Risala mbili fupi kuhusu Zaka na Saumu(Funga) (Kiswahili)

Kitabu hiki kinazungumzia faradhi mbili za Zaka na Saumu (Funga), kikiweka wazi hukumu zake na faida zake, sambamba na kuwakumbusha waja haki za Allah juu yao. Kinajumuisha ufafanuzi wa hukumu za Zaka na aina za mali zinazotozwa Zaka, pamoja na fadhila za Ramadhani, na hukumu za Saumu na adabu zake, kwa mfumo wa kielimu unaounganisha uwekaji wa misingi ya kisheria na muongozo wa kimalezi.

  • earth Lugha
    (Kiswahili)
  • earth Mtunzi:
    الشيخ عبد العزيز بن باز
PHPWord

 

 

رِسَالَتَانِ مُوجَزَتَانِ فِي الزَّكَاةِ وَالصِّيَامِ

 

Risala mbili fupi kuhusu Zaka na Saumu(Funga)

 

سَمَاحَةُ الشَّيْخِ

عَبْدِ الْعَزِيزِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ بَازٍ رَحِمَهُ اللَّهُ

 

 

Cha Mheshimiwa, Sheikh,

Abdul Aziz bin Abdillah bin Baaz

Mwenyezi Mungu Mtukufu amrehemu

 


بِسْمِ اللهِ الرَّحمَنِ الرَّحِيمِ

Risala ya kwanza

Kuhusu tafiti muhimu juu ya Zaka

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

Kila sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu peke yake, na rehema na amani ziwe juu ya yule ambaye hakuna nabii baada yake, na ziwe juu ya watu wa familia yake na Maswahaba wake. Ama baada ya hayo:

Hakika kilichopelekea kuandika neno hili ni kutoa nasaha na kukumbusha juu ya uwajibu wa Zaka, ambayo Waislamu wengi wamezembea kuhusiana nayo, wakawa hawailipi kwa njia ya kisheria, licha ya hadhi yake kubwa, na ukweli kwamba ni moja ya nguzo tano za Uislamu ambazo bila hiyo muundo wake hauwezi kusimama sawasawa. Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake:

 

 

 

 

"Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano: Kushuhudia kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na kusimamisha Swala, kutoa Zaka, kufunga Ramadhani, na kuhiji Nyumba Tukufu."1 (Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wake).

Kuwafaradhishia Waislamu Zaka ni katika sifa nzuri za Uislamu na utunzaji wake mambo ya wafuasi wake. Hili ni kwa sababu ya manufaa yake mengi na hitajio kubwa la Zaka kwa Waislamu walio masikini .

Miongoni mwa faida zake ni: Kuimarisha uhusiano wa upendo kati ya matajiri na maskini; Kwa sababu nafsi zimeumbwa na sifa ya kuwapenda wale wanaozifanyia wema.

Na miongoni mwake ni: Kuisafisha na kuitakasa nafsi, na kuiweka mbali na tabia za ubakhili na uchoyo, kama ilivyoashiria Qur-ani Tukufu maana hii katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿خُذۡ مِنۡ أَمۡوَٰلِهِمۡ صَدَقَةٗ تُطَهِّرُهُمۡ وَتُزَكِّيهِم بِهَا...﴾

"Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo." [At-Tawba: 103].

Na miongoni mwake ni: Kuwazoesha Waislamu kuwa na sifa ya kutoa kwa wingi, ukarimu na kuwahurumia wale wanaohitaji.

Na miongoni mwake ni: Kuleta baraka, kuongezewa na kurudishiwa mema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...وَمَآ أَنفَقۡتُم مِّن شَيۡءٖ فَهُوَ يُخۡلِفُهُۥۖ وَهُوَ خَيۡرُ ٱلرَّٰزِقِينَ﴾

"Na chochote mtakachokitoa, Yeye atakilipa. Naye ni Mbora wa wanaoruzuku." [Saba: 39]. Na amesema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika hadithi sahihi(Al-qudsi): Mwenyezi Mungu anasema:“Ewe mwanadamu,toa, na sisi tutakupa…”2 Na faida nyingine nyingi.

Imekuja ahadi ya adhabu kali kwa wale wanaofanya ubakhili katika kuitoa au wale wanaopuuza kuilipa. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿...وَٱلَّذِينَ يَكۡنِزُونَ ٱلذَّهَبَ وَٱلۡفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ ٱللَّهِ فَبَشِّرۡهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٖ 34 يَوۡمَ يُحۡمَىٰ عَلَيۡهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكۡوَىٰ بِهَا جِبَاهُهُمۡ وَجُنُوبُهُمۡ وَظُهُورُهُمۡۖ هَٰذَا مَا كَنَزۡتُمۡ لِأَنفُسِكُمۡ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمۡ تَكۡنِزُونَ35﴾

"Na wale wanaokusanya dhahabu na fedha, wala hawazitoi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wape habari ya adhabu iumizayo.

