PHPWord

 

 

 

التَّحْذِيرُ مِنْ بِنَاءِ المَسَاجِدِ

عَلَى القُبُورِ

 

TAHADHARI DHIDI YA KUJENGA MISIKITI JUU YA MAKABURI

 

 

لِسَمَاحَةِ الشَّيْخِ العَلَّامَةِ

عَبْدِ العَزِيزِ بْنِ عَبْدِ اللهِ بْنِ بَازٍ

رَحِمَهُ اللهُ

 

Mtunzi Mheshimiwa, Sheikh,

Abdulaziz bin Abdillah bin Baaz

 

 


بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Makala ya kumi: Kutahadharisha dhidi ya kujenga misikiti kwenye makaburi

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehema na amani ziwe juu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Ama baada ya hayo: Nimeona kile kilichochapishwa katika toleo la tatu la Jarida la Raabitwatul-Uluum Al-Islaamiyya katika mlango wa "Habari za Waislamu katika mwezi mmoja": 'Hakika Raabitwatul-Uluum Al-Islaamiyya katika Ufalme wa Kihashimi wa Yordani inakusudia kujenga msikiti kwenye pango jipya lililogunduliwa katika kijiji cha Ar-Rahiib, nalo ni pango ambalo linasemwa kuwa wale Watu wa pango waliotajwa katika Qur'ani Tukufu walilala humo.' Mwisho.

Kwa sababu ya wajibu wa kushauri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kuwashauri waja wake, niliona kwamba nielekeze neno katika jarida lenyewe la Raabitwatul-Uluum Al-Islaamiyya katika Ufalme wa Kihashimi wa Yordani likijumuisha nasaha kwa jumuiya hiyo dhidi ya kutekeleza kile ilichokusudia cha kujenga msikiti kwenye pango lililotajwa hapo juu. Na hilo si isipokuwa ni kwa sababu kujenga misikiti kwenye makaburi ya Manabii, watu wema na athari zao ni katika yale ambayo sheria kamili ya Kiislamu ilikuja kukataza na kuonya dhidi yake, na kumlaani mwenye kufanya hivyo; kwa sababu ni katika mambo ya ushirikina na kupitiliza kiasi kuhusiana na Manabii na watu wema. Hali halisi ya mambo ni ushahidi juu ya usahihi wa yale ambayo Sheria ilikuja nayo, na ni ushahidi kwamba yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, na ni uthibitisho wa wazi na hoja thabiti ya ukweli wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika yale aliyoyasema juu ya Mwenyezi Mungu na akaufikishia umma wake. Kila mtu anayezingatia hali ya ulimwengu wa Kiislamu na kile kilichotokea ndani yake cha ushirikina na kupitiliza kiasi kwa sababu ya kujenga misikiti juu ya makaburi na kuyatukuza, na kuyavika mavazi, kuyapamba, na kuyawekea wahudumu, kwa hakika atajua kwamba ni miongoni mwa njia za ushirikina, na kwamba katika mazuri ya sheria ya Kiislamu ni kuyazuia hayo na kuonya dhidi ya kuyajenga.

Na katika yale yaliyokuja kuhusiana na hilo ni yale yaliyosimuliwa na Masheikh wawili Bukhari na Muslim, Mwenyezi Mungu awarehemu, kutoka kwa Aisha, Mwenyezi Mungu amridhie, kwamba alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alisema: "Mwenyezi Mungu aliwalaani Mayahudi na Wakristo. Waliyafanya makaburi ya manabii wao kuwa misikiti." Aisha akasema, hapo alikuwa anaonya dhidi ya kile walichokifanya. Aisha akasema: Kama si kwa sababu ya hilo, basi wangeliweka wazi kaburi lake, lakini alihofia kwamba linaweza kufanywa msikiti. Na katika Sahihi mbili pia kuna kwamba "Ummu Salama na Ummu Habiba, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, walimueleza Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kanisa waliloliona katika ardhi ya Uhabeshi (Ethiopia), na picha zilizokuwa ndani yake. Basi Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake akasema: "Hao pindi mtu mwema miongoni mwao anapokufa, wanajenga msikiti juu ya kaburi lake, na kuchora picha hizo ndani yake. Hao ndio viumbe waovu mbele ya Mwenyezi Mungu."

