بَيَانُ كُفْرِ وَضَلَالِ مَنْ زَعَمَ أَنَّهُ يَجُوزُ لِأَحَدٍ الخُرُوجُ
مِنْ شَرِيعَةِ مُحَمَّدٍ ﷺ
KUBAINISHA UKAFIRI NA UPOTOVU WA WALE WANAODAI KUWA INARUHUSIKA KWA MTU YEYOTE KUTOKA KATIKA SHARI ́A YA MUHAMMAD, REHEMA NA AMANI ZIWE JUU YAKE
لِسَمَاحَةِ الشَّيْخِ العَلَّامَةِ
عَبْدِ العَزِيزِ بْنِ عَبْدِ اللهِ بْنِ بَازٍ
رَحِمَهُ اللهُ
Mtunzi Mheshimiwa, Sheikh,
Abdulaziz bin Abdillah bin Baaz
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ
Makala ya Kumi na Mbili: Kubainisha ukafiri na upotofu wa anayedai kuwa inaruhusiwa kwa yeyote kutoka katika Sheria ya Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake
Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote, na rehema na amani ziwe juu ya mwisho wa Manabii na Mitume, Nabii wetu Muhammad, na familia yake na Maswahaba wake wote.
Ama baada ya hayo: Nilisoma makala iliyochapishwa katika jarida la Ash-Sharq Al-Awsat nambari (5824) ya tarehe 5/6/1415 Hijria, ilioandikwa na anayejiita: Abdul-Fattah Al-Haaiki, kwa anwani: (Ufahamu usio sahihi).
Na muhtasari wa makala yenyewe ni kukataa kwake kile kinachojulikana katika dini ya Uislamu bila ya shaka yoyote, na kwa maandiko (matakatifu) na makubaliano ya wanazuoni; ambacho ndiyo ujumla wa ujumbe wa Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake, kwa watu wote, na madai yake kwamba yeyote ambaye hakumfuata Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na hakumtii, lakini akabakia katika Uyahudi au Ukristo, yuko katika dini ya haki, kisha akamfanyia kiburi Mola wa walimwengu wote -Aliyetakasika- kuhusiana na hekima yake katika kuwaadhibu makafiri na waasi, yeye akaona kwamba hilo ni mchezo mtupu.
Aliyapotosha maandiko ya dini, akayaweka katika sehemu zisizokuwa zake, na akayafasiri kama yanavyotaka matakwa yake, na akapuuza ushahidi wa kisheria na maandiko ya wazi yanayoonyesha ujumla wa utume wa Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake, na ukafiri wa anayesikia habari zake kisha asimfuate, na kwamba hakika Mwenyezi Mungu hatakubali dini nyingine isipokuwa Uislamu, na maandiko mengine ya wazi ambayo nimeyaacha. Alifanya hivi ili wajinga wadanganyike na maneno yake. Hiki alichokifanya ni ukafiri wa wazi, kutoka katika Uislamu, na kumkanusha Mwenyezi Mungu aliyetakasika, aliyetukuka, na pia Mtume wake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kama anavyojua hayo anayesoma makala hiyo miongoni mwa watu wenye elimu na imani.
Basi la wajibu kwa kiongozi mkuu ni kumpeleka mahakamani, kumtaka atubu na kumhukumu kulingana na inavyotakiwa na Sheria safi.