 

 

Siku zitakapotiwa moto Mali zao katika Moto wa Jahannamu, na kwazo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, na huku wakaambiwa: Haya ndiyo mliyojilimbikizia nafsi zenu.Basi onjeni mliyokuwa mkilimbika."[At-Tawba: 34-35]. Kwa hivyo, mali zote ambazo hazitolewi Zaka, hizo ni mali zilizolimbikwa ambazo mwenye mali ataadhibiwa Siku ya Kiyama kwa ajili yake, kama ilivyoashiriwa na Hadithi Sahihi kutoka kwa Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, kwamba alisema: “Hakuna yoyote mwenye kumiliki dhahabu wala fedha ambaye hazitolei haki yake isipokuwa Siku ya Kiyama atatandikiwa sahani za moto. Kisha zitatiwa moto katika Moto wa Jahannam, kisha utapigwa pasi kwazo ubavu wake, paji la uso wake na mgongo wake. Kila zitakapopoa, zitatiwa moto tena kwa ajili yake katika siku ambayo urefu wake ni miaka elfu hamsini, mpaka itakapohukumiwa kati ya waja. Hapo ataona njia yake: Ima kwenda Peponi au Motoni."3

Kisha Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akamtaja mwenye ngamia, ng’ombe na kondoo asiyetoa Zaka, na akatufahamisha kuwa ataadhibiwa kwa ajili ya wanyama hao siku ya Kiyama.

 

Na imepokelewa kwa njia sahihi kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema: “Yeyote atakayepewa mali na Mwenyezi Mungu na asitoe Zaka yake, atafanywa mali hiyo kuwa nyoka mwenye kipara, mwenye madoa mawili meusi juu ya macho yake. Atamzunguka kwenye shingo lake Siku ya Kiyama, kisha atamshika kwa taya zake mbili na aseme: ‘Mimi ni ile mali yako. Mimi ni hazina yako.’” Kisha Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake akasoma, “Wala wasidhani wale ambao wanafanya ubakhili katika aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake kuwa ni kheri kwao. Bali hiyo ni shari kwao. Watafungwa kongwa(yoke) za yale waliyoyafanyia ubakhili Siku ya Kiyama." [Al Imran: 180].4

Na Zaka ni wajibu katika makundi manne ya mali: Nafaka na matunda yanayozalishwa katika ardhi, mifugo wanaoachiliwa kula wenyewe kwenye malisho, dhahabu na fedha, na bidhaa za biashara.

Na kila kimoja kati ya makundi haya manne kina kiwango maalumu, na Zaka si wajibu kwa mali ambayo haikufikia kiwango. Kiwango cha chini cha nafaka na matunda ni wasq tano. Nayo wasq ni swa’a sitini kwa mujibu wa swa’a ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.

Nafaka na matunda haya ni kama vile tende, zabibu, ngano, mchele, shayiri na mfano wake. Wasq tano ni sawa na swa'a mia tatu kwa kipimo cha swa'a ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Nayo swa'a ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ni sawa na machoto manne yaliyojaa kwa mikono ya mtu wa maumbile ya wastani.

Kilicho wajibu kutoa katika hivyo ni moja ya kumi ikiwa mitende na mazao hayo yalinyweshelezwa maji bila gharama ya mkulima, kama vile maji ya mvua, mito, chemchemi zinazotiririka na mfano wake.

Ama ikiwa yalimwagiliwa maji kwa juhudi na gharama ya mkulima, kama vile kutumia magurudumu ya kunyunyizia na mashine za kunyunyizia maji, na vinginevyo, basi kilicho wajibu kutoa ni nusu ya ushuri, kama ilivyopokelewa kwa njia sahihi katika Hadithi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake:

Ama kiasi cha chini kabisa cha mifugo wanaoachiliwa kula wenyewe katika malisho kama vile ngamia, ng'ombe na kondoo, basi kuna maelezo ya kina juu ya hili katika hadithi sahihi za Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Kwa hivyo, mwenye kutaka kujua maelezo hayo ya kina, basi anaweza kuwauliza wenye elimu juu ya jambo hili.

Na lau si kwa sababu tulitaka kufupisha makala hii, basi tungeliyataja hapa kwa ajili ya kukamilisha manufaa.

Na ama kiwango cha chini zaidi cha fedha, hicho ni mithqal mia moja na arobaini, na kiasi chake kwa dirhamu za Saudi Arabia ni riyali hamsini na sita. (Tanbihi: Fatwa hii ilitolewa miaka mingi iliyopita na bila shaka kiwango kilichotajwa hapa cha dirhamu za Saudi Arabia si kama kilivyo sasa).

Kiwango cha chini kabisa cha dhahabu ni mithqal ishirini, na thamani yake katika pauni za Saudia ni pauni kumi na moja na sehemu tatu za saba za pauni. Na ikipimwa kwa gramu ni gramu tisini na mbili, na kiwango cha kutolewa katika fedha na dhahabu ni robo ya kumi kwa yeyote mwenye kiwango hiki cha chini katika viwili hivyo au moja yake na akazungukiwa na mwaka mmoja kamili tangu alipovimiliki.

