyaji wake, na kujiepusha nayo pamoja na watu wake.
Haya yalichukua miaka kumi akilingania katika Tauhidi, na baada ya miaka kumi alipandishwa kwenda mbinguni na zikafaradhishwa kwake swala tano, na akaswali Makka miaka mitatu, na baada ya hapo akaamrishwa kuhamia Madina.
Na kuhama (Hijra): Ni kutoka katika mji wa kishirikina kwenda katika mji wa Uislamu.
Na kuhama ni wajibu kwa umma huu kutoka katika mji wa ushirikina kwenda katika mji wa Uislamu, nalo ni jambo endelevu mpaka kitakaposimama Kiyama.
Na ushahidi wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّ ٱلَّذِينَ تَوَفَّىٰهُمُ ٱلۡمَلَٰٓئِكَةُ ظَالِمِيٓ أَنفُسِهِمۡ قَالُواْ فِيمَ كُنتُمۡۖ قَالُواْ كُنَّا مُسۡتَضۡعَفِينَ فِي ٱلۡأَرۡضِۚ قَالُوٓاْ أَلَمۡ تَكُنۡ أَرۡضُ ٱللَّهِ وَٰسِعَةٗ فَتُهَاجِرُواْ فِيهَاۚ فَأُوْلَٰٓئِكَ مَأۡوَىٰهُمۡ جَهَنَّمُۖ وَسَآءَتۡ مَصِيرًا97 إِلَّا ٱلۡمُسۡتَضۡعَفِينَ مِنَ ٱلرِّجَالِ وَٱلنِّسَآءِ وَٱلۡوِلۡدَٰنِ لَا يَسۡتَطِيعُونَ حِيلَةٗ وَلَا يَهۡتَدُونَ سَبِيلٗا98﴾
"Hakika Malaika watawaambia wale ambao wali wafisha nao wamejidhulumu nafsi zao: Mlikuwa vipi? Watasema: Tulikuwa tunaonewa. Watawaambia: Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa na wasaa wa kuhamia humo? Basi hao makazi yao ni Jahannamu, nayo ni marejeo mabaya kabisa.
Isipokuwa wale waliokuwa wanyonge miongoni mwa wanaume na wanawake na watoto wasio na uwezo wa hila ya kuongoka njia ya kuhama. [An-Nisaa: 97-98].
Na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿يَٰعِبَادِيَ ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓاْ إِنَّ أَرۡضِي وَٰسِعَةٞ فَإِيَّٰيَ فَٱعۡبُدُونِ56﴾
"Enyi waja wangu mlioamini! Kwa hakika ardhi yangu ina wasaa. Basi niabuduni Mimi peke yangu." [Al-Ankabut: 56].
Na amesema Imamu Baghawi, Mwenyezi Mungu
amrehemu: "Sababu ya kuteremka kwa Aya hii ni Waislamu waliokuwa Makka hawakuhama, Mwenyezi Mungu akawaita kwa jina la imani."
Na ushahidi unaoonyesha kuwa kuhama ni katika mafundisho ya Mtume ni kauli yake, rehema na amani ziwe juu yake: "Hakutakatika kuhama mpaka ikatike Toba, na wala Toba haitakatika mpaka Jua lichomoze kutokea Magharibi yake."
Alipopata utulivu katika mji wa Madina, aliamrishwa sheria zingine za Uislamu zilizobakia, kama: Zaka, na Swaumu, na Hija, na Adhana, na Jihadi, na kuamrisha mema na kukataza mabaya, yalimchukua hayo miaka kumi.
Na alifariki, rehema na amani ziwe juu yake, na Dini yake ikabakia, na Dini yake hii, hakuna jambo zuri lolote isipokuwa aliujulisha Umma wake jambo hilo, wala jambo la shari isipokuwa aliutahadharisha Umma wake shari hiyo.
Na heri aliyoujulisha umma wake ni Tauhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) na yote anayo yapenda Mwenyezi Mungu na kuyaridhia.
