PHPWord

 

 

 

 

 

صِفَةُ العُمْرَةِ

 

NAMNA YA KUFANYA UMRAH

 

 

 

 

 

Mtunzi

Abdulaziz bin Abdillah bin Baaz

 


بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

NAMNA YA KUFANYA UMRAH

Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu peke yake, na baada ya hayo:

Huu ni muhtasari mfupi wa matendo mbalimbali ya ibada ya Umrah. Na kwa msomaji, maelezo ya hayo ndiyo haya:

Mwenye kufanya Umrah atakapofika kwenye Miqat (sehemu za kunuia Hija au Umrah), inapendekezwa aoge na kujisafisha. Mwanamke pia atafanya hivyo hata kama atakuwa katika hedhi au katika damu ya baada ya kuzaa (nifasi), isipokuwa hataruhusiwa kuzunguka Al-Ka'aba mpaka atwahirike na aoge.

Mwanamume anaweza kujipaka manukato kwenye mwili wake kabla ya kuvaa nguo zake za Hija au Umrah (ihramu). Ikiwa haitawezekana kuogea kwenye Miqat, basi hakuna ubaya wowote katika hilo na itapendekezwa kwamba aoge anapofika Makka kabla ya kuizunguka Al-Ka'aba ikiwa hilo litawezekana.

Mwanamume atavua nguo zote za kawaida zilizoshonwa na avae kikoi na shuka, na inapendekezwa ziwe nyeupe na safi.

Ama mwanamke, yeye atahirimia katika nguo zake za kawaida (isipokuwa hatavaa nikabu, barakoa wala glovu. Hivyo atavivua na aufunike uso wake na mikono yake kutokana na wanaume wasiokuwa maharimu wake kwa nguo nyinginezo) ambazo hazina mapambo wala si za umaarufu.

Kisha ataweka nia ya kuingia katika ibada ya Umra moyoni mwake na kuitamka kwa ulimi wake akisema: Labbayka umrah yaani, “Nimekuitikia kwa kufanya Umrah.” au “Allahummma labbayka umrah yaani,Ewe Mwenyezi Mungu, nimekuitikia kwa kufanya Umrah.”

Iwapo aliyehirimia Umrah atachelea kwamba hataweza kutekeleza ibada zake kwa sababu ni mgonjwa au anaogopa kuzuiliwa na adui au mfano wa hayo, basi anaruhusiwa kuweka sharti anapohirimia kwa kusema: "Fa-in habasanii haabisun, famahil-lii haythu habastaniiyaani, Ikiwa nitazuiliwa na kizuizi, basi mahali pangu pa kutoka katika ihramu ni pale utakaponizuilia." Haya ni kwa mujibu wa Hadithi ya Dhwuba’ah bint Az-Zubayr, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi.(1)

Kisha atafanya Talbiyah, yaani mwitikio wa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ambao ni, Labbayka-llaahumma labbayka. Labbayka laa shariika laka labbayka. Innalhamda wanni'imata laka walmulk laa shariika laka yaani, Nimekuitikia ewe Mwenyezi Mungu nimekuitikia! Nimekuitikia hauna mshirika nimekuitikia. Hakika sifa njema, neema na ufalme ni vyako, huna mshirika.

((لَبَّيْكَ اللَّهُمَّ لَبَّيْكَ، لَبَّيْكَ لَا شَرِيكَ لَكَ لَبَّيْكَ، إِنَّ الْحَمْدَ وَالنِّعْمَةَ لَكَ وَالْمُلْكَ، لَا شَرِيكَ لَكَ)).

Na anafaa kusema kwa wingi mwitikio huu, na kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kumuomba dua hadi afike kwenye Nyumba ya Al-Ka'aba.

Atakapoufikia Msikiti Mtakatifu wa Makka, atautanguliza mguu wake wa kulia wakati wa kuingia na aseme: Bismillaahi was-swalaatu was-salaamu 'alaa rasuulillaahi. A'uudhu billaahi al-'adhwiim, wabiwajhihi alkariim, wasultwaanihi alqadiim, minash-shaytwaan arrajiim. Allaahummaftah lii abwaaba rahmatika” yaani, Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na rehema na amani ziwe juu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Ninajilinda kwa Mwenyezi Mungu Mkuu, na kwa uso wake mtukufu, na kwa utawala wake wa kale, kutokana na Shetani aliyelaaniwa. Ewe Mwenyezi Mungu, nifungulie milango ya rehema zako.