Na faida ina hukumu ya mali ya asili na wala haihitaji kupitiwa na mwaka mpya. Vile vile wanyama waliozaliwa wana hukumu ya mifugo waliowazaa na wala hawahitaji kupitiwa na mwaka mpya ikiwa wale waliowazaa wamefika kiwango cha chini cha kutoa Zaka.

Vile vile, pesa za karatasi ambazo watu hutumia leo, sawa ziwe zinaitwa dirhamu, dinari, dola, au jina lingine lolote zinaingia katika hukumu ya dhahabu na fedha. Iwapo thamani yake itafikia kiwango cha chini cha fedha au dhahabu na mwaka mmoja ukapita, basi mwenyewe atalazimika kutoa Zaka.

Vile vile vito vya wanawake vilivyotengenezwa kwa dhahabu au fedha vinachukua hukumu ya dhahabu au fedha, haswa ikiwa vinafikia kiwango cha chini na vikapitiwa na mwaka mmoja, basi inalazimu kuvitolea Zaka hata ikiwa vimetayarishwa kwa ajili ya matumizi au kukopeshwa, kulingana na maoni sahihi zaidi ya wanachuoni, na kwa ujumla wa kauli ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie:Hakuna mwenye dhahabu wala fedha ambaye hazitolei Zaka yake isipokuwa Siku ya Kiyama atatandikiwa sahani za moto."5 Hadi mwisho wa Hadithi iliyotangulia.

Na kwa yale yaliyothibiti kwamba Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, aliona bangili mbili za dhahabu kwenye mkono wa mwanamke mmoja, kwa hivyo akasema: "Unatoa Zakat ya hizi?" Akasema: 'Hapana.' Akasema: “Je, inakupendeza kwamba Mwenyezi Mungu akutengenezee kwazo bangili mbili za moto siku ya Kiyama!” Kwa hivyo, akazitupa chini na kusema: “Ni vya Mwenyezi Mungu na Mtume wake.”6

Ilithibiti kutoka kwa Ummu Salama, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, kwamba alikuwa akivaa vito vya dhahabu, hivyo akasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, je, hivi ni hazina?" Akasema:

"Kinachofikia kiwango cha kutoa Zaka na kikatolewa Zaka, basi si hazina."7 Pamoja na Hadithi zingine zenye maana hii.

Ama bidhaa zilizoandaliwa kwa ajili ya biashara, hizo zinafaa kutathminiwa mwishoni mwa mwaka kisha itolewe Zaka ya robo ya kumi ya thamani yake, sawa iwe thamani yake ni sawa na bei yake, zaidi au chini yake. Hili ni kwa sababu ya hadithi iliyosimuliwa na Samura, kwamba alisema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alikuwa akituamrisha kutoa sadaka (Zaka) katika vile tulivyovitayarisha kwa ajili ya kuuza.”8

Hili linajumuisha mashamba yaliyotayarishwa kwa ajili ya kuuzwa, majengo, magari, mashine za kuvuta maji, na aina nyinginezo za bidhaa zilizotayarishwa kwa ajili ya kuuzwa.

Ama majengo ambayo yamekusudiwa kukodishwa, sio kuuzwa, Zaka yake itatolewa kwa kodi yake ikiwa mwaka utaipitia.Ama majengo yenyewe, hayo hayatolewi Zaka.

Kwa sababu hayajaandaliwa kwa ajili ya kuuzwa. Vile vile magari ya kibinafsi na ya teksi hayatolewi Zaka ikiwa hayajaandaliwa kwa ajili ya kuuzwa, bali mmiliki wake alizinunua kwa ajili ya matumizi yake mwenyewe.

Ikiwa mwenye teksi au mtu mwingine ana pesa zinazofikia kiwango cha chini kabisa cha kutoa Zaka, basi ni lazima alipe Zaka yake baada ya mwaka mmoja kuzipitia, sawa awe alikusudia kuzitumia katika matumizi ya nyumbani, kuoa, kununua majengo na mashamba, kulipa deni au madhumuni mengine yoyote. Hili ni kwa sababu ya ujumla wa ushahidi wa kisheria unaoonyesha wajibu wa kutoa Zaka katika hali hizi.

Maoni sahihi ya wanachuoni ni kwamba deni halizuii kutoa Zaka, kama ilivyotajwa hapo awali.