Na shari aliyoutahadharisha umma wake dhidi yake ni Ushirikina na yote anayoyachukia Mwenyezi Mungu na kuyakataa.
Mwenyezi Mungu alimtuma kwa watu wote, na akawajibisha kumtii yeye kwa viumbe wawili waliopewa majukumu, yaani Majini na Binadamu. Na ushahidi ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿قُلۡ يَٰٓأَيُّهَا ٱلنَّاسُ إِنِّي رَسُولُ ٱللَّهِ إِلَيۡكُمۡ جَمِيعًا...﴾
"Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume kwenu nyinyi nyote..." [Al A'araf: 158].
Na Mwenyezi Mungu alikamilisha Dini kupitia yeye; na ushahidi wa hilo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...ٱلۡيَوۡمَ أَكۡمَلۡتُ لَكُمۡ دِينَكُمۡ وَأَتۡمَمۡتُ عَلَيۡكُمۡ نِعۡمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ ٱلۡإِسۡلَٰمَ دِينٗاۚ...﴾
"Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini." [Al-Maidah: 3].
Na ushahidi wa kifo chake ni kauli yake Mtukufu:
﴿إِنَّكَ مَيِّتٞ وَإِنَّهُم مَّيِّتُونَ30 ثُمَّ إِنَّكُمۡ يَوۡمَ ٱلۡقِيَٰمَةِ عِندَ رَبِّكُمۡ تَخۡتَصِمُونَ31﴾
"Kwa hakika wewe utakufa, na wao watakufa. Kisha bila ya shaka mtagombana Siku ya Kiyama mbele ya Mola wenu Mlezi." [Azzumar: 30,31].
Na watu watakapokufa, watafufuliwa, na ushahidi wa hilo ni kauli yake Mtukufu:
﴿مِنۡهَا خَلَقۡنَٰكُمۡ وَفِيهَا نُعِيدُكُمۡ وَمِنۡهَا نُخۡرِجُكُمۡ تَارَةً أُخۡرَىٰ55﴾
"Kutokana nayo, tumekuumbeni, na humo tuna kurudisheni, na kutoka humo tutakutoweni mara nyingine." [Surat Twaha: 55] Na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَٱللَّهُ أَنۢبَتَكُم مِّنَ ٱلۡأَرۡضِ نَبَاتٗا17 ثُمَّ يُعِيدُكُمۡ فِيهَا وَيُخۡرِجُكُمۡ إِخۡرَاجٗا18﴾
"Na Mwenyezi Mungu amekuotesheni katika ardhi kama mimea. Kisha atakurudsheni humo na atakutoeni tena." [Nuh: 17-18].
Na baada ya kufufuliwa, wataulizwa juu ya matendo yao na watalipwa kwa matendo yao hayo, na ushahidi wa hilo ni kauli yake Mtukufu:
﴿...لِيَجۡزِيَ ٱلَّذِينَ أَسَٰٓـُٔواْ بِمَا عَمِلُواْ وَيَجۡزِيَ ٱلَّذِينَ أَحۡسَنُواْ بِٱلۡحُسۡنَى﴾
"...ili awalipe wale waliotenda ubaya kwa waliyo yatenda, na wale waliotenda mema awalipe mema." [An-Najm: 31].
Na atakayepinga kufufuliwa, atakuwa kakufuru, na ushahidi wa hilo ni kauli yake Mtukufu:
﴿زَعَمَ ٱلَّذِينَ كَفَرُوٓاْ أَن لَّن يُبۡعَثُواْۚ قُلۡ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبۡعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلۡتُمۡۚ وَذَٰلِكَ عَلَى ٱللَّهِ يَسِيرٞ7﴾
"Waliokufuru wanadai kuwa hawatafufuliwa. Sema: Kwani? Naapa kwa Mola wangu Mlezi! Hapana shaka mtafufuliwa, na tena hapana shaka mtaambiwa mliyo yatenda. Na hayo ni mepesi kwa Mwenyezi Mungu." [At-Taghabun: 7].