Mwenyezi Mungu Mtukufu aliuweka wazi ujumbe wa ujumla wa Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake, na wajibu wa kumfuata kwa viumbe wazito wawili (majini na watu), na hili hakosi kulijua mtu yeyote mwenye elimu hata chache tu miongoni mwa Waislamu.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿قُلۡ يَٰٓأَيُّهَا ٱلنَّاسُ إِنِّي رَسُولُ ٱللَّهِ إِلَيۡكُمۡ جَمِيعًا ٱلَّذِي لَهُۥ مُلۡكُ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضِۖ لَآ إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ يُحۡيِۦ وَيُمِيتُۖ فَـَٔامِنُواْ بِٱللَّهِ وَرَسُولِهِ ٱلنَّبِيِّ ٱلۡأُمِّيِّ ٱلَّذِي يُؤۡمِنُ بِٱللَّهِ وَكَلِمَٰتِهِۦ وَٱتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمۡ تَهۡتَدُونَ158﴾
"Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume kwenu nyinyi nyote, niliyetumwa na Mwenyezi Mungu Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Hapana mungu ila Yeye anayehuisha na anayefisha. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake asiyejua kusoma na kuandika, ambaye anamuamini Mwenyezi Mungu na maneno yake. Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka." [Al-A'raaf: 158] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...وَأُوحِيَ إِلَيَّ هَٰذَا ٱلۡقُرۡءَانُ لِأُنذِرَكُم بِهِۦ وَمَنۢ بَلَغَ...﴾
"Na nimefunuliwa Qur'ani hii ili kwayo nikuonyeni nyinyi na kila inayemfikia." [Al-An-aam: 19] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿قُلۡ إِن كُنتُمۡ تُحِبُّونَ ٱللَّهَ فَٱتَّبِعُونِي يُحۡبِبۡكُمُ ٱللَّهُ وَيَغۡفِرۡ لَكُمۡ ذُنُوبَكُمۡۚ وَٱللَّهُ غَفُورٞ رَّحِيمٞ31﴾
"Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu." [Al-'Imran: 31] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَمَن يَبۡتَغِ غَيۡرَ ٱلۡإِسۡلَٰمِ دِينٗا فَلَن يُقۡبَلَ مِنۡهُ وَهُوَ فِي ٱلۡأٓخِرَةِ مِنَ ٱلۡخَٰسِرِينَ85﴾
"Na anayetafuta dini isiyokuwa Uislamu, haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa miongoni mwa wenye kupata hasara." [Al-Imran: 85] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَمَآ أَرۡسَلۡنَٰكَ إِلَّا كَآفَّةٗ لِّلنَّاسِ بَشِيرٗا وَنَذِيرٗا...﴾
"Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mbashiri na muonyaji." [Saba: 28] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَمَآ أَرۡسَلۡنَٰكَ إِلَّا رَحۡمَةٗ لِّلۡعَٰلَمِينَ107﴾
"Nasi hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu wote." [Al-Anbiya: 107]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...وَقُل لِّلَّذِينَ أُوتُواْ ٱلۡكِتَٰبَ وَٱلۡأُمِّيِّـۧنَ ءَأَسۡلَمۡتُمۡۚ فَإِنۡ أَسۡلَمُواْ فَقَدِ ٱهۡتَدَواْۖ وَّإِن تَوَلَّوۡاْ فَإِنَّمَا عَلَيۡكَ ٱلۡبَلَٰغُۗ وَٱللَّهُ بَصِيرُۢ بِٱلۡعِبَادِ﴾
"Na waambie wale waliopewa Kitabu na wale wasio na kisomo: 'Je, mmesilimu?' Wakisilimu, basi wameongoka. Na wakikengeuka, basi juu yako ni kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake." [Al-'Imran: 20]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿تَبَارَكَ ٱلَّذِي نَزَّلَ ٱلۡفُرۡقَانَ عَلَىٰ عَبۡدِهِۦ لِيَكُونَ لِلۡعَٰلَمِينَ نَذِيرًا1﴾
"Ametukuka aliyeteremsha Furqani (Qur'ani) kwa mja wake, ili awe muonyaji kwa walimwengu wote." [Al-Furqan: 1].
Na wamesimulia Bukhari na Muslim, kutoka kwa Jabir radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: "Nilipewa vitu vitano ambavyo hakuna mtu mwingine aliyepewa hivyo kabla yangu: Nimenusuriwa kwa hofu kwa safari ya mwezi mmoja. Na nilifanyiwa ardhi kuwa msikiti na safi, kwa hivyo mtu yeyote katika umma wangu atakayepatwa na wakati wa swala mahali popote, basi na aswali. Na nilihalalishiwa ngawira, na hakuna mtu yeyote aliye halalishiwa hizo kabla yangu. Na nimepewa uombezi (mkuu). Na Nabii alikuwa akitumwa kwa watu wake hasa, nami nilitumwa kwa watu kwa wote."