Vivyo hivyo inalazimu kutoa Zaka katika mali za mayatima na wendawazimu kwa mujibu wa wengi wa wanavyuoni ikiwa zinafikia kiwango cha chini cha kutoa Zaka na mwaka mmoja ukazipitia. Ni wajibu kwa walezi wao kutoa humo Zaka kwa niaba yao mwaka utakapokamilika. Haya ni kwa ujumla wa ushahidi mbalimbali kama vile kauli ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika Hadithi ya Muadh, Mwenyezi Mungu amwiye radhi, alipomtuma kwa watu wa Yemen:

“Mwenyezi Mungu amewafaradhishia kutoa sadaka (Zaka) katika mali zao. Ichukuliwe kutoka kwa matajiri wao na wapewe masikini wao.”9

Zaka ni haki ya Mwenyezi Mungu, na hairuhusiki kujipendekeza kwayo kwa wale wasioistahiki, wala mtu kujiletea manufaa au kujikinga na madhara kwa kutumia mali hiyo, wala mtu kuilinda mali yake au kuiepusha mbali na lawama. Bali ni lazima Muislamu atoe Zaka na kuwapa wanaoistahiki kwa sababu wao ni miongoni mwa wenye mali hiyo, si kwa lengo lingine lolote. Vile vile anapaswa kufanya hivyo kwa moyo mwema na kumkusudia Mwenyezi Mungu peke yake kwa hilo; ili dhima yake iondolewe na astahiki malipo makubwa na kurudishiwa na Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu ameeleza katika Kitabu chake kitukufu makundi ya wale wanaostahiki kupata Zaka. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿إِنَّمَا ٱلصَّدَقَٰتُ لِلۡفُقَرَآءِ وَٱلۡمَسَٰكِينِ وَٱلۡعَٰمِلِينَ عَلَيۡهَا وَٱلۡمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمۡ وَفِي ٱلرِّقَابِ وَٱلۡغَٰرِمِينَ وَفِي سَبِيلِ ٱللَّهِ وَٱبۡنِ ٱلسَّبِيلِۖ فَرِيضَةٗ مِّنَ ٱللَّهِۗ وَٱللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٞ60﴾

 

 

 

"Hakika wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanaozitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni wajibu uliofaridhiwa na Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujuwa mno, na Mwenye hekima." [At-Tawbah: 60].

Katika kuhitimisha Aya hii tukufu kwa majina haya mawili makubwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu anawahadharisha waja wake kwamba Yeye, Mwenyezi Mumgu ndiye ajuaye zaidi hali za waja wake: Ni nani miongoni mwao anastahiki Zaka na asiyeistahiki. Naye ndiye Mwenye hekima katika sheria na mipango yake. Kwa hivyo, hawezi kuweka vitu isipokuwa mahali pake panapostahiki, hata ikiwa baadhi ya siri za hekima yake zitafichikana kwa baadhi ya watu. Haya ni ili waja wapate kupata utulivu juu ya sheria yake na kujisalimisha kwayo.

Mwenyezi Mungu ndiye anayeombwa atuwezeshe sisi na Waislamu katika kuifahamu dini yake, tuwe wakweli katika kuamiliana naye, na kushindania katika yale yanayomridhisha, na atuweke salama kutokana na sababu za ghadhabu yake. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, aliye karibu zaidi!

 

Na rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mja wake na Mtume wake Muhammad, familia yake na Maswahaba wake.

Kiongozi Mkuu wa Idara za Tafiti za Kisayansi

Na fat'wa, Kulingania kwa Mwenyezi Mungu na Kuelekeza,

Muheshimiwa, Sheikh, Abdul Aziz bin Abdillah bin Baaz.

 

 

***

 


Risala ya Pili

Kuhusu fadhila za kufunga na kuswali wakati wa Ramadhani, pamoja na kueleza hukumu muhimu ambazo zinaweza kufichikana kwa baadhi ya watu

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

Kutoka kwa Abdul Aziz bin Abdillah bin Baaz, kwenda kwa yeyote atakayeiona miongoni mwa Waislamu, Mwenyezi Mungu aniongoze mimi na wao kupitia kwenye njia ya watu wa imani, na aniwezeshe mimi na wao kuifahamu Sunna na Qur-ani. Amin!

Amani iwe juu yenu, na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka zake.

Ama baada ya hayo: Hii ni nasaha fupi kuhusiana na ubora wa kufunga na kuswali katika Ramadhani, na ubora wa kushindana katika mambo mema, pamoja na kueleza hukumu muhimu zinazoweza kufichikana kwa baadhi ya watu.

Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba alikuwa akiwapa Maswahaba wake habari njema ya kufika kwa mwezi wa Ramadhani, na alikuwa akiwaambia kwamba ni mwezi ambao hufunguliwa ndani yake milango ya rehema na milango ya Peponi,

na hufungwa ndani yake milango ya Jahannam, na mashetani hufungwa pingu. Alikuwa akisema: “Unapoingia usiku wa kwanza wa Ramadhani, hufunguliwa milango ya Pepo na haufungwi hata mmoja wake, na milango ya Motoni hufungwa na haufunguliwi hata mmoja wake, na mashetani hufungwa pingu, na mwitaji anaita: 'Ewe mtafutaji heri, njoo. Na ewe mtafutaji uovu, komeka.' Na Mwenyezi Mungu anao anaowaachilia huru kutokana na Moto, na hilo ni kila usiku."