Anapofika kwenye Nyumba Tukufu ambayo ni Al-Kaaba, ataacha kufanya mwitikio (Talbiyah), kisha aende kwenye Jiwe Jeusi, alielekee, kisha aliguse kwa mkono wake wa kulia na kulibusu kama hilo litawezekana, lakini asiwaudhi watu kwa kuleta msongamano. Aseme wakati anapoligusa: Bismillahi, wallahu akbar” yaani, Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mkubwa. Kama itakuwa vigumu kulibusu, ataligusa kwa mkono au kwa fimbo au kwa kitu mfano wake, kisha akibusu kile alicholigusa kwacho. Na kama itakuwa vigumu kuligusa, basi ataliashiria na aseme: Allahu akbar yaani, Mwenyezi Mungu ni Mkubwa.na asibusu kile alichoashiria kwacho.

Ili tawafu iwe sahihi, ni sharti kwamba mwenye kutufu awe safi kutokana na hadathi (uchafu wa kiibada) ndogo na kubwa. Kwa sababu, tawafu ni kama swala, isipokuwa iliruhusiwa kuzungumza ndani yake.

Ataiweka Al-Kaaba upande wake wa kushoto na aizunguke mara saba. Kila anapokuwa sawa na kona ya Yemeni, ataigusa kwa mkono wake wa kulia ikiwezekana na kusema: “Bismillahi, wallahu akbar” yaani, “Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mkubwa.lakini asiibusu. Ikiwa itakuwa vigumu kwake kuigusa, ataiacha na kuendelea na tawafu yake, na asiiashirie wala asiseme: “Allahu akbar” yaani, Mwenyezi Mungu ni Mkubwa.” Kwa sababu hilo halikusimuliwa kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake.

Ama Jiwe Jeusi, kila anapokuwa sawa nalo, ataligusa na kulibusu kama tulivyotaja hapo awali. Vinginevyo, ataliashiria tu na kusema: “Allahu akbar” yaani, Mwenyezi Mungu ni Mkubwa. Inapendekezwa kutembea haraka lakini kwa hatua za karibu karibu katika mizunguko mitatu ya kwanza ya Tawafu ya kufika Makka (Tawaf al-Qudum), kwa wanaume tu.

Pia inapendekezwa kwa mwanamume kufanya Idhtwibaa katika Tawaf al-Qudum (Tawafu ya kufika Makka) katika mizunguko yote. Idhtwibaa inamaanisha kuweka sehemu ya katikati ya upande wa juu wa shuka lake kwenye kwapa lake la kulia na ncha zake mbili za juu kwenye bega lake la kushoto.

Na ni sunna pia kufanya dhikri na kuomba dua kwa wingi, kiasi iwezekanavyo katika mizunguko yote.

Hakuna dua wala dhikri mahususi katika tawafu. Bali mtu ataomba na kumjata Mwenyezi Mungu kwa dua na utajo wowote anaoweza. Na atasema baina ya kona mbili za Al-Ka'aba, yaani, kona yenye Jiwe Jeusi na kona ielekeayo Yemeni:

﴿رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ (سورة البقرة، 201)

“Rabbanaa aatinaa fid-dun-yaa hasana, wafil-aakhirati hasana, waqinaa 'adhaaban-naar” yaani,Mola wetu Mlezi, tupe duniani mema, na Akhera mema, na utulinde kutokana na adhabu ya Moto.” [Suratul-Baqara: 201]

Haya atayasema katika kila mzunguko. Kwa sababu, hili lilithibiti kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.

Ataumaliza mzunguko wa saba kwa kuligusa Jiwe Jeusi na kulibusu ikiwezekana, au kuliashiria huku akisema Allahu Akbaryaani, Mwenyezi Mungu ni Mkubwa.” kulingana na maelezo yaliyotajwa kabla ya muda mfupi. Baada ya kukamilisha mzunguko huu, atavaa shuka lake kwa kuliweka juu ya mabega yake na kona zake mbili za upande wa juu ataziweka kwenye kifua chake.

Kisha ataswali rakaa mbili nyuma ya Maqam Ibrahim ikiwa itakuwa rahisi kufanya hivyo. Lakini kama hataweza kufanya hivyo, basi ataswalia mahali popote pale Msikitini. Baada ya kusoma surat Al-Fatihah, atasoma:

Qul yaa ayyuhalkaafiruunyaani,Sema: Enyi makafiri. [Suratul-Kafirun: 1-6] katika rakaa ya kwanza, na Qul huwallaahu Ahadyaani, Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni wa Pekee. [Suratul-Ikhlas: 1-4] katika rakaa ya pili.

Hilo ndilo bora zaidi, lakini akisoma sura nyinginezo, basi hakuna tatizo. Kisha, baada ya kumaliza rakaa mbili hizi, ataelekea kwenye Jiwe Jeusi, ikiwa hilo litawezekana.

Kisha atatoka aende kwenye Safaa na apande juu yake au asimame hapo karibu. Kupanda juu yake ndiyo bora zaidi ikiwezekana. Kisha atasoma maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿إِنَّ ٱلصَّفَا وَٱلمَرۡوَةَ مِن شَعَآئِرِ ٱللَّهِ.. (سورة البقرة، 158)

Innasswafaa wal Marwata min sha'aairillahyaani,Hakika vilima vya Safaa na Marwa ni katika alama za Mwenyezi Mungu. [Suratul-Baqarah: 158]

Na inapendekezwa kwamba aelekee Kiblah, amsifu na kumtukuza Mwenyezi Mungu. Atasema: Laa ilaaha illallaahu wallaahu akbar. Laa ilaaha illallaahu wahdahuu laa shariika lahuu, lahulmulku walahulhamdu wahuwa 'alaa kulli shay-in qadiir. Laa ilaaha illallaahu wahdahuu, anjaza wa'adahuu, wanaswara 'abdahuu, wahazamal-ahzaaba wahdahuu” yaani, Hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mkubwa. Hakuna mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu asiye na mshirika. Ufalme ni wake, na sifa njema ni zake, naye ni Muweza wa kila kitu. Hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu peke yake, alitekeleza ahadi yake, na akamnusuru mja wake, na akayashinda makundi (ya maadui) peke yake.(2) Kisha ataomba awezacho huku ameinua juu mikono, na atairudia dhikri hii na kuomba dua mara tatu.

Kisha atateremka na atembee akienda Marwah mpaka aifikie alama (taa ya rangi ya kijani kibichi), na hapo mwanamume ataharakisha mwendo wa kutembea mpaka aifikie alama ya pili.

Ama mwanamke, yeye haruhusiwi kuharakisha mwendo katika kutembea; kwa sababu yeye ni uchi. Kisha atatembea na kupanda juu ya Marwah au kusimama hapo karibu. Kupanda juu yake ndiyo bora zaidi ikiwezekana. Kisha atasema na kufanya juu ya Marwah namna alivyosema na kuyafanya juu ya Safaa. Kisha atateremka chini na kutembea katika sehemu aliyotembea na kuongeza kasi katika sehemu ambayo aliongeza kasi mpaka afike Safaa. Atafanya hivyo mara saba. Kwenda kwake ni raundi, na kurudi kwake ni raundi pia. Ikiwa atafanya Sa'yi huku amepanda, basi hakuna ubaya, hasa inapobidi.

Inapendekezwa kwamba afanye dhikri na kuomba dua kwa wingi katika Sa'yi yake awezavyo. Pia inapendekezwa kwamba awe safi kutokana na hadathi (uchafu wa kiibada) kubwa na ndogo. Hata hivyo, ikiwa ataifanya bila twahara, basi hilo bado litamtosheleza.

Anapomaliza Sa’yi, mwanamume atanyoa nywele za kichwa chake au atazifupisha. Kuzinyoa ndiyo bora, lakini ikiwa kuwasili kwake Makka ni karibu na wakati wa Hija, basi kuzifupisha ndiyo bora kwake ili aweze kunyoa sehemu ya kichwa chake iliyosalia wakati wa Hija. Ama mwanamke, yeye atakusanya nywele zake na kuzipunguza kiasi cha ncha ya kidole au chini ya hivyo. Mtu aliyehirimia Umrah atakapofanya kile kilichotajwa, basi Umrah yake itakuwa imekamilika, na sifa njema ni za Mwenyezi Mungu. Hapo, kila alichoharamishiwa kwa sababu ya ihramu, sasa kitakuwa halali kwake.

Mwenyezi Mungu atuwezeshe sisi na ndugu zetu Waislamu wote kuifahamu Dini yake na kuwa imara ndani yake, na aikubali kutoka kwa kila mtu. Kwani, Yeye aliyetakasika ndiye Mpaji, Mkarimu.

Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wake na Mtume wake, Nabii wetu Muhammad, na ahali zake, Maswahaba wake, na wafuasi wake waliomfuata kwa wema mpaka Siku ya Malipo.

Huu ni Muhtasari Mfupi wa Matendo mbalimbali ya Ibada ya Umrah. Ulitolewa na Ofisi ya Mheshimiwa, mtunzi wake, tarehe 13/2/1416 Hijria (Mkusanyiko wa Fatwa na Makala ya Sheikh Ibn Baaz, 17/425).


() Imepokelewa na Muslim, nambari 1218.

() As-Sunan Al-Kubraa, cha Al-Bayhaqii, nambari 10117.