Na katika Sahihi Muslim, Jundab bin Abdillah, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, alisema: Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, siku tano kabla ya kufa kwake, akisema: "Hakika mimi ninakimbilia kwa Mwenyezi Mungu kwamba nisijekuwa na rafiki mwendani miongoni mwenu. Kwani Mwenyezi Mungu amenifanya mimi kuwa mwendani kama alivyomfanya Ibrahim kuwa mwendani. Na lau kama ningekuwa wa kujifanyia mwendani katika umma wangu, basi ningemfanya Abubakari kuwa mwendani wangu. Fahamuni kuwa hakika wale waliokuwa kabla yenu walikuwa waki yafanya makaburi ya Manabii wao kuwa Misikiti. Tambueni kuwa, msiyafanye makaburi kuwa Misikiti, kwani hakika mimi ninakukatazeni hilo." Na Aya na hadithi katika mlango huu ni nyingi.

Na maimamu wengi miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu kutoka katika madhehebu yote manne na mengineyo walisema kwamba misikiti isijengwe juu ya makaburi, na wakaonya dhidi ya hili, kwa mujibu wa Sunnah ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na kwa njia ya kunasihi umma na kuuonya usije ukaanguka katika upotofu ambao wale waliokuwa kabla ya umma huu walianguka ndani yake miongoni mwa Wayahudi na Wakristo.

Kwa hivyo, la wajibu juu ya Jumuiya ya Al-Uluum Al-Islaamiyya ya huko Yordani, na Waislamu wengine wote ni kufuata Sunnah, kufuata njia ya Maimamu, na kutahadhari yale ambayo Mwenyezi Mungu na Mtume wake wametahadharisha. Kwani katika hilo kuna kutengenea kwa waja, furaha yao na kuokoka kwao duniani na akhera. Na baadhi ya watu katika mlango huu walishikamana na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kuhusiana na kisa cha wale Watu wa Pangoni:

﴿...قَالَ ٱلَّذِينَ غَلَبُواْ عَلَىٰٓ أَمۡرِهِمۡ لَنَتَّخِذَنَّ عَلَيۡهِم مَّسۡجِدٗا﴾

"Wakasema wale walioshinda katika shauri lao: Bila ya shaka tutawajengea msikiti juu yao." [Al-Kahf: 21]

 

 

Jibu la hilo ni kusema kwamba: Mwenyezi Mungu Mtukufu alieleza kuhusu viongozi na watu wenye udhibiti wa Mamlaka wakati huo kuwa walisema maneno haya, lakini hilo si kwamba Mwenyezi Mungu aliridhia maneno yao hayo na kuyakubali. Bali aliyasema kwa njia ya kashifa, kuonyesha kasoro yake, na kuwaweka watu mbali na kitendo chao hicho. Hili linathibitishwa na ukweli kwamba Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ambaye aya hii iliteremshwa juu yake, na ambaye ndiye mjuzi wa tafsiri yake zaidi ya watu wote alikataza umma wake kujenga misikiti juu ya makaburi, na akawaonya juu ya hili na kuwalaani na kuwakashifu wale wanaofanya hivyo.

Lau kuwa hilo lingekuwa linaruhusiwa, basi Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani zimshukie, asingekuwa mkali kiasi hicho kikubwa, na akakwenda mbali zaidi katika hilo hadi kumlaani anayefanya hivyo, na akajulisha kwamba wao ni miongoni mwa viumbe waovu mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na hili linamtosha na kumridhisha mtafutaji haki. Na hata kama tungekubali kwamba kujenga misikiti juu ya makaburi kuliruhusika kwa wale waliotangulia kabla yetu, hilo halingeruhusiwa kwetu kuwafuata katika suala hili. Kwa sababu, sheria yetu inafuta sheria zilizotangulia, na Mtume wetu, rehema na amani ziwe juu yake, ndiye mwisho wa Mitume, na sheria yake ni kamilifu na ya ujumla. Naye alitukataza kujenga misikiti juu ya makaburi. Kwa hivyo, haturuhusiwi kumhalifu, na tunalazimika kumfuata, kushikamana na kile alichokuja nacho, na kuacha kile kinachohalifu hilo katika sheria za zamani, na desturi zinazopendekezwa tu na wale wanaozifanya, kwa sababu hakuna kilicho kamili zaidi kuliko sheria ya Mwenyezi Mungu, wala hakuna muongozo mzuri zaidi kuliko muongozo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.

Na Mwenyezi Mungu ndiye aombwaye atuwezeshe sisi na Waislamu wote kuwa imara katika dini yake, na kushikamana na sheria ya Mtume wake Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake; katika maneno na vitendo, kwa nje na ndani, na katika mambo mengine yote mpaka tutakapokutana na Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Aliye karibu mno.

Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wake na Mtume wake Muhammad, jamaa zake na Maswahaba wake, na wale wanaofuata muongozo wake mpaka Siku ya Malipo.

 

***