Vile vile, yeye, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alikuwa akisema: "Umekujieni Mwezi wa Ramadhani, mwezi wa baraka ambao Mwenyezi Mungu anakufunikeni ndani yake: Anateremsha rehema, anaondoa madhambi na anaitikia maombi. Mwenyezi anaangalia kushindana kwenu ndani yake, kisha anajisifu kwenu mbele ya Malaika wake. Kwa hivyo, mwonyesheni Mwenyezi Mungu yaliyo bora katika nafsi zenu. Kwani hakika, muovu ni yule ambaye atanyimwa rehema za Mwenyezi Mungu ndani yake."

Vile vile, yeye, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alikuwa akisema: "Atakayefunga Ramadhani kwa imani na kwa kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.

 

 

 Na atakayesimama (katika swala) katika mwezi wa Ramadhani kwa imani na kwa kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia. Na atakayesimama katika Usiku wa Cheo kwa imani na kwa kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia."

Vile vile, yeye, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake alikuwa akisema: Mwenyezi Mungu anasema: Kila tendo la mwanadamu linalipwa mara kumi mfano wake na kuzidishwa mpaka kufikia mia saba, isipokuwa saumu. Kwani, hiyo kwahakika ni yangu, nami ndiye nitakayeilipa. Aliacha tamaa zake, chakula chake na vinywaji vyake kwa ajili yangu. Mfungaji ana furaha mbili: Furaha anapofungua, na furaha atakapokutana na Mola wake Mlezi. Na hakika, harufu mbaya ya mdomo wa mtu aliyefunga ni nzuri zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko harufu ya miski."

Kuna hadithi nyingi kuhusu ubora wa kufunga na kuswali ndani ya Ramadhani na pia ubora wa kufunga saumu wakati wowote.

Hivyo basi, Muumini anafaa kuchangamkia fursa hii, ambayo ni kile ambacho Mwenyezi Mungu amemneemesha kwacho cha kuupata mwezi wa Ramadhani. Basi na aharakishe kufanya vitendo vya utiifu, na ajiepusha mbali na maovu, na ajitahidi kutekeleza yale ambayo Mwenyezi Mungu alimuamrisha, haswahaswa Swala tano za kila siku.

Hizo hakika ndizo nguzo ya Uislamu, na ndizo wajibu mkubwa zaidi baada ya Shahada mbili. Basi la wajibu kwa kila Muislamu mwanamume na mwanamke ni kuitunza na kuitekeleza katika nyakati zake zilizowekwa kwa unyenyekevu na utulivu.

Miongoni mwa wajibu wake muhimu kwa wanaume ni kuitekeleza katika mkusanyiko (jamaa) katika nyumba za Mwenyezi Mungu ambazo Mwenyezi Mungu ameruhusu linyanyuliwe na litajwe humo jina lake, kama alivyosema:

﴿وَأَقِيمُواْ ٱلصَّلَوٰةَ وَءَاتُواْ ٱلزَّكَوٰةَ وَٱرۡكَعُواْ مَعَ ٱلرَّٰكِعِينَ 43﴾

"Na simamisheni Swala, na toeni Zaka na inameni pamoja na wanaoinama(walio waislamu)."[Al-Baqara: 43]. Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿حَٰفِظُواْ عَلَى ٱلصَّلَوَٰتِ وَٱلصَّلَوٰةِ ٱلۡوُسۡطَىٰ وَقُومُواْ لِلَّهِ قَٰنِتِينَ 238﴾

"Zilindeni Swala, na hasa Swala ya katikati, na simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu nanyi ni wenye kunyenyekea." [Al-Baqara: 238]. Na alisema:

﴿قَدۡ أَفۡلَحَ ٱلۡمُؤۡمِنُونَ 1 ٱلَّذِينَ هُمۡ فِي صَلَاتِهِمۡ خَٰشِعُونَ 2﴾

"Hakika wamefanikiwa Waumini.

Ambao ni wanyenyekevu katika Sala zao."

[Al-Mu-minun: 1-2] Mpaka aliposema:

 

﴿وَٱلَّذِينَ هُمۡ عَلَىٰ صَلَوَٰتِهِمۡ يُحَافِظُونَ 9 أُوْلَٰٓئِكَ هُمُ ٱلۡوَٰرِثُونَ 10 ٱلَّذِينَ يَرِثُونَ ٱلۡفِرۡدَوۡسَ هُمۡ فِيهَا خَٰلِدُونَ 11﴾

9. "Na ambao Swala zao wanazihifadhi. 10. Hao ndio warithi. 11. Ambao watairithi Pepo ya Firdausi, wadumu humo." [Al-Mu-uminun: 9-11] Na alisema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie: “Agano lililo baina yetu na wao ni Swala. Kwa hivyo, mwenye kuiacha, basi atakuwa amekufuru."