Huku ni kubainisha kwa wazi kwa ujumla wa utume wa Mtume wetu Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwa wanadamu wote, na kwamba ulifutilia mbali sheria zote zilizotangulia, na kwamba yeyote ambaye hamfuati Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na hamtii, basi yeye ni kafiri muasi, anayestahili kuadhibiwa. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...وَمَن يَكۡفُرۡ بِهِۦ مِنَ ٱلۡأَحۡزَابِ فَٱلنَّارُ مَوۡعِدُهُۥ...﴾
"Na anayemkufuru katika makundi, basi Moto ndio pahala pa miadi yake." [Hud: 17]. Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...فَلۡيَحۡذَرِ ٱلَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنۡ أَمۡرِهِۦٓ أَن تُصِيبَهُمۡ فِتۡنَةٌ أَوۡ يُصِيبَهُمۡ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴾
"Basi na watahadhari wanaohalifu (kwenda kinyume na) amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu chungu). [An-Nur: 63] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَمَن يَعۡصِ ٱللَّهَ وَرَسُولَهُۥ وَيَتَعَدَّ حُدُودَهُۥ يُدۡخِلۡهُ نَارًا خَٰلِدٗا فِيهَا وَلَهُۥ عَذَابٞ مُّهِينٞ14﴾
"Na anayemuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akaipindukia mipaka yake, (Mwenyezi Mungu) atamtia Motoni adumu humo, na atapata adhabu ya kudhalilisha." [An-Nisaa: 14] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿...وَمَن يَتَبَدَّلِ ٱلۡكُفۡرَ بِٱلۡإِيمَٰنِ فَقَدۡ ضَلَّ سَوَآءَ ٱلسَّبِيلِ﴾
"Na anayebadilisha Imani kwa ukafiri, bila ya shaka huyo amepotea njia iliyo sawa). [Al-Baqarah: 108] Na aya zenye maana hii ni nyingi sana.
Mwenyezi Mungu Mtukufu ameunganisha kumtii Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, pamoja na kumtii Yeye, na akaeleza wazi kwamba yeyote anayeamini kinyume cha Uislamu, basi amepata hasara, na hatakubali kutoka kwake malipo yoyote wala fidia. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿وَمَنْ يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَنْ يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ 85﴾
"Na anayetafuta dini isiyokuwa Uislamu, haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa miongoni mwa wenye kupata hasara." [Al-Imran: 85] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿مَنْ يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّهَ...﴾
"Mwenye kumtii Mtume, basi atakuwa amemtii Mwenyezi Mungu." [An-Nisaa: 80] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿قُلْ أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ فَإِنْ تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُمْ مَا حُمِّلْتُمْ وَإِنْ تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا...﴾
"Sema: Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume. Na mkigeuka, basi yaliyo juu yake ni aliyobebeshwa, na yaliyo juu yenu ni mliyobebeshwa nyinyi. Na mkimtii yeye, mtaongoka." [An-Nur: 54] Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَالْمُشْرِكِينَ فِي نَارِ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا أُولَئِكَ هُمْ شَرُّ الْبَرِيَّةِ 6﴾
"Hakika wale waliokufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu na washirikina wataingia katika Moto wa Jahannamu wadumu milele humo. Hao ndio viumbe waovu kabisa." [Al-Bayyina: 6].
Na Muslim alipokea katika Sahihi yake kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: "Ninaapa kwa yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake. Hakuna yeyote katika umma huu atakayenisikia mimi sawa awe ni Myahudi au Mkristo, kisha akafa bila ya kuamini yale niliyotumwa nayo isipokuwa atakuwa katika watu wa Motoni."
Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe juu yake aliweka wazi kwa vitendo vyake na maneno yake ubatili wa dini ya wale ambao hawakuingia katika Uislamu; kwani alipigana vita na Mayahudi na Wakristo, kama vile alivyopigana na makafiri wengineo, na akachukua kodi ya ulinzi (jizia) kwa wale waliompa ili wasizuie wito wa Uislamu kuwafikia wengine zaidi yao, na ili miongoni mwao waingie katika Uislamu wale wanaotaka kufanya hivyo bila ya kuwaogopa watu wake kuwazuia au kuwaua.
Bukhari na Muslim walisimulia kutoka kwa Abuu Huraira, Mwenyezi Mungu amridhie, kwamba alisema: Tulipokuwa msikitini, Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alitoka nje na akasema: "Nendeni kwa Mayahudi." Basi tukatoka pamoja naye mpaka tukafika katika nyumba ya mafunzo (chuo cha mafunzo), na Mtume rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akasimama na kuwaita akisema: "Enyi kundi la Wayahudi, silimuni, mtasalimika." Wakasema: 'Umeshafikisha, ewe Abul-Qasim.' Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akawaambia: "Hicho ndicho ninachotaka, silimuni, mtasalimika." Wakasema: 'Umeshafikisha, ewe Abul-Qasim.' Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akawaambia: "Hicho ndicho ninachotaka." Kisha akayasema mara ya tatu..." hadi mwisho wa Hadithi.
Kinachokusudiwa ni kwamba Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, alienda kwa watu wenye dini miongoni mwa Wayahudi katika nyumba yao ya mafunzo, kisha akawalingania kwenye Uislamu, na akawaambia: "Silimuni, mtasalimika." na akarudia kuwaambia hayo mara kadhaa.
Vile vile, alituma barua yake kwa Hiraqli huku akimuita kwenye Uislamu, na kumfahamisha kwamba akikataa, basi atabeba dhambi za wale walioukataa Uislamu kwa sababu ya kukataa kwake kusilimu. Bukhari na Muslim walisimulia katika Sahihi zao kwamba: Hiraqli aliitisha barua ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na akaisoma, na tazama, ndani yake kulikuwa: "Bismillahir Rahmanir Rahiim. Kutoka kwa Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwenda kwa Hiraqli, mkuu wa Warumi. Amani iwe juu ya mwenye kufuata uongofu. Ama baada ya kusema hayo: Kwa hakika, mimi ninakuita kwa wito wa Uislamu. Silimu, utasalimika. Na silimu, Mwenyezi Mungu atakupa malipo yako mara mbili. Na ikiwa utapeana mgongo, basi yatakuwa juu yako madhambi ya wakulima wa huko."
﴿يَٰٓأَهۡلَ ٱلۡكِتَٰبِ تَعَالَوۡاْ إِلَىٰ كَلِمَةٖ سَوَآءِۭ بَيۡنَنَا وَبَيۡنَكُمۡ أَلَّا نَعۡبُدَ إِلَّا ٱللَّهَ وَلَا نُشۡرِكَ بِهِۦ شَيۡـٔٗا وَلَا يَتَّخِذَ بَعۡضُنَا بَعۡضًا أَرۡبَابٗا مِّن دُونِ ٱللَّهِۚ فَإِن تَوَلَّوۡاْ فَقُولُواْ ٱشۡهَدُواْ بِأَنَّا مُسۡلِمُونَ64﴾
"Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lililo sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Miungu Walezi badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka, basi semeni: Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu." [Al-'Imran: 64].
Kisha, walipogeuka na wakakataa kuingia katika Uislamu, Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akawapiga vita yeye na Maswahaba wake, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, na akawatoza kodi (jizya).