Na aliwatuma Mwenyezi Mungu Mitume wote ili watoe habari njema na wawaonye watu; na ushahidi wa hilo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿رُّسُلٗا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى ٱللَّهِ حُجَّةُۢ بَعۡدَ ٱلرُّسُلِۚ...﴾
"Mitume hao ni wabashiri na waonyaji, ili watu wasiwe na hoja juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kuletewa Mitume..."[An-Nisaai: 165].
Na wa mwanzo wao ni Nuhu, amani ziwe juu yake.
Na wa mwisho wao ni Muhammadi, rehema na amani ziwe juu yake, na yeye ndiye mwisho wa Manabii, hakuna Nabii baada yake; na ushahidi wa hilo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَآ أَحَدٖ مِّن رِّجَالِكُمۡ وَلَٰكِن رَّسُولَ ٱللَّهِ وَخَاتَمَ ٱلنَّبِيِّـۧنَ...﴾
"Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii..." [Al-Ahzaab: 40].
Na ushahidi wa kuwa wa mwanzo wao ni Nuhu ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّآ أَوۡحَيۡنَآ إِلَيۡكَ كَمَآ أَوۡحَيۡنَآ إِلَىٰ نُوحٖ وَٱلنَّبِيِّـۧنَ مِنۢ بَعۡدِهِ...﴾
"Hakika Sisi tumekuteremshia wahyi wewe kama tulivyowateremshia wahyi Nuhu na Manabii walio kuwa baada yake..." [An-Nisaa: 163].
Na kila umma alioutumia Mwenyezi Mungu Mtume kwanzia kwa Nuhu mpaka kwa Muhammadi alikuwa akiwaamrisha kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na akiwakataza kumuabudu shetani, na ushahidi ni kauli yake Mtukufu:
﴿وَلَقَدۡ بَعَثۡنَا فِي كُلِّ أُمَّةٖ رَّسُولًا أَنِ ٱعۡبُدُواْ ٱللَّهَ وَٱجۡتَنِبُواْ ٱلطَّٰغُوتَ...﴾
"Na kwa hakika kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni Shetani..." [An-Nahli: 36].
Na akawawajibishia Mwenyezi Mungu waja wote kwamba kumkufuru Shetani, na kumuamini Mwenyezi Mungu.
Amesema bin Qayim, Mwenyezi Mungu Mtukufu amrehemu: "Maana ya Twaghuti (shetani): Ni kila ambacho mja atavuka mpaka wake, kuanzia chenye kuabudiwa au kufuatwa au kutiiwa.'
Matwaghuti (vinavyo abudiwa kinyume na Mwenyezi Mungu) ni mengi. Na wakuu wao ni watano: Ibilisi Mwenyezi Mungu amlaani, na atakayeabudiwa naye akaridhia, na atakayewaita watu wamuabudu, na atakaye dai kujua chochote katika elimu ya mambo yaliyo fichikana, na atakayehukumu kinyume na yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu.
Na ushahidi wa hilo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿لَآ إِكۡرَاهَ فِي ٱلدِّينِۖ قَد تَّبَيَّنَ ٱلرُّشۡدُ مِنَ ٱلۡغَيِّۚ فَمَن يَكۡفُرۡ بِٱلطَّٰغُوتِ وَيُؤۡمِنۢ بِٱللَّهِ فَقَدِ ٱسۡتَمۡسَكَ بِٱلۡعُرۡوَةِ ٱلۡوُثۡقَىٰ لَا ٱنفِصَامَ لَهَاۗ وَٱللَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ256﴾
"Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uongofu umekwishapambanuka mbali na upotofu. Basi anaye mkataa Shetani na akamuamini Mwenyezi Mungu, bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisicho vunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua." [Al-Baqara: 256] Na hii ndiyo maana ya "Laa ilaaha illa llaah (Hapana mungu apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu)." Na ilikuja katika Hadithi: "Kichwa cha mambo yote ni Uislamu, na nguzo yake ni Swala, na kilele chake ni Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu."
Na Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye zaidi.
***
***