Faradhi muhimu zaidi baada ya swala ni kutoa Zaka, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَمَآ أُمِرُوٓاْ إِلَّا لِيَعۡبُدُواْ ٱللَّهَ مُخۡلِصِينَ لَهُ ٱلدِّينَ حُنَفَآءَ وَيُقِيمُواْ ٱلصَّلَوٰةَ وَيُؤۡتُواْ ٱلزَّكَوٰةَۚ وَذَٰلِكَ دِينُ ٱلۡقَيِّمَةِ 5﴾

"Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu, na washike Swala, na watoe Zaka. Na hiyo ndiyo Dini madhubuti." [Al-Bayyina: 5]. Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَأَقِيمُواْ ٱلصَّلَوٰةَ وَءَاتُواْ ٱلزَّكَوٰةَ وَأَطِيعُواْ ٱلرَّسُولَ لَعَلَّكُمۡ تُرۡحَمُونَ 56﴾

"Na simamisheni Sala, na toeni Zaka, na mtiini Mtume, ili mpate kurehemewa." [An-Nur: 56].

Kitabu Kikuu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume wake Mtukufu vimeashiria kwamba asiyetoa Zaka ya mali yake, ataadhibiwa kwayo Siku ya Kiyama.

Na jambo muhimu zaidi baada ya swala na zaka ni funga ya Ramadhani ambayo ni moja ya nguzo tano za Uislamu zilizotajwa katika kauli ya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano: Kushuhudia kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, kusimamisha Swala, kutoa Zaka, kufunga Ramadhani na kuhiji Nyumba Tukufu."

Mwislamu anapaswa ailinde saumu yake na kisimamo chake katika swala kutokana na yale ambayo Mwenyezi Mungu amemharamishia miongoni mwa maneno na vitendo. Kwa sababu makusudio ya saumu ni kumtii Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuheshimu makatazo yake, na kupambana na nafsi juu ya kuhalifu matamanio yake katika kumtii Mola wake, na kuizoesha kuwa na subira juu ya yale aliyoharamisha Mwenyezi Mungu. Na makusudio sio kuwacha tu vyakula, vinywaji na mambo yote mengineyo yanayomfanya mtu kufungua. Ndiyo maana ikapokewa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba alisema: “Saumu(Funga) ni ngao. Kwa hivyo, inapokuwa ni siku ya funga ya mmoja wenu, basi na asiseme maneno machafu wala asipaze sauti yake.

 

 

Na kama mtu atamtukana au kupigana naye, basi na aseme, 'Hakika mimi nimefunga.'" Imepokelewa kwa njia sahihi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba alisema: "Yeyote asiyeacha maneno ya uongo na kuyafanyia kazi na upuuzi, basi Mwenyezi Mungu hana haja ya kuacha kwake chakula chake na kinywaji chake." Basi ikajulikana kwa maandiko haya na mengine, kwamba la wajibu kwa mtu mwenye funga ni kujihadhari na kila kitu ambacho Mwenyezi Mungu amemharamishia na kudumisha kila kitu ambacho Mwenyezi Mungu amemwajibishia, na kwa hayo, anatarajiwa kusamehewa, kuachiliwa huru kutokana na Moto, na kukubalika kwa Saumu yake na kusimama kwake katika swala.

Kuna mambo ambayo yanaweza kufichikana kwa baadhi ya watu:

Miongoni mwake ni kwamba wajibu uliopo juu ya Muislamu ni kufunga kwa ajili ya imani na kutarajia malipo, si kwa ajili ya kujionyesha, kutafuta kusikiwa, kujifananisha na watu, au kufuata familia yake au watu wa nchi yake. Bali la wajibu kwake ni kwamba linalomfanya kufunga ni kwa sababu anaamini kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyemlazimisha kufanya hivyo, na anatarajia malipo kwa Mola wake Mlezi kwa sababu ya hayo.

 

Vile vile, Muislamu anatakiwa kusimama usiku kwenye swala katika Ramadhani kwa sababu ya kumuamini Mwenyezi Mungu na kutarajia malipo, si kwa sababu nyingine. Ndiyo maana Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, akasema: “Mwenye kufunga Ramadhani kwa imani na kwa kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia. Na atakayesimama usiku kwenye swala katika mwezi wa Ramadhani kwa imani na kwa kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia. Na atakayesimama Usiku wa Cheo kwenye swala katika mwezi wa Ramadhani kwa imani na kwa kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia."

Na miongoni mwa mambo ambayo hukumu yake inaweza kufichikana kwa baadhi ya watu ni yale yanayoweza kumtokea mfungaji kwa namna ya majeraha, kutokwa na damu puani, kutapika, au maji au petroli kuingia kooni mwake bila ya hiari yake; mambo yote haya hayabatilishi saumu. Lakini mtu akitapika kwa kukusudia, saumu yake inaharibika, kama alivyosema Mtume: “Mwenye kutapika bila hiari yake, basi si lazima kufidia saumu. Lakini mwenye kujitapisha, basi na alipe saumu ya siku hiyo."

 

 

Na miongoni mwake ni hali ya mfungaji kuchelewesha kuoga janaba mpaka kupambazuka kwa alfajiri, na yale yanayowapata baadhi ya wanawake ya kuchelewesha kuoga kutokana na hedhi au kutokana na damu baada ya kuzaa hadi kuchomoza kwa alfajiri. Ikiwa ataona hali ya usafi kabla ya kupambazuka kwa alfajiri, basi atalazimika afungue, wala kuchelewesha kwake kuoga mpaka kuchomoza kwa alfajiri hakumzuii kufunga, lakini hafai kuchelewesha hilo hadi kuchomoza kwa jua. Bali anatakiwa kuoga na kuswali swala ya alfajiri kabla ya kuchomoza kwa jua. Vivyo hivyo, mtu aliye katika hali ya janaba hafai kuchelewesha kuoga mpaka baada ya kuchomoza kwa jua. Bali inamlazimu aoge na aswali Alfajiri kabla ya kuchomoza kwa jua. Inamlazimu mwanamume kuharakisha kufanya hivyo ili aweze kuswali swala ya alfajiri pamoja na jamaa (msikitini).

Na miongoni mwa mambo ambayo hayabatilishi saumu ni: Vipimo vya damu na kudungwa sindano ambazo hazikusudiwi kupitisha lishe. Hata hivyo, kuchelewesha hayo hadi usiku ndiyo bora na ndilo lenye tahadhari zaidi ikiwa inawezekana; kama alivyosema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Achana yale yanayokupa shaka uendee yale ambayo hayakupi shaka."

Na kauli yake Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, "Mwenye kujiepusha na mambo ya shaka,

basi hakika atakuwa amejitoa lawamani kuhusiana na dini yake na heshima yake."

Na miongoni mwa mambo ambayo hukumu yake imefichikana kwa baadhi ya watu ni kutokuwa na utulivu katika swala, iwe ni swala ya faradhi au ya hiari. Hadithi sahihi za Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ziliashiria kwamba utulivu ni moja ya nguzo za swala ambayo bila ya hiyo swala haiwi sahihi. Nayo ni kutulizana katika swala na kunyenyekea, na kutokuwa na papara hadi kila kiungo kirudi mahala pake. Na watu wengi huswali katika Ramadhani swala ambayo hawaielewi wala hawatulii ndani yake. Bali wanaidonadona tu. Kwa hivyo, swala ya namna hii ni batili, na mwenye kuifanya anapata dhambi na hatapata malipo yake.

Na miongoni mwa mambo ambayo hukumu yake inaweza kufichikana kwa baadhi ya watu ni kwamba baadhi yao wanadhani kuwa Tarawehe haiwezi kuwa chini ya rakaa ishirini, na baadhi yao wanadhani kuwa haiwezi kuongezwa zaidi ya rakaa kumi na moja au kumi na tatu. Yote haya ni dhana isiyo sahihi. Bali ni kosa linalopingana na ushahidi.

 

 

 

 

Hadithi sahihi za Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ziliashiria kwamba swala ya usiku ina wasaa mkubwa, na hakuna kikomo maalumu cha rakaa ambacho hakiwezi kukiukwa. Bali imethibiti kwamba yeye, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alikuwa akiswali rakaa kumi na moja usiku, na wakati mwingine alikuwa akiswali rakaa kumi na tatu, na hata huenda akaswali rakaa chini ya hizo katika Ramadhani na wakati mwingineo. Alipoulizwa kuhusu swala ya usiku, akasema: "Ni rakaa mbili mbili. Na ikiwa mmoja wenu atahofia Alfajiri kuingia, basi na aswali rakaa moja ili iwe Witiri ya rakaa alizokwisha swali." (Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wake).

Hakuweka kikomo mahususi cha rakaa, si katika Ramadhani wala katika mwezi wowote ule. Ndiyo maana Maswahaba katika zama za Umar, Mwenyezi Mungu amwiye radhi, wakati mwingine walikuwa wakiswali rakaa ishirini na tatu na wakati mwingine rakaa kumi na moja. Yote haya yamethibiti kutoka kwa Umar, Mwenyezi Mungu amwiye radhi, na kutoka kwa Maswahaba katika zama zake.

Baadhi ya Waislamu wa mwanzo walikuwa wakiswali rakaa thelathini na sita katika mwezi wa Ramadhani, na kuswali Witiri rakaa tatu.

 

Na baadhi yao walikuwa wakiswali rakaa arubaini na moja. Haya yalisimuliwa kuwahusu kutoka kwa sheikhul-Islam Ibnu Taymiyya na wengineo miongoni mwa wanazuoni. Vile vile, alitaja - Mwenyezi Mungu amrehemu - kwamba suala hili lina wasaa mkubwa. Pia akataja kuwa ni bora mwenye kusoma kisomo kirefu, rukuu na sijda afupishe idadi ya rakaa. Na mwenye kuhafifisha kisomo, rukuu na sijida, ni bora aongeze idadi ya rakaa. Hii ndiyo maana ya maneno yake – Mwenyezi Mungu amrehemu.

Mwenye kutafakari Sunna za Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, atajua kwamba lililo bora katika yote haya ni kuswali rakaa kumi na moja au kumi na tatu katika Ramadhani na nyakati nyinginezo. Kwa sababu hayo ndiyo yanayokubaliana na yale aliyoyafanya Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika hali zake nyingi, na kwa sababu ni mepesi zaidi kwa wanaoswali, na ya karibu zaidi na unyenyekevu na utulivu. Hata hivyo, mwenye kuzidisha, basi hana ubaya wala hilo halichukizi, kama ilivyotajwa hapo awali.

Nia ilivyo bora kwa mwenye kuswali pamoja na imamu katika swala ya usiku wa Ramadhani asiondoke isipokuwa pamoja na imamu; kama alivyosema Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake:

 

“Hakika mtu akisimama pamoja na imamu mpaka aondoke, basi Mwenyezi Mungu atamuandikia malipo ya kusimama usiku mzima katika swala.”

Inaruhusiwa kisheria kwa Waislamu wote kujitahidi kufanya ibada za aina mbalimbali katika mwezi huu uliobarikiwa, zikiwemo swala za hiari, kusoma Qur-ani kwa kuitafakari na kuizingatia, kumtakasa Mwenyezi Mungu, kusema hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, kumsifu, kumtukuza, kuomba msamaha, kuomba dua za kisheria, kuamrisha mema na kukataza maovu, kulingania kwa Mwenyezi Mungu, kuwasaidia mafukara na maskini, kufanya bidii katika kuwafanyia wema wazazi, kuwaunga jamaa, kuwakirimu majirani, kuwatembelea wagonjwa na aina nyingine za wema. Kwa sababu Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, alisema katika hadithi iliyotangulia: "Mwenyezi Mungu anaangalia kushindana kwenu ndani yake, kisha anajisifu kwenu mbele ya Malaika wake. Kwa hivyo, mwonyesheni Mwenyezi Mungu yaliyo bora katika nafsi zenu. Kwani hakika, Muovu ni yule ambaye atanyimwa rehema za Mwenyezi Mungu ndani yake."

Na kwa yaliyopokewa kutoka kwake, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwamba alisema:

 

 

"Mwenye kujiweka karibu na Mwenyezi Mungu ndani yake kwa kitendo miongoni mwa vitendo vyema, atakuwa kama kwamba amefanya jambo la faradhi katika miezi mingineyo. Na atakayefanya humo jambo la faradhi, atakuwa ni kama kwamba amefanya faradhi sabini katika miezi mingineyo."

Na kwa maneno yake Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, katika hadithi sahihi: "Umra katika Ramadhani ni sawa na Hija." au alisema: "Ni sawa na Kufanya Hijja pamoja nami."

Kuna hadithi nyingi na riwaya zinazoonyesha uhalali wa kushindana katika aina mbalimbali za matendo mema katika mwezi huu uliobarikiwa.

Na Mwenyezi Mungu ndiye anayeombwa atuwezeshe sisi na Waislamu wote kufikia kila linalomridhisha, na kwamba atukubalie saumu zetu na kusimama kwetu katika swala, na kwamba azitengeneze hali zetu, atulinde sote kutokana na vishawishi vinavyopotosha. Vile vile, tunamuomba Yeye aliyetakasika kwamba awaboreshe viongozi wa Waislamu na aliunganishe neno lao juu ya haki. Kwani, Yeye ndiye Mlinzi wa hayo na Mweza wa kufanya hivyo.

Amani iwe juu yenu, na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka zake.

***

 

Yaliyomo

 

Risala ya kwanza 2

Kuhusu tafiti muhimu juu ya Zaka 2

Risala ya Pili 15

Kuhusu fadhila za kufunga na kuswali wakati wa Ramadhani, pamoja na kueleza hukumu muhimu ambazo zinaweza kufichikana kwa baadhi ya watu 15

***


Imepokelewa na Muslim, nambari 987.

Imepokelewa na Bukhari, nambari 1338.

Imepokelewa na Muslim, nambari 987.

Imepokelewa na Abu Daawuud, nambari 1563, na An-Nasaai, nambari 2270, kwa msururu mzuri wa upokezaji (sanad).

Imepokelewa na Abu Daud, nambari 1564.

Imepokelewa na Abu Dawud, nambari 1562.

Imepokelewa na Bukhari, nambari 1395, na Muslim, nambari 19.

Imepokelewa na Bukhari, nambari 8, na Muslim, nambari 16.

Imepokelewa na Muslim, nambari 993.