Na ili kusisitiza upotovu wao na kwamba wako kwenye dini batili baada ya kufutwa na dini ya Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, Mwenyezi Mungu akamuamrisha Muislamu kumuomba Mwenyezi Mungu kila siku, katika kila swala na katika kila rakaa kwamba amuongoze kwenye njia iliyonyooka iliyo sahihi inayokubalika, ambayo ni Uislamu. Na kwamba amuokoe kutokana na njia ya wale aliowakasirikia, yaani Wayahudi na mfano wao ambao wanajua kwamba wako katika batili lakini wanasisitiza kusalia juu yake. Na kwamba amuepushe na njia ya wale waliopotea, wanaoabudu bila ya elimu, na wanadai kwamba wako kwenye njia ya uongofu ilhali wako kwenye njia ya upotofu, yaani Wakristo, na wengineo wanaofanana nao miongoni mwa umma mwingine ambao wanaabudu kwa upotofu na ujinga. Haya yote ni ili Muislamu ajue kwa uhakika kwamba kila dini isiyokuwa ya Kiislamu ni batili, na kwamba kila anayemuabudu Mwenyezi Mungu si kwa Uislamu, ni mpotofu. Na asiyeamini hivi, basi yeye si katika Waislamu. Na ushahidi katika mlango huu ni mwingi katika Kitabu na Sunna.
Basi la wajibu kwa mwandishi wa makala hayo 'Abdul-Fattaah, ni kuharakisha kutubu kisawasawa, na kwamba aandike makala ambayo atatangaza ndani yake toba yake, na mwenye kutubia kwa Mwenyezi Mungu kwa dhati, Mwenyezi Mungu atamsamehe; kwa kauli ya Mwenyezi Mungu aliyetakasika:
﴿...وَتُوبُوٓاْ إِلَى ٱللَّهِ جَمِيعًا أَيُّهَ ٱلۡمُؤۡمِنُونَ لَعَلَّكُمۡ تُفۡلِحُونَ﴾
"Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa". [Surat An-Nur: 31] Na kauli yake Mtukufu:
﴿وَٱلَّذِينَ لَا يَدۡعُونَ مَعَ ٱللَّهِ إِلَٰهًا ءَاخَرَ وَلَا يَقۡتُلُونَ ٱلنَّفۡسَ ٱلَّتِي حَرَّمَ ٱللَّهُ إِلَّا بِٱلۡحَقِّ وَلَا يَزۡنُونَۚ وَمَن يَفۡعَلۡ ذَٰلِكَ يَلۡقَ أَثَامٗا68 يُضَٰعَفۡ لَهُ ٱلۡعَذَابُ يَوۡمَ ٱلۡقِيَٰمَةِ وَيَخۡلُدۡ فِيهِۦ مُهَانًا69 إِلَّا مَن تَابَ وَءَامَنَ وَعَمِلَ عَمَلٗا صَٰلِحٗا فَأُوْلَٰٓئِكَ يُبَدِّلُ ٱللَّهُ سَيِّـَٔاتِهِمۡ حَسَنَٰتٖۗ وَكَانَ ٱللَّهُ غَفُورٗا رَّحِيمٗا70﴾
"Na wale wasiomuomba mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyoiharimisha Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa haki, wala hawazini. Na atakayefanya hayo, atapata madhara.
Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo akifedheheshwa."
Isipokuwa atakayetubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu". [Al-Furqan: 68-70].
Na kwa kauli ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Uislamu unabomoa yaliyokuwa kabla yake, na toba inabomoa yaliyokuwa kabla yake." Na kauli yake Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie: "Mwenye kutubia dhambi, ni kama asiyekuwa na dhambi."
Na kuna hadithi nyingi zenye maana hii.
Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atuonyeshe haki kuwa ni haki na atujaalie kuifuta, na atuonyeshe batili kuwa ni batili na atujaalie kujiepusha nayo. Na atuneemeshe sisi na mwandishi Abdul-Fattaah na Waislamu wote kutubu kisawasawa, na atuepushe sote na fitina za kupotosha, kutii matamanio na Shetani. Hakika yeye ndiye msimamizi wa hayo na Mwenye uwezo juu yake.
Na rehema na amani ziwe kwa Nabii wetu Muhammad, jamaa zake, na Maswahaba wake, na wote wanaowafuata kwa wema mpaka Siku ya Malipo.
***