PHPWord

 

 

 

دَفْنُ المَوتَى فِي المَسَاجِدِ

 

KUZIKA MAITI MISIKITINI

 

 

لِسَمَاحَةِ الشَّيْخِ العَلَّامَةِ

عَبْدِ العَزِيزِ بْنِ عَبْدِ اللهِ بْنِ بَازٍ

رَحِمَهُ اللهُ

 

Mtunzi Mheshimiwa, Sheikh,

Abdulaziz bin Abdillah bin Baaz

 

 

 


بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Makala ya kumi na moja: Kuzika wafu misikitini

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehema na amani zimshukie Mtume wa Mwenyezi Mungu, na ali zake, na wote wanaofuata muongozo wake. Ama baada ya hayo:

Nilisona gazeti la "Al-Khartum" lililotolewa mnamo 17/4/1415 Hijria, na nikapata yamechapishwa humo maelezo ya kumzika bwana Muhammad Al-Hasan Al-Idrisii karibu na baba yake katika msikiti wao katika mji wa Umdurman... n.k.

Mwenyezi Mungu alipowajibisha kuwapa nasaha Waislamu, na kuweka wazi kukanusha kwa mwenye kukanusha, niliona kwamba nitahadharishe ya kuwa kuwazika maiti katika misikiti ni jambo lisiloruhusiwa. Bali ni katika njia za ushirikina, na ni katika matendo ya Mayahudi na Wakristo ambayo Mwenyezi Mungu aliwakemea kwa sababu yake, na Mtume wake, rehema na amani ziwe juu yake, aliwalaani, kama ilivyokuja katika Sahihi mbili kutoka kwa Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, kwamba alisema: "Mwenyezi Mungu aliwalaani Mayahudi na Wakristo. Waliyafanya makaburi ya manabii wao kuwa misikiti." Na katika Sahihi Muslim, kutoka kwa Jundab bin Abdullah, kutoka kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alisema: "Sikilizeni! Hakika wale waliokuwa kabla yenu walikuwa wakifanya makaburi ya manabii wao na wema wao kuwa misikiti. Sikilizeni! Msiyafanye makaburi kuwa misikiti. Kwani ninakukatazeni hilo?" Na kuna hadithi nyingi zenye maana hii.

Basi la wajibu kwa Waislamu kila mahali -kuanzia serikali na raia -ni kumcha Mwenyezi Mungu, na kujihadhari na yale aliyoyakataza, na wawazike wafu wao nje ya misikiti, kama Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, na Maswahaba wake walivyokuwa wakiwazika wafu nje ya misikiti, na vile vile wale waliokuja baada yao na kuwafuata kwa wema.

Na ama kupatikana kwa kaburi la Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, katika msikiti wake, na pia kupatikana humo makaburi ya Maswahaba wake wawili, Abubakari na Omari, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao, hilo si hoja ya kuwazika maiti katika misikiti. Kwa sababu yeye, rehema na amani ziwe juu yake, alizikwa ndani ya nyumba yake - katika nyumba ya Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie - kisha Maswahaba wake hao wawili wakazikwa pamoja naye. Wakati Al-Walid bin 'Abdul-Malik alipoupanua msikiti wa Mtume, akaiingiza nyumba yake (Mtume) ndani ya msikiti baada ya miaka mia moja ya kwanza ya Hijiria. Wanazuoni walimpinga kwa hilo, lakini yeye aliona kuwa hilo haliwezi kuzuia upanuzi, na kwamba jambo hilo lilikuwa wazi na haliwezi kumchanganya yeyote.

Kwa hayo, inadhihirika wazi kwa kila Muislamu kwamba yeye, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na Maswahaba wake wawili, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, hawakuzikwa msikitini. Kuingizwa kwao humo kwa sababu ya upanuzi sio hoja ya kuruhusu kuzika katika misikiti; kwa sababu hawako msikitini, bali wako nyumbani kwa Mtume, rehema na amani ziwe juu yake. Na kwa sababu matendo ya Al-Walid hayawezi kuwa hoja ya mtu yeyote katika hilo. Bali hoja iko katika Kitabu na Sunna, na katika makubaliano ya watangulizi wema wa umma huu, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, na atujaalie kuwa miongoni mwa wafuasi wao kwa wema.

Kwa ajili ya Nasaha na kuondoa dhima, imeandikwa barua hii mnamo: 14/5/1415 Hijiria.

Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuafikisha, na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad, jamaa zake, na Maswahaba wake, na wafuasi wao kwa wema.